Nokora mpumbavu
Iko hadithi ya nokora mpumbavu. Nokora ni mnyapara wa watumwa; lakini yeye mwenyewe pia ni mtumwa, ila kavikwa kilemba cha ukoka kupewa cheo cha kuwaangalia wenzake. Basi alikuwako Mwarabu mmoja tajiri sana jina lake El-Mahdi. Alikuwa na shamba kubwa na minazi na mikarafuu, akafuga na ng'ombe; pia alikuwa na watumwa wengi. Akamteua mtumwa mmoja jina lake Mondo, na kumfanya nokora wake.
Basi Mondo kupewa unokora kajiona mtu mkubwa sana; akawakataza wenzake wasimwite jina la Mondo tena, maana hilo ni la kitumwa, akajipachika jina la Maftaha. Mondo akawa mkali kwa wenzake kuliko hata El-Mahdi mwenyewe; asubuhi-subuhi huwaamsha wenzake na kuwatia shambani kwa viboko. Kwa kikiri za Mondo, na mvua kunyesha vizuri, mavuno yakaja mazuri sana mwaka ule, na El-Mahdi akazidi kutajirika. Basi El-Mahdi akamsifu sana Mondo, lakini kwa maneno matupu, kwa kazi nzuri ya mwaka ule, bali faida yote ya mwaka ule akaimeza mwenyewe. Maana ingawa Mondo alivimba kichwa kwa sifa za El- Mahdi, na ingawa amewakataza watumwa wasimwite jina lake la zamani, wamwite Maftaha, lakini El-Mahdi alimwona yule Mondo, ni mtumwa tu.
Wale watumwa wengine wakachoka na vitimbi vya Mondo, wakafanya shauri watege, lakini wamweke doria, ili akitokea tu waanze kufanya kazi, tena kwa vishindo na kelele nyingi, na halafu wamtolee shida yao.
Mara doria kamwona Bwana Maftaha anakuja. Ikaanza kazi, kwa kelele nyingi na majembe kugongana. Bwana Maftaha akaridhika kazi inakwenda barabara, akawaambia wapumzike kidogo. Basi mmoja wa watumwa akamsifu sana Bwana Maftaha kwa upole na upendo wake, akasema kazi ingeongezeka maradufu, kama tu wangepata chakula. Hapo watumwa wote wakaangua kilio, "Njaa, njaal"
Ikawa Bwana Maftaha, kwa sifa alizopata kwa watumwa na kwa El-Mahdi, hakutaka shauri hili limshinde, akatoka mbio hadi kwa El-Mahdi. Kufika tu na yeye akamlilia Bwana Mkubwa, na huku chozi linamtoka, "Watumwa tuna njaa!"
El-Mahdi akamwona Mondo kama juha tu, lakini kwa kuwa alitaka kumridhisha kidogo ili kazi iendelee, basi akampa chakula ili kazi iendelee. Watumwa wakafurahi mno, na kumsifu Bwana Maftaha pamoja na El-Mahdi, eti kwa ajili ya kuwapenda sana.
Siku ya pili watumwa wakatumia hila ile ile, safari hii wakajidai wanaharisha. Wakaangusha kilio, "Tunaharisha, tunaharisha!"
Bwana Maftaha naye akakichukua kilio kile, mbio hadi kwa El-Mahdi, "Wanaharisha, wanaharisha!" na huku machozi yakimtoka. Lakini safari hii El-Mahdi hana dawa, akamwamuru Mondo arudi awaambie wasubiri kidogo, atafute dawa. Alipotamka neno hilo tu watumwa wakaja juu, wakawalaani vikali Bwana Maftaha na El-Mahdi pia.
Haya ndiyo yakawa mazoea yao. Wakitaka cho chote kwa El-Mahdi hulia kwa Maftaha, na Maftaha naye hupeleka chozi lile kwa El-Mahdi.
Hatimaye El-Mahdi akafa, lakini hakuwa na mrithi; basi shamba likawa mikononi mwa watumwa wake, likawa shamba lao. lla, kwa sababu ya mazoea yao ya zamani, mambo yakawa yale yale. Wakiwa na njaa huanza kulia, na Maftaha naye huanza kulia, "Njaa, njaa!" Lakini, kwa sababu sasa El- Mahdi kesha kufa, kilio chao hakikuweza kuwapatia, japo yale makombo ya zamani. Shamba wanalo, lakini dhiki ikazidi sana, mpaka walipozindukana na kutambua kuwa sasa shamba ni lao; na kazi yao ya sasa ni kulilima shamba, na kugawana matunda ya juhudi zao kwa haki: siyo tena kupeleka kilio kwa marehemu El-Mahdi.
Na sisi Watanzania zamani wote tulikuwa watumwa; watumwa wa Mwingereza na Mjarumani pia. Tulikuwa na manokora wetu enzi hizo, waliosaidia kutawala, waliojidhania kuwa wamepata u-Maftaha, kumbe Mondo tu. Kama Maftaha, kazi yao ilikuwa kupeleka mbele kilio cha wananchi: "Wanataka barabara, wanataka shule, wanataka hospitali."
Basi, leo El-Mahdi kafa; mkoloni kaondoka, wala harudi tena. Lakini Maftaha bado wapo, ndiyo sababu Baba wa Taifa anasisitiza wakuu wa Serikali wasiwe tena watu wa kutawala, bali watu wa kuhimiza maendeleo vijijini. Huu si wakati tena wa wanyapara wetu kulialia kama Maftaha; huu ni wakati wa kuwaeleza wananchi watumie ardhi yao waliyopewa na Mwenyezi Mungu. Kama wananchi wanataka maji, basi wafanye kazi ya kuyaleta maji; kama wanataka barabara, basi walime barabara.
Na sisi je, tuliokuwa nyuma ya mwenzetu Maftaha? Sisi tulikuwa na mawazo ya kitumwa siku nyingi. Zamani tulikuwa tunamfanyia kazi El-Mahdi, lakini leo tunafanya kazi kwa manufaa yetu sisi wenyewe, na ya watoto wetu. Tusimweke doria tena kutazama kama Maftaha anakuja, ndipo tufanye kazi; bali tufanye kazi kwa roho moja, tujisaidie wenyewe, kwa kuwa sasa nchi hii ni yetu.