Kitabu: Zamani mpaka siku hizi; yaani habari za Tanganyika tangu zamani za kale mpaka siku hizi, 1966

Kitabu: Zamani mpaka siku hizi; yaani habari za Tanganyika tangu zamani za kale mpaka siku hizi, 1966

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Joined
Jan 31, 2021
Posts
9,189
Reaction score
16,128
Baada ya kumaliza kitabu cha Maisha ya Malcom X sasa na tusome kitabu kuhusu historia ya Tanganyika. Vitabu hivi na vingine vingi unaweza kuvisoma bure ndani ya app ya Maktaba Sauti


zamani_cover_with_bgc.png


UTANGULIZI

(Uliotangulia kitabu hiki kilipotolewa mara ya kwanza)​

KWANZA inafaa wasomaji wote wafahamu ya kuwa hatuwezi kutunga habari za zamani za makabila yote ya nchi hii ya Tanzania, maana ni mengi mno na habari zao hazipatikani. Watu waliotangulia kukaa huku hawakutuachia maandiko yo yote wala sanamu zo zote zinazoweza kutupa habari za mambo ya kale kama walivyofanya watu wa nchi nyingine duniani. Tena watu wa bara hawakujulikana na watu wa nchi zilizo nje ya Afrika mpaka katika miaka iliyo karibu na 1800. Basi habari tunazoweza kupata ni zile tu zinazokumbukwa na wazee, na mapokeo waliyoyapokea kwa baba zao, ambayo mara nyingi yale yaliyo ya kweli yamefungwa katika yale yasiyo kweli hata kufichika kabisa.

Ni vigumu sana kupata habari za kweli za mambo yaliyotokea zamani kabla ya 1900, na zile zinazopatikana zimechanganyika katika akili za watu wanaozisimulia. Lakini tusipoandika habari zinazohusu kila sehemu siku hizi, habari zitazidi kusahauliwa na kupotea kabisa.

Tena ni lazima tukumbuke ya kuwa makabila yaliyoko siku hizi labda hayakuwako zamani za miaka mia moja, na tena baadhi ya makabila yaliyokuwako zamani yamekwisha kutoweka au kuingizwa katika makabila mengine. Makabila mengi yametwaa majina ya nchi yanazokaa, au yanajulikana na watu wa pwani kwa majina hayo, na kwa hivi ni vigumu kutambua kuwa watu wale wale ni kabila fulani au ni sehemu ya kabila fulani lililositawi zamani likapatwa na bahati mbaya na kutawanyika.

Basi kwa sababu hizi zote, mtu hana budi asite kidogo kabla hajajaribu kutunga habari na kufanya kazi inayoonekana kama haitawezekana, na wasomaji wasifikiri kuwa habari zilizomo ndani ya kitabu hiki zimethibitishwa kama zile tulizo nazo juu ya mataifa mengine ya dunia. Maana, mataifa yale mengine yalikuwa yameelimishwa zaidi na walimu wao waliandika habari zao nyakati zile zilizotokea, au wakazichora juu ya mawe yaliyotumiwa katika kujenga nyumba na mahekalu yao, au juu ya mawe na matofali yaliyowekwa katika makaburi yao. Basi, hivyo habari zao za zamani ziliweza kuthibitishwa kwa maandiko hayo.

Wabantu hawakuandika wala kuchora habari zao, na kwa hivi habari nyingi katika kitabu hiki si hakika kabisa. Lakini kama habari za kweli za nchi yetu zinatakiwa, au tuseme habari zinazokaribia kuwa kweli, basi huu sasa ndio wakati wa kukusanya nyuzi za habari tupate kujaribu kuzifuma tuwezavyo ili ziwe habari nzima, maana tukiacha kazi hii mpaka wakati unaokuja yamkini kuwa tutachelewa wala haitawezekana kabisa.

Basi kitabu hiki ni makusanyiko ya nyuzi za habari zilizofumwa kadiri zilivyowezekana ili kufanya habari za zamani za kale za nchi hii.
 
SURA YA KWANZA

ASILI YA WATU WA NCHI HIZI NA LUGHA ZAO

Somo 1-Asili ya watu wa nchi hizi

WAKO watu wa namna nyingi wanaokaa duniani, wako watu weupe, watu wekundu, watu wenye rangi ya kimanjano, na watu wenye rangi nyinginezo. Watu wengine hufuata namna moja ya kuishi, na wengine hufuata namna nyingine. Wengine huchunga ng'ombe na mbuzi, wengine hukaa katika nchi zisizo na ng'ombe wala mbuzi. Wengine huvua samaki, na wengine hukaa mahali pasipo na samaki. Wengine hujenga nyumba za kukaa, wengine hukaa mapangoni na mashimoni na mwituni. Kweli wako watu wa namna nyingi sana, na wenye tabia na desturi zilizo mbalimbali kabisa.

Tena watu wa dunia hutumia lugha nyingi. Watu wa nchi fulani hawawezi kusikilizana na watu wa nchi nyingine mpaka wajifunze lugha yao. Hata katika nchi yetu ya Tanzania wako watu wa namna nyingi wanaotumia lugha nyingi sana. Wako Wazungu, na kumbe, wote si wa namna moja wala hawasikilizani mpaka wajifunze lugha ya wenzao. Wako Waingereza, Wafaransa, Waitaliano, Wagiriki, Wadachi, na wengineo, na kila taifa lina desturi na lugha yake. Wako Wahindi, nao si wa namana moja wala hawasemi lugha moja tu. Wako Waarabu na desturi zao na lugha yao zimeachana kabisa na desturi na lugha za wale wengine tuliowataja.

Tena wako watu weusi wenyeji wa nchi hizi, na tukifikiri tutakumbuka mara moja ya kuwa hata sisi watu wa Afrika si wa taifa moja. Basi ni dhahiri tukitaka kuandika na kuzungumza habari za watu wa dunia itakuwa rahisi watu wote wakitengwa na kuwekwa katika jamii au mataifa, ndipo tutakapowataja watu wa jamii fulani au taifa fulani. Tena ni dhahiri ya kuwa watu wa jamii moja au taifa moja lazima wafanane kwa sura au kwa lugha au kwa desturi zao.

Basi watu wenye maarifa walipoanza kufikiri na kuandika habari za wanadamu wenzao waliwatenga, na jamii moja iliitwa kwa jina fulani, na nyingine kwa jina fulani na vivi hivi, ikawa rahisi kuwataja katika vitabu na katika mazungumzo.

Watu weupe walipofika katika nchi hizi, sisi watu wa Afrika tuliwaita Wazungu, maana tuliona kwamba si kama sisi, tena si kama Waarabu, wala Wahindi, tukataka kupambanua kati ya wageni tulipoongea juu yao, kwa hivi tuliwaita watu weupe wote Wazungu. Nimekwisha sema kuwa hata Wazungu si wa taifa moja wala wa namna moja, lakini sisi watu wa nchi hizi hatukujua hivi, tulijua ya kuwa wote wanatoka mbali kwa merikebu, wote ni weupe, wote wanavaa nguo zilizofanana, na lugha wanazotumia ni ngeni masikioni mwetu. Baadaye tulianza kupambanua kati ya watu hawa, tukajua ya kuwa wengine ni Waingereza, wengine ni Wafaransa, wengine ni Wareno, na wengine wa mataifa mbali mbali.

Basi, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Wazungu na wengine walipofika nchi hizi. Waliweka watu weusi wote katika jamii moja wakawaita watu weusi tu. Baadaye walipoanza kujua habari za desturi zao na za lugha zao walibaini ya kuwa si jamii moja, maana hutumia lugha nyingi na tena watu wa sehemu moja ya nchi hawasikilizani na watu wa sehemu nyingine. Basi watu wengine walianza kuchungua habari, na baadaye waliwatenga na kuwaweka katika jamii au taifa mbali mbali.

Katika kitabu hiki mataifa yanayoruhusu ni yale yaliyopewa majina haya: Watukoko; Wabilikimo; Wahamiti; Wasemiti na Wabantu.

Kwanza afadhali tueleze habari kidogo juu ya kila taifa namna linavyohusu habari za nchi hii na wenyeji wanaokaa humu.

Tutatumia majina hayo yanayotumiwa katika vitabu vyenye habari za mataifa ya dunia kwa sababu labda wasomaji wengine wanaojua Kiingereza watapenda kuendelea na kusoma habari nyingine katika vitabu vya Kiingereza, tena kwa sababu majina hayo yanaweza kukumbukwa na kusemwa kwa urahisi kuliko kutumia mafungu ya maneno yanayoeleza tabia zao kila tunapotaka kutaja mataifa mbali mbali.

Watukoko.-Maana yake 'Watu wakaao mwituni' (Bushmen ni Kiingereza, Bush, maana yake ni Koko, na men, maana yake ni Watu). Zamani sana kabla babu zetu hawajafika katika nchi hizi, wenyeji walikuwa watu wakaao mwituni tu wala hawakujenga nyumba wala miji. Waliwinda wanyama wa porini wakala nyama zao, na vitu walivyopata mwituni kama matunda, na majani ya namna nyingine, na mizizi. Labda Wakindiga wanaokaa katika nchi ya kaskazini mwa Mkalama, na Wasandawi wanaokaa katika Kondoa Irangi ni wazao wa Watukoko waliobaki katika nchi hii. Wasandawi hutumia sauti nyingine mfano wa kupiga kidogo katika usemi wao, na sauti hizo hazitumiwi na watu wengine katika nchi yetu, ila watu wengine wakaao Afrika ya Kusini wanazitumia hata siku hizi. Watu hao wanadhaniwa kuwa wazao wa watu waliokaa zamani katika nchi hizi, wakahama kwenda huko, au labda tangu zamani walienea toka huku mpaka huko.

Jambo linaloelekea kuthibitisha ya kuwa Watukoko walikaa katika nchi yetu ni picha nyingine zinazoonekana juu ya miamba na mawe na ndani ya mapango katika nchi ya Mkalama na Kondoa Irangi. Picha hizo zimeandikwa juu ya miamba na mawe kwa rangi nyekundu. Watu wengine wa huko hata sasa wanaweza kuandika picha za namna hizo, lakini hapana anayejua namna ya kutengeneza rangi hiyo, wala anayejua nani aliyeziandika picha hizo. Picha hizo ni za wanyama, yaani nyati, mbuni, twiga, pofu na wengine, na wanadamu, nazo zimefanana kabisa na picha zinazoonekana katika nchi za Afrika ya Kusini zilizo kazi za Watukoko, na rangi iliyotumiwa ni namna ile ile.

Watu wengine hudhani Wakindiga na Wasandawi ni wazao wa Watukoko na watu wa taifa la Wahamiti waliochanganyika pamoja. Makabila mengine, yaani Wasi na Wanege na wengine, ya namna ya hayo yalikuwako, lakini sasa yametoweka au kuingilia makabila mengine.

Wabushmen hao, yaani wenyeji wa asili, walifukuzwa au kuuawa au waliingizwa katika kabila la Wabantu walipokuja kutoka nchi za kaskazini, na waliobaki hukaa sasa katika Afrika ya Kusini.

Wabilikimo.-(Neno hili maana yake ni watu wafupi mno.) Watu hao ni wafupi sana, nao walikaa katika sehemu nyingine za nchi yetu kabla hawajafika babu zetu na kufanya makao huku; pengine huitwa Mbilikimo. Watu hao hawakujenga nyumba wala kufuga wanyama kama wenyeji wanaokaa huku sasa. Wazao wengine wa watu hao wanakaa hata sasa katika nchi hizi, maana hudhaniwa kuwa watu wanaokaa katika misitu ya nchi ya Kongo (Congo) ni wazao wao. Tena hadithi zinazosimuliwa na wazee wetu hutaja habari za watu hao wafupi, kama vile Wakoningo ambao habari zao zinahadithiwa na Wachaga. Katika nchi ya Urundi wako watu wanaoitwa Watwa, na jina hilo linatumiwa katika nchi ya Kongo kwa watu wafupi wakaao huko sasa. Hao Watwa wanaokaa Urundi si wafupi kuliko Warundi wenyewe, lakini Warundi wengine ni wafupi. Haikosi watu hao Warundi na Watwa wamechanganyikana katika kuoana, na sasa Watwa wameongezeka kimo chao na Warundi wamepunguka kimo chao.

Wagogo huhadithia kuwa wao walipofika katika nchi wanayokaa sasa, walikuta watu wafupi walioitwa Ngulimba wakikaa katika mapango na mashimo, na katika nchi ya Wakikuyu yako mapango na mashimo ambayo watu husema kwamba ni makazi ya watu wafupi wa zamani walioitwa Gumba.

Wahamiti.-Kwanza tufikiri kidogo namna watu hawa walivyopata jina hili. Watukoko waliitwa watu wa mwituni kwa ajili ya desturi yao ya kukaa mwituni. Wabilikimo waliitwa jina hilo kwa sababu ni mbilikimo, yaani watu wafupi sana. Lakini Wahamiti walipata jina hilo namna gani?

Watu wa zamani walipojaribu kueleza kwa nini watu wa dunia wameachana kwa tabia, walisema ya kuwa watu wote wa dunia ni wazaliwa wa wana wa Nuhu: Shemu, Hamu, na Yafethi. Wakasema, wana wa Yafethi ni watu wa Ulaya, yaani Wazungu, wana wa Shemu ni watu wa Asia, na watu wa Hamu ni watu weusi, yaani wenyeji wa Afrika.

Basi, hatutaki kuingia katika shauri la kuthibitisha wala kukanusha hadithi hiyo, tumeisimulia tu ili kueleza namna watu wa Afrika walivyopata kuitwa Wahamiti, yaani wa Kiham.

Lakini tumeona ya kuwa watu waliozidi kuchungulia habari hii ya kutenga watu wa dunia na kuwaweka katika jamii zao, waliona ya kuwa watu wote wa Afrika si wa namna moja, na wengine waliwaita Watukoko na wengine Wabilikimo, na wengine Wahamiti, na wengine Wabantu. Basi wale wanaoitwa Wahamiti sasa ni wale waliokuwa wakikaa katika nchi za kaskazini mwa Afrika, yaani kupita Uganda na Kenya. Tutasoma baadaye namana watu wengine wa taifa hilo walivyoingia nchi yetu wakasimamisha falme mahali pengine, tena namna walivyosaidia kuongoza mambo ya nchi yetu mpaka yakawa kama yalivyo sasa. Makabila mengine ya taifa hilo la Wahamiti ni Wamasai, Wambugu, Watatoga, Wamang'ati, Waburungi, Wasegeju na Wagala, na hao wote watatajwa baadaye katika habari za nchi yetu.

Wasemiti.-Hatuna haja kueleza mengi juu ya watu hao waitwao Wasemiti, yaani wa Shemu, maana liko kabila moja tu la Wasemiti linaloingia sana katika habari za nchi yetu, ndilo Waarabu. Hapa nitataja tu ya kuwa imehadithiwa kuwa Waarabu wa kwanza waliofika na kufanya makao katika nchi hizi za Afrika ya Mashariki walifika Pate katika mwaka 689.

Wabantu.-Maana yake Watu.

Watu wa taifa hilo linaloitwa Wabantu katika elimu ya watu wa dunia na lugha zao, wameenea katika nchi ya Afrika kutoka Uganda na Kenya mpaka Afrika ya Kusini, na tena kwa upande wa Afrika ya Magharibi vile vile, yaani katika sehemu ile ya tatu kwa moja iliyo katika kusini ya Afrika nzima. Kweli wapo watu wa mataifa mengine wanaokaa humo, lakini ni wachache tu, tena wametengwa mpaka wamekuwa mfano wa visiwa vidogo katika bahari ya Wabantu. Tumekwishataja wengine wa watu hao wasio Wabantu, yaani Wamasai, Waburungi, Wasandawi na wengineo, na katika Afrika ya Kusini, wako Watukoko, na wengine wanaoitwa Wahotentot, wanaokaa pengine.

Taifa hili kubwa la Wabantu lilipewa jina la Bantu na Mwingereza mmoja jila lake Bleek. Huyu Bleek alichungua sana habari za watu wa Afrika na lugha zao, akaona ya kuwa wako wengi sana ambao lugha zao zimefanana mno. Akazidi kutafuta habari na katika mwaka 1862, aliandika kitabu ili kuonyesha namna lugha nyingi za Afrika zilivyofanana, na kwa sababu katika lugha hizo nyingi hutumia neno kama Bantu au Watu au Wandu au atu kwa wanadamu, basi alianza kutaja taifa hilo kubwa, yaani jumla ya watu wanaotumia lugha hizo zilizofanana, kwa jina la Bantu.

Hatukosi tumekwisha jua jinsi ilivyo rahisi kufahamu lugha ya watu wa makabila mengine. Nchi ya Wanyamwezi ni mbali sana kutoka nchi ya Wayao, lakini Myao akisafiri kwenda huko anaweza kusikia maneno mengine anayoyajua, na ingawa kwa siku za kwanza hawezi kusikilizana na Wanyamwezi, lakini baada ya kukaa miezi miwili mitatu ataweza kuzungumza nao. Mganda akitoka kwao kusafiri pwani, labda kwanza ataona shida kusikilizana na watu wa pwani, lakini kabla hajakaa siku nyingi utamsikia anasema Kiswahili kama mtu aliyezaliwa kulelewa pwani. Je, imekuwaje? Ni kwa sababu lugha ya Wayao, na ile ya Wanyamwezi, na ile ya Waganda na ile ya Waswahili zina asili katika lugha moja, na wote ni Wabantu, yaani ni makabila ya taifa lile kubwa linaloitwa Bantu, na lugha zao ni Kibantu. Lakini kama Myao au Mnyamwezi au Mganda au Mswahili akisafiri katika nchi ya Wamasai au Waburungi au Wasandawi au watu wale wengine tuliosema kuwa si Wabantu ila ni Wahamiti, je, ataweza kusikilizana nao kwa upesi? La, hata akikaa kwao miezi mingi sana atashindwa kusikilizana nao mpaka ajifunze lugha yao, na tena ataona ni kazi ngumu. Kwa nini? Kwa sababu lugha yao si Kibantu ila ni lugha ya jamii nyingine ya watu isiyofanana na Kibantu, yaani ni Kihamiti. Siwezi kuandika hapa majina ya makabila yote ya Wabantu maana ni mengi mno, lakini watu wote wa Tanzania ni Wabantu ila wale wale niliowataja, yaani Wamasai, Wasandawi, Waburungi, Wambugu, Wakindiga, Wamang'ati na wengine wachache.



Somo 2-Maingilio ya Wabantu na wengine

Nchi hii tunayokaa sasa si yetu kwa asili. Watu wenye maarifa waliotafuta asili ya taifa hilo la Wabantu hawapatani juu ya nchi ya asili yake, wala hawapatani juu ya miaka mingapi iliyopita tangu watu wa taifa hilo walipoanza kuenea kutoka nchi yao ya asili. Husemwa walianza kuenea katika nchi nyinginezo zamani za miaka elfu mbili hata elfu tatu, wakaanza kuenea kwenda upande wa kusini na mashariki. Yadhaniwa kuwa watu wengine wa taifa hilo la Wabantu walikuwa wamekwisha kufika na kukaa pwani za nchi yetu zamani za miaka 2,000.

Wakati huo tunaosimulia, taifa la Wahamiti lilikuwa likikaa katika nchi zilizo kaskazini zaidi, na labda wao walianza kuja kusini wakawasukuma Wabantu au labda Wabantu walizidi na nchi haikuwatosha wakaanza kutafuta nchi nyingine za kukaa na malisho ya ng'ombe zao. Wengine hufikiri kwamba watu wa taifa hilo walienea wakaja katika nchi hii ya Tanzania kwa pande za Uganda na Ruanda; wengine walifuata kando ya Ziwa Tanganyika wakaendelea kusini, na wengine walifuata upande wa mashariki wakaenea pwani. Basi walizidi kuenea pote mpaka walikaa tokea Lamu katika pwani ya Mashariki, na Uganda kati kati ya nchi, mpaka Fernando Po katika pwani ya Magharibi, hata katika nchi yote ya Afrika ya kusini mpaka Port Elizabeth na Kaferaria.

Lakini tusifikiri walienea nchi yote kwa mara moja. La, labda maingilio yalikuja pole pole. Labda kwanza mtu mmoja na jamaa zake walihama mbele kutafuta mahali pa kukaa, halafu, mtu mwingine alihama pamoja na jamaa zake wakaenda mbele zaidi, na vivi hivi mpaka walienea nchi yote. Labda walipigana wakashindwa na kufukuzwa, lakini hatuna habari ya hakika, tunakisi tu. Tena tusifikiri waliingia katika nchi bila ya kushindana na watu wengine. Maana tumekwishaona ya kuwa wenyeji wa kwanza walikuwa wale Watukoko na Wabilikimo, na haina budi mara kwa mara ilikuwa lazima kupigana nao wapate mahali pa kukaa.

Basi, yumkini watu hao Wabushmen na Wabilikimo wa asili walifukuzwa au kuawa na Wabantu au pengine labda waliingizwa katika kabila lao, yaani labda Wabantu walichukua wanawake wao kukaa nao na hivyo walichanganyika pamoja. Labda zamani Wabantu walikuwa watu wakali sana wakawashinda wote waliojaribu kuwazuia wasienee walipotaka. Lakini kwa kadiri tunavyojua habari zao, walikuwa watu wapendao amani na kulima na kuchunga ng'ombe zao kuliko kupigana. Tena hawakuwa na yale maarifa katika kazi ya kutawala ya kuwavuta wajaribu kushinda mataifa mengine ili wapate kuyatawala. Pengine watu wengine walitokea wenye maarifa hayo, lakini tukisoma habari hizi zinazofuata, tutaona ya kuwa watalawa wengi, na hasa wale waliokuwa na nguvu wakatawala nchi kubwa, walitokea katika makabila ya nchi za mbali. Tena tutaona kuwa wale waliokuwa wakubwa katika watawala hao ndio wa makabila ya taifa la Wahamiti, na labda wa jamaa au ukoo mmoja ule wa Wagala walitoka nchi kaskazini mwa Afrika. Watu hao walitoka kwao wakapita katika nchi ya Uganda na zile wanazokaa Wamasai, na wengine walifuata nchi za pwani ndio Wasegeju.

Watu hao Wahamiti hawakuenea sana kwenda kusini, ila walizuiliwa mumu humu katika nchi yetu. Jambo lililowazuia wasienee zaidi lilikuwa safari za Wazulu, yaani kabila moja la Wabantu waliotoka nchi za kusini wakivuruga mambo katika nchi hii katika mwaka 1850 na miaka ya karibu iliyofuata. Lakini yaliyobadili mambo zaidi katika nchi yetu kuliko safari za Wabantu na Wahamiti ni kuingia kwa watu Wasemiti na Waasia waliokuja katika nchi za pwani. Watu hawa walileta mambo ya ustaarabu na ya dini ya Kiasia yaliyoshinda kwa ubora na akili yale yaliyojulikana na watu wa makabila ya Afrika.

Waarabu walikuwa wa kwanza katika watu hao wa Wasemiti na Waasia waliofika katika nchi yetu, na ijapokuwa nguvu zao, na utawala na ustaarabu wao, haukuenea bara upesi ila ulionekana katika nchi za pwani tu kwa muda wa miaka mingi, lakini ziliunganisha Afrika ya Mashariki pamoja na nchi nyingine, zikafanya mfano wa fungu la ustaarabu lililoambatana na nchi za pwani zote za mashariki za bahari ya Hindi, yaani Indian Ocean. Wazungu hawakufika katika nchi hizi na kukaa mpaka karibu na mwaka 1550, lakini walipofika walianza kujishughulisha na kusitawisha biashara na utawala, na tangu wakati huo wamefungua nchi na kuzitengeneza imara kusudi zisivurugike, ila zikae kwa amani na kusitawi.



Somo 3-Namna Wabantu wa asili walivyotengwa wakawa makabila mengi​

Tumekwisha ona ya kuwa Wabantu wote walikuwa wakikaa katika nchi yao ya asili kaskazini zamani za miaka 2,500 au 3,000. Wakati ule labda walikuwa kama kabila moja au sehemu ya taifa jingine, wakawa na lugha yao moja wakasikilizana pamoja. Baadaye tutachungua habari za lugha tuone namna maneno mengine yanavyofanana hata sasa, yaani baada ya kupita miaka hiyo yote.

Kwa pole pole Wabantu walianza kuhama kwenda mashariki na kusini, na kama tulivyosema, watu wote hawakuhama pamoja kwa wakati mmoja. Wengine walihama kwanza wakakuta wenyeji wa asili, labda waliwafukuza au labda waliwaua, au labda walichukua wanawake wao wakakaa nao, au labda walipatana nao wakakaa pamoja. Baadaye wengine walienea kwenda mahali pengine, au kwenda mbele zaidi, na vivi hivi, ikawa kila walipofanya makao walichanganyika pamoja na wenyeji wa asili. Basi watoto waliozaliwa walifundishwa maneno mengine kwa kusikia lugha za mama zao, na maneno mengine kwa kusikia lugha za baba zao, ikawa baadaye lugha zikachanganyika vile vile. Halafu ikatokea ya kuwa maneno mengine ya lugha ya asili yalisahauliwa na watu wengine, yakatumika yale ya wenyeji wa asili. Lakini maneno yale waliyosahauliwa hayakusahauliwa na wote, maana wengine wa mahali pengine walisahau maneno mengine wakayakumbuka yale yaliyosahauliwa na wenzao, na wengine kadhalika. Tena lazima tufahamu ya kuwa ni desturi ya lugha kubadilika, maana kila walipokutana na mambo mapya katika nchi ngeni lugha iliongezeka ili waweze kuyaeleza mambo yale mapya. Kama taifa au kabila linaendelea, basi lugha vile vile lazima iendelee. Watu waliokuwa wawindaji tu walipoanza kulima walikuwa hawana maneno ya kutumia kwa kazi na vyombo vya kulimia, wala hawakuwa na maneno ya kutaja namna nyingine za mavuno. Watu walipoanza kuvua samaki walikuwa hawana maneno ya kutumia kwa vyombo vya kuvulia. Basi ikawa lazima watunge maneno mapya au kutumia yale yaliyotumiwa na watu wa nchi waliyokuwa wakikaa, maana wale walikuwa wamekwisha tunga maneno kwa sababu walizoea kuwinda au kuvua samaki.

Tukifikiri kidogo tutafahamu kuwa hayo ni kweli, maana Kiswahili cha sasa si sawa sawa na kile kilichotumiwa zamani za miaka 100 au zaidi, na tena hata sasa kinaendelea kubadilika, kwa sababu watu wanashughulika na mambo mapya na vitu vipya. Tutaje vitu vichache tu ili tufahamu vizuri. Sasa watu wanashughulika na kazi ya reli, kazi ya taa za umeme, baisikeli, motokaa, simu na vinginevyo, lakini vitu hivi ni vya siku hizi, basi ni lazima watafute maneno ya kueleza habari hizo mpya, na hivyo lugha zinaongozwa na kuongezeka katika nchi zote.

Basi, vivyo hivyo zamani, watu wa taifa la Wabantu walienea wakatengana na sehemu nyingine za taifa, lugha ikabadilika na baada ya kupita miaka mingi ikawa si lugha moja tu ila nyingi, yaani kila kabila lina lugha yake. Lakini kama tulivyosema, asili ya lugha ni moja, na maneno mengine ya asili yanatumiwa na makabila mengi hata sasa, na hii ndiyo sababu si vigumu kwa Myao kujifunza Kinyamwezi, wala Mnyamwezi kujifunza Kiyao, wala Mswahili kujifunza lugha nyingine ya Wabantu. Watu wa taifa hilo la Wabantu wanazo lugha nyingi, lakini zote zimefanana sana, ingawa nyingine zimeachana sana kwa namna nyingine.



Somo 4-Namna lugha ya Kiswahili ilivyojengwa na kuenea

Lugha ya Kiswahili inajulikana na watu walio wengi katika nchi yetu ya Tanzania, tena watu wengi wa Kenya na Uganda na Kongo na nchi nyingine wanajua Kiswahili. Basi inafaa tuchungulie kidogo asili yake na namna ilivyoenea kama ilivyo siku hizi.

Watu wengine, na hasa wale wanaojiita Waswahili, hufikiri kuwa zamani kulikuwa kabila moja la Waswahili kama yaliyo makabila mengine. Lakini hatuna habari zake katika habari za dunia, na huelekea kuwa halikuwako kabisa. Huelekea kuwa Waswahili ni mchanganyiko la watu wa makabila ya Afrika na wageni wa nchi nyingine waliokuja pwani.

Tumekwisha simulia ya kuwa Waarabu wengine walikuja wakafanya makao Lamu katika mwaka 689, na hata kabla ya wakati huo Waarabu na wageni wengine walizoea kuja huko kufanya biashara.

Waarabu wale walipokuja walikaa Lamu na nchi nyingine za pwani wakaoa wanawake wa kienyeji, yaani Wabantu, na watoto wao vile vile walioa wanawake wa Kibantu na hivyo Waarabu na Wabantu walichanganyika pamoja. Tena, baadaye Waarabu na Waajemi na wageni wengine wakaja wakafanya makao katika nchi za pwani, na wao vile vile walichanganyika pamoja na Wabantu mpaka asili yao iliwapotea wakawa mchanganyiko tu. Basi Waarabu walikuwa na lugha yao na Wabantu walikuwa na lugha yao, ikawa watoto wao walichanganya lugha au kwa kusema kweli waliingiza maneno mengi ya kigeni katika lugha za Wabantu waliokuwa wakikaa pwani. Ni dhahiri kuwa waliingiza maneno tu kwa sababu taratibu za lugha, yaani sarufi haikubadilika, ilidumu kuwa na taratibu au sarufi za Kibantu. Waarabu walikuja kufanya biashara, ikawabidi kujifunza maneno mengine ya wenyeji, yaani Wabantu, na vile vile wenyeji walikuwa hawana budi kujifunza maneno ya Kiarabu wasiwe wajinga wanapofanya biashara nao.

Basi, hii ndiyo asili ya Kiswahili, na labda mwanzo wa kukua kwake ni mwaka 689 walipokuja Waarabu wale wakakaa Lamu. Kiswahili ni lugha ya Wabantu wa pwani wa zamani waliokaa kutoka Lamu mpaka mto Ruvuma iliyochukua maneno mengi ya Kiarabu na Kiajemi, na Kireno na Kihindi, na siku hizi inachukua maneno ya Kizungu.

Kwa kawaida maneno mengi yaliyochukuliwa na kuingizwa katika lugha hiyo ya Kibantu yalibadilishwa kidogo na yote yalifuata taratibu za sarufi ya lugha ya Kibantu. Lugha ya Kibantu haikubadilika hata kidogo ila ilisitawishwa na kutukuka na kuongezeka kwa ajili ya kupata faida ya maneno yaliyotoka katika lugha za watu waliostaarabika zaidi kuliko Wabantu. Lugha ya Kiswahili imeenea pote katika nchi hizi kwa sababu watu wa nchi hizi hutumia lugha nyingi sana na kila lugha inatumiwa na watu wachache tu. Kama watu wakitaka kukaa peke yao katika kabila lao na kuishi maisha ya kishenzi, lugha yao inawatosha, lakini wakitaka kuongea na wenzao wa makabila mengine na kustaaribika, lazima wajifunze lugha nyingine. Wakijifunza lugha ya wenzao wa kabila lililo jirani nao, basi wataweza kuongea nao kweli, lakini je, wataweza kuongea na watu wa makabila mengine? La, na hii ndiyo sababu inafaa wajifunze lugha inayojulikana na watu wengi, ndipo watakapoweza kuongea na watu wa makabila mengi. Basi kama tulivyosema, Kiswahili ni lugha inayojulikana na watu wengi katika nchi yetu na hivyo inawapasa watu wa makabila yote wajifunze Kiswahili.

Wageni waliokuja kwa njia za pwani ndio walioleta ustaarabu na biashara na elimu katika nchi hizi, wakajifunza lugha iliyotumiwa pwani, yaani Kiswahili, na kila walipokwenda kufanya biashara au kufanya makao walieneza lugha hiyo na hivi ikaenea nchi nzima.

Basi hivyo ndivyo lugha ya Kiswahili ilivyoenea na kutukuka, na kwa ajili ya maneno mengi yaliyochukuliwa katika lugha ya mataifa yaliyostaarabika, basi sasa imekuwa ndiyo lugha inayotumiwa katika Tanzania kwa kazi ya biashara, tena ni lugha inayotumiwa na Serikali na katika shule za nchi hizi, na kwa hiyo ni lugha ya kuelimisha watu. Siku hizi watoto na watu wazima hujifunza Kiingereza pia maana lugha hiyo inatusaidia katika elimu za juu na kufahamiana na mataifa mengine.

Vitabu vingi na magazeti yanapigwa chapa kwa Kiswahili na kila mwaka vinazidi.

Basi sasa tumekwisha ona namna tulivyokuja kukaa katika nchi hii. Tuendelee tusome habari za babu zetu walipokuwa wamekwisha kuingia na kukaa katika nchi hizi wakatengwa katika makabila mengi.

Kama tulivyosema, hatuwezi kutunga habari kama ni hadithi moja tu, na kwa hivi tumegawanya nchi katika sehemu, na katika sura zinazofuata tutasoma habari za watu wa kila sehemu mbali mbali.

Kwanza tutasoma habari za watu wa nchi za Magharibi; kisha, tutasoma habari za watu wa nchi za Kaskazini; kisha, habari za watu wa nchi za Kusini; kisha, habari za watu wa nchi za pwani. Tutasoma habari za nchi yetu namna ilivyokuwa chini ya utawala wa Wadachi; kisha, tutasoma namna utawala wa Wadachi ulivyoondolewa na nchi ikawekwa chini ya himaya ya Waingereza na kuendeshwa mpaka leo kuwa nchi inayojitawala.
 
SURA YA 2
HABARI ZA NCHI ZILIZO MAGHARIBI

Somo 1-Wahima

KATIKA sura ya kwanza tulisoma ya kuwa sisi Wabantu si watu wa asili wa nchi tunazokaa sasa maana tulitoka nchi nyingine tukawasukuma watu waliokuwa wakikaa huku au labda tulichanganyika pamoja nao. Hatuna hakika miaka mingapi imepita tangu tulipoanza kuhama kuja katika nchi hizi, lakini imedhaniwa inapata miaka 2,000 mpaka 3,000. Basi tukaja tuakenea pote tukatawanyika tukafanya makabila mengi na lugha vile vile iligawanyika ikafanya lugha nyingi.

Lakini hatukuachiliwa kukaa peke yetu, na baada ya miaka mingi, watu waliokuwa wakikaa kaskazini walianza kuingia katika nchi hizi kama sisi tulivyoingia zamani sana. Labda walikuwa wale wale waliosukuma babu zetu wakawafanya kuhama kutoka nchi zile walizokaa zamani katika kaskazini. Yaani sisi tulisukuma Watukoko na Wabilikimo tukakaa katika nchi yao, na halafu sisi tulianza kusukumwa na watu wengine. Watu hawa hawakuingia katika nchi hii, lakini wameacha alama za nguvu zao na kwa hiyo imetuhusu tujue habari zao. Hatuna maandiko wala sanamu zinazoweza kutusaidia kueleza habari zao wala kujua walikuja zamani gani, lakini pengine tumehadithiwa watawala wangapi waliotawala katika nchi fulani na hivi tunaweza kukisia tarehe.

Tena tunaweza kujifunza habari zao kidogo kwa habari walizozikusanya Wazungu wa kwanza waliokuja kusafiri katika nchi hizi.

1.jpg


Basi katika sura hii tutasimuliwa habari za sehemu ya nchi iliyo katika magharibi ya kaskazini mwa Tanzania, yaani wilaya za Bukoba, Mwanza, Tabora na Kigoma.

Wenyeji wanaokaa katika sehemu hii ya nchi yetu ni wengi sana, jumla yao ni sehemu ya tatu kwa moja ya wenyeji wote wa Tanzania. Watu hao wote ni Wabantu ila kuna wachache wenye damu ya wageni, lakini watawala walio wengi si Wabantu ila ni wageni. Watawala hao waliojiweka juu ya wenzao ni Wahima, na asili yao wametoka katika taifa la wale watu waitwao Wahamiti waliotoka Kaskazini.

Labda zamani Wahima hao walifanana na Wamasai wanaokaa katika nchi yetu sasa, nao vile vile walitembeatembea wakitafuta malisho kwa makundi ya wanyama wao, lakini baadaye walifuata desturi ya kukaa mahali pamoja kama wanavyokaa Wabantu. Labda walipigana na Wabantu wakawashinda, au labda Wabantu walijiweka chini yao kwa hiari zao, hatuna habari.

Wahamiti hao wanakaa hasa katika nchi ya Ruanda, na hapo wanaitwa Watusi. Hata leo wanajulikana kwa kuwa ni watu warefu tena wembamba, na sura zao ni za kipanga, na rangi yao ni nyekundu kuliko ile ya Wabantu. Watu hao ndio walioleta ng'ombe wale wenye pembe ndefu sana kutoka kwao ambao tunaweza kuwaona Bukoba, na Ankole, na Ruanda na mahali pengine ambapo Watusi walipojiweka kuwa wakubwa wa nchi.

Watu wenye maarifa juu ya mataifa hukubali kuwa Wahima ni Wahamiti, na hudhani ni Wagala au taifa jingine lililo asili ya Wasegeju na Wamasai. Ni ajabu sana ya kuwa karibu kila mahali wanapokaa watu hao katika nchi yetu, lugha yao ya asili imewapotea na sasa hutumia lugha ya watu walioshindwa nao na hata wakitaka kutaja babu zao huwaita kwa majina ya Kibantu. Lakini wengine wanayo lugha ya Kihamiti hata sasa, kama vile Wamasai na wengineo.

Kama tulivyosema, hatuwezi kujua hakika Wahima hao walifika lini katika nchi hii mara ya kwanza, na kwa kuwa habari zao za zamani zimechanganyika sana na hadithi, hatuwezi kupambanua zilizo za kweli na zilizo hadithi tu. Lakini Padre mmoja wa Misioni ya Kikatoliki huko Uganda amezichungua sana, kwa hiyo tutafuata maneno yake katika kusimulia habari zao. (Père Julien Gorju, ndiye aliyetunga kitabu cha Kifaransa chenye habari za Wahima kiitwacho 'Entre le Victoria, l'Albert et l'Edouard'.)

Wahima wote wanajua asili yao walitokea nchi za kaskazini, na ya kuwa ufalme mkubwa ulisimamishwa na babu zao katika nchi ya Bunyoro, tena husema kuwa watawala wote wa Wahamiti walitokea ufalme huo. Bunyoro si katika nchi yetu ila ni katika nchi ya Uganda, lakini inatuhusu tujue habari hizi kwa sababu watawala waliotoka huko walijiweka katika nchi yetu pia. Ufalme huo uliitwa Kitara ukasimamishwa zamani kabla ya kusimamishwa ufalme wa Buganda unaoendelea hata sasa. Hatujui Kitara ulisimamishwa zamani gani, lakini tunajua kuwa ni zamani sana kwa sababu tunayo hakika kuwa wafalme 32 au pengine wanahesabiwa kuwa 36, wametawala katika ufalme wa Buganda, na kama tulivyosema, Kitara ulisimamishwa kabla hajaanza kutawala yule mfalme wa kwanza wa Buganda.

Watu waliosimamisha ufalme huo wa Kitara walikuwa Wahamiti. Lakini ufalme wa Kitara haukudumu miaka mingi sana ukaisha. Labda watu wa jamaa au ukoo mwingine walishindana ili kusudi wapate utawala, au labda waliugawanya ufalme sehemu nyinginezo.

Wakati huo Wahamiti walikuwa wakihama kutoka kaskazini wakitafuta nchi nyingine ili wapate mahali pazuri pa kukaa, au labda walikuwa wakisukumwa na watu wengine waliokuwa wakikaa kaskazini zaidi, hatuna hakika. Lakini huelekea kuwa kweli, maana kama ilivyo katika historia ya nchi za dunia ndivyo baba zetu walivyokuja wakawasukuma Watukoko na Wabilikimo, tena ndivyo Wahamiti walivyotusukuma sisi Wabantu tuliokaa kaskazini.

Basi miaka ikapita na zamani ya mwaka 1,300 hivi, watu wengi zaidi walihama kutoka kaskazini pamoja na mkubwa wao aliyeitwa Ndahura, wa jamaa ya Bachwezi. Ndahura alikuwa na nguvu, maana alisimamisha ufalme mkubwa sana ulioenea kutoka Ziwa Albert mpaka Ziwa Victoria, na ufalme huo uliitwa Kitara vile

****

vile. Ufalme huo ulisitawi sana na hasa wakati aliotawala mfalme mmoja aitwaye Wamala, lakini ndipo habari za jamaa hiyo ya Bachwezi zikakoma kabisa. Wengine husema kuwa jamaa ilitoweka, lakini sasa watu huhadithia kwamba watu wa jamaa hiyo waligeuka miungu! Imedhaniwa ya kuwa wakati huo ulikuwa katika miaka iliyo karibu na 1675.

Basi huku nyuma ufalme mwingine ulisimamishwa katika nchi ya Bunyoro na mtu jina lake Mpugu wa kabila moja la Wahamiti. Mpugu alianzisha jamaa ya Babito akaitwa Mpugu kwa sababu alikuwa mweupe kidogo, au labda alikuwa zeruzeru. Baba yake Mpugu alikuwa wa jamaa ya Bachwezi akaitwa Kyomya. Imehadithiwa kuwa Kyomya alitembeatembea sana mpaka alifika kilima kiitwacho Elgon katika nchi ya Kenya, na hapo alikutana na mwanamke chini ya mti unaoitwa Bito akakaa naye, na halafu yule mwanamke alizaa pacha. Mtoto mmoja aliitwa Mpugu na wa pili aliitwa Kintu.

Basi baadaye Mpugu alisafiri akafika mji mkuu wa Bachwezi akaushika ufalme, lakini wakati huo aliitwa kwa jina jingine, ndilo Wunyi. Mwingereza mmoja Baker alisafiri katika nchi hizi katika mwaka 1871 ili apeleleze habari za mito na milima na maziwa ya nchi, naye ameandika habari kuwa alikutana na mfalme mmoja aliyekuwa wa kumi na tatu kutawala tokea wakati ule aliotawala Wunyi.

Yule mtoto wa pili, Kintu, alisimamisha ufalme mwingine. Watu wengine husema kuwa Kintu alikwenda akashika ufalme wa Ntege aliyekuwa mkubwa wa Buganda wakati ule, lakini alimwacha atawale chini yake. Baadaye Kintu alitoweka na Ndahura aliyekuwa mfalme wa kwanza wa jamaa ya Bachwezi aliyetawala katika Bunyoro, alimwua Ntege, akampa mwanawe Kyomya ufalme wa Buganda kuutawala.

Ufalme mwingine ulisimamishwa Toro na mtu wa jamaa hiyo hiyo, na George David Kumurasi Rukidi III anayeitawala nchi hiyo sasa ni mfalme wa kumi na moja kutawala tokea uliposimamishwa.

Mpaka sasa tumesimulia habari kidogo za nchi zilizo jirani na nchi yetu ili tufahamu vizuri mambo yaliyotokea halafu katika nchi yetu. Basi sasa na tuache tukasimulia habari za Wahima waliokuja wakakaa katika nchi yetu ya Tanganyika.

Katika nchi ya Bukoba kwa upande wa kusini mwa mto uitwao Kagera kuna nchi inayoitwa Kiziba; huko ufalme ulisimamishwa na Kaganda, mtu wa taifa lile lile la Wahamiti. Katika hadithi ya Kibunyoro imesimuliwa kwamba Kaganda ni mwanawe Wunyi yule tuliyemtaja, naye ndiye aliyeusimamisha ufalme wa Babito katika Bunyoro. Lakini hadithi ya Kiganda inasimulia kuwa Kaganda ni mwanawe Kintu aliyekuwa mfalme wa kwanza wa Buganda. Basi Kaganda alitoka kwao Kyagwe akafika Buddu iliyo upande wa kaskazini mwa mto Kagera. Kutoka huko alisafiri mpaka Buyaga kando ya Ziwa Victoria, alipotoka huko alivuka kisiwa Sese. Kutoka Sese alisafiri tena mpaka Bwende katika ghuba iitwayo Sango, na mwisho alisafiri akafika Kyawa.

Tumetaja safari hizo kwa sababu zingali zinakumbukwa na watu wa huko, maana zinaonyeshwa katika desturi zinazoshikwa wakati wa kumweka mtawala mpya. Mtawala mpya huogeshwa kwa heshima kwa maji yanayoletwa kutoka Kibiro iliyo kando ya Ziwa Albert, tena hutiwa chumvi inayoletwa kutoka Kitunga iliyo katika nchi ya Buddu mahali alipokaa Kaganda kwa muda, na hapo ndipo alipowaacha wengine wa wafuasi wake. Mioto yote katika nchi huzimwa, na moto mwingine huletwa kutoka kisiwa cha Sese, kwa sababu yasemwa Kaganda alichukua moto unaoheshimiwa sana na Wanyoro akauacha Sese, na kwa hiyo alirudi huku kutoka Bwende ili aje auchukue.

Basi alipokuwa akitoka kaskazini, Kaganda alifika Kyowa, na hapo alikutana na mwana wa mfalme aliyekuwa amefukuzwa kutoka Kiziba, akafanya shauri naye la kumwua Ntumwa aliyekuwa mfalme wakati huo. Shauri lao likafanyika, na yule mwana wa mfalme aliushika ufalme, na Kaganda akawa waziri wake. Hatimaye yule mwana wa mfalme alikufa, na Kaganda alishika ufalme wa Kiziba akautawala. Basi hii ndiyo namna alivyopata ufalme wake. Lakini tendo hili la kuuliwa mfalme wao liliwachukiza sana wenyeji wa nchi kwa sababu walisadiki kuwa ni ishara mbaya itakayowaletea misiba na taabu. Basi tokea wakati huo walimwita Kaganda kwa jina la 'Kibi' na maana yake ni 'Kiovu' au 'Kibaya'. Imesemwa ya kuwa Kibi aliishi sana mpaka akawa mkongwe, akafa akazikwa mahali kaskazini mwa mto Kagera, yaani kukumbuka mahali alipotokea.

Kabla ya kufa kwake, Kibi aliusia kwamba mwanawe Samula awe mfalme baada ya kufa kwake, lakini jamaa ya yule Ntumwa mfalme aliyeuawa aliweza kuushika tena ufalme kwa muda, mpaka Samula alipata msaada wa mfalme wa Buganda wakamfukuza yule jamaa ya Ntumwa. Ndipo Samula alipopata jina la Nyakabinga' maana yake, 'Yule aliyefukuza.'

Samula hakupenda watoto wake wala wakubwa wa taifa lake wadhaniwe kuwa wenyeji, yaani Wabantu, hivi aliwaita kwa majina ili asili yao isisahauliwe, akawaita watoto 'Waziba' na wakubwa wa nchi aliwaita 'Wahima.' Tena hakupenda wachanganye damu na ile ya wenyeji, na kwa muda mrefu wana wa mfalme walioa watoto waliozaliwa na wale waliofuatana na Kaganda kutoka kwao. Hata sasa jamaa za watawala wanaheshimu sana miiko ya kabila la Babito, lakini mtawala mwenyewe hufuata desturi ya Kiganda, yaani hushika mwiko wa jamaa za mke wake ili kusudi kuwaheshimu. Desturi hiyo ililetwa na Kimera wa Buganda.

Hatujui tarehe alipoanza kutawala Kibi, lakini tokea wakati wake, wafalme kumi na watano wa jamaa yake wametawala ufalme wa Kiziba mpaka Mutahangarwa alipoanza kutawala. Mutahangarwa alikufa katika mwaka 1916.

Sasa tuchungulie kidogo habari za ufalme wa Wahinda. Kuna nchi nyingine inayoitwa Kiziba ya Kusini, na pengine inaitwa Ihangiro, lakini lazima tukumbuke ya kuwa ni mbali mbali na nchi ya Kiziba tuliyokwisha taja. Tulisimulia kuwa watu walidhani ukoo wa Bachwezi wa Bunyoro walitoweka kabisa wakageuka nchi nyingine wapate kuzishinda. Hadithi zinashuhudia kuwa miungu, lakini kwa kweli haikosi walihama kwenda kutafuta ufalme huu ambao tutasimulia habari zake sasa, ulisimamishwa zamani ya mwaka kama 1675, yaani wakati ule walipotoweka jamaa ya Bachwezi.

Imehadithiwa ya kuwa mtu aitwaye Ruhinda au Luhinda alihama kutoka kwake akaenda Buddu, kisha akaondoka akaenda Koki. Labda Bachwezi walishindwa au labda walihama kutafuta nchi nyingine, yaani walitoweka, na Ruhinda alikuwa mmojawapo waliohama. Basi alipofika Koki alikutana na mhunzi mmoja aliyetoka nchi ya Uzinza, ambayo ni nchi inayojulikana sana kuwa nchi ya wahunzi wa jamaa ya Warongo. Mhunzi huyo alianza kueleza habari za nchi ya Uzinza na Ruhinda aliposikia kuwa mfalme wa nchi hiyo ni mtu dhaifu, aliazimia kwenda huko. Alipofika, alijidai kuwa mganga mkubwa awezaye kuleta mvua, na baada ya kupita muda alipata nguvu akajifanya mtawala wa nchi ya Uzinza na Ihangiro na Karagwe na Urundi. Lakini halafu alipokuwa akisafiri kwenda Kagera kutoka Ihangiro alikufa katika kijiji kiitwacho Lwazi, na ule ufalme aliousimamisha ulivunjika ukagawanywa katika sehemu tatu, yaani Uzinza na Ihangiro, na Urundi na Karagwe.

Nchi ya Ankole iliyo jirani inatawaliwa na Wahima, nao hudai ya kuwa wametokea ukoo wa Ruhinda. Lakini yule Padre tuliyemtaja kuwa amechungua sana katika habari hizi, anadhani kuwa hawakutokea jamaa ya yule Ruhinda aliyetawala Uzinza na Karagwe na Ihangiro, ila labda ya Ruhinda mwingine.

Imesemwa kuwa Ruanda pia ilikuwa katika ufalme huo wa Wahinda, lakini hatuna habari safi juu ya hayo, na kwa kuwa Ruanda si sehemu ya Tanzania, basi habari zake hazituhusu sana. Yatosha kusema kuwa Watusi ambao ni kabila kuu la Ruanda, ni damu moja na Wahinda, yaani wale wanaoitwa pengine Wahima na pengine Wahuma. Tena imehadithiwa asili ya jina hilo Tusi ni jina la milima mirefu iliyo upande wa magharibi inayoitwa Ututsi na Warundi, na labda watu hawa Wahamiti walipewa jina hilo na wenyeji wa nchi hiyo.



Somo 2-Kuendelea na habari za Wahima

Ruhinda alipokufa, ufalme wake uligawanywa katika sehemu tatu, na wafalme wa Karagwe, yaani sehemu moja na ufalme, walitwaa majina ya Ruhinda na Ntare. Wa kwanza aliitwa Ruhinda na wa pili Ntare, na wa tatu Ruhinda na kuendelea hivi kwa vizazi kumi na moja. Wafalme kumi na wanane walitawala katika ufalme huo. Mwingereza mmoja jina lake Speke aliyesafiri katika nchi hizi kutafuta habari nyinginezo, alifika hapa katika mwaka 1861 akamkuta Rumanyika mwanawe Dagara akitawala nchi. Rumanyika alimpokea vizuri sana akamfurahisha kwa ajili ya akili na wema wake. Speke aliandika kitabu chenye habari za safari zake, na tukikisoma tutaona kuwa Rumanyika alikuwa mtu mwenye nguvu nyingi, na watawala wengine wa Kihinda walikubali kuwa yeye ni mkubwa wa jamaa yào, na mfalme wao.

Kwa muda kidogo ufalme huo wa Karagwe uliharibika, maana nchi ya Ihangiro ilitengwa ikawa ufalme wa peke yake ukatawaliwa na mtu aitwaye Sebahinda. Lakini baadaye uliunganishwa tena na Wadachi, na Kahigi aliyekuwa jamaa wa Sebahinda ambaye alipendwa sana na Wadachi, alipewa ufalme kwa sababu walitaka kumfurahisha. Kahigi alikufa katika mwaka 1916. Wahinda wanaotawala kisiwa cha Ukerewe walitoka Ihangiro, na Makaka aliyeanza kutawala katika mwaka 1895 ni mtawala wa kumi na nane tangu walipokiteka kisiwa.

Nchi ya Uzinza, yaani Usui iliyo katika wilaya ya Bukoba, na Uzinza katika wilaya ya Mwanza zilikuwa zikitawaliwa na mtawala mmoja wa Kihinda mpaka katika enzi ya Dagara wa Karagwe, ndipo alipotawala Rwona au Lwoma, na Dagara alimshauri kugawanya nchi na kufanya falme mbili. Basi watoto wa Rwoma, Suwarora na Ruhinda, walipewa kila mmoja sehemu yake. Suwarora alipewa nchi ya Usui na Ruhinda alipewa Uzinza iliyo upande wa Mwanza.

Baada ya kupita muda, Uzinza uligawanywa tena ukafanywa falme nne, ukakaa hivyo mpaka mwaka 1926, ndipo sehemu hizo zilipounganishwa kuwa ufalme mmoja ukatawaliwa na mtu mmoja aliyechaguliwa na wenyeji waliotoka Ukerewe.

Mhinda mmoja alisimamisha ufalme mwingine ulio mdogo, na nchi zilizokuwa katika ufalme huo ni Kiyanja na Kyamtwala na Bugabo, lakini hakuweza kuzishika, na Bankango wa Usui akaja akamnyang'anya nchi za Kyamtwala na Bugabo akamwachia nchi ya Kiyanja tu.

Haya ni majina ya utawala wa Uzinza na Ihangiro: Ruhinda; Ntare (huyu alifia kisiwa kiitwacho Kome); Kabambo Katobaa; Kabula; Nyamulasya (huyu alifanya Kome kuwa mji wake mkuu); Kyeda; Kinwa; Kabambo wa pili; Kabula wa pili; Kakalaza (huyu alifanya Butendwe kuwa mji wake mkuu akafia safarini wakati alipokuwa akienda Uha); Mwiyakabi; Ruhinda wa pili (huyu alipewa jina la Muhangakyaro baada ya kufa kwake).

Kabla hatujaacha kusimulia habari za nchi zilizo karibu na Ziwa Victoria na Ziwa Albert na Ziwa Tanganyika, inafaa tutazame kidogo dalili za utawala wa Wahamiti zinazoonekana pengine katika nchi hizo.

Nchi za Nera na Buhungukira na Usmao ni katika upande wa mashariki wa Uzinza katika wilaya ya Mwanza. Imesemwa kuwa nchi hizo zilikuwa ufalme mmoja ulioanzishwa na mtu mmoja jina lake Wile. Imehadithiwa kuwa huyu Wile alitoka Uzinza akaonana na mwanamke mmoja aitwaye Mhindi, na yeye vile vile alikuwa ametoka Uzinza. Basi walikaa pamoja wakashika nchi wakaitawala na walipokufa, mwana wao Solasi alirithi ufalme. Solasi alipokufa nchi iligawanywa sehemu tatu na nduguze wanawake walizirithi, ndipo zilipoitwa Nera, na Buhungukira na Usmao. Nchi hizi hazikuunganishwa tena mpaka mwaka 1927, ndipo alipoanza tena kutawala mtu mmoja.

Jina la nchi waliyotoka watu hao, yaani Uzinza, na jina la yule mwanamke Mhindi ambalo labda lilikuwa Mhinda yaonyesha dalili ya asili ya watawala hao. Tena mtawala wa Nera asema kuwa jamaa zake ni Watusi, na kwa hakika sura yake inaonyesha dalili ya kabila hilo. Dalili nyingine inayofaa kukumbuka ni ya kuwa tambiko na sadaka hufanyiwa babu zake Solasi, na mzee anayezitoa huitwa Mgabe, na jina hilo linatumika kuita watawala wa Uzinza.

Wasukuma husimulia habari za Mungu wa magharibi anayeitwa Luhinda, lakini labda hadithi zinachanganya jina la Luhinda na Mungu kwa sababu ya nguvu zake na namna alivyoanzisha utawala wa Kihinda. Kwa hakika haiwezekani kukanushwa kuwa ufalme huo wa Usukuma kwa asili yake ni wa Kihinda, tena imesemwa kuwa wenyeji wa Usmao walitoka Uzinza.

Tukizidi kwenda kuelekea upande wa mashariki tutawakuta Wabinza, na watu hawa husimulia habari za mtawala wao wa kwanza aliyeitwa Nkande. Husema kuwa alitokea upande wa magharibi ya kusini mwa Ziwa Victoria, yaani nchi iliyo upande wa mashariki ya Uzinza. Nkande aliwashinda watu wa Mwagala akatawala nchi yote iliyopakana nayo, lakini baada ya kupita miaka kadha wa kadha ufalme ulivunjika wala haukusimamishwa tena na kuwekwa chini ya mtawala mmoja mpaka mwaka 1927.

Basi kwa kadiri tujuavyo, falme hizo zilikuwa za mwisho katika upande huo wa mashariki wa magharibi zilizotawaliwa na Wahinda.

Turudi tena kwenda magharibi tuzidi kutazama dalili zilizopo za utawala wa Wahinda. Usambiro ni nchi iliyo upande wa kusini mwa Uzinza, na sehemu yake imo katika ufalme wa Uzinza wa siku hizi. Imesemwa kuwa wenyeji wa Usambiro walitoka Uzinza na watawala wao hudai kwamba walitoka Bunyoro. Kwa

****

pande zile za kusini kuna nchi ya Usumbwa na huko watawala wengine hudai kuwa ni kabila la Watusi au Warongo, yaani kabila la wahunzi waliofanana na kabila lile la wahunzi linaloitwa El Konono walio katika kabila la Wamasai.

Hatuwezi kusema kwa dhahiri kuwa watu wanaokaa upande wa kusini zaidi wana damu ya Wahamiti, lakini mtu mmoja aliyechungua sana habari hizo, asema kuwa watawala wa asili wa Unyamwezi wengi ni Wahima. Lakini habari hizo haziwezi kuhakikishwa sasa, tunaweza kubahatisha tu. Maana miaka mingi sana imepita na watawala wa Unyamwezi waliotawala katika miaka hiyo ni wengi mno, na hivi ni vigumu kuthibitisha jamaa au ukoo wa wale waliotawala kwa asili.

Kwa upande wa magharibi kuna nchi ya Uha, na watawala wa nchi hiyo kwa hakika ni Wahima, nao wanajua asili yao.



Somo 3-Wafipa

Sasa tutasoma habari kidogo za Wabantu wengine waitwao Wafipa wanaokaa upande wa kusini mwa magharibi, na kumbe, hata huko twaona ya kuwa kabila hilo la ajabu, yaani Wahima, lilienea na kufika mpaka upande wa kusini mwa Ziwa Tanganyika. Kwa miaka mingi kabla hawajafika Wahima hao, yasemwa kuwa Wafipa walitawaliwa na watawala wadogo, na mkubwa wao aliitwa Mwene Milanzi. Basi katika zamani za Mwene Milanzi mmoja aitwaye Ntatakwa, kundi la wageni lilifika nchi yake wakati mwenyewe hakuwako. Wageni hao walikuwa warefu, tena weupe kidogo na sura zao zilikuwa za kipanga, na tena walikuwa kama watu wenye kiburi mno. Katika watu hao walikuwamo wanawake watatu, na mmoja wao jina lake Mwati alikuwa akichukua jiwe. Mwanamke huyo aliomba kiti apate kupumzika. Basi mke wa Ntatakwa alipoona jinsi walivyo na kiburi aliogopa, akatoa kiti cha kifalme akampa akikalie. Imesimuliwa katika hadithi hii ya kuwa asubuhi yake huyo mwanamke Mwati alichukua jiwe lake akapanda nalo mpaka juu ya mlima uitwao Itweleli, na hapo akatangaza habari ya kuwa amekwisha ichukua nchi yote iwe yake. Ntatakwa aliporudi hakufanya matata hata kidogo, bali alikubali kwa unyenyekevu, maana alisema kuwa amekwishaonywa na mzuka ya kuwa wageni watakuja na kushika nchi yake, akaridhika.

Hadithi nyingine husimulia ya kuwa Mwati alimwuliza Ntatakwa nchi yake inafika mpaka wapi, naye alinyosha mkono wake apate kumwonyesha mipaka ya nchi yake, lakini aliona haya kuinua mkono juu Mwati asione chini ya kwapa lake, na hivi alionyesha kipande kidogo cha nchi tu. Kisha, Mwati hakuwa na haya hata kidogo akainua mkono wake juu sana akasema kuwa nchi yake inaenea mpaka mbali sana.

Basi kundi hilo la watu lililotokea Ruanda na imehadithiwa kuwa walikuwa wa jamaa ya Abahinda wa kabila la Watusi. Tumetaja jina hili Hinda mara nyingi katika habari hizi mpaka sasa, tena tutakumbuka kuwa ule ufalme ule wa Karagwe uliosimamishwa na Ruhinda ulienea mpaka Ruanda, yaani nchi waliyotokea Watusi. Hivyo tunaweza kusadiki kwamba watu hao walikuwa Wahima, yaani watu Wahamiti.

Watu wengine katika kundi hilo waliotoka Ruanda walibaki katika nchi ya Kibondo na wazao wao wamekaa huko hata leo, tena wako watawala walio katika nchi hiyo wenye damu ya Watusi. Imesemwa ya kuwa wale waliofika kusini katika nchi ya yule Mwene Milanzi Ntatakwa walisafiri kwa upande wa magharibi wa Ziwa Tanganyika na walipofika mwisho wa ziwa, walizungukia upande wa kusini, ndipo walipotokea wakafikia nchi yake. Wazao wa kundi hilo la watu ni watawala wa nchi ya Ufipa na sehemu nyingine za wilaya ya Kigoma. Zaidi ya haya, mtawala wa kabila la Washamba wanaokaa kusini mwa nchi ya Ufipa hudai kwamba babu yake aliitwa Luhinda.

Yule mwanamke Mwati tuliyemtaja, alizaa mtoto mwanaume akamwita Msili Mkokwe, na alipokua, Ntatakwa alimchukua akamweka awe mtawala. Basi tangu hapo mpaka leo hivi, watawala wa huko huwekwa na mtu anayeitwa Mwene Milanzi ambaye ni mlinzi wa ule mlima aliouwekea Mwati jiwe lake nao unaheshimiwa sana.

Baadaye Msili Mkokwe hakuridhika na nchi yake, akaanza kujaribu kushinda nchi zilizotawaliwa na watawala wadogo apate kutawala nchi yote ya Ufipa mwenyewe. Lakini hakuweza, na alipopigana na Ndasi mtoto wa mjomba wake akashindwa, basi aliona uchungu mwingi akajiua. Basi Ndasi alijiweka kuwa mtawala, lakini hakuwa na siku nyingi, akafa. Ndipo Zumba Mwana Mzia alipoirithi nchi, na katika wakati wa utawala wake nchi iligawanywa sehemu mbili, yaani Nkanzi kwa kaskazini, na Lyangalile kwa kusini. Wakati huo nchi ya Ufipa iliingiliwa na Wanyika walioiharibu sana, lakini mkubwa wao jina lake Chalo alipouawa, ndipo wafuasi wake walishindwa na kuuawa.

Lakini hata baada ya hayo nchi haikustarehe, maana katika wakati walipotawala watawala wanane waliofuata, nchi ilisumbuliwa sana mara kwa mara kwa fitina na vita za kindanindani mpaka alipoanza kutawala Zumba Kalonga, ndipo walipokuja Watuta walioingia nchi na kuwashinda Wafipa. Habari za Watuta zitasimuliwa baadaye. Basi Watuta walikaa katika nchi kitambo, kisha waliondoka wakaenda zao, wala hawakurudi tena. Hivyo, Wafipa walipata nchi yao tena, na katika wakati wa watawala wawili waliofuata hakuna habari kubwa iliyotokea, ndipo Sangu Chapiti Punda alipoanza kutawala, na wakati huo Waarabu walifika katika nchi ya Ufipa mara ya kwanza.

Sangu Chapiti Punda alikuwa mtu mnyonge sana na watu wake walimchukia kabisa kwa sababu ya tabia yake. Basi waliwaomba Wawungu waje wamwondoe katika utawala wake. Wakati ule, Kilanga alikuwa mkubwa wa Wawungu, akaja pamoja na watu wake wakaunguza nyumba ya Sangu Chapiti Punda, wakateka nyara, kisha walikwenda zao. Huku nyuma Sangu Chapiti Punda aliwakimbilia Waarabu wakamwokoa.

Nchi ya Lyangalile vile vile iliathirika, maana watu waliotoka Usangu walikuja pamoja na Kimalunga mkubwa wao, wakaenea katika ponde la Ziwa Rukwa, wakapanda mpaka juu milimani, wakamshinda Ulamasi aliyekuwa mtawala wa Lyangalile. Basi Kimalunga aliishika nchi, na Wadachi walipofika katika nchi hii wapate kuitawala, alikuwa angali akiitawala.

Sura ya pili itaendelea.
 
Somo 4-Kuendelea na habari za Wafipa

Sasa turudie nyuma kidogo. Sangu Chapiti Punda alipokufa, Nandi Kapufi aliurithi utawala, na katika wakati wake Wazungu wa kwanza wa mission wanaoitwa 'White Fathers' walifika katika nchi yake. Ntinde Kiteta alifuata Nandi Kapufi lakini alitawala muda wa miezi mitatu tu, ndipo aliporithi Nandi Msulwa. Nandi Msulwa alitawala nchi kwa miaka saba, kisha alijiua, na Mtinde Kapere aliurithi utawala. Lakini kwa kuwa Wadachi hawakufahamu vema desturi za urithi wa Wafipa, walimwondoa wakamweka Kiatu mwanawe Msulwa katika urithi wa Mtinde Kapere. Kiatu alikufa katika mwaka 1915 na dada yake aitwaye Ngalu alirithi utawala, lakini serikali ya Kiingereza ilimweka Mtinde Kapere awe waziri wake.

Mpaka siku hizi za karibu, jamaa za Mtinde Kapere walioana katika ukoo wao, maana katika desturi zao walikatazwa kabisa wasioe wenyeji wa nchi. Na kwa kuwa walitengwa kabisa na watu wa kabila lao, iliwalazimu kuoana katika ukoo wao, na kwa hivi wamepungua sana hata karibu kwisha, maana desturi hiyo huharibu uzazi.

Imedhaniwa kuwa ufalme huu wa Kitusi ulio katika Ufipa ulisimamishwa zamani ya miaka 200 kama hivyo, nao ni ufalme wa mwisho uliosimamishwa na kabila hilo linalotawala mahali pengi katika nchi yetu.

Kabla hatujamaliza kusimulia habari za taifa la Wahima, imetupasa tukumbuke kuwa hata Wataturu au Watatoga wanaokaa pande za Ziwa Victoria husema kwamba walitokea Ruanda. Tutasimulia habari za kabila hilo la Wahamiti baadaye, lakini labda hii ndiyo sababu Watatoga walihama kutoka nchi ya Mbulu wakati waliposhindwa na Wamasai, wakaenda kukaa pande za Ziwa Victoria. Kama ni kweli asili yao walitoka Ruanda, basi yaonyeshwa safari nyingine iliyo kubwa ya watu hao wa Wahamiti.

Sasa tumekwisha onyesha namna watawala wa Kihamiti walivyoenea katika nchi yetu. Kwanza walitoka Ugala, wakafika Bunyoro, kisha walizunguka Ziwa Victoria wakafika pande za mashariki kupita Mwanza. Kutoka Ruanda walisafiri mpaka pande za kusini mwa Ziwa Tanganyika na hapa wakakaa wakajifanya watawala. Ni vigumu sana kusadiki kuwa walifanya mambo waliyoyafanya kwa nguvu ya silaha zao kwa sababu Wabantu walikuwa wengi sana kuliko Wahamiti waliokuja. Hadithi nyingi zinazosimulia jinsi wenyeji, yaani Wabantu, walivyokubali kutawaliwa nao bila ya kukaidi, huelekea kuonyesha kuwa Wahamiti walifaulu kwa sababu ya tabia zao jinsi zilivyokuwa bora kuliko nguvu za silaha.

Labda wenyeji wa nchi walifikiri kuwa wageni hao waliotoka katika nchi za kaskazini wana nguvu za ajabu za uganga. Labda walidhani wanaweza kuleta mvua na maajabu mengine, maana pengine hata sasa wenyeji husadiki kuwa wanazo nguvu hizo. Lakini juu ya hayo yote lazima tukumbuke ya kuwa kwa desturi za tokea asili yao, Wabantu hawana matengenezo ya ufalme wala ya utawala. Walikuwa walimaji tu na kila ukoo ulitawaliwa na babu au mkubwa wa jamaa au ukoo. Basi ni dhahiri ya kuwa namna walivyozoea kukaa, haikosi iliwafanya wakubali kutawaliwa na wageni waliokuja katika nchi yao. Hatuna habari za nchi yo yote iliyotawaliwa na watu wa Afrika kwa muda mrefu kama hivi walivyotawala Wahamiti hao. Tena hatuna habari za nchi kubwa iliyotawaliwa na Wabantu kama hizi zilizotawaliwa na Wahamiti.

Kweli Wabantu wengine walitokea wakatawala wakawa washindaji kwa ushujaa, lakini kwa desturi utawala wao haukudumu sana, wala haukuendelea kwa vizazi vingi.

Haujatokea ufalme mwingine uliofanana na ufalme huo ulioitwa Kitara hata katika nchi yote ya Afrika ya Mashariki.

Utawala wa Wahima ulienea kutoka mstari tokea Mwanza kufika Uzinza, na kupita mstari huo hawakusimamisha ufalme. Labda hawakuweza kwa sababu walikutana na watu wengine wa taifa lao, maana walikutana na Wagala walio kabila lenye asili yake karibu na mto Nile. Wagala walikuja pande za kusini mpaka mto uitwao Mara, wakawashinda watu waliokuwa wakikaa huko. Walipopita mto Mara, walianza kuchanganyika pamoja na Wamasai, na sasa huitwa Waruri. Katikati ya Waruri na Wasukuma, Washashi wanakaa. Washashi ni Wasukuma waliochanganyika pamoja na Wamasai na Watatoga.

Basi, sasa tumekwisha ona kuwa Wahima ndio waliotawala nchi zote zinazozunguka yale maziwa makubwa, Ziwa Victoria, Ziwa Edward, na Ziwa Tanganyika. Wenyeji ni Wabantu wa makabila mengineyo, lakini watawala walio wengi wana asili yao katika taifa lile la Kihamiti, ingawa sasa mahali pengi hata na wao wamechanganyika pamoja na Wabantu mpaka sura na tabia zao za asili zimewapotea kabisa.

Somo 5-Wanyamwezi

Yale mambo tuliyokwisha soma, yaani kuwekwa falme hizo za Kihamiti ndiyo mambo makubwa yaliyotokea katika nchi za magharibi mpaka mwaka 1700 kama hivi. Mambo makubwa mengine yaliyotokea ni mahamio ya Watatoga, na vita za Wamasai waliowafukuza Watatoga huku na huko. Tutazisoma habari hizi halafu. Tena nchi za kando ya Ziwa Victoria zilisumbuliwa sana na watu waliotoka Uganda na wale Wagala au Waruri waliokuwa wakinyang'anya watu mali zao kila mara.

Katika miaka iliyofuata karibu na 1800, wageni wengine walifika nchi hizi, nao ni Waarabu na wengine waliotoka pwani kuja kufanya biashara na hasa biashara yao ya kununua watumwa. Kabla ya wakati huo, watu wa pwani hawakushughulika sana na watu wa bara. Lakini sultani wa Kiarabu alipoanza kutawala Unguja, Waarabu walio pwani walishikwa na tamaa ya kuingia katika nchi za bara ambazo hazikujulikana kwa wakati huo. Hasa walithubutu kusafiri katika nchi hizo kwa sababu walikuwa na bunduki za kujilinda.

Tumekwisha simulia kuwa Waarabu walifika katika nchi ya Ufipa kwa mara ya kwanza wakati alipokuwa akitawala Sangu Chapiti Punda. Hatujui tarehe kwa hakika, lakini tangu walipofika, watawala watano au sita wametawala huko. Waarabu hawakuonekana katika nchi za upande wa Kilimanjaro mpaka katika mwaka 1850 kama hivi.

Husemwa kuwa Waarabu wa kwanza waliofika katika nchi ya Unyanyembe walifika wakati alipotawala Swetu wa kwanza, naye tunajua alitawala katika miaka ya kwanza ya 1800. Imehadithiwa kuwa wawindaji wa ndovu wengine walikuwa wakisafiri kutoka Unyanyembe kwenda pande za mashariki, wakakutana na watu wa pwani wakifanya biashara, wakafuatana nao mpaka pwani, halafu wakarudi tena Unyanyembe.

Waarabu walipofika nchi za bara ilikuwa desturi yao kujenga miji au kambi walizoita bandari. Imesemwa ya kuwa bandari moja ilijengwa Msene katika nchi ya Sumbwa, yaani Kahama, katika mwaka 1830, na moja Ujiji katika mwaka 1845. Lakini mji mkuu wao uliitwa Kazeh na baadaye uliitwa Tabora, nao hudhaniwa haukujengwa mpaka mwaka 1852.

Mtawala wa kwanza ambaye tunazo habari zake ni Swetu wa kwanza, na Fundikira alimfuata katika kutawala. Fundikira na baba yake Swetu walipatana sana na Waarabu, na binti mmoja wa Fundikira aliolewa na yule Mwarabu Hamed Hamadi anayejulikana hasa kwa jina la Tipu Tipu.

Katika mwaka 1858 Waingereza wawili Burton na Speke ambao walikuwa Wazungu wa kwanza waliosafiri katika nchi hizi, walikutana na Fundikira na Waarabu waliokuwa wakikaa Kazeh, wakaandika habari za safari zao. Burton ameandika ya kuwa wakati huo Waarabu walikuwa wamekaa Usukuma kwa miaka kumi, lakini labda alitaka kutaja Sumbwa wala si Usukuma. Akasema kuwa, kwa desturi Waarabu walikaa kwa makundi idadi ya watu ishirini na tano kama hivi, na kwa kuwa walikuwa hodari matata yo yote yalipotokea hawakukubali kutekwa na kuonewa bila kupigana, lakini hawakuwa na nguvu za kutosha kushinda na kutawala nchi kabisa.

Katika mwaka 1858 Mwarabu mmoja aliuawa katika nchi ya Uvinza na mara vita ikavumbuka. Wenziwe walikusanya watumwa wao idadi ya mia mbili au tatu wakawapa bunduki na silaha kwenda kupigana na wenyeji. Lakini kumbe, kila mmoja alitaka wenziwe watoe dhamana juu ya maisha na mali yake kuwa itakuwa salama, kwa hivi walirudi mahali pao bila kufanya neno. Kwa kawaida, ndivyo ilivyokuwa tabia zao: walikuwa na askari wengi wenye silaha na bunduki za kutosha, lakini hawakuwa na majemadari hodari wa kuwaongoza vitani. Lakini hata hivyo waliweza kukaa salama katika nchi za bara, na kwa kawaida walipatana sana na wenyeji, wakaoa wanawake wa wenyeji wakachanganyika na Wabantu. Wasingalipatana nao wasingaliweza kuleta watumwa pwani, maana waliwaleta kutoka mbali sana kupita nchi za wenyeji.

Katika habari alizoandika Burton, asema ya kuwa walikuwako watawala wawili waliokuwa wakubwa katika nchi ya Unyamwezi, ndio Fundikira na Msanga wa Msene, na wote wawili walipatana sana na Waarabu. Wakati huo, Mwarabu mkubwa wa Kazeh alikuwa Snei bin Amiri. Kweli Tipu Tipu alikuwa na nguvu nyingi katika nchi za bara, lakini kazi yake hasa ilikuwa kufanya biashara, na zaidi katika nchi za Kongo, akakaa kwa amani.

Fundikira na Msanga walisaidiwa sana na Waarabu katika matata yaliyotokea mara kwa mara, na kwa msaada wao Fundikira aliteka sehemu ya Uyui, na Msanga alifukuza Watuta waliokuja kumshambulia.

Yule msafiri Speke tuliyemtaja, alisafiri katika nchi hizi mara ya pili katika mwaka 1861 akamkuta Fundikira amekwisha kufa; na Manua Sera, au labda jina lake ni Manasele mwanawe, alikuwa akitawala nchi. Huyu Manasele hakupatana na Waarabu kama baba yake alivyopatana nao, maana alipofika Speke Manasele alikuwa amekwisha gombana nao kwa sababu aliwatoza ushuru juu ya bidhaa zao walizozipitisha katika nchi. Lakini Waarabu walikuwa na nguvu wakamweka mtawala mwingine wasikubali utawala wa Manasele; walimweka Mkisiwa aliyekuwa mwana wa suria wa Fundikira mahali pake. Manasele alikuwa hodari mwenye moyo wa kiburi, akakataa kabisa kutii amri za Waarabu, akajilipiza kisasi kwa kushambulia safari zao zilizopitapita akateka bidhaa na mali zao.

Speke alipofika aliwakuta Waarabu wamekwisha kusanya watu mia nne ili waende wakamkamate Manasele. Basi Manasele alimwendea Speke akaomba msaada, na Waarabu hawakufaulu katika shauri lao, na Manasele aliendelea kuwasumbua sana kwa siku nyingi. Katika mwaka 1873 msafiri Mzungu mwingine jina lake Stanley alifika nchi hizi na Waarabu walimwomba aamue shauri na kuwapatanisha na Manasele. (Stanley alikuwa Mwingereza aliyetumwa kumtafuta Livingstone katika nchi hii, maana kwa muda wa miaka mitatu rafiki zake walikuwa hawajapata habari zake, wakafikiri kuwa amepotea, au amekufa.)

Katika mapatano waliyoyataka Waarabu walikusudia kumpa Manasele nchi nyingine badala ya Unyamwezi, lakini alikataa kabisa kufanya shauri lo lote nao mpaka wamtoe Mkisiwa katika utawala wa Unyamwezi. Basi hapo vita ikaanza tena na mara nyingi Manasele alizingirwa akawa karibu kukamatwa, lakini bahati yake ilikuwa kuokoka kila mara. Basi akaendelea kuwasumbua Waarabu na kuteka bidhaa zao mpaka hatimaye alifia Ugogo.



Somo 6-Habari za Mirambo

Haikosi wasomaji wengi wamesikia jina la mtu huyu Mirambo aliyejulikana sana zamani kwa ajili ya nguvu zake.

Mirambo alikuwa mkubwa wa nchi inayoitwa sasa Urambo. Alikuwa nusu Mha na nusu Mkimbu; alizaliwa kati kati ya miaka 1840 na 1845, yaani aliishi wakati ule ule wa Manasele.

Kabla hajafa Manasele alikuwa amegombana na nduguye jina lake Kiungi, yaani mwana wa mjomba wake, na Kiungi alikimbia akajiweka chini ya ulinzi wa Mirambo. Basi Waarabu walimchagua Kiungi awe mtawala wa Unyanyembe. Labda walimchagua kwa sababu walimweza sana akawa chini yao kabisa, na tena alikuwa akipatana sana na Mirambo ambaye walitaka urafiki wake sana.

Katika mwaka 1870 Mirambo alianza kujitokeza na kupigana vita na kushinda nchi. Majeshi yake yalikuwa makundi ya watu waliotoka kila mahali, na hasa watu wasiotii watawala wao. Akazidi kupata nguvu mpaka akashinda sehemu yote ya magharibi ya kaskazini mwa Unyamwezi. Katika mwaka 1871 aliwashambulia Waarabu waliokaa Tabora akawashinda, lakini hakustarehe huko. Alipigana sana na Watuta akawashinda, lakini alipoona ya kuwa ni watu wakali sana, na tena hodari katika vita, aliona kuwa watamfaa kuwa askari zake, basi akawapa mahali pa kukaa paitwapo Ugala katika nchi ya Kigoma, akawafanya raia zake.

Mirambo alishambulia nchi ya Shinyanga akarudi kwake tena akichukua mateka mengi sana. Watawala wa Shinyanga hawakuthubutu kupigana naye wakampa kila kitu alichotaka kusudi aende zake na kuwaacha kwa amani. Lakini mtawala mmoja jina lake Kajala wa Usule hakukubali kushindwa. Alijenga boma kubwa juu ya mwamba, na humo alipigana na Mirambo na watu wake, nao hawakuweza kumtoa. Mahali walipopigana panajulikana hata leo.

Katika mwaka 1880 Mirambo alianza kujiingiza Ufipa akachoma nyumba ya mtawala wa Wapimbwe. Katika vita hii Waingereza wawili waliuawa. Waingereza hao walikuwa wakirudi pwani baada ya kuchukua ndovu wawili kutoka Bagamoyo mpaka misioni ya Kibeleji iliyo Karema.

Mirambo hakuendelea sana na vita hii ya Ufipa, na alipofika chini ya milima iliyo Ufipa aligeuka akarudi kwake.

Yule Kiungi tuliyemtaja alitawala Unyanyembe kwa muda wa miaka 20, yaani mpaka mwaka 1882. Ndipo Isike alipoanza kutawala akajenga mji wenye boma la nguvu karibu na Tabora. Wakati huo Nungu aliyekuwa mpwa wa Fundikira aliipiga nchi ya Wakimbu iitwayo Kiwere akaishinda, akamwomba Mirambo amsaidie vita wamwondoe Isike, lakini hawakuweza. Katika vita hii Mirambo alizingiwa akakamatwa, lakini aliachiliwa kwenda huru tena.

Labda vita hii ilikuwa vita ya mwisho ya Mirambo, maana katika mwaka 1886 alikufa, na zile nguvu alizokuwa ameziamsha zikafa pia. Mwanawe Siki alijaribu kufuata desturi zake asiweze. Katika mwaka huo huo Wadachi walijitegemeza Tabora wakampiga Isike mwana wa Fundikira wakamshinda kabisa. Isike alipoona ameshindwa alijiharibu mwenyewe pamoja na nyumba yake yote kwa baruti, lakini tutasoma habari zake baadaye.

Isike alipokufa, Nyaso binti Fundikira alirithi utawala, akatawala mpaka mwaka 1889 akafa. Ndipo Karunde binti Gumati alipoanza kutawala. Karunde binti Gumati alizaliwa na mjakazi wa Fundikira, akatawala mpaka mwaka 1917, akafa, na Saidi Fundikira alianza kutawala.

Kabla ya kuacha habari za Unyamwezi, lazima tutaje mtawala mwingine. Katika mwaka 1873 alipofika yule Mzungu Stanley katika nchi, alikuta mtawala mwingine mwenye nguvu, jina lake Mtinginya wa Usongo.

Mtinginya alimsaidia sana Mirambo katika vita zake. Tena alikusanya jeshi la askari kama alivyokusanya Mirambo, lakini hasa walikuwa Wamasai, au labda walikuwa Watatoga, maana Stanley alisema kuwa ni Wamasai lakini labda alikosa, maana ni vigumu sana kuona Wamasai wakitumikia watu wengine, na labda walikuwa Watatoga na yeye aliwadhani kuwa Wamasai kwa sababu walifanana nao.

Lakini Mtinginya hakupata nafasi kufuata desturi za Mirambo kwa sababu Wadachi walikuwa wamekwisha weka imara serikali yao, na tangu wakati huo vita za namna hiyo hazikuwezekana tena.

Mwisho wa sura ya pili
 
SURA YA TATU

HABARI ZA NCHI ZILIZO KASKAZINI

Somo 1-Maingilio ya Wahamiti, yaani Wamasai na Wakwavi

TULIPOSOMA habari za nchi zilizo magharibi tuliona namna Wahamiti walivyoingilia nchi na kujiweka juu ya Wabantu, na tukichungulia habari za zamani za nchi za kaskazini tunaelezwa vile vile habari za maingilio ya watu wa taifa hilo hilo waliotoka katika nchi za mbali sana kwa upande wa kaskazini. Katika Wahamiti hawa, Watatoga, au pengine huitwa Wataturu, walikuwa kwa kwanza kufika na labda hawa walitokea nchi ya Ruanda.

Wahamiti waliofika nchi hii kufuata baada ya Watatoga ni wale wanaoitwa Waasa au Wandorobo, nao kila mara walikuwa wakipigana na Watatoga mpaka nguvu zao zilikwisha. Halafu Wakwavi wakaja kutoka nchi zilizo kaskazini na kwa kuwa nguvu za Wandorobo zilipungua, Wakwavi waliwashinda na kuwatawanya na kuwanyang'anya mali zao. Wandorobo wengine walikimbilia mwituni wakawa wawindaji, na hata leo wazao wao hukaa mumo humo mwituni.

Baada ya hayo Wakwavi walipigana sana na Watatoga ili wamiliki nchi za tambarare kwa ajili ya kuwalisha ngombe zao, na kwa hivi nguvu zao zilipungua kama zilivyopungua nguvu za Wandorobo. Ikawa walipofika Wamasai ambao walikuwa wahamiti wa mwisho walioingilia nchi hii, Wakwavi waliomba msaada wa Watatoga wawasaidie kupigana vita na Wamasai. Basi tumeona ya kuwa yalikuwa maingilio manne, yaani ingilio la Watatoga, la Wandorobo, la Wakwavi, na la Wamasai.

****

Hatujui miaka mingapi imepita tangu walipoanza kufika Wahamiti hao, lakini tunajua ya kuwa Wamasai hawakufika mpaka miaka inayokaribia mwaka 1800.

Kabla hawajafika Wamasai katika nchi yetu, walikuwa wakikaa upande wa Afrika ya Mashariki unaoitwa sasa Kenya kwa miaka mingi, wakahama taratibu wakiingia nchi hii kutafuta malisho kwa wanyama wao. Katika mwendo wao wa kuhama waliingia nchi za tambarare zilizo chini ya mlima Kilimanjaro kwa upande wa kaskazini, na wakati ule hawakuwa wengi, maana mtawala wa Wachaga jina lake Rongoma aliweza kuwazuia wasienee sana. Imesemwa ya kuwa wale waliowahi kuingia nchi yake iliyo kati kati ya Kilimanjaro na Upare, walijiweka chini yake na yeye akawa mtawala wao. Wakati huo tunaosimulia sasa labda ulikuwa mwaka 1820, maana tunazo habari za Wachaga za tangu vizazi vingi vinavyotangulia wakati huo, lakini Wamasai hawatajwi mpaka wakati huo aliotawala Rongoma.

Kama tulivyosema, Wamasai walitaka kuingia zile nchi za tambarare zilizo chini ya mlima Kilimanjaro, na kwa hivi walikuwa hawana budi wapite upande huu au upande huu, ndipo waweze kuziingilia. Lakini Wachaga walikuwa wamekwisha weka imara utawala wao, na Wamasai wangalitaka kushika nchi yao wangalikuwa na kazi ngumu sana kuwashinda. Lakini Wamasai walikuwa hawana nia ya kushika nchi za mlimani, walitaka malisho yaliyo chini ya mlima tu, na hayo ndiyo yaliyoleta ugomvi kati ya Wamasai na wenyeji.

Mtawala mmoja mwenye nguvu jina lake Horombo alikuwa amejiweka juu ya nchi za watawala wadogo wote wa Wachaga wa upande wa kaskazini na upande wa mashariki, naye alikuwa na makundi makubwa ya ng'ombe, kwa hivi alitaka malisho akadai kuwa nchi za tambarare zote ni zake. Basi kila walipokuja Wamasai aliwafukuza na kuwanyang'anya ng'ombe zao. Wamasai hawakuweza kuvumulia hivi, wakaenda kwao wakakusanya kabila lao lote, likafanyika jeshi moja kubwa mno, likaja likakusanyika karibu na Kibong'oto kwa upande wa magharibi mwa Kilimanjaro. Horombo alijifanya tayari kwa vita akafanya hila. Aligawanya jeshi lake, na nusu alipeleka upande wa kusini mwa mashariki ili kuwavuta Wamasai wapiganie huko, na huku nyuma yeye mwenyewe aliwashambulia pamoja na askari zake waliobaki akitokea upande mwingine wa mlima. Lakini hakuwa na bahati, maana mwanawe aliyekuwa akiongoza jeshi lile la kwanza alifanya ujinga, akajaribu kuwashambulia Wamasai kabla ya wakati uliowekwa, na kwa hivi yeye na watu wake wote waliangamizwa kabisa. Basi hapo Wamasai walikuwa hawana wa kuwazuia, wakamwendea Horombo katika nchi yake yeye, naye alikuwa hana budi apigane nao pamoja na jeshi lake lililopungua sana. Horombo na watu wake walikuwa hodari wakapigana vita kali sana kwa muda wa siku tatu. Watu wengi sana wakafa katika vita hii na imehadithiwa ya kuwa harufu za maiti zilikuwa mbaya mno hata hazikuvumilika, ikawa kila usiku majeshi yote mawili hayana budi kuondoka mahali walipopigania kwa sababu ya uvundo.

Horombo na watu wake waliwazuia Wamasai barabara wakawa karibu kuwashinda na kuwarudisha nyuma, lakini msiba uliwapata Wachaga. Yasemwa Horombo alikuwa mtu mkubwa sana na kwa hivi adui zake waliweza kumwona vizuri na kumpiga shabaha. Basi mara ilipoanza vita alipata kupigwa na rungu, na mkono wake uliumia sana na kwa hivi hakuweza kushika ngao yake. Jioni ya siku ya tatu alipigwa mshale wa mbavu akaanguka, na mara pale pale watu wake walishikwa na hofu wakatawanyika. Lakini usiku ulikuwa unaingia na vita ilitulia, na Wamasai ambao wamepigwa sana hawakuweza kustahimili zaidi wakarudi nyuma. Basi kwa vile ambavyo Wachaga wametawanyika, na Wamasai wamerudi nyuma, ikawa hapana aliyeshinda wala hapana aliyeshindwa. Lakini tangu siku hiyo mlima wa Kilimanjaro haukuweza tena kuwazuia Wamasai, wakapita mpaka sehemu za chini yake na kuingia nchi za tambarare kukaa. Yasemwa kuwa vita hii ilitokea kati ya miaka 1820 na 1825.

Imedhaniwa ya kuwa Wakwavi na Wamasai walikaa pamoja kwa amani kwa muda, lakini baadaye Wakwavi walichagua mkubwa wao awatawale, yaani Laibon, na hivi ugomvi uliotokea na vita ikaendelea siku nyingi. Kwa mwisho walipigana sana Kisongo ambapo ni mwendo wa saa sita kutoka mlima Meru kwa upande wa magharibi, na hapo Wakwavi walishindwa kabisa wakakimbilia milimani. Lakini Wamasai hawakuwaachilia, maana Laibon Mbatyan aliyekuwa mkubwa wa Wamasai alipeleka watu wake kuwafuatia, wakawateka wakawafanya sawasawa na watumwa. Wakwavi wengine waliokoka wakaanza kuwa wawindaji, na baada ya kupita miaka kadha wa kadha waliweza kupata makundi ya ng'ombe tena wakashika desturi zao za zamani. Wamasai huwaita Wamuli, nao wamefanana sana na Wamasai. Wengine waliendelea kuwa wawindaji mpaka leo, na mara nyingi wanadhaniwa na watu kuwa ni Wandorobo, lakini Wamasai huwaita Wasiti (El Asiti).

Wamasai walizidi kupata nguvu, na baadaye kabila dogo moja linaloitwa Waarusha lilijiweka chini yao, wakawatii wakafuata desturi zao na kusema lugha yao, na labda makabila ya Wakahe na Wataveta walifanya vile vile. Mkubwa wa Wamasai aliwapa Waarusha ruhusa kukaa mlima Meru na wengi wanakaa huko hata leo.

Nchi za Ushambala na za Kilimanjaro zilikuwa salama wakati wa vita za Wamasai kwa sababu wenyeji walikuwa wamekwisha kutungamana na kuweka watawala wenye nguvu. Wapare walisumbuliwa mara kwa mara wakanyang'anywa mali zao, lakini Wamasai hawakushughulika sana nao kwa sababu hawakuwa na mali nyingi. Wazigua walikuwa na makundi mengi ya ng'ombe, kwa hivi Wamasai waliwanyang'anya kila mara.

Kwa muda Wamasai walizuiliwa wasienee katika nchi zilizo mbali zaidi, maana milima ile inayopita kati kati ya nchi yetu ambayo imepakana na bonde refu liitwalo Bonde la Ufa (Rift valley) katika elimu ya Jiografia, ilikuwa kama boma la kuwalinda watu wa pande hizo. Tena Wambugwe wanaokaa chini ya milima hiyo ni watu hodari sana kwa vita, na mara nyingi waliwapiga na kuwafukuza Wamasai na kuwahasiri sana. Basi kwa hivi Wamasai hawakuweza kupanda juu ya milima na kuivuka mpaka kati ya miaka 1850 na 1860 na hapo walikutanana na Watatoga.



Somo 2-Wamasai na Watatoga

Watatoga walikuwa wamegawanyika kuwa jamaa tatu, yaani ukoo wa Wabrariga, na ukoo wa Wabayuta, na ukoo wa Wasimityek au pengine huitwa Wanonega. Kwanza Wamasai waliwafukuza Wabayuta kutoka Ngorongoro. Wengine walikimbilia mlima Gamrit na wengine walifuatana na mkubwa wao Sagiro wakahama kwenda pande za ziwa Manyara kwa upande wa kusini kuelekea Mbugwe. Walipofika huko Wambugwe waliwakataza wasiingie nchi yao, kwa hiyo wengine waliwafuata jamaa zao waliokwenda Gamrit wakamwacha Sagiro. Wale waliomfuata Sagiro waliongozwa naye mpaka Unyamwezi. Walipokuwa wamekaa Unyamwezi kwa muda kidogo Wanyamwezi walitambua kuwa wageni hawa wanawaletea udhia, maana Wamasai waliwafuata Watatoga hata katika Unyamwezi wakanyang'anya mali zao na pia walinyang'anya mali za Wanyamwezi. Basi waliambiwa watoke nchi za Unyamwezi. Lakini mtawala mmoja jina lake Mtinginya aliyekuwa na nguvu nyingi aliwakaribisha waende kukaa katika nchi yake ambayo siku hizi inaitwa Nzega. Tuliposoma habari za Mirambo, tuliona ya kuwa Mtinginya alitaka kufuata desturi zake, yaani kuweka jeshi kubwa, na hasa askari zake walikuwa Wamasai. Lakini tulisema labda hawakuwa Wamasai ila Watatoga, maana walifanana sana. Labda Mtinginya alifikiri kuwa watu hao wataweza kuwa rafiki wenye nguvu za kumsaidia katika vita zake, lakini alijuta upesi alipoona namna tabia zao zilivyo za jeuri, akawakaribisha Wamasai waje kuwatoa Watatoga katika nchi yake. Hapo ikawa vita kali sana na Watatoga walishindwa kabisa wakanyang'anywa makundi ya ng'ombe zao zote. Sasa Sagiro aliwaongoza watu wake waliobaki kwenda nchi ya Ntusu, na huko walipigana na Wakerewe, lakini Wamasai waliwafuatia tena wakawapiga hata karibu kuwafuta kabisa. Basi alipoona hivi, Sagiro aliwakusanya watu wake akawaongoza akawarudisha tena katika nchi ya Mbulu.

Wamasai walitawanya jamaa ile ya Wabrariga vile vile, wakaondoka wakaenda kukaa katika nchi zilizo upande wa ghuba iitwayo Speke Gulf kando ya Ziwa Victoria. Lakini hawakuruhusiwa kukaa kwa amani, maana Wamasai waliwafuatia wakawapiga na kuwanyang'anya mali zao. Kisha Wabrariga hao walitawanyika kabisa. Wengine waliopona walikimbilia kisiwa kiitwacho Ukerewe; wengine walijificha katika kabila la Washashi wa Ikoma pande za ghuba ya Speke Gulf, na wengine walikimbilia Meatu na mahali penginepo katika nchi ya Usukuma.

Basi hivyo kabila la Watatoga lililokuwa na nguvu nyingi sana, lilivunjwa na kuangamizwa kabisa na Wamasai, na siku hizi hawaonekani kwa wingi ila katika nchi ya Mang'ati pande za Mbulu, na wengine wachache waliotawanyika katika nchi nyinginezo walizowahi kuzikimbilia na kujificha huko ili waokoke.



Somo 3-Habari nyingine za Wamasai

Tumekwisha taja Mzungu mmoja jina lake Burton aliyefika nchi hizi katika miaka iliyokaribia 1856, basi yeye amesimulia ya kuwa alipofika Wamasai walikuwa wameingia nchi ya Ugogo, lakini hawakuonekana kwa wingi. Burton mwenyewe hakuwaona, ila alisikia habari zao tu.

Kabila la Waburungi wanaokaa nchi ya Kondoa Irangi lilipata hasara nyingi sana kwa Wamasai, na mara kwa mara Wanyaturu walikuwa hawana budi kujilinda wasipate kushindwa na Wamasai. Lakini Wanyiramba na Wanisanzu wanaokaa nchi ya Mkalama walikuwa salama kwa sababu kuna milima mingi katika nchi zao ikawa kama boma za kuwalinda. Wanisanzu hasa walikuwa salama zaidi maana milima iliyo katika nchi yao ni miamba mikali isiyopandika upesi.

Wamasai walipoanza kwenda kusini zaidi walionana na makabila mengine ambayo hawakuweza kuyashinda, yaani Wangoni na Wahehe. Na siku zile Wazungu walifika nchi hizi, basi kazi yao ya kupigana na kunyang'anya ilikwisha.

Baada ya miaka michache kupita, yaani katika mwaka 1891 ugonjwa wa sotoka, yaani kuhara sana, uliingia katika makundi ya ng'ombe ya Wamasai, na wengi mno walikufa. Wamasai tokea zamani hawalimi mashamba, basi sasa waliona dhiki kabisa, maana damu na maziwa ya ng'ombe ndiyo chakula chao na sasa hayakuwatosha. Walikuwa maskini kabisa, na Wambugwe waliwaingilia wakawaua wengi sana. Wengine walikimbia wakajificha katika nchi za Iringa na Ugogo.

Mzungu mmoja jina lake Baumann aliyeshuhudia taabu iliyowapata Wamasai wakati huo, aliandika maneno haya yanayofuata.

'Watu hao maskini waliotusikitisha sana, walikuwa wakizunguka kambi yetu. Walikuwako wanawake waliodhoofika sana hata wakawa kama mifupa mitupu, na ule wazimu unaoletwa na njaa ulionekana machoni mwao, na watoto wao walifanana na vyura kuliko wanadamu. Wamoran wao waliona taabu hata kwenda jinsi walivyokuwa dhaifu, wakawa wakitambaa chini kwa miguu na mikono. Wazee wenye kichaa cha njaa wakawa taabuni na karibu kufa.

'Watu hao walikula kitu cho chote. Nyama ya mizoga ya punda waliokufa ilikuwa kama karamu kwao wakakubali kwa furaha mifupa na ngozi na hata pembe za ng'ombe.

'Wazazi walitaka kubadilisha watoto wao kwa kipande kidogo cha nyama, na tulipowakatalia walijaribu kuficha watoto wao katika kambi yetu, na wao wenyewe walikimbia. Basi mambo hayo ya kusikitisha na ya huzuni yalikuwa mbele ya macho yetu kila siku katika nchi ya Wamasai.'

Tangu wakati huo Wamasai wamepona, na makundi yao ya ng'ombe yameongezeka sana, tena wamekuwa watu wenye mali nyingi mno. Lakini sasa si kama walivyokuwa, maana wameoana sana na Wabantu wa makabila mengineyo na kwa hivi wanazidi kila mwaka kuchanganyika pamoja nao. Ingawa hata sasa wengi wana sura za Kihamiti, lakini wengi wamefanana sana na Wabantu. Hata sasa Wamasai hufuata desturi zao za kuishi kama zilivyokuwa zamani, na hasa ni wachungaji wa ng'ombe na kwa kawaida hufuata maisha ya kutembeatembea wakitafuta malisho kwa makundi yao.

Sasa tufikiri kidogo jinsi walivyovuta watu wa mabakila mengine kuiga desturi zao na mavazi yao. Watu wa makabila mengine hawakuwaiga sana isipokuwa desturi zao za kivita, na pengine za dini yao. Watu wengi walianza kutumia silaha kama zile walizotumia Wamasai, wakavaa mavazi yao ya kivita. Wachaga hasa walifuata sana desturi hizo katika miaka iliyopita. Kadhalika, watu wengine waliiga namna zao za kusokota nywele na kujipaka udongo ule mwekundu, na jinsi Wamoran wanavyokaa. Wengine walifuata desturi zao za majando, na jinsi wanavyowagawanya hirimu kwa umri wa miaka yao. Lakini katika yote, labda jambo lenye maana zaidi ni kutumia jina wanalotumia kwa kumtaja Mungu, yaani Ngai, na kufikiri kwao juu ya Mungu kwa namna wanavyofikiri Wamasai. Maana kwa kawaida ya makabila mengine ya Wabantu fikira zao juu ya Mungu na uwezo wake hazikudhihirika.

Wamasai hawakujifanya watawala kama vile walivyojifanya wale Wahamiti walioingilia nchi ya Uganda. Walijiweka juu ya makabila mengine yaliyo madogo kama vile Waarusha na Wakahe na Wataveta, lakini makusudi yao ya kupigana hayakuwa ya kushika nchi wapate kuzitawala, ila kunyang'anya watu ng'ombe zao na kupata malisho kwa makundi yao.

Hawakusimamisha ufalme wala kuweka watawala, ila walichafua nchi na kuwasumbua watu mpaka wote walikuwa wakikaa kwa wasiwasi. Tena kwa desturi hawakupigana vita zilizotengenezwa mbele kwa akili na ushujaa. Kazi yao hasa ilikuwa kupigana na Watatoga ambao hata na wao pia walikuwa wakitaka makundi makubwa na ng'ombe na malisho. Kwa kifupi, mwanzo na mwisho wao ni ng'ombe na malisho, basi.

Somo 4-Nchi za Kilimanjaro na Usambara

Mpaka sasa tumesimuliwa habari za Wahamiti hasa, lakini sasa tutasimuliwa habari za makabila mawili ya Kibantu yaliyokaa nchi za kaskazini ambayo yaliendeleza sana mambo huko. Kwanza tuchungue habari za Wachaga wanaokaa nchi za Kilimanjaro.

Zamani sana wale watu wafupi, Wabilikimo tuliowataja, walikaa nchi za Kilimanjaro kama vile walivyokaa nchi nyingine za Afrika ya Mashariki. Walikaa katika misitu minene iliyofunika mlima, wakaenea katika tambarare za chini. Wenyeji wanaokaa sasa mlima wa Kilimanjaro wanajua sana habari za watu wafupi hao, nao huwaita Wakonongo.

Wachaga husimulia kuwa wao walipofika huko waliwafukuza Wakonongo.

Wachaga waliingilia nchi hii kutoka Ukamba na Utaita katika nchi za Kenya, na nchi nyingine za kaskazini. Wakamba wanakaa nchi zilizo katikati ya njia ya gari la moshi inayopita Kenya, na mto uitwao Tana, na zamani walizoea kutembeatembea sana. Katika safari zao walifika hata nchi ya Uzaramo inayozunguka Dar es Salaam na hapo walipigana na Wadoe wakawashinda. Imesemwa ya kuwa baadaye Wakamba walipigwa na kushindwa na Wazaramo waliotoka nchi pande za Morogoro, yaani na Pazi Kibamanduke, ambaye alipewa jina la Pazi Mwingakamba, maana yake Pazi aliyefukuza Wakamba.

Wengine wa ukoo wa watawala wa Kichaga wanaweza kuhesabu vizazi kumi na tano tangu walipofika wazee wao katika mlima Kilimanjaro, na kwa kuwa wao hawakuwa wa kwanza waliokaa kule mlimani, tunaweza kukisia kuwa watu wamekaa Kilimanjaro tangu zamani za miaka 300 au labda 500. Kwanza watu hao hawakukaa wote pamoja, ila kila kabila lilikaa na jamaa zake zimetengwa mbali mbali. Lakini baadaye wakubwa wa jamaa nyingine walijifanya wakubwa wa jamaa zote zilizokuwa jirani nao, na hivi mambo yaliendelea pole pole mpaka nchi zote za mlima ziligawanywa kuwa nchi ndogo 30 na wazao wengine wa watawala waliotawala nchi hizo wanatawala mpaka leo. Siku zote wakubwa hao walipigana wenyewe kwa wenyewe lakini tokea mwaka 1800, kwa kawaida mmoja au wawili walijifanya kuwa wakubwa wa mlima wote au mkubwa wa sehemu moja, maana wakati huo mlima uligawanywa katika sehemu tatu. Upande wa kaskizini magharibi uliitwa Hai, sehemu ya kati iliitwa Vunjo na upande wa mashariki kwa kaskazini uliitwa Rombo; lakini watu hawakupenda kukaa upande wa kaskazini.

Ufalme mkubwa wa kwanza ulisimamishwa katika nchi ya Mamba iliyo upande wa mashariki wa miteremko ya Kilimanjaro. Ufalme huo ulisitawi ukawa na nguvu sana wakati alipotawala mwanamke mmoja jina lake Mashina. Lakini Mashina alipigwa na kushindwa na yule Rongoma tuliyemtaja tuliposimulia habari za Wamasai. Halafu Rongoma alishindwa na Horombo, na nchi yake yote ilichukuliwa. Tumekwisha hadithia habari za vita za Horombo alizopigana na Wamasai. Basi, Horombo alitawala nchi nzima ya Rombo na Vunjo, lakini hakujaribu kuteka upande wa magharibi kwa sababu Rengwa aliyekuwa mkubwa wa Machame alikuwa amejifanya mkubwa wa huko. Basi ikawa nchi za Kilimanjaro zilitawaliwa na watawala wawili wenye nguvu nyingi, na wakati huo ulikuwa mwaka 1800 mpaka 1825, yaani wakati ule ule wa vita aliyopigana Horombo na Wamasai.

Horombo alipokufa nchi hizo ndogo ndogo alizoziunganisha pamoja zilitengana, na kwa hiyo ufalme mkubwa ulivunjika ukabaki ule wa upande wa magharibi uliotawaliwa na Rengwa. Ufalme wa Rengwa uliendelea kuwa na nguvu kwa siku nyingi na hata uliporithiwa na Mamkinga mwanawe Rengwa, na Ndeseruo mwanawe Mamkinga, ulisitawi sana.

Wakati huo alipotawala Mamkinga, ulikuwa karibu na mwaka 1848, maana katika mwaka ule Mzungu mmoja wa misioni jina lake Rebmann alifika Kilimanjaro, na katika mwaka 1849 alifika tena. Katika nchi ya Vunjo alipokewa vizuri na Masaki mtawala wa Kilema, akapendezwa sana na majeshi yake namna yalivyofundishwa, na jinsi ufalme wake ulivyokuwa imara. Wakati huo Masaki alikuwa akipigana vita ndefu tena kali na jirani yake Ndaalio mtawala wa nchi ya Marangu.

Yule Rebmann alikwenda kumtazama Mamkinga mtawala wa Machame, lakini huko hakupokewa vizuri ila alinyang'anywa mali zake akafungwa mpaka alipoweza kujiponya kwa kukimbia.

Tokea mwaka 1855 mkubwa mmoja aliyejulikana sana ni Rindi mtawala wa Moshi, jina lake jingine aliitwa Mandara. Katika mwaka 1861 msafiri Mdachi mmoja jina lake Van der Decken alionana na Rindi, akasimulia kuwa wakati huo alikuwa kijana mzuri mwenye umri wa miaka 20 kama hivi. Imedhaniwa kuwa karibu na wakati huo, Rindi alianza kupigana vita na watawala wengine, akajifanya mkubwa wa Vunjo na sehemu kubwa ya Rombo, tena alitwaa nchi nyingine iitwayo Mbokomu iliyo upande wa magharibi wa Moshi. Kwa kwaida, wakubwa hao waliposhinda wengine, waliwaachia nchi zao wazitawale chini yao.

Rindi aliingilia nchi za Upare na Ushambala vile vile kwa vita, tena yasemwa kuwa alifanya vita na Wamasai wa Loita. Lakini wakati ule ule alipokuwa na nguvu zaidi alipatwa na ajali.

Karibu na upande ule wa mlima unaoitwa Rombo, kuna nchi iitwayo Useri, na mpaka wakati huo ilikuwa bado haijashindwa, na hata Horombo alishindwa kuiweka chini yake. Basi Rindi alikusudia kuishinda, akakusanya jeshi lake lote, likapata watu idadi ya 4,000 kama hivi. Lakini hakufuata desturi yake ya kuongoza jeshi lake yeye mwenyewe, na tena hakutengeneza mambo ya vita kama ilivyokuwa kawaida ya vita zake. Jeshi lake liligawanywa sehemu mbili, na sehemu moja ilipigwa vibaya sana na watu wakaanza kuingiwa na hofu, hivi sehemu zote mbili zilikimbia ovyo, ikawa watu wa Useri pamoja na watu wengine wa Rombo wakawafuatia mbio. Watu wachache tu wa jeshi zima walichopoka.

Tangu zamani Rindi na Ndeseruo mtawala wa Machame walipatana sana; tena walisaidiana katika vita nyingine, na hasa katika vita za nchi za mbali kama vile zilizopiganiwa Usambara. Lakini hapo nguvu za Ndeseruo zilianza kupungua kwa sababu wakubwa wa nchi ya Kibosho iliyo jirani na Machame, walikuwa wamejibagua kusudi wajipatie nguvu zaidi katika nchi zao. Basi kuona nguvu za Rindi imevunjika, Lokila mtawala wa Kibosho alimshambulia, na kwa kuwa hakuweza kujitetea, Rindi alikimbia. Kwanza alikimbilia Kahe akakaa huko kwa muda; lakini baadaye alifanya mapatano na Waarusha wakakubali kumsaidia apate tena nchi yake. Wakati huo Lokila amekwisha kufa na kwa muda wa miaka michache hapakuwa na mtawala mwenye nguvu nchini Kibosho. Basi hivyo Rindi alikuwa na raha, maana yule aliyekuwa akishindana naye sana amekwisha kufa, na Ndeseruo alidumu kupatana naye, maana ndiye aliyemficha nchini Machame kwa muda kabla hajaweza kurudi tena Moshi.

Rindi aliporudi Moshi alianza kuzifufua nguvu zake, akaenda kushambulia mtawala kijana Mareale wa Marangu katika Vunjo, akamfukuza. Huku nyuma Ndeseruo alimweka rafiki yake Sina awe mtawala wa Kibosho, lakini Sina alimlipia ubaya, maana Ndeseruo alipokufa Sina aliipiga nchi ya Machame akaitwaa.

Sasa ikawa vita iliyoendelea sana kati ya Sina na Rindi, na na pengine upande wa mmoja ulikuwa kama ushindao, na pengine upande mwingine ulikuwa kama ushindao, lakini hapana mmoja aliyeshinda kabisa.

Katika mwaka 1888 Rindi alianzisha shambulio lake la mwisho kujaribu kumpiga Sina, akasaidiwa na Wamasai wengine, lakini kwa kweli hawakumsaidia kitu, na ndio hasa walioharibu vita yake asiwashinde watu wa Sina. Baada ya kupita miaka miwili Rindi aliwasaidia Wadachi kupigana na Sina, na Sina alishindwa. Katika mwaka 1891 Rindi akafa. Hapana mtawala aliyejulikana mahali pote nchini humu kama vile alivyojulikana yeye, na jina lake lilijulikana hata Ulaya. Rindi aliwajua Wazungu wote waliofika Kilimanjaro, na wote walimkiri kuwa mtawala wa Wachaga.

Alipokuwa mtoto alionana na Rebmann, na alipokuwa kijana alionana na Van der Decken. Katika mwaka 1873 Mwingereza msafiri mmoja, jina lake Joseph Thomson alikwenda kumtazama akapokewa vizuri sana. Katika mwaka 1884 Mwingereza mmoja msafiri maarufu jina lake Sir Harry Johnston alikaa huko kwake muda wa miezi sita, akamsaidia kuitetea nchi yake ilipojiwa kushambuliwa na watu wa Kibosho, tena ameandika habari zake na kueleza mambo yote vizuri sana. Rindi alimwomba Johnston ampe bendera ya Kiingereza, lakini Johnston alikataa kwa sababu aliona labda ataitumia katika safari zake za kuteka watumwa, na hivi bendera ya heshima itapata aibu. Ndipo Rindi alipotaka kujiweka chini ya Sultani wa Unguja, lakini katika mwezi wa Mai 1885 Mdachi mmoja jina lake Juchlke alimshauri kujiweka chini ya utawala wa Wadachi akakubali.

Rindi alipewa heshima moja ya ajabu, maana kwa wakati huo, aliletewa pete kutoka kwa malkia wa Waingereza, yaani Queen Victoria . Alikuwa mtu hodari sana mwenye maarifa mengi ya vita, na imesemwa kuwa watu wake walimpenda mno. Ingawa watawala wengine walishindana naye, lakini kwa kweli alikuwa mtawala mkubwa wa nchi za Kilimanjaro mpaka mwisho wa maisha yake, naye alitawala nchi kwa muda wa miaka 30.
****
 
Sura ya 3 inaendelea. . .

Somo 5-Kuendelea na habari za nchi za Kilimanjaro na Usambara

Wachaga husimulia habari za watu wanaoitwa Waumba au Waomba waliotoka kwa wingi katika nchi ya Usambara wakaenea katika nchi yote ya Kilimanjaro, wakaendea upande wa magharibi. Wengine husema walikwenda Sonjo, na wengine husema walikwenda Ufiome. Maneno hayo yaelekea kuwa ya kweli, maana tunajua kuwa Wafiome ni Wahamiti na Wosonjo hudai ni jamaa wa Wasegeju waliotoka nchi za kaskazini, nao hudhaniwa kuwa ukoo mmoja wa Wagala.

Tena tunajua kuwa katika mwaka 1500 na miaka iliyofuata karibu, Wasegeju walikuwa wakikaa katika nchi za ujirani na Malindi upande wa nchi ya Kenya. Maana hapo walisaidia sana Wareno ili kuitetea nchi iliposhambuliwa na Wazimba waliokuja kutoka nchi zinazozunguka mto Zambezi. Lakini tutasoma habari hizi baadaye.

Wazimba hao wanadhaniwa kuwa jamaa za Wazulu na wazao wao ni Wangoni wanaokaa katika nchi yetu sasa. Wakati huo walikuwa na nguvu nyingi maana hata Wareno walikuwa wakiwalipa kodi.

Hawa Waomba bila shaka walikuwa Wasegeju, na wengine wao walibaki wakakaa nchi iliyo karibu na Tanga, lakini wengi walipita kwa nguvu katika nchi za Usambara na Kilimanjaro mpaka Sonjo. Katika mwaka 1596 Wareno waliwakuta Wasegeju Malindi, na labda Waomba waliingia nchi ya Kilimanjaro katika miaka iliyo karibu na mwaka 1700. Huko waliacha alama ambazo zinashuhudia kuwa walipita, maana waliweka chungu ya mawe mfano wa minara. Yasemwa waliweka chungu ya mawe hivyo kila mahali walimofanya kambi, nazo huonekana vivyo hata leo.

Tena, nchini mwa Wamasai yapo maboma ya kuzuilia maji na mifereji ya maji, na mashimo ya zamani yaliyofukuliwa katika mawe kwa juu kusudi la kuwekea maji, lakini siku hizi hayatumiwi. Wamasai husema hayo yalitengenezwa na wale watu wanaoitwa Waomba, tena husema walipita wakaenda upande wa magharibi, yaani maneno yao yanapatana na maneno wanayosema Wachaga. Katika nchi za kaskazini mwa Ukamba nchini Kenya, kuna mashimo yaliyofukuliwa juu ya mawe kama yale yanayoonekana katika nchi ya Wamasai, na huko watu husema kuwa yalitengenezwa na Wagala, yaani watu wa taifa lile lililofikiriwa kuwa ndiyo asili ya Wasegeju. Mpaka zamani za miaka 100 Wagala walikuwa wakikaa nchi hizo. Basi mambo haya yaelekea kushuhudia kuwa hao Waomba ni wale wanaoitwa Wasegeju, nao ni mbegu zile zile za Wagala.

Watu hao ni dhahiri kuwa si Wasambara wa siku hizi, maana tumeambiwa ya kuwa Wasambara walipofika waliikuta nchi haina watu, na hata Upare ilikuwa haina watu. Labda Waomba waliwaua watu waliokuwa wakikaa huko zamani wakati walipopita, lakini hatuwezi kuhakikisha hayo.

Wakubwa wengine wa jamaa za Wachaga na hasa ile ya Watawala wa Machame na Moshi walitoka Usambara, nao walikuwa miongoni mwa watu wa mwisho kufika nchi za Kilimanjaro. Neno wanalotumia kwa mtawala, yaani Mangi, husema ni Kisambara, nalo husaidia kuthibitisha asili yao.

Wasambara na Wabondei ni Wazigua kwa asili yao. Hapo zamani Wazigua walikuwa kabila kubwa kuliko lilivyo sasa, tena walikuwa na makundi makubwa ya ng'ombe. Lakini ugonjwa uliingilia makundi yao na ng'ombe wengi walikufa. Tena Wazigua walikuwa na desturi ile hafifu ya kuwaua watoto wao wengine, yaani wale wanaoitwa vigego, na hivi kabila zima lilikuwa karibu kufutwa. Lakini hata hivyo, katika wakati uliopita karibu Wazigua waliogopwa sana, maana walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupata bunduki, na hivi waliweza kushinda na kuwafukuza Wadoe waliosifiwa sana zamani kwa sababu ya nguvu zao. Wadoe ni kabila linaloachana kidogo na makabila mengine yaliyo jirani nalo, maana wana desturi nyingine zisizoonekana katika nchi hizi za Afrika ya Mashariki ila ya Magharibi, yaani West Africa. Bwana mmoja jina lake Brunner asema kuwa katika mwaka 1886, sehemu ya kabila hilo la Wadoe ilihama kwenda upande wa kaskazini kupita Mombasa, na huko watu wake walichanganyika na makabila mengine.

Zamani, nchi ya Wabondei ilienea kutoka hapo walipo sasa mpaka mto Umba ulio mpakani mwa nchi ya Kenya na nchi yetu Tanzania.

Tumesema kuwa Wasambara na Wabondei na Wazigua kwa hakika walikuwa kabila moja zamani, na hata leo lugha zao zimefanana sana. Lakini huko Usambara liko kabila moja dogo lililo geni kabisa. Kabila hilo ni Wambugu, na kwa asili ni Wakwavi.

Watu hao walitoka katika nchi za tambarare zinazozunguka milima ya Nguu, wakaja kukaa milima ya Upare. Labda walipokuja hapakuwa na watu Upare, lakini baadaye walionana na Wabantu waliokuja kutoka Utaita wakachanganyika pamoja, na sasa ndio wanaoitwa Wapare. Katika nchi za kusini mwa Upare, Wakwavi au Wambugu hao hawakuchanganyika na Wabantu mpaka katika wakati wa njaa kubwa iliyotokea zamani za vizazi vitatu au vinne, ndipo walipohama kwenda Usambara. Safari yao ya mwisho ya kuhama ilikuwa katika mwaka 1887.

Sasa lazima tuchungue kidogo habari za kabila moja, au kwa kweli si kabila ila ni jamaa au ukoo, lililokuwa na asili ya kigeni. Imehadithiwa ya kuwa zamani Mwarabu mmoja alikaa kilima kinachoitwa Kilindi ambacho kipo kaskazini mwa Nguu si mbali na Handeni. Hatujui kama alikuwa Mwarabu asiyechanganyika na damu ya Wabantu, maana lazima tukumbuke kuwa Waarabu walifika wakakaa katika nchi za pwani tokea mwaka 689. Basi alioa wanawake wa kienyeji, yaani Wabantu, na watoto wao waliitwa Wakilindi. Basi hata leo wazao wao hujulikana kwa jina hilo. Pengine hata siku hizi watu hao wanatambulikana kwa alama za umbo kwa sababu ni weupe kidogo na sura zimefanana na sura za Waarabu, lakini wengi ni kama Wabantu wenzao.*

*Kuna kitabu kikubwa chenye historia ya kabila hilo: HABARI ZA WAKILINDI bei yake Sh. 15/-. Kimetolewa na E.A. Literature Bureau.

Mwanawe au mpwawe Mwarabu huyo aliitwa Mbega, akahama kwenda nchi ya Ushambala. Hapo aliona wenyeji wametengana katika ujamaa na kukaliana kwa uadui, wakipigana wenyewe kwa wenyewe siku zote. Mbega alikuwa mtu hodari, tena mwenye nguvu na busara, na kwa upesi alipata kujulikana na watu wa nchi nzima kwa sababu ya ustadi wake kuwinda na mbwa wake, na tena kwa sababu alijitahidi kuwapatanisha wakae vizuri. Basi ikatokea hatimaye walimfanya kuwa mtawala wao.

Mbega alipokufa Bughe mwanawe alirithi utawala, na yeye alipokufa Shebughe alitawala.

Shebughe aliuawa katika vita aliyofanya na Wazigua, na Kimweri mwanawe alirithi utawala. Huyo Kimweri alikuwa mtu mwenye maarifa mengi sana katika kazi ya utawala, akasitawisha nchi yake, akaziteka nchi za Wabondei na sehemu kubwa ya Uzigua akaziweka chini ya utawala wake. Tena aliteka Upare na nguvu zake zilienea sana hata watu wa miji ya Tanga na Pangani walitii amri zake.

Yule Mzungu Krapf, tuliyemtaja, alikwenda kumtazama Kimweri katika mwaka 1848 akaandika habari za safari yake. Asema Kimweri aliitwa Simba Mwene, akawa mtu mkubwa kama mfalme hasa na tena alikuwa kama simba kweli kweli kwa uhodari.

Katika mwaka 1857 yule Mzungu mwingine Burton tuliyemtaja, alikwenda Vuga apate kuongea na Kimweri, lakini wakati ule amekwisha kuwa mzee, alimkuta mkongwe kabisa, mwembamba, na tena dhaifu sana hata hakuweza kuondoka kitandani bila msaada wa watu wake.

Katika mwaka 1867 au 1868, yule Mzungu wa Misioni ya U.M.C.A. jina lake Alington, alikwenda kufanya shauri naye apate mahali pa kuanzisha Misioni. Lakini alimkuta anaugua ndui, akafanya shauri na mjukuu wake jina lake Shekulwavu, ndiye aliyempa ruhusa kuanzisha misioni Magila.

Kimweri alikufa katika mwaka 1869 mwenye umri wa miaka 70 au zaidi. Mkande, mwanawe Kimweri alikufa kabla ya kufa baba yake, na katika uzee wake Kimweri alimfanya Shekulwavu mjukuu wake, yaani mwanawe Mkande, kuwa mrithi wake na mtawala wa nchi.

Aliporithi utawala Shekulwavu alitwaa na jina la Kimweri wa pili, maana ndivyo alivyousia Kimweri, Mtoto wa Kimweri aliitwa Shebughe na mtoto wa Shebughe aliitwa Kimweri na watoto wao walifuata utaratibu huu wa daraja.

Ilikuwa kawaida ya watawala wa Vuga kutawala nchi yao kwa kuweka watoto wao katika utawala wa sehemu za nchi zilizo chini yao na kumbe hivi ndivyo namna nchi ilivyoharibika. Maana hao watoto walijibagua na kujifanya wakubwa. Katika habari za nchi nyingine ni hivyo nchi zilivyoharibika vile vile; maana mara nyingi hutokea jamaa waliowekwa kuimarisha nchi huiharibu, na hasa kama yule anayetawala ni mtu dhaifu.

Mambo hayo yalikuwa yamekwisha anza wakati alipotawala Kimweri. Maana alipokuwa mzee dhaifu mwanawe Semboja alianzisha fitina akakusanya makundi ya Wazigua na watu wa pwani, akamwasi baba yake. Mara alipokufa Kimweri, Semboja alishambulia Vuga na Kimweri Shekulwavu alikimbilia Bumbuli. Hapo Kimweri Shekulwavu aliwaita wafuasi wake wote kwenda kumsaidia, na labda wangalimshinda Semboja, maana watu wake hawakumpenda, lakini Kimweri Shekulwavu aliumia vitani kwa bunduki yake kupasuka ikamkata mkono; katika kuuguza mkono akafa.

Kimweri Shekulwavu alipokufa, mwanawe Kinyasi alikuwa bado kijana, na kwa kuwa watu wake hawakuwa na mkubwa mwenye nguvu wa kuwaongoza vitani, basi hakuweza kupigana na Semboja. Lakini hawakukubali kukaa chini yake, na watu wengi walihama kwenda kukaa milimani Upare. Mambo hayo yaliendelea, na wakubwa wengine walijibagua na kujifanya watawala, na wenzao walianzisha vita kati yao na Semboja. Semboja hakutawala ingawa Wakilindi walimchagua yeye, alimweka mwanawe kutawala mahali pake, kwa sababu alisema mimi si mahali pangu kutawala mahali pa mpwa wangu Shekulwavu. Basi Semboja alimweka mwanawe Kimweri kuwa mtawala wa Vuga, na yeye mwenyewe alikwenda kutawala nchi yake Masinde ndio mji wake mkuu.

Wakati huo Wadachi walifika nchi hii, na pia wakati huo Mwarabu mmoja jina lake Mbaruku bin Rashidi, aliyekuwa wa jamaa ya Mazrui ambayo tutasoma habari yake baadaye, alidai kuwa nchi za pwani zote zilizo kati ya Gasi na Mombasa ni zake akawapa Wadachi hizo nchi katika mwaka 1886.

Lakini Sultani wa Unguja vile vile alidai kuwa nchi hizo ni zake, na mara aliposikia zile habari za kuwapa Wadachi nchi zake, alipeleka jeshi kupigana na Mbaruku. Lakini Mbaruku hakungojea vita, ila alikimbilia bara. Kinyasi mwanawe Shebuge alifanya ujinga sana, akampokea Mbaruku akajitia upande wake; hivi alijiingiza ugomvi na Sultani wa Unguja. Basi Mbaruku alikimbia ikamlazimu Kinyasi kukimbilia Kipanga mjomba wake, ambaye alikuwa amejibagua na Semboja, na kuweka ufalme wa peke yake. Matata hayo yaliongezwa na Rindi mtawala mkubwa wa Moshi, maana wakati huo huo majeshi yake yaliingilia nchi ya Usambara yakavuruga mambo na kuteka mali. Basi kwa muda nchi yote ilichafuka.

Wadachi walipojiweka imara nchini humu, Usambara ilikuwa imegawanywa sehemu sita, na watawala sita walikuwa wakitawala, maana utawala wa Wakilindi umekwisha vunjika nchini Uzigua na Ubondei na Upare. Chini ya utawala wa Wadachi, jamaa hiyo ya Wakilindi walizidi kuvunjika, na ufalme wa Vuga ulikuwa kusanyiko la wakubwa wa Wakilindi tu.

Katika mwaka 1926, Kinyasi mwana wa Shekulwavu aliwekwa Vuga na serikali ya Waingereza akatawala kabila zima la Wasambara. Lakini Kinyasi hakutawala kwa muda mrefu na mwanzoni mwa mwaka 1929, alijitoa katika utawala na wakubwa walimchagua Bila mwana wa Kimweri yule aliyekuwa mwana wa Semboja.
Mwisho wa Sura ya tatu.
 
Back
Top Bottom