Kiukweli huyu mchezaji wa soka zamani Alphonce Modest anahitaji msaada

Kiukweli huyu mchezaji wa soka zamani Alphonce Modest anahitaji msaada

REJESHO HURU

JF-Expert Member
Joined
Mar 6, 2014
Posts
4,664
Reaction score
9,929
Unaeweza tazama maswahibu anayopitia Mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania na vilabu vya Mtibwa Sugar, Pamba, Simba na Yanga.

Screenshot 2024-11-02 at 09.02.29.png

Hapa tunamzungumzia, Alphonce Modest, beki aliyesifika kwa kukaba kwa nguvu na akili, kupandisha timu kwa kutengeneza mashambuliaji na kupiga krosi zilizozalisha mabao enzi akiupiga uwanjani.

Leo hii ukimuona alivyolala kitandani akiugulia, huwezi kumtambua kwa haraka kama ndiye Modest. Na ukiwa na roho nyepesi kwa hakika ni lazima machozi yatakutoka kwa simanzi na uchungu.


View: https://youtu.be/R8pxbM8GR7Q

Hali ya kiafya kwa beki huyo aliyewatia tumbo joto mawinga na washambuliaji wasumbufu enzi akicheza ndani na nje ya nchi, imebadilika sana; maisha yake sasa yamehamia kitandani. Anaishi maisha tofauti kabisa na yale alioyokuwa akiishi enzi akiwa na nguvu zake na kupapatikiwa na timu mbalimbali.

Unaweza ukashangaa, lakini ni uhalisia kwamba ni miaka mitano sasa imepita tangu alione jua au kufahamu kinachoendelea nje ya mlango wa chumba anakolala mkoani Kigoma.

Kwa wanaomfahamu, Modest aliyekuwa akipamba viwanja vya soka, akiwafurahisha mashabiki kwa ustadi wake, leo ni mtu tofauti kabisa. Sura yake imebadilika, nguvu alizokuwa nazo enzi hizo hazipo tena. Ni sauti pekee ikisikika inayoweza kumfanya yeyote akumbuke ustadi na heshima aliyokuwa nayo uwanjani.

Screenshot 2024-11-02 at 09.01.02.png


Imepita miaka zaidi ya 14 tangu Modest aache kucheza soka, timu ya mwisho ikiwa Mtibwa Sugar ya Manungu, Morogoro ambako ugonjwa wake ndipo ulipoanzia na kuuchukulia kama utani kabla ya kumlaza.

Ugonjwa uliomlaza kitandani ulianza taratibu kama masihara, lakini sasa umefikia hatua mbaya zaidi ambayo kuielezea yataka moyo. Katika toleo la kesho nitajaribu kukupa picha halisi. Itakupa uchungu mkubwa zaidi na kusadiki hiki ninachokieleza ni kweli kimemtukia beki huyo nyota wa zamani wa Tanzania.

Aliyekuwa nguli uwanjani sasa anaishi kitandani, akiwa na matumaini kwamba ipo siku ataona jua kwa mara nyingine. Ingawa inafika wakati anatamani hata angepumzika mbele za haki asisumbue watu.

Safari yangu kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, umbali wa kilomita 1,088, haikuwa rahisi. Gari niliyokuwa nikisafiria liliharibika kabla ya kufika Mlandizi, na ilinichukua muda mrefu kufika Kigoma. Lengo langu kubwa lilikuwa kumuona Modest. Beki shujaa wa zamani, ili kuelewa hali yake baada ya ukimya wa miaka mingi.

Modest sasa anaishi maisha ya faragha tofauti kabisa na alivyokuwa akiwasha moto viwanjani. Sura yake imebadilika kiasi kwamba hata marafiki wa zamani wanapata ugumu kumtambua. Yeyote anayemwona kwa mara ya kwanza atapata huzuni, kwani hali aliyokuwa nayo shujaa huyu wa zamani imebadilika kuwa ya maumivu makali ya muda mrefu.

Screenshot 2024-11-02 at 09.01.59.png

Katika nyumba ya Baba yake ndipo anapoishi hapa Kigoma. Nyumba hiyo ipo Mwanga Kisangani, mitaa iliyo na majengo na mitaa kama yale ya Tanga mjini.

Ukiingia hapa kwao kuna geti la mabati yaliyochakaa, na ndani ya geti hilo kuna nyumba mbili za rangi nyeupe. Modest ni kifungua mimba kati ya watoto 10, kutoka katika familia ya mzee Modest Songoro na marehemu mkewe Leah.

Nilipokelewa na mdogo wake huyo (Agustino), ananionyeshea geti la mabati na kusema usishangae nikikwambia tutaingia ndani ya lile geti, huenda ulitegemea utakutana na bonge la nyumba, ila uhalisia wa maisha yetu ndio huo.

“Karibu usiogope, unasubiriwa kwa hamu na baba, wajomba na mdogo wangu Teddy, ujio wako utatupa mwanga, baada ya kukaa gizani kwa muda mrefu.

“Samahani sikukwambia ukweli wakati nawasiliana na wewe ukiwa Dar es Salaam, kaka Modest hataki kabisa mahojiano, ila familia inahitaji jamii ifahamu kuhusiana na changamoto zake, ikiwezekana kupata msaada wa pesa za matibabu na mahitaji mengine.

“Amekata tamaa kabisa na laiti mikono yake ingekuwa inafanya kazi huenda angekuwa amejizuru kitambo, kwani muda wote kinywa chake kinatamka kifo na ndio maombi anayokuwa anayaomba kwamba afe.

“Utatakiwa kupambana ili kufanikisha kuzungumza naye, kwani kuna waandishi wa nje ya Tanzania, walifika hapa nyumbani, lakini aliwakatalia na waliondoka bila kuambulia kitu.”

Baada ya kusalimiana na baba yake Modesti (bado anaonekana mzee kijana) pamoja na ndugu zake, niliingia ndani kwenye chumba mgonjwa. Chumba hicho kina mwanga wa wastani na sakafu ya kawaida, lakini kitandani, mtu mwenye mwili mdogo amelala. Ukikadiria kwa macho kama ana kilo nyingi sana ni 50.

---

Huyu ndiye Alphonce Modest ambaye enzi zake akikiwasha uwanja alikuwa mwamba mwenye afya na nyama za kumtosha. Alinisalimia kwa kufungua mdomo wake na kunipa ishara kwa kope za macho. Sura yake imepoteza nuru, na mwili wake ni dhaifu hawezi kufanya kitu chochote. Muda wote upo ndani ya shuka. Kichwa chake na macho ndivyo tu vinavyoonyesha uhai wake. Na muda wote amekiinua juu akitazama kwenye bati au tivii.

Mikono yake na miguu imepinda katika umbo la zigizagi, na mwili wake umepungua sana. Umbo lake la mwili limepoteza kabisa uhalisia wa yule staa aliyewahi kung’ara uwanjani.

Muda mwingi hawezi kujisogeza, ni kichwa na macho tu ndivyo vinavyoweza kujitikisa tena si muda wote. Anaweza kutulia na kuangalia jambo moja kwa muda mrefu kwa hisia kubwa.

Chumbani kwake kuna televisheni ndogo, ambayo mara nyingi huitumia kuangalia mechi za Ligi Kuu ya Tanzania. Ingawa hawezi kutoka nje, anajua kinachoendelea kwenye ligi ya Tanzania. Kumbukumbu zake ziko vizuri, na bado anakumbuka mambo mengi ya maisha yake na soka. Hata hivyo, hawezi tena kunyanyuka kitandani, wala kwenda viwanjani kushuhudia mchezo anaoupenda.

Maisha ya Modest yamebadilika na sasa yana huzuni. Amekuwa mfungwa wa kitanda kwa miaka mitano, akiwa na maumivu na upweke mwingi. Kwa yeyote aliyemfahamu, hali ya sasa ya Modest inatia huzuni, lakini bado anakumbukwa kwa ustadi na moyo wake wa kupenda mpira.

STORI ZILIPOANZIA

Baada ya kumsalimia na kunijibu nikaona kama inzi wanamkosesha raha kwenye uso na anatokwa jasho nikataka nimfute akaniambia hapana, niitie mtu hapo nje.

Ndani ya stori nikagundua Modest yapo mambo aliyoyapitia ambayo jamii haijui na hataki kupata aibu ya kushambuliwa katika mitandao ya kijamii pindi atakapoonekana anaomba msaada.

Lakini bila kificho anahitaji msaada wa hali na mali na hata ndugu zake wanaomba jamii na wadau wawasaidie.

Baada ya kujitambulisha Modest anajibu kwa kuhoji; “Nimefurahia kuwafahamu, lakini hapa mmefuata kitu gani, sina taarifa na ujio wenu, ama mmepita kunisalimia tu kwa vile mpo na mambo yenu katika mkoa huu?”

Ghafla baba mzazi wa nyota huyo wa zamani, Modesti Songoro anadakia na kumjibu kijana wake; "Ujio huo ni kwa ajili yako na familia kwa ujumla. Mwanangu mimi nimezeeka, sina nguvu ya kupambana kupata pesa ya kukutibia, ndio maana nataka Watanzania wajue, ikitokea watakaoguswa na changamoto yako watushike mkono, angalau tuwe tunapata pesa za dawa ukijisikia vibaya, kama mzazi naumia sana kukosa pesa za kukutibia.”

Modest akajibu; “Baba mnajua kabisa sitaki hayo mambo, kwa nini mnawasumbua watu wanatoka Dar es Salaam, humuoni kama mnawaingiza hasara kwa gharama walizotumia.”

Kabla ya maongezi mengine kuendelea, nikamuomba Modest tusalia kwanza. Jambo hilo linaonekana kumfurahisha na kuridhia. Nami, bila ajizi, nikaomba Mungu kwa takribani dakika tano.

Kitendo hicho, kilimstaajabisha Modest na kukiri kwamba hajawahi kuona kokote katika maisha yake na wanahabari.

“Hii ni mara ya kwanza, kuona mwandishi anasali kabla ya kuanza kazi yake, niseme ukweli umenishangaza sana,” anasema huku uso ukiwa umechanua kwa bashasha, kisha zikaanza stori za hapa na pale za kimaisha, kutiana moyo, kuchekesha, zilizochukua takribani kwa saa tatu, huku ndugu zake wakiwa wanachungulia kupitia dirishani, wakiwa hawaamini kinachoendelea.

Baada ya stori kuanzia kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi 7:00 mchana, Modest akaonyesha utayari wa kukubali mahojiano, yaliyochukua muda wa saa mbili na ukijumuisha na zile saa tatu za stori za hapa na pale za kuvutiana kasi, ni kwamba Mwanaspoti lilikaa na Modest kuchukua muda wa takribani saa tano kumalizana naye.

KAULI YA AWALI
Modest anaanza, kufunguka kwa kusema ukweli nyie wanawake ni wanyama sana, mliokosa huruma na utu. Akaulizwa kwa nini unasema hivyo? Akajibu “Tuachane na hayo dada yangu, tuendelee na mengine.”

Kabla ya kuanza kuulizwa maswali, akatoa kauli nyingine “Unaona mazingira haya, mtu akija hapa anaondoka na picha gani ya kuwaambia watu, kwa jina langu lilivyokuwa kubwa, watu wanaweza wakawa wanaongea kila wanachojisikia, nina watoto ambao sitaki wapitie magumu ya kuona natukanwa mtandaoni, ndio maana hujawahi kuona nafanya mahojiano tangu nije Kigoma.

“Kuna wakati nikimtazama baba yangu ameinamisha kichwa najua anawaza siku nikifa mikononi mwake na kunizika badala ya mimi baba yangu anifie mikononi mwangu nimzike, kuna wakati akitaka kunilisha najikaza nisimuonyesha kwamba naumia ila nawaza nilipaswa kumtunza yeye na siyo kunitunza mimi, najikuta najiuliza maswali mchana na usiku yanayokosa majibu, sijui huko nje nini kinaendelea, wanapataje pesa ya kuhakikisha mimi nakula.

“Nafanya mahojiano ili kumpa amani Mzee na mjomba wangu, najua wanaumia kwa ajili yangu.” Kisha anakaa kimya kama dakika kadhaa akitafakari huku macho yake yakiwa yamejaa machozi anayoyazuia yasidondoke.

Licha ya mwili wa Modest, kutoka shingoni kwenda chini ukiwa haujiwezi, miguu yake anaweza akaitingisha lakini haiwezi kusimama wala kufanya chochote, pamoja na hayo yote bado akili yake imesimama kama kiongozi dhidi ya wadogo zake, kuhakikisha wanakwenda katika njia sahihi, misimamo yake mikali, hapendi kuendeshwa licha ya kuwa kitandani, anasimamia kile anachokiamini, bila kujali wengine wanamchukuliaje.

ITAENDELEA...
 
Hizi team zetu kubwa kusaidia watu kama hawa kama taasisi kubwa na pesa na uhakika sio issue. Hata kama mtu ana akiba miaka 14 kuumwa sio mchezo.
Msaada ni msaada tu, unategemea na moyo wa mtoaji. Ulishawahi kusikia wapi mwajiri wa zamani anahangaika na aliyekuwa mfanyakazi wake?
 
Waweke utaratibu mzuri tu hilo mbona jambo dogo kaka, naskia alikua mwanasimba kipindi hicho anacheza sasa taasisi ya Simba, Familia yake binafsi na wanasoka aliocheza nao kipindi waseme tufanye hivi baaas tumsaidie jamaa
Nadhani wamesikia....utaratibu mzuri watu tutachanga.....atapata vizuri tu alikuwa kitasaaaa hasaa...
 
Mtu mmoja basi angeweka kwa muhtasari ni nini hasa kinahitajika ili basi kama ni Wadau washiriki kwa njia mbalimbali kwani msaada sio pesa pekee.
 
Back
Top Bottom