Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
Novemba 21, 2024 huko katika kizuizi cha Polisi [Police Check Point) kilichopo mpakani Kijiji cha Igawa wilaya ya Mbarali, Jeshi la Polisi liliwakamata Shamim Maxwell [37] na Itika Bugale [36] wote wakazi wa Uyole Jijini Mbeya wakiwa na dawa za kulevya aina ya Bhangi Kilogramu 33.5
Watuhumiwa walikamatwa wakiwa wanasafirisha bhangi hiyo wakitokea Uyole kuelekea Dar es Salaam wakiwa abiria kwenye Gari yenye namba za usajili T.792 EDR Zhongtong Bus mali ya kampuni ya Achimwene.
Watuhumiwa walitumia mbinu ya kuficha dawa hizo za kulevya kwenye mabegi mawili ambayo ndani yake yalikuwa na nguo na walibainika baada ya kufanyika ukaguzi.
Wakati huo huo, Novemba 21, 2024 huko katika kizuizi cha Polisi kilichopo mpakani Kijiji cha Igawa Wilaya ya Mbarali, katika ukaguzi wa magari, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata Kondakta wa Basi la Abood aitwaye Erick Patrick Mathew [46] na Tingo wa Basi hilo aitwaye Stanslaus Medson Nyagawa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Bhangi zenye uzito wa kilogramu 20.
Watuhumiwa walikuwa wakisafirisha dawa hizo kwenye Basi la Abood lenye namba za usajili T.823 DXJ Youtong wakitokea Mkoa wa Songwe kuelekea Dar es Salaam ambapo walificha dawa hizo kwenye mifuko miwili mikubwa ya sandarusi.
Sambamba na hayo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Askari wa TANAPA likiwa katika doria ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha, linamshikilia Adam Bandari Katani [58] mkazi wa Chunya kwa tuhuma za kupatikana na silaha aina ya Gobore bila kuwa na kibali cha kumiliki silaha hiyo.
Mtuhumiwa alikutwa na vipande 30 vya chuma ambavyo huvitumia kama risasi katika silaha hiyo, Unga wa baruti ukiwa kwenye kopo, Fataki 5 na vipande 7 vya nyama ya mnyama pori aina ya pimbi bila kuwa na kibali. Mtuhumiwa amekuwa akijihusisha na matukio ya uwindaji haramu ndani ya hifadhi ya taifa ya Ruaha.