elivina shambuni
JF-Expert Member
- May 31, 2018
- 461
- 295
BALOZI wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, amesema kuanzishwa kwa safari za ndege kutoka Dar es Salaam hadi China kutasaidia kuongeza utalii kwa kiwango kikubwa kwa kuwa Wachina wanasubiri kwa hamu.
Kairuki aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuzinduliwa kwa mitandao miwili ya China ambao utakuwa unatangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii (TTB). Alisema bila ya kuwa na ndege ya uhakika, kuutangaza utalii ni changamoto kwa kuwa Wachina wanapenda kwenda katika nchi ambazo zina ndege za moja kwa moja kutokana na tatizo la lugha.
“Wakipita katika nchi nyingine inawalazimu wakae waanze kuzungumza, hii inakuwa ni changamoto, lakini shirika letu la ndege likianza safari zake kama kuanzia Kilimanjaro kwenda China au Dar es Salaam kwenda China itawavutia Wachina wengi na wanasubiri kuanza kwa ndege hiyo,” alisema. Kairuki alisema watakapoona matangazo wawe na uelewa jinsi ya kufika Tanzania, hivyo ikiwapo ndege ya kufika hadi China itawasaidia.
Kairuki alisema Tanzania inafahamika katika masuala ya utalii kwa upande wa Serengeti na Ngorongoro bado kuna maeneo mengine hayajafahamika na yanahitajika kutangazwa. Alisema mtandao wa Baidu unatumika China pamoja na nchi nyingine duniani, hivyo itaitangaza nchi na watu wengi kuona utalii wa Tanzania. “Hii ni fursa ya kujitangaza lengo letu ifikapo mwakani kuongeza idadi hadi kufikia watalii 50,000 na ifikapo mwaka 2025 tuwe tunapokea watalii zaidi ya 100,000 kutoka nchini China na hii inawezekana kwa kuwa serikali imefanya jitihada kubwa katika masuala ya utalii,” alisema.
Mjumbe wa Bodi ya TTB, Richard Rugimbana, alisema tukio la kampuni mbili za China kuamua kuja kuitangaza Tanzania ili waweze kupata vitu vya utalii vizuri wakavitangazwe nchini kwao ni la kihistoria.
Alisema kutangazwa kwa vivutio vya Tanzania katika mitandao hiyo itawawezesha Wachina kufahamu vitu vilivyopo nchini na kuongeza utalii. Mhadhiri wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Mawasiliano ya Habari ya China, Maria Lee, alisema kutangaza vivutio katika mtandao huo wa Baidu kutasaidia kufahamika kwa utalii uliopo Tanzania ili Wachina wahamasike kuja kuvitembelea.
Alisema kuna timu ya wafanyakazi 12 wa mtandao huo wamewasili nchini kwa ajili ya kupiga picha za maeneo ya vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania kwa ajili ya kuwaonyesha Wachina. Mtandao huo unaongoza kutumiwa China kwa asilimia 75 ya watumiaji wote wa intaneti nchini China.