Katika miaka ya hivi karibuni dunia imeshuhudia madhara ya mwelekeo wa dunia ya ncha moja (unipolar world), na matendo ya umwamba yanayotokea duniani kutokana na hali hiyo. Tunaweza kukumbuka baada ya shambulizi la kigaidi la Septemba 11 2001, aliyekuwa Rais wa Marekani Bw. George Bush alipotoa lugha ya vitisho kwa dunia nzima, akisema kwenye mapambano dhidi ya ugaidi kuna machaguo mawili tu (you are either with us, or against us), yaani “uko pamoja na sisi, au unapingana na sisi”. Kauli hii ilichukuliwa kuwa ni kuwalazimisha wale wasiotaka kuhusika kwenye vita hiyo wachague upande mmoja, na upande huo uwe Marekani.
Tabia hii pia haikuishia hapo iliendelea hata kufikia hatua ya Marekani kusema waziwazi inataka kubadilisha serikali za nchi fulani (regime change) ambazo haziendani na mfumo wake, kama ilivyofanya nchini Iraq na Libya, na majaribio yake yaliyoshindwa nchini Syria, Venezuela, na Korea Kaskazini.
Hivi karibuni mshauri wa mambo ya usalama wa Marekani Bw. Jake Sulivan alinukuliwa na televisheni ya CNN akisema moja ya dosari za kisera kuhusu sera ya Marekani kwa China, ni kudhani kuwa mfumo wa China utabadilika wenyewe kutokana utekelezaji wa sera ya Marekani kwa China. Kauli yake ambayo kwa upande mmoja inaonyesha Marekani kukiri kuwa imeshindwa kubadilisha mfumo wa China, haina maana kuwa Marekani imeacha tabia hiyo, au haitatafuta njia nyingine za kufanikisha azma hiyo kwa nchi dhaifu.
Tukiangalia kwa undani tunaweza kuona tabia hii ya Marekani inatokana na hofu ya kupoteza nguvu yake ya ushawishi duniani. Kwa muda mrefu Marekani imeziaminisha nchi nyingine duniani kuwa mfumo wake ndio mfumo pekee sahihi unaowezesha watu kuwa na serikali nzuri na waishi kwa uhuru, neema na demokrasia. Lakini sasa dunia imeanza kuona kuwa hilo si lazima, na kuna mifano iliyojitokeza ya nchi zinazofuata mifumo tofauti na ule wa Marekani, na watu wake wamepata maendeleo makubwa. Umoja wa Falme za Kiarabu ni nchi ambayo imepata maendeleo makubwa ikiwa inafuata mfumo tofauti kabisa na wa Marekani, China pia imepata maendeleo makubwa ikifuata mfumo wake ambao ni tofauti na ule wa Marekani.
Siku zote China imekuwa inasisitiza kuwa nchi zinatakiwa kufuata mifumo inayoendana na utamaduni wa watu wake, kiwango cha maendeleo na hata mazingira yake. Tofauti na hivyo ni kutafuta matatizo ambayo mwisho wake unakuwa mbaya. Tunaweza kuona jinsi Russia ilivyoacha mfumo wake na kufuata mfumo unaofanana na Marekani, ambao hauendani kabisa na historia na utamaduni wa Russia, matokeo yake ni kuwa imebaki kuwa nchi yenye nguvu ya kijeshi lakini kiuchumi bado ina changamoto nyingi. Nchini Iraq na Libya ambako serikali zimebadilishwa kwa nguvu ya kijeshi kwa matakwa ya Marekani, kila mtu anaona watu wanaishi katika hali ya taabu na mateso, tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya hapo.
Kuzibadilisha nchi nyingine ni msingi mkuu wa sera ya kidiplomasia ya Marekani, kwani kwa kufanya hivyo Marekani inakuwa inajihakikishia usalama wake na maendeleo yake. Lakini hii haina maana kuwa usalama na maendeleo ya Marekani ndio usalama na maendeleo kwa nchi nyingine. Tukubali kuwa hali ya dunia sasa imekuwa tofauti sana na ilivyokuwa katika kipindi cha vita baridi au miaka michache baada ya vita ya baridi, na mwelekeo wa dunia kuwa dunia ya ncha nyingi ambapo kila nchi inajiamulia kufuata mfumo inaotaka.