KUCHAGUA CHA KUPANGA NA KUPANGA KIMNUFAISHEJE MNYOGE
Kwa wale wenye umri kama wa kwangu, watakumbuka ule mgawanyo wa dunia kiuchumi kuwa kuna nchi zilizoendelea, za uchumi wa kati na zisizoendelea (underdeveloped). Tanzania iliangukia kundi la tatu. Baadae wakabadili na kutumia majina mengine mengine na sasa hivi Tanzania, inasemakana, iko mahali fulani katika uchumi wa kati. Ili kutambua kundi gani nchi ilipo, ni lazima kujua mahesabu yanayoitwa GDP per capita, National Income, exports, Imports...nk. Na haya, ikiwa huna uelewa fulani wa somo la Uchumi, utatia aibu kujitutumua kuyaongelea.
Kwetu sisi ni rahisi zaidi kuzungumzia mgawanyo kati ya nchi zilizoendelea kama nchi tajiri, na nchi maskini - Tanzania tukiwemo. Ni rahisi pia, kuzungumzia kuwa ndani ya nchi kuna matajiri na kuna maskini. Kama ilivyo kwa nchi tajiri kutawala sera za kiuchumi za nchi maskini – na hili hadi sasa limekuwa halikwepeki, hali kadhalika katika nchi maskini, matajiri wanayo nguvu za kumiliki maisha ya maskini waitwao wanyonge. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, mtu anayeishi kwa mkate mmoja kwa siku, anachangia faida ya mwenye kiwanda cha mikate. Waliochukizwa na mifumo hii huko nyuma walianzisha mikakati ya kimapinduzi ya Kijamaa, wakiwemo Wachina, Warusi na hata WaCuba nk, bila kusahau Ujamaa wetu. Kwa jinsi gani wamefanikiwa bado ni mjadala mrefu.
Tulishawahi kuambiwa kuwa lengo la maendeleo ni watu, sio vitu, kwamba uongozi unatakiwa kutengeneza mazingira ya kimwili na kiroho ya kumwezesha mwananchi kufikia malengo yake. Kwamba ni kweli kuwa binadamu anakuwa alivyo kufuatana na mazingira aishiyo – kwamba akiishi katika mazingira ya kihayawani basi naye atakuwa hayawani. Kwa misingi hiyo nchi zinatakiwa kuhakikisha wananchi wake wanatengenezewa mazingira ya kuishi maisha wayatakayo – yaani yenye maendeleo na raha.
Hivi karibuni, nchi yetu tumekuwa tukiimba wimbo wa Uchumi wa Kati, kwamba kwa sasa hali ya uchumi ni bora kuliko miaka ya nyuma. Wimbo huu umeimbwa na wanasiasa kwa nguvu kiasi kwamba katika vijiwe, mtu yeyote anayeleta pingamizi kuhusu Tanzania kuwa katika Uchumi huo, alijikuta akipelekeshwa na washabiki wa siasa, hususan wale wenye kushabikia upande wa utawala. Pamoja na yote hayo, tuna maswali ya kujiuliza – kwamba, wananchi walioko katika uchumi wa kati wanaishi maisha ya aina gani? Mambo gani yanayowatofautisha na wanaoishi maisha ya uchumi wa ngazi za chini? Uchumi wa nchi ya ngazi ya chini ukoje? Una tofauti gani tunayoiona inayotufanya tutambe kuwa tuko katika uchumi wa kati? Mwananchi aishiye katika uchumi wa kati kama sisi ana raha gani sasa kulinganisha na kabla? Ni nani mtu sahihi atakayetupa takwimu zenye kuelezea hali halisi ya Mtanzania wa uchumi huo?
Tanzania ina umri wa miaka 60 toka kupata Uhuru. Ina mambo mengi ya kujivunia ikiwemo amani inayotajwatajawa na wanasiasa kila wakati. Kuna maendeleo katika maeneo fulani ikiwemo hizo barabara za juu kwa juu, ndege nyingi, reli ya umeme na hata bwawa la umeme. Baada ya kuambiwa na wanasiasa kuwa tuko katika uchumi wa kati, maana yake ni kwamba waTanzania sasa wameendelea kiuchumi kuliko, kwa mfano, miaka kumi iliyopita, kwamba wanaoshindwa kujikimu kimaisha wamepungua. Wanaopinga wanasema takwimu za Umoja wa Mataifa hazisemi hivyo na wengine wanasema kwamba tungetumia vigezo vya maisha ya raha au maisha ya huzuni, huenda muono ungekuwa tofauti. Takwimu Gongana, tuamini zipi!?
Toka tupate uhuru tumetawaliwa na chama kimoja – TANU/ASP iliyobatizwa na kuitwa CCM. Sera zilizotamalaki ni zile zilizoasisiwa na chama hicho, katiba inayotumika ni ile iliyoasisiwa na chama hicho. Kwa hiyo, ikiwa nchi inaendeshwa kufuatana na katiba, sheria na sera na ikiwa mipango ya maendeleo inapangwa kufuatana na sera hizo, ni ukweli usiopingika kuwa, ikiwa kumekuwepo maendeleo, basi yanatokana na mipango ya chama hicho. Lakini pia ikiwa kuna mapungufu yoyote, hayo pia yanatokana na chama hichohicho. Katika mfumo tulionao, wakuyaelezea mafanikio Tanzania ni wengi – rasmi na wasio rasmi, lakini ni kweli pia kuna mapungufu mengi. Inaeleweka kuwa vyama vya upinzani vingeweza kusaidia katika kuyaainisha mapungufu yatokanayo na sera au mapungufu katika kuendesha nchi lakini serikali imewadhibiti. Ni nani sasa ayaelezee mapungufu hayo na waTanzania tuyaelewe? Yupo?
Wengi tunakumbuka habari za ile katiba iliyoasisiwa na CCM – maarufu kama Katiba ya Warioba ambayo ilituhusisha waTanzania wengi bila kujali vyama wala dini. Mzee wa watu akazunguka nchi nzima kuielezea na watu wakahamasika, wakahudhuria katika mchakato uliogharimu fedha za walipakodi wakutosha. Ingepita, hii pia ingelikuwa jambo jingine katika mambo makuu yatokanayo na chama tawala. Kinachoshangaza ni kwamba, wanaopinga kwa nguvu zote suala la katiba ile, kwa sasa, ni haohao waliouanzisha mchakato huo. La kujiuliza ni Kwa nini?! Uoga wa katiba mpya iliyokubaliwa na wananchi kwa ujumla wao umesababishwa na nini, kiasi kwamba nguvu zinatumika nyingi kuhakikisha jambo hili linazimwa na wanaolihitaji wanaonekana kama wahaini!
WaTanzania wanaoipinga wanasema, cha msingi sio katiba nzuri kwani hata katiba iwe nzuri vipi, ikitupatia dikteta, haisaidii kitu, na kwamba sio kipaumbele cha chama tawala. Kwamba cha msingi ni mifumo yenye kutenda kazi vyema, kwamba kukiwa na vyombo vyenye kutimiza wajibu, hakutakuwa na haja ya katiba hiyo ya Warioba. Lakini je, vyombo hivyo vipo? Pia kuna wanaoamini kuwa katiba ndiyo yenye kuweka hivyo vyombo vitakavyo timiza wajibu. Kwa mfano, ikiwa Rais, Mbunge au Waziri anashindwa kutimiza wajibu wake, kwa nini pasiwe na mfumo rasmi wa kumwajibisha, badala yake aachwe au angojewe mwenyewe ajiuzulu kwa mapenzi yake! Lakini pia, ikiwa katiba ni hitaji la wananchi, inakuwaje uwepo wa katiba bora utegemee matakwa ya chama tawala pekee?!
Sasa tuvinjari katika kile kilichoitwa “Vicious Circle of Poverty (VCP)” au kwa tafsiri yangu: “Mzunguko hatari wa Umaskini” ambacho tatizo moja linasababisha lingine ambalo linaleta jingine na kurudiarudia hadi basi, inayosababisha watu wanaishi kwa mkate mmoja kwa siku. Kifupi ni kwamba, unapoishi kwa huo mkate tu ina maana huwezi kula nyama wala pilau, watoto wako watapata kwashokoo…nk. Akiugua hawezi pata dawa muafaka na wala watoto hawatapata elimu ipasayo hata kama elimu hiyo inatolewa bure kama tunavyoambiwa na wanasiasa.
VCP inahusisha maadui watatu wanaoitwa Umaskini, Ujinga na Maradhi. Tunajua kuwa ili kuamini kuwa tumeendelea kwa kiwango muafaka, tunajipima ni kiasi gani tumefanikiwa katika maeneo hayo. Kiasi kwamba unapozungumzia kununua midege mingi, barabara za juu kwa juu na mambo mengine ya aina hiyo, watakuelewa wale tu wenye uwezo wa kutawala maisha ya wanyonge, yaani matajiri, sio maskini, kiasi kwamba ukiona wanyonge wanakushangilia na kukupa kura zao mara zote, utakuwa umefanikiwa vya kutosha kuwazamisha katika lindi la VCP, kwani maskini atakuwa kazidiwa na ujinga. Ili kutoboa, wanyonge hawana budi kuishi katika mazingira wezeshi, na hili ndilo jukumu la serikali yoyote duniani yenye kuthamini maendeleo ya watu wake. Kila Mtanzania na ajitathmini mwenyewe kila anapozisikia tambo hizi za wanasiasa, jinsi binafsi alivyonufaika katika maendeleo hayo na kwa misingi hiyo, alivyoingia katika uchumi wa kati.
Juzi hapa tumefafanuliwa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 21/22-25/26. Katika mpango huo, serikali imepanga kupunguza umaskini kwa kupandisha hali ya maisha - standard of living kwa kuboresha huduma za jamii kwa ujumla wake. Mengine yaliyoahidiwa ni pamoja na kupunguza tozo mbalimbali ikiwemo ushuru katika mazao ya kilimo, mikopo nafuu kwa vijana – imeshatolewa kwa vijana 2,560 tayari wakati wa utayarishaji wa mpango huo, masoko, maji, afya, elimu na ujenzi wa viwanda katika kila mkoa. Kinadharia mpango huo ni wa kupongezwa kwani una malengo ya kumuinua mnyonge.
Katika mpango huo, kuna miradi inayoitwa Flagship Projects ambayo kwa tafsiri yangu ni miradi yenye kipaumbele cha kipekee. Hii ni ile tunayoijua ya Stiglers Gorge, ya Hoima ya mafuta, ya Mchuchuma/Liganga…nk. Tunajua hii inakula pesa nyingi. Je, zitabaki za miradi mingine kwa ajili ya wanyonge?
Wataalamu wameshapanga, kwamba katika miaka mitano ijayo, mambo gani yatafanyiwa kazi. Kilichobaki sasa ni kuchagua vipaumbele – watu au vitu. Na hapa ndipo penye mkwamo kila mwaka. Kwamba kinachowekwa kwenye makaratasi sicho kinachotekelezwa.
Kwa mfano, wameshaweka hizo flagship projects ambazo ndizo zitakazopewa vipaumbele, je, si kweli kwamba ikiwa nguvu zote zitaelekezwa huko inawezekana yaliyopangwa kuhusu wanyonge yataendelea kuishi katika makaratasi tu, na mnyonge ataendelea kula mkate wake kwa siku kama alivyozoea!? Hebu piga hesabu, ikiwa unaweza kutoa fedha za kumjengea kiongozi jumba la kifahari la mabilioni na/au masanamu ya viongozi, inakuwaje unambana mnyonge achangie, tena kwa nguvu, michango ya madarasa au mabweni kwa kisingizio cha kuchangia maendeleo! Nijuavyo mimi, hata wanyonge wanalipa kodi kulingana na uwezo wao mdogo. Unapozichukua hizo za mnyonge na kuzitumia katika kuwanunulia wenye nazo bila kuwalazimisha kulipia kodi au chochote kile, inakuwa dhuluma kwa hao maskini. Lakini, ni kweli pia maskini ana macho, anaona yanayoendelea, tatizo ni VCP.
Kuna wanaokataa kuwa Tanzania ni maskini kwa sababu tu ya maliasili tulizonazo. Kwa bahati mbaya baadhi yetu hatuoni hatua wanazochukua kufuta jina hilo katika macho ya walimwengu. Ukiingia Google utaambiwa Tanzania iko katika orodha ya nchi kumi maskini kuliko zote duniani – 10 poorest countries in the world, ya mwisho kumi watu wake kutokuwa na raha duniani – 10 saddest countries in the world na nchi 10 ambazo thamani ya fedha yake ni ya chini kuliko zote duniani. Wanaoyasema haya ni wale ambao wanaaminika katika vyombo mbalimbali duniani. Kama ni uongo, ni uongo unaoaminika kwa mataifa mengi.
Tumefika mahali haya masimango yametosha. Kuwa maskini kunahusiana na wanyonge, kutokuwa na raha kunahusiana na wanyonge na thamani ya fedha ina uhusiano na manunuzi yanayomhusu mnyonge. Kutambia maliasili zilizopo kuendane na utekelezaji wa mipango. Umefika wakati wahusika wachague maslahi ya wanyonge badala ya maslahi yao – ni kuchagua unataka nini ili kupanga kumfaidishe mnyonge. Matambo yasiyomfaidisha mnyonge hayana maana tena. Ni hayo tu
LANGLANG
Upvote
1