Uandikishwaji wapigakura waleta vituko
Richard Makore
Zoezi la uandikishwaji wapiga kura jijini Dar es Salaam jana lilijawa na vitimbi baada ya mjumbe wa CCM tawi la Mkunduge kukamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi na wafuasi wa CUF kwa madai ya kutaka kujiandikisha sehemu asiyostahili.
Kadhalika wafuasi wa CCM jana walimteka mwandikishaji na kumuamuru awaandikishe kwa nguvu katika mtaa wa Tandale kwa Tumbo.
Ofisa Mtenadji wa mtaa huo, Peter Mkongereza, alikiri kutokea matukio hayo na kusema kuwa kutokana na hali hiyo alilazimika kufunga vituo vitano kati ya saba vilivyokuwa vikitumika.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana alisema kuwa wafuasi wa CUF ndiyo waliomgundua mjumbe huyo aliyetoka eneo lingine na kwenda mtaa usiokuwa wa kwake na kutaka aandikishwe. Wafuasi wa CUF baada ya kumshtukia mjumbe huyo kuwa sio mkaazi wa pale walimkamata na kumuweka chini ya ulinzi lakini baadaye walimuachia.
Aidha, katika zoezi hilo ziliibuka vurugu baada ya wafuasi wa CUF kupinga kuwepo vituo saba katika mtaa huo kinyume na makubaliano ya viongozi wa vyama vya siasa ya kutaka kituo kiwe kimoja.
Mkongereza alikiri kufungwa kwa vituo hivyo na kudai kuwa aliamua kuweka vituo vingi baada ya kupata maagizo kutoka kwa Mtendaji wake wa Kata.
Wafuasi wa CUF mapema jana asubuhi waliwahi vituoni ili kuangalia zoezi linavyokwenda na baada ya kuingiwa na wasiwasi ndipo walipoamua kumhakiki kila mtu aliyekuwa akifika hapo kujiandikisha.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Ofisa Mtendaji wa mtaa wa Tandale kwa Tumbo, wafuasi hao baada ya kuendelea kuhakiki watu waliokuwa wakifika hapo kujiandikisha walipomgundua mjumbe wa CCM na walipomuuliza maswali alikiri kuwa yeye sio mkaazi wa pale na kwamba alitaka ajiandikishe kinyemela.
Kuhusu wafuasi wa CCM kumteka mwandikishaji na kumuingiza ndani ya nyumba ya mtu na kamuamuru awaandikishe alikiri kuwepo kwa tukio hilo.
Alisema kilichozua vurugu na kusababisha kuwachukua waandikishaji na kuwaweka ofisini kwake ni kutokana na kukiukwa kwa makubaliano ya awali yaliyofikiwa ambapo walikubaliana kiwepo kituo kimoja ambapo waandikishaji wote watakuwa pamoja.Mtaa wa Tandale kwa Tumbo una idadi ya wakaazi 21,415 na Kaya 4,283 ni moja ya ngome ya CUF.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo anayemaliza muda wake anatoka CUF.
NIPASHE