Alpha Isaya Nuhu
Member
- Apr 30, 2024
- 6
- 2
NA ALPHA NUHU
KUANDIKA makala maalum kuhusu “Tanzania Tuitakayo” miaka 5 au 25 ijayo, ni kujadili mada nzito na pana inayohitaji maelezo marefu ya kina yanayoweza kutosheleza hata utunzi wa kitabu.
Mada kama hii ina mvuto kwa wasomaji kwa sababu imebeba matumaini ya Watanzania kuiona nchi yao inakimbia kwa kasi kuelekea kilele cha ubora wa maendeleo.
Kila mtu mzima Tanzania anatamani siku moja kuiona nchi yake imejivika sura mpya katika nyanja zote za maendeleo. Hivyo ndivyo alivyotamani Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwanzoni mwa uhuru kuiona Tanzania ikitimua mbio kufikia maendeleo wakati nchi nyingine zikitembea mwendo wa kinyonga wa kusuasua.
Je ni Tanzania gani tunayotaka kuiona miaka 5 au 25 ijayo? Tuko tayari kuvuja jasho kwa kutekeleza mambo ya msingi kufikia lengo hilo?
Haya ndiyo maswali ya msingi ya kujiuliza tunapotafakari hatima ya Tanzania ya siku zijazo. Jibu la maswali haya wanalo Watanzania wenyewe – viongozi na wananchi. Ni lazima wajipange kuigeuza nchi yao iwe na kicheko badala ya kuvaa uso wa manung’uniko.
Siri ya mafanikio ni kujituma na kujitoa mhanga kwa kufanya kazi kufa na kupona kama mataifa mengine duniani yalivyopambana kujiletea maendeleo. Hakuna muujiza mwingine wa maendeleo zaidi ya kuheshimu kazi kwa kujituma.
Dhana ya kujituma alitufundisha Mwalimu Nyerere kupitia usemi wake maarufu kwamba kila kitu duniani kinawezekana iwapo kila mtu atatimiza wajibu wake. Huo ulikuwa wito maalum kwa taifa huru kutumia amali na ujuzi kujiletea maendeleo.
Kwa watu wenye dhamira, hakuna kisichowezekana katika kuukabili umaskini na madhara yake ambukizi.
VITA DHIDI YA UMASKINI
Umaskini ni eneo nyeti na muhimu linalohitaji kufanyiwa kazi kwa umakini ili kuutokomeza kwa sababu bado ni kizingiti cha ustawi wa maisha ya wananchi. Donda ndugu hili lisilopona kwa kukosa tiba madhubuti linatishia uhai wa taifa kwa kuwagawa watu katika makundi hasimu ya “walionacho” na “wasionacho”.
Wananchi wamechoka kusikia nyimbo na ngonjera nyingi zikiimbwa na wanasiasa juu mapambano dhidi ya umaskini. Nyimbo na ngonjera hizo zimebaki kuwa ni mwangwi unaogonga kwenye mlima na kutoweka kwa sababu wananchi wengi wanaoelea kwenye dimbwi la umaskini haziwasaidii.
Watanzania wanataka kuona umaskini unaowang’ang’ania kama kupe unakomeshwa; wanataka kuona kuna hatua za makusudi za kuwatajirisha kutokana na jasho lao katika sekta kuu ya kilimo.
Kwa Tanzania Tuitakayo, wananchi wengi maskini wanataka kuona hakuna tofauti kubwa ya mapato kati ya mtu na mtu kwa makundi yote ya watu katika jamii.
TUPUNGUZE UTEGEMEZI
Tanzania ni tajiri kwa kuwa na kila aina ya raslimali, na hivyo hakuna sababu ibaki kuwa tegemezi licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa ndani kukuza uchumi wake kwa kutumia raslimali hizo kwa maendeleo. Utegemezi wa misaada kokote inakotoka unadidimiza na kudumaza fikra na utu wa Watanzania katika kubadili hali zao za maisha.
MATUMIZI YA NGUVUKAZI
Kwa “Tanzania Tuitakayo” wananchi watapenda kuona watu wabunifu na mahiri kwa kila fani ya maendeleo wanajitokeza kutumia ujuzi wao kuivusha Tanzania kufikia muujiza wa mafanikio. Pengine kinachohitajika ni kufufua na kuendeleza kampeni ya `Kila Mtu Afanye Kazi’ iliyoanzishwa na utawala wa Mwalimu Nyerere miaka ya 1980 kwa nia njema ya kutumia raslimaliwatu kuleta maendeleo.
Kuzuka kwa tatizo la ukosefu wa ajira duniani kumezua janga la kuundwa kwa bomu linalosubiri kulipuka la wimbi la vijana wasio na kazi wanaokimbilia mijini baada ya kumaliza elimu ya msingi, sekondari na vyuo wakidhani kwamba huko ndiko kwenye asali na maziwa.
Mlundikano wa jeshi la vijana hawa waliobatizwa jina la kejeli la “Kula-Kulala” ni hatari kwa usalama wa taifa ingawa watawala wanaliona kana kwamba ni jambo la kawaida!
NINI KIFANYIKE?
Kwa “Tanzania Tuitakayo”, uzururaji katika taifa lililodhamiria kujikomboa kiuchumi inabidi lihesabike ni kosa lisilovumiliwa. Kutofanya kazi au aina yoyote ya kukwepa kazi ni kukiuka maagizo ya Mungu kama misahafu inavyotuonya kwamba “asiyefanya kazi, na asile” na “kila mtu ataishi kwa jasho lake”.
Tangu zamani jamii ya Tanzania iliwalea watoto kwa kuwafundisha maadili ya kuheshimu kazi kama kipimo cha utu. Leo hii watoto wengi wametumbukia kwenye lindi la msiba wa kudharau kazi na kuacha mzigo huo mabegani mwa wazazi wao.
Hii ni balaa kwa wazazi wenyewe kuwadekeza watoto wao kwa sababu uhai wa mwanadamu una mwisho; na mwisho wake ni kuwaacha wale anaowapenda wakihangaika kutafuta heri duniani.
HUDUMA ZA KIJAMII
Katika eneo la huduma za jamii yamefanyika maboresho mengi yenye kutia moyo. Hata hivyo, bado jitihada kubwa zinahitajika kuimarisha sekta za afya, maji, elimu, barabara, umeme na nyingi nyinginezo ili ziwe endelevu kukidhi mahitaji yanayoongezeka katika jamii. Hili ni suala linalotekelezeka kwa miaka 5 au 25 ijayo.
UVUNDO WA RUSHWA
Mapambano dhidi ya uvundo wa rushwa ni suala linaloendelea kuzua mijadala katika majukwaa mbalimbali. Janga hili la hongo, au kwa neno geni la Kibantu “mafupo”, bado linawakanganya hata watawala licha ya kufanyika kwa makongamano mengi na kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi, maarufu`Tume ya Warioba` kushughulikia gonjwa hilo mwaka 1996.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, hayati Meja Jenerali Anatory Kamazima, yeye bila unafiki alikiri hadharani mwaka 1995 kuwa rushwa imejipenyeza na kuitafuna Tanzania katika kila sekta ya maendeleo “kwa sababu ya kuwepo kwa mazingira wezeshi.”
Kwa andiko hili kansa hii bado ni kikwazo cha maendeleo tunapotamani “Tanzania Tuitakayo”. Ufumbuzi wake ni kuchukuliwa kwa hatua kali kama alivyofanya Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Sokoine, za kuwakamata walanguzi na wahujumu uchumi mwaka 1983.
Wala rushwa na wezi, kama alivyotamka Mwalimu Nyerere mwaka 1995, ni lazima watishwe, watiwe msukosuko na kuadhibiwa badala ya kushangiliwa kama ni watu hodari katika jamii kwa kupora mabilioni ya fedha za watu maskini.
HITIMISHO
Kwa ufupi, andiko hili limeainisha maeneo muhimu ya kufanyiwa maboresho katika kuijenga “Tanzania Tuitakayo” yenye neema na ustawi kwa watu wote.
Mambo mengi, kama ilivyoelezwa kwenye aya ya utangulizi wa andiko hili, yanaweza kuandikwa na kufafanuliwa zaidi kukidhi kiu ya Watanzania kwa “Tanzania Tuitakayo” miaka mitano au miongo miwili na nusu ijayo.
MWISHO

Tanzania Tuitakayo kamwe haitapenda kuwa nchi ya kufuga kupe wanaoishi kwa kuwanyonya wengine. Kujikomboa kiuchumi si jambo la lelemama bali ni vita; na katika vita hii watawala wetu ni lazima waache woga wa kukabiliana na tatizo la wazururaji ana kwa ana bila kuogopa watalaumiwa na kusutwa kwamba wanakiuka haki za binadamu.Tangu zamani jamii ya Tanzania iliwalea watoto kwa kuwafundisha maadili ya kuheshimu kazi kama kipimo cha utu. Leo hii watoto wengi wametumbukia kwenye lindi la msiba wa kudharau kazi na kuacha mzigo huo mabegani mwa wazazi wao.

Upvote
2