Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,771
- 41,027
Wapo watu wanaopenda - kwa kujua au kutokujua - kugombana mbele ya watoto wao. Utakuta kitu kidogo kinaanzisha majibizano makali kati ya wapendanao kiasi cha kwamba wanashindwa kujizuia kabisa kugombana na watoto. Mara nyingi majibizano ya namna hii yanaweza kuanza na kitu kidogo na wakati mwingi kuna aina mbili za vitu vinavyosababisha vurugu hizi.
a. Masuala ya fedha - kati ya vitu vinavyosababisha ugomvi wa haraka zaidi ni suala la matumizi ya fedha au mambo yanayohusiana na fedha. "Umefanyia nini fedha yote ile"; "fedha haitoshi" au majibu ya mkato kuhusiana na masuala ya fedha. Kwa mfano mtu anasema "umenifanya miye ATM" au "au una mwanamke wako huko unayempa pesa". Masuala haya ya fedha yanaweza kuwa ndio mambo makubwa yanayosababisha majibizano ya haraka haraka (snap arguments).
b. Majibu mabaya - hakuna kitu kinachoudhi sana kwenye mahusiano kama majibu mabaya ambayo hayana heshima wala staha mbele ya watoto. Wazazi wanapojibizana hivi huwa wanashindana na mwisho wa siku wanaanza kusemezana yale maneno ambayo kwa kweli wangekuwa na uwezo wasingeyasema mbele ya watoto.
Tatizo kubwa hapa ni kuwa yote hayo yote huleta 'mashindano' yaani mke na mume huanza kushindana nani anaweza kusema zaidi, na nani anaweza kusema kitu kibaya zaidi kwa mwenzake. Mara nyingi hili hutokea kwa watu ambao wanaamini wako sawa kwa kila kitu na hivyo hakuna ambaye yuko tayari kunyenyekea kwa mwenzake. Mmoja anapomvunjia mwenzie heshima na mwingine naye anarudisha jibu hilo hilo la kumvunjia heshima - 'ukimwaga unga, miye namwaga maji!'
Sasa wataalamu wa saikolojia wametuonesha mara nyingi kuwa kuna uhusiano wa tabia ya mtoto na tabia anayoiona ya wazazi. Mtoto ambaye amezoea kuona wazazi wake wakigombana gombana au kujibizana jibizana naye anauwezekao mkubwa wa kuwa kama wazazi wake. Kuna watu ambao wanapofikia utu uzima wanapoanza kujibizana na wenza wao wanajikuta wanatumia maneno na kauli zile zile walizozisikia utotoni kwa wazazi wao wakigombana! Watoto wamegeuka kuwa wazazi wao na mnyororo wa tabia hizi za ugomvu hurithishwa toka kizazi kimoja kwenda kingine.
Tabia hizi za kugombana zinarithisha siyo tu kugombana bali pia aina ya mahusiano ambayo mtu anakuja kuwa nayo anapofikia utu uzima - wengi wamekuja kujikuta wakivutwa na watu wenye tabia za wazazi wao. Kwa mfano, wapo wanawake ambao wanaweza kujikuta wanaolewa na kuvumilia wanaume wenye tabia zinazofanana na baba zao. Wanaume nao hujikuta wako hivyo hivyo na matokeo yake huanza kuwatendea wanawake wale kama baba zao walivyowatendea mama zao!
Nini cha kufanya:
Makubwa ni mawili tu; kwanza mkubaliane kutojibishana mbele ya watoto - NO MATTER WHAT. Nakumbuka baadhi ya wazee wetu walikuwa na tabia ya kwenda chumbani ambako huko walisemezana na kuambiana ukweli na mara nyingi ili kuhakikisha watoto hawasikii; walisubiri hadi watoto wameenda kulala tena usiku wa manane. Lengo siyo kwamba ni kukwepa matatizo bali kulinda watoto na hisia zao. Kuwapatia mfano mzuri wa mahusiano.
Jambo la pili ni kuahirisha majibizano kama mahali na muda si mzuri kuanza mjadala. Hii ina maana ni vizuri mmoja kuwa tayari kunyenyekea kwa mwingine kwa lengo la kuahirisha mjadala badala ya kuanza kushindana. Kwa mfano, mmeenda kwenye harusi na mara moja mmoja anajisikia kuondoka na mwingine hataki na kuanza kulalamika. Sasa, anaweza kutumia maneno mabaya na ni kweli yule mwingine hayuko tayari kuondoka bado. Well, katika mazingira hayo mmoja anaweza kuamua kuondoka ili kuacha kufanya vituko hadharani au mbele ya watoto (mara nyingi watu wengine huamua kukubali kuondoka baada ya kufanya vituko vya kutoshaaa na kuacha simulizi!)
Kimsingi ni kuwa wazazi wanajukumu kubwa la kuwa mfano kwa watoto hasa kwenye suala la kutatua migogoro kwenye mahusiano. Kama wazazi hawajui jinsi ya kutatua matatizo matokeo yake kwa watoto yao ni mabaya sana. Na yanakuwa mabaya zaidi kama namna yao ya kugombana huendana na kupigana na kutia kucha! kuna msemo kwenye sociology kuwa "the abused becomes the abuser" hivyo mtoto ambaye anapata emotional abuse anaweza kujikuta na yeye ana abuse wengine.
Ili kuanza kuvunja mnyororo wa tabia hizi za kugombana na kuumizana mbele ya watoto, wazazi wanatakiwa kuamua kwa makusudi kuchagua ni vitu gani vya kubishania, ni wapi pa kubishania na namna gani ya kubishania. Na njia kubwa ya kupunguza hili ni utani!
next time!
JISOMEE ZAIDI KUHUSU ATHARI ZA KUPIGANA MBELE ZA WATOTO HAPA