Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
TAARIFA YA WAZIRI KIVULI WA AFYA, MAENDELEO, YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KWA VYOMBO VYA HABARI
Kumekuwepo na sintofahamu kubwa miongoni mwa Watanzania juu ya ufahamu wa aina gani sahihi ya barakoa (mask) wanazopaswa kuvaa pale wanapokuwa katika shughuli zao za kila siku ili kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona, vinavyosababisha Ugonjwa wa COVID19.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za kitaalamu ambazo zimethibitishwa na mamlaka za masuala ya afya kimataifa, hasa kwenye mapambano ya kujikinga na ugonjwa huo, barakoa sahihi ni za aina ya N95 na Surgical Mask (Varsoy Care Health). Pamoja na umuhimu wake kwa wakati huu wa dharura kubwa ya kulinda afya na uhai, hapa nchini kwetu upatikanaji wake umekuwa ni adimu na aghali baada ya bei zake kuanza kupanda/kupandishwa kiholela, hali ambayo iwapo haitawekewa utaratibu wa udhibiti kwa njia zinazokubalika, itazidi kuongeza ugumu katika mapambano ya kujikinga na kupunguza maambukizi ya COVID19.
Kutokana na kuadimika kwa aina hizo za barakoa ambazo ni sahihi kwa matumizi ya wakati huu au bei zake kuwa juu, watu mbalimbali wameanza kutengeneza barakoa bila kujali kama zinakidhi mahitaji kusudiwa ya kujikinga na virusi vya Corona, hivyo naishauri Serikali itekeleze, iratibu na kusimamia masuala muhimu yafuatayo kwa haraka;
1. Wataalamu wetu wa masuala ya afya waelekeze ni aina gani ya vitambaa/ malighafi zitumike kutengenezea barakoa.
2. Viwanda vya nguo hapa nchini vitumike kutengeneza barakoa zilizoelekezwa na wataalamu. Aidha, Serikali iviondolee kodi viwanda hivyo ili kurahisisha upatikanaji kwa bei nafuu na kuongeza uzalishaji wa barakoa za kutosha kukidhi mahitaji ya wakati huu.
3. Serikali ijikite katika kuhakikisha elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya uvaaji wa barakoa inatolewa kila mahali kupitia njia mbalimbali vikiwemo vipeperushi, matangazo kwenye vyombo vya habari (magazeti, redio, luninga na video au sauti fupi zenye maelezo fasaha kwenye mitandao ya kijamii) badala ya kutoa amri tu za kuwataka watu kuvaa.
4. Serikali ihakikishe barakoa za viwango vya N95 na Surgical Masks zinapatikana kwa wingi na kupatiwa wataalamu wote wa afya hapa nchini ili kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona kwa kuwa wapo mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa COVID19.
Katika hali ya dharura, ni muhimu sana Serikali ikatambua kwamba ugonjwa huu ni mapambano ya kulinda uhai, dhidi ya ugonjwa wenyewe na dhidi ya uchumi na kulinda maisha ya watu wetu ya kila siku ambayo yameathiriwa kwa kiasi kikubwa. Vyote hivi vikipata tafakuri ya pamoja na kuwekwa katika mizania sawa bila shaka dhamira yetu ya kupambana na COVID19 itakuwa katika njia nyoofu ya kuishinda vita hii iliyoko mbele yetu.
Kwa mara nyingine tena naendelea kusisitiza wito muhimu kwa Watanzania wote tuendelee kuchukua tahadhari zote zinazoelekezwa na wataalam wa afya kujikinga na maambukizi dhidi ya Virusi vya Corona. Kila mmoja wetu achukue tahadhari yeye mwenyewe, familia yake na jamii inayomzunguka ili kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Cecilia Daniel Paresso (Mb),
Dodoma.
19/04/2020