Kuinuka na Kuanguka kwa UDSM!

Yona F. Maro

R I P
Joined
Nov 2, 2006
Posts
4,201
Reaction score
236
Kuinuka na Kuanguka kwa UDSM!

Kwa aliyewahi kusoma, kukipenda, kufundisha na kufanya kazi maeneo ya chuo, na yote kabisa Mtanzania mzalendo!

Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, palikuwa mahala pa cheche ya fikra na mbubujiko wa mijadala makini na ya huru kwa maslahi ya Taifa na Afrika kwa ujumla.

Palikuwa mahala pa ndoto ya kila kijana kuweza kufika na kupata fursa ya kusoma hapo. Ilikuwa ndoto na fahari ya kila mzazi kuweza kumfikisha mtoto wake hadi ngazi hiyo. Ilikuwa ndoto kwa wanataaluma (wa ndani na nje ya Tanzania) kupata fursa kufundisha katika chuo hicho. Mlimani palikuwa kizio cha kupima taaluma ya juu nchini!

Hakika waswahili walisema “hakuna marefu yasiyo na ncha”! na kila lenye mwanzo halikosi kuwa na mwisho! Kama kilivyoanza kwa juhudi za dhati ndivyo kinavyomalizwa kwa juhudi za dhati na kundi la watu wachache wasiotaka kusikia la mwazini wala mnadi swala wakiwa na kiburi cha nguvu ya vyombo vya dola na ushosti wa wakuu wa nchi.

Kwa sasa ni chuo ambacho kinasifika kwa kuongozana kwa migogoro na hata migomo na kusimamishwa mara kwa mara kwa wanafunzi wake! Hii ni historia nyingine inajengwa katika chuo hiki makini.

Historia inayojengwa sasa ya kukithiri kwa migogoro na kusimamishwa kwa wanafunzi inapelekea kwa watu makini kuhoji uwezekano wa kufinywa mianya ya majadiliano na uibukaji mpya wa fikra hasa kama hazifurahishi tabaka tawala.

Hii ni ishara ya mlipuko! Mlipuko unaotokana na kukandamizwa kwa muda mrefu sana kwa fikra pevu za wanazuoni(hususan chipukizi), bongo huru, na hamasa ya mabadiliko. Hali hii inakuwa ishara mpya ya machweo ya chuo hiki adhimu, chuo hiki kilichojengwa kwa nguvu za Hayati Mwl. Nyerere kuelekea anguko ambalo haliwezi zuilika mpaka sasa kutokana na ukosefu wa utashi wa kulizuia anguko hilo.

Kukithiri kwa matumizi ya nguvu na ubabe zaidi ya busara na umakini wa kisomi na kustaarabika, kukithiri kwa uongozwaji wa kisiasa zaidi ya kiweledi “professionalism”, kukithiri kwa umimi na kiburi cha kutosikiliza wanaokuzunguka wala wananchi dhidi ya kuwa mtumishi na msikivu na kutenda kwa maslahi ya umma!!

Hii inadhihirishwa na ufinyu wa miundo mbinu kama vyumba vya mihadhara dhidi ya wanafunzi, kuchakaa kwa vyumba vya mihadhara hivyo na haswa makazi ya wanafunzi, ukosefu wa vitabu na vifaa vingine muhimu kwa kitaaluma, kutokwenda na mabadiliko mathalani ukosefu wa vitabu vipya vinavyozinduliwa kila pembe duniani ama matumizi ya TEKNOHAMA, ufinyu wa wahadhiri na walimu kwa ujumla ambao unachochewa sana na urasimu! Kukithiri kwa roho za kiroho na kifisadi zinazopelekea kurudisha nyuma utendaji hususan ufundishwaji na kujikita katika kusaka “madili na fedha”. Ni baadhi tu ya ishara za dhati kuelekea anguko la chuo hiki isipochukuliwa juhudi za dhati.

Hapo nimeamua kutoyajadili shutuma za kukithiri kwa rushwa haswa ya mapenzi, uvunjwaji wa mitihani, kukithiri kwa kufeli kwa wanafunzi, mrundikano katika vyumba vya kulala na hadi katika madarasa, kutokuwepo tena kwa wakaguzi kipindi cha mafunzo ya vitendo “practical training-PT” (ati sababu hakuna fedha)!!

Ufinyu wa wahadhiri wa ngazi zote, na kukimbiwa na wahadhiri wa chache waliopo kwenda katika vyuo hivi vinavyoanzishwa nchini na nje ya nchi ni ishara hasi kwa upande wa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam.

Kupungua kwa idadi ya wanafunzi wa shahada ya pili “uzamili” na ya “uzamifu” katika chuo cha Dar-es-Salaam mwaka hadi mwaka inatoa ishara mbaya sana kwa chuo cha Mlimani. Kasi kubwa ya vijana wabichi wahadhiri kujiunga na taasisi za vyuo vya juu nchini tofauti za Chuo Kikuu Mlimani (ambacho bado kinalia ukosefu wa wahadhiri) kina imarisha kifo cha Chuo hiki nchini.

Kuibuka kwa vyuo vingi mbadala nchini vya umma na binafsi inakuwa ahueni kwa wazazi ambao hawana uwezo wa kuwakimbiza watoto wao ng’ambo. Vyuo hivi ambavyo vilipoanza vimekuwa vikidharauliwa na kupata kebehi sasa vimeanza kuimarika siku hata siku na kuwa “jiwe kuu la pembeni baada ya kukataliwa na “mwashi”(Mlimani)”!!

Kufutika fikra na mtazamo wa wazazi na wanafunzi kuwa chuo kikuu bora ni “Mlimani” pekee nayo ni fursa mpya ya mapinduzi katika sekta ya elimu ya juu nchini. Ingawa kwa upande wa Chuo cha Dar-es-Salaam kuongeza msumari katika jeneza la kuelekea kaburini kwa chuo hicho nchini.

Hiki ndicho Chuo cha Dar-es-Salaam, chuo ambacho kilishasimama na kuimarika si tu nchini katika taaluma ya elimu ya juu bali hata Afrika. Licha ya takwimu za kuporomoka toka nafasi ya 13 Afrika iliyowahi kufikiwa!

Inasikitisha sana, lakini ni kutokana na kuchanganya “urafiki” wa kinafiki, ukabila, siasa mahala penye kuhitaji ufanisi na utaalamu. Hakika anguko la chuo hiki ni anguko kubwa sana nchini, na sikitiko kwa kila ambaye amepitia katika chuo hiki.

Wenu,

Asha Miguubaja.
 
Kimeshaanguka Shy, wala hakitainuka mpaka hawa maprofesa wazee wote hawa waondoke as per human nature!

huyu naye anasupport hii title;

HALI YA CHUO KIKUU DAR ES SALAAM INATISHA

NA JUVENALIS NGOWI

UNAPOZUNGUMZIA chuo kikuu unapata picha ya eneo ambalo kuna mitekenyo ya akili,
fikra pevu zikikinzana na wakati mwingine kukubaliana, mnyukano wa mawazo,
kisima cha hekima, rejeo la maarifa. Hii ndiyo picha ya Chuo Kikuu popote
duniani.

Kwa hili nadhani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa sasa kimepoteza sifa
hizo.

Badala ya vitabu na tafiti tunaona askari wakali na bunduki. Pamekuwa kama eneo
lisilo salama kiasi kwamba mabomu ya machozi yanaweza kurushwa muda wowote.
Mgeni akipita karibu na chuo hicho atauliza kama Tanzania inapoitwa ‘kisiwa cha
amani' ni kweli.

Wanafunzi na walimu wao wote wametangaza kukerwa na mazingira ya elimu
yanayozingirwa na mitutu ya bunduki. Hakuna ambaye angependa kuongeza maarifa
huku askari wale wanaoitwa mtaani fanya fujo uone (FFU) wakirandaranda kando
yao, kwa madaha kama wanamuziki maarufu wanavyoshika magitaa yao wakati wakati
wakitumbuiza katika majukwaa. Mafanya fujo uone huona fahari maana baadaye
wanakwenda kupewa posho za ulinzi wa ile kwa gharama za kodi za walalahoi.

Wananchi hamuoni kuwa utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umeshindwa kazi ya
kutawala. Wanatawala kwa kutumia Jeshi la Polisi. Hii ni aibu. Ni mapinduzi hasi
katika elimu inayotolewa na chuo chetu hicho tulichojivunia.

Ni vigumu kuamini hiki ndicho chuo kilichozalisha watu wenye fikra za
kimapinduzi (hata kama si lazi
ma tukubaliane nazo) kama kina Yoweri Kaguta
Museveni, Dk Harrison Mwakyembe, Profesa Issa Shivji, Dk Asha-Rose Migiro na
mzee Daudi Mwakawago, Wilbert Chagula na wenzake.

Ni msiba mkuu kuona chao kikigeuzwa chekechea ambako wanafunzi wanafunzwa kunywa
uji, kwetu wanaita vidudu. Ni kilio kuamini kwamba watu kama Profesa Walter
Rodney wananasibishwa na chuo kilichoamua kuziba mbubujiko wa fikra mbadala
katika jamii.

Ni matanga yasiyosemekana kuona chuo cha kina Profesa Chachage Seith Chachage
kikikubali kuwa kuwadi wa sera haramu za Magharibi zinazoleta msiba kwa familia
za wazazi maskini. Ni kilio. Ni machozi.

Naona kwamba watu kama Profesa Haroub Othman na Dk. Seng'ondo Mvungi wakijiita
wahadhiri wa chuo kile. Kimefifisha nuru ya mawazo mbadala. Kimetangaza kuwa
wakala wa kuzuia maisha bora kwa familia maskini. Kimekuwa msumari wa mwisho
kwenye jeneza la ukombozi wa mtoto wa mkulima. Bila elimu nani atamudu nini?

Haya yangefanywa na wanasiasa tungewasamehe maana hao ni bendera fuata upepo.
Magharibi wakikuhakikishia ulaji utafungamana nao. Lakini hawa ni wasomi.
Wamepekua kurasa za vitabu kwa kiwango kikubwa. Wamekalia madawati kwa karibu au
zaidi ya nusu ya umri wao. Leo wanafanya tujiulize kwa mara nyingine ikiwa kuna
tofauti ya kusoma na kuelimika. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, we acha tu!

Magazeti yanaeleza kwamba wakazi wa eneo hilo na majirani wanalalamika kwamba
wanaishi kama walioko kwenye ukanda wa gaza. Magari na askari wa kuzuia
fujo
wamejazana sehemu isiyo na fujo. Katika hali ya kawaida muungwana hafanyi fujo
hadi achokozwe.

Kwani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimemchokoza nani hadi wajiandae kwa
kujihami? Bila shaka utawala wa chuo hicho umeng'amua kwamba wamesaliti umma.
Wamekuwa watekelezaji wa mfumo usiotoa haki ya elimu kwa mafukara ambao ndio
wengi katika jamii yetu.

Nafsi zao zinawasuta. Wanafahamu kwamba wao walisomeshwa na Mwalimu Nyerere kwa
jasho la wakulima na wafanyakazi maskini wa nchi hii. Leo wanasema serikali
haina uwezo wa kuwakopesha, si kuwagharamia, wanafunzi wa elimu ya juu. Nini
faida ya uhuru ikiwa kadiri miaka inavyokwenda uwezo wa serikali nao unapungua?
Mwalimu Nyerere aliwezaje kuwasomesha tangu rais, sehemu kubwa ya mawaziri wake,
watawala wa chuo kikuu, na wengine wenye nafasi nyeti wakati huo, lakini hao
wanashindwa kufanya hivyo kwa kizazi hiki?

Mwalimu Nyerere hakuwa na dhahabu kwa kiwango kinachochimbwa leo katika ardhi
yetu. Nyerere hakuwa na tanzanite, hakuwa na fedha kutoka kwenye mauzo ya minofu
ya samaki. Ni kahawa, pamba, korosho na pareto zilizowasomesha watawala wetu wa
leo. Gharama zinazotumika leo kudahili upya wanafunzi zingeweza kulipia
wanafunzi wangapi?

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanatoa utetezi wa kitoto kabisa. Eti ambaye hawezi
kutimiza masharti ya kugharamia elimu akate rufaa kwa waziri wa elimu. Kesi ya
tumbili anapelekewa ngedere, uliona wapi! Wanafunzi walifutiwa udahili kwa madai
ya kukaidi amri ya20waziri. Sera ya uchangiaji kinara wake ni waziri. Leo
unaambiwa ukakate rufaa kwa waziri huyo huyo. Haiyumkini huu ni mchezo ambao
mwamuzi ni mchezaji mwenzio. Igizo.

Hata kama kungekuwa na ukweli katika hili, bado tunahoji busara inayotumika.
Hivi unamfutia udahili mwanafunzi wa mwaka wa nne au wa tatu au hata wa pili,
hasara zaidi ni ipi? Ameshatumia shilingi ngapi na sasa unataka kuzibwaga zote
nje? Ndiyo ule ubabe wa kusema ‘ukimwaga mboga mimi namwaga ugali?' Tukose wote.

Hapa kuna watu wanaotaka nguvu zao zidhihirike kwa umma? Kwamba wakiwa kwenye
vikao wakinywa kahawa au togwa au mvinyo au kilevi wanatamba kwamba ‘si
nilikwambia hao wataishia kupoteza?' Hukumu ipo na itawapata kama si wakati
wakiwa hai hata wakiwa maiti. Hatuwezi kuchezea taifa kwa kiwango hiki.

Katika hali ya kushangaza zaidi hawa tuliowapa madaraka makubwa katika nchi yetu
wakataka kuingilia hadi uhuru wa kikatiba wanaopata raia wa nchi hii. Tuliambiwa
kwamba wanafunzi waliokuwa na mabango walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Hilo
sawa, wacha sheria ichukue mkondo wake. Lakini wakataka kwenda mbali zaidi. Eti
wanafunzi wale wasipewe dhamana. Kweli ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni.

Kwamba wanafunzi wale wanaotuhumiwa kuwa vinara wa kuanzisha maandamano haramu
ni hatari na tishio kwa jamii, wasipewe dhamana. Mungu ambariki sana hakimu yule
jasiri aliyesimamia haki bila kujali jazba ya hao waliomtaka asitoe dhamana.
Akaamua vema kwamba dhamana ipo
wazi. Huu ni ushindi wa Daudi kumpiga Goliati
kwa kombeo!

Watu hawa wanasahau kwamba mwishoni mwa mwaka jana walitwambia kwamba kuna raia
wa kigeni kutoka Uganda anayechochea migomo ya vyuo vikuu? Wakamtimua nchini.
Sasa ghafla hilo limekwisha. Wanasema watuhumiwa wale watano ni hatari mno. Hivi
kweli wanafunzi watano wawe hatari kiasi cha kuomba wasipewe dhamana? Kama ni
kweli basi inabidi polisi wajiuzulu au warudi vyuoni.

Tena watuhumiwa wenyewe mnawafahamu na mmeshawakamata. Maajabu hayakomi. Hii ni
dalili ya woga. Ni ishara ya kushindwa kuongoza. Kiongozi bora haongozi kwa
kutumia nguvu za dola. Dikteta ndiye anayetumia nguvu hizo. Viongozi wa chuo
kikuu wameshindwa kutumia hoja? Ni kweli kwamba hawawezi kuendelea kutawala chuo
hicho bila kutumia kodi yetu kuweka ulinzi usio wa lazima?

Lakini wanafanya pia maamuzi yaliyokosa utu. Wanafunzi hao hawawezi kuishi ndani
ya chuo hadi udahili wao ukamilike. Tanzania si Dar es Salaam. Wanajua watoto
wetu hawa wanatoka kila kona ya nchi yetu. Mtoto wa mwenzio unamzuia kuingia
chuo akalale wapi? Kwa gharama za nani? Tumemwazima nani busara zetu? Juu ya
gharama hizo unataka alipie sehemu ya karo yake. Wanafunzi wale hawakusema
wanataka kusoma bure.

Wamesema mfumo wa ukopeshwaji uangaliwe upya. Ni aibu kwa mtu anayedhania ni
profesa kwa kuwa alipewa jina hilo kushindwa kujua uhalisia wa maisha ya
Mtanzania wa kawaida. Ufisadi si kukwapua tu fedha benki kuu au kuingia mikataba
mibovu tu. Ni p
amoja na kupotosha mwelekeo wa elimu kwa taifa. Tuone aibu.

Tuwe waungwana tukubali kwamba au tumeteleza au tumeanguka. Tujiangalie upya na
kunyanyuka. Turudishe hadhi ya chuo kikuu chetu. Nani angependa chuo kikuu kiwe
kama watu wanaoishi bila uhuru? Sasa wanashurutishwa kuvaa vitambulisho popote.
Wamenikumbusha enzi za ‘vipande system' wakati wa ukoloni. Tusipokubali
tumeanguka hatutaweza kunyanyuka.
 
Last edited:
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…