Kuipenda afrika kulivyomponza sepp blatter

Kuipenda afrika kulivyomponza sepp blatter

Mchuja Nafaka G

JF-Expert Member
Joined
Oct 1, 2014
Posts
763
Reaction score
253
Mwaka 1996, Shirikisho la Soka Afrika (Fifa), lilikuwa linaongozwa na raia wa England, Stanley Rous na mwaka huo England ndiyo ilitwaa ubingwa wa dunia.

Zilikuwa ni fainali za Dunia jina, kwani wakati huo fainali hizo zilikuwa na timu nyingi za Ulaya na Amerika, huku mabara ya Afrika na Asia yakiwakilishwa na timu moja kila moja.

Katikati ya miaka ya 1970, nchi nyingi za Afrika na Asia zilikuwa zimepata uhuru na nyingi zilikuwa zimepata uhuru kutoka kwa Mwingereza na zilianza kupata sauti. Fifa wakati huo ilikuwa kama sehemu ya mamlaka ya ukoloni na ilikuwa ikifahamika kwamba inaunga mkono serikali ya ubaguzi wa rangi ya Afrika Kusini.

Mwaka 1974, mwanasheria kutoka Brazil, Joao Havelange alimshinda Rous katika uchaguzi na hivyo kuwa Rais mpya wa Fifa na ndipo alipoanza kufanya mageuzi makubwa ndani ya Fifa.

Havelange alisaidia kuongeza idadi ya timu katika Fainali za Kombe la Dunia kutoka timu 16 hadi 32 na hivyo kuongeza idadi ya timu nyingi za Afrika na Asia kushiriki katika fainali hizo. Pia alianzisha mashindano ya dunia ya vijana kwa umri tofauti na kuifanya Fifa kuwa shirika kubwa linaloongoza mchezo wa soka.

Mwaka 1998 akiwa na miaka 82 aliacha kuiongoza Fifa na kumpendekeza Sepp Blatter (raia wa Uswisi) kuwa ndiye anafaa kuliongoza Shirikisho hilo. Wakati huo Blatter alikuwa katibu mkuu wa Fifa. Wakati huo huo, Ulaya ya Kaskazini ilikuwa ina mpango wa kutaka kupata tena nafasi ya kuiongoza Fifa, kwa hiyo ilikuwa ikiona Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Lennart Johansson ndiye anayefaa kuiongoza Fifa, lakini alishindwa na Blatter.

Kushindwa kwa Johansson kulichangiwa pia na kauli aliyoitoa baada ya kuja Afrika na kurudi Ulaya, alisema, “Nilipokwenda Afrika Kusini, chumba chote cha mkutano kilikuwa na watu weusi na kilikuwa na giza wakikaa chini kwa pamoja, jambo jingine hawana mzaha wanapokasirika kwa hiyo nilikuwa nikifikiria kwamba itakuwaje watakapokasirika.”

Kauli hiyo iliwaudhi viongozi wa soka wa Afrika kwa hiyo kura zao walimpa Blatter.

Blatter ambaye alishinda uchaguzi huo kirahisi, aliamua kuvunja utawala wa Ulaya na Amerika katika kuandaa Fainali za Kombe la Dunia na kuipa Japan na Korea Kusini kuandaa Fainali za Kombe la Dunia 2002.

Hata hivyo, ugomvi wa Blatter na nchi za Ulaya ulianza alipotangaza kuwa anataka kuzipeleka Fainali za Kombe la Dunia barani Afrika na alikaribia kuzipeleka mwaka 2006. Hata hivyo, mjumbe wa Bara la Oceania, Charlie Dempsey alijitoa katika dakika za mwisho za upigaji kura, hivyo Ujerumani ikaishinda Afrika Kusini.

Baada ya hapo Blatter alikuja na mpango kwamba Fainali za Kombe la Dunia zifanyike kwa mzunguko katika mabara yote. Kwa hiyo Fainali za Kombe la Dunia za 2010 alichagua zifanyike Afrika. Kura zikapigwa kati ya Morocco na Afrika Kusini ambayo iliibuka mshindi.

Miaka michache baada ya kura hizo kupigwa, vyombo vya habari vya England vikaanza kutoa habari mbaya kuhusu Afrika Kusini vikionyesha kwamba nchi hiyo ina uharifu wa hali ya juu. Matukio ya ubakaji na mauaji mengi.

Pia vilitangaza kwamba viwanja havitakamilika kabla ya mashindano, watu wengi wanaishi kwenye makazi yasiyo rasmi na viliwahoji baadhi ya watu wa Afrika Kusini ambao walikuwa wakiiponda nchi yao kwa kuwekeza fedha nyingi katika fainali hizo badala ya kuzitumia katika sekta ya elimu.

Vyombo hivyo vya habari pia vilianza kuchagua nchi ambazo zitafaa kuandaa fainali hizo kwa madai kuwa Afrika Kusini inaonekana haiwezi na waliitaja England ndiyo inayofaa na nafasi ya pili wakaipa Ujerumani.

Kabla ya kufanyika kwa Fainali za Kombe la Dunia, hufanyika mashindano ya mabara ambayo yalifanyika Afrika Kusini mwaka 2009 kwa mafanikio.

Pia, kabla ya kufanyika kwa Fainali za Kombe la Dunia, huwa inapangwa ratiba, dakika chache kabla matangazo ya televisheni hayajaanza, mpiga picha kutoka Ujerumani aliweka begi ndani ya ukumbi na kupiga kelele za bomu akitaka watu wakimbie, lakini polisi waliwatuliza na polisi mmoja alilifuata begi lile na kukuta ndani yake kuna vitabu tu. Siku zote kama kuna bomu ndani ya jengo ina maana watu wote huondolewa ili kuwapisha askari ambao ni wataalamu wa mabomu ili kuliondoa, hiyo ina maana matangazo ya moja kwa moja yangechelewa na hivyo nchi za Ulaya zingesema Afrika bado haina uwezo wa kuandaa fainali hizo.

Baada ya Fainali za Kombe la Dunia 2010 kumalizika nchini Afrika Kusini, Rais wa klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani, Uli Hoeness alisema uamuzi wa Fifa kuzipeleka fainali hizo Afrika ulikuwa wa makosa na kudai kuwa uamuzi huo ulifanyika kwa rushwa.

Hata hivyo, Blatter alimjibu Hoeness kwa kusema, “Kuna ule mtazamo wa kizamani kwa nchi za Ulaya kwamba kwa nini Afrika iandae Fainali za Kombe la Dunia, unajua wakoloni kwa zaidi ya miaka 100 walienda Afrika na kuchukua vitu vyao vizuri vingi na mpaka sasa wanachukua wachezaji wao bora, hakuna heshima kabisa.”

Baada ya Afrika kupewa nafasi ya kuandaa fainali za 2010, fainali hizo zilipelekwa Amerika Kusini na Brazil iliziandaa 2014. Baada ya hapo fainali hizo zilitakiwa kufanyika Ulaya, hivyo England ilikuwa ikiona ina nafasi kubwa ya kuandaa fainali za 2018, lakini ikapewa Urusi.

Baada ya England kushindwa ndipo walipoibuka kwa nguvu kubwa kwamba Fifa imejaa rushwa na kufanya kampeni za kumwangusha katika uchaguzi wa 2015. Hata hivyo alishinda, lakini siku chache baada ya ushindi huo aliamua kutangaza kujiuzulu baada ya kuona nchi za Ulaya zinampinga.

Sawa, Blatter anaondoka atakuja kiongozi mwingine, lakini ukiacha kuzileta fainali za dunia barani Afrika, Blatter ndiye alifanya klabu za Afrika ziingie katika mashindano ya dunia ya klabu.

Kwani awali mashindano hayo yalishirikisha klabu za Ulaya na Amerika ya Kusini. Blatter pia ndiye aliyeanzisha mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika.

Blatter ndiye aliyeanzisha mpango wa kutoa fedha sawa kwa mashirikisho yote ya soka duniani baada ya kumalizika kwa fainali za kombe la dunia.

Fedha hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya mashirikisho mbalimbali ya soka ya nchi za Afrika. Baada ya kumalizika kwa fainali za 2014, kila shirikisho lilipewa Dola 750,000 za Marekani.
Blatter alianisha utaratibu wa kulipatia kila shirikisho la soka Dola 250,000 za Marekani kila mwaka.

Baada ya Fainali za Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini, Blatter aliziongeza na kuanzisha miradi mingi kwa ajili ya kusaidia soka la Afrika. Kwa mfano, ulianzishwa mradi wa ‘Win in Africa with Africa’ ukiwa na bajeti ya zaidi ya Dola 39 milioni kwa ajili ya kutengeneza viwanja (sehemu ya kuchezea) katika nchi 52 za Afrika.

Blatter alianzisha pia mradi wa ‘Goal’ wenye lengo la kusaidia miradi mbalimbali ya soka Afrika hasa miundombinu kama sehemu za kuchezea, vifaa, malazi na vituo vya ufundi, mradi huu hufanyika pale Shirikisho husika linapoomba fedha Fifa.

Blatter hakuishia hapo, kwani alianzisha mradi wa ‘Football for Hope’ na kujenga vituo mbalimbali barani Afrika vyenye viwanja vya soka ili watoto au vijana walio na maambukizi ya Ukimwi, mazingira magumu au nchi iliyokosa amani na majanga mengine waweze kucheza mpira wa soka.

Alihakikisha Fifa inaendesha kozi mbalimbali za makocha, waamuzi, utabibu na utawala kwa lengo la kuhakikisha mafunzo hayo yanasaidia maendeleo ya soka la Afrika.

Kwa ujumla, kwa mujibu wa Fifa, toka mwaka 1999, shirikisho hilo likiwa chini ya Blatter, limetoa zaidi ya Dola 500 milioni za Marekani kwa ajili ya maendeleo ya soka la Afrika.Ndiyo maana kuondoka kwa Blatter kutakuwa pigo na pengo kubwa kwa Afrika kwani aliipigania ndiyo maana uchaguzi uliopita alipata kura 54 za nchi za Afrika.



 
Tafakuri yangu baada ya kusoma Makala hii

mabadiliko yaliyotokea FIFA hayana maslahi yoyote kwa bara la amerika na afrika kwa sababu yamelenga kunufaisha nchi za ulaya. sababu yamefanyika kutokana na fitina za marekani na uingereza ambao daima wamekuwa wakali pale masilahi yao yakipuuzwa. Kosa kubwa alilofanya Blatter kupuuza maslahi ya Uingereza na Marekani kwa kuzipa uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia Urusi na Qatar badala ya Marekani na Uingereza.

Jambo ambalo tunapaswa kuwa nalo makini nchi za kiafrika sera za wagombeaji nafasi hiyo ya urais pindi utapoitishwa uchaguzi mwingine. Kwa sababu wazungu hawatuoni sisi binadamu timamu kama wao, hatustahili kupata mgao sawa alioanzisha Blatter, wala kupewa upendeleo kusaidiwa kupandisha kiwango cha soka la Afrika ili kuleta ushindani.
Rushwa ni mtaji wao mkubwa kurejesha mambo kama ilivyokuwa enzi za ukoloni
 
Pia ni funzo kwa wengine kuwa Wazungu wakiamua hata mzungu mwenzao humgeuka
 
MASAHIHISHO:
Mwaka 1996, Shirikisho la Soka Afrika (Fifa), lilikuwa linaongozwa na raia wa England, Stanley Rous na mwaka huo England ndiyo ilitwaa ubingwa wa dunia.
Enlangland ilitwaa WC mwaka 1966, boss wa FIFA akiwa
Stanley Rous
 
Kwa nini waafrika kila mara tuna - side na corruption? Kwa maoni yangu waafrika tuache kujitambulisha na watu (individuals) badala yake tujitambulishe na taasisi. Hata kama Blatter angekua malaika iko siku angeondoka tu lakini FIFA is there to stay. Tusimshangile mtu anayetupa samaki ila tumshangilie mtu anayetupa mbinu na uwezo wa kuvua. Mimi ningempenda Blatter ambaye angeweka misingi ya uendelezaji wa soka duniani, misingi ambayo itaendelea kuwepo hata kama yeye hayupo. Lakini kama Blatter huyu amekaa for 19 years bado tunamtegemea yeye tu kama binadamu then ni vyema akaondoka maana hatufai.
 
Kiongozi kabla ya Blatter alianzisha mabadiliko kidogo kidogo na alipoingia Blatter aliongeza kasi ya mabadiliko. Na kumbuka siku zote watu hawapo tayari kuyakubali mabadiliko kwa sababu yanaathiri maslahi yao.
Lengo la kubadili structure nzima ya FIFA lipo na lisingewezekana kwa ghafla, na hilo lilikuwa lifanyike kipindi cha tano cha Blatter. Lakini kutokana na jeuri yake wazungu wenzake wakaona ni bora aje mtu mwingine kufanya mabadiliko ya kitaasisi kuliko huyu Blatter.
 
kumbe ndio maana platin alikuwa anampiga vita sana
 

Mwaka
1996, Shirikisho la Soka Afrika (Fifa), lilikuwa linaongozwa na raia wa England, Stanley Rous na mwaka huo England ndiyo ilitwaa ubingwa wa dunia.
Zilikuwa ni fainali za Dunia jina, kwani wakati huo fainali hizo zilikuwa na timu nyingi za Ulaya na Amerika, huku mabara ya Afrika na Asia yakiwakilishwa na
timu moja kila moja.
Sawa, Blatter anaondoka atakuja kiongozi mwingine, lakini ukiacha kuzileta fainali za dunia barani Afrika, Blatter ndiye alifanya klabu za Afrika ziingie katika mashindano ya dunia ya klabu.
Kwani awali mashindano hayo yalishirikisha klabu za Ulaya na Amerika ya Kusini. Blatter pia ndiye aliyeanzisha mashindano ya
Kombe la Shirikisho la Soka Afrika.
  • Fainali zilizofanyika England ni za Mwaka 1966
  • kabla ya Blatter Afrika tulipeleka timu 3
  • Kina Maulid Dilunga na nduguye walicheza mashindano ya Kombe la Afrika
 
Back
Top Bottom