Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
MAMLAKA YA USIMAMIZI WA WANYAMAPORI TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA
HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA TAWA KATIKA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA MAMBA NA BOKO KATIKA BWAWA LA MTERA
TAARIFA KWA UMMA
HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA TAWA KATIKA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA MAMBA NA BOKO KATIKA BWAWA LA MTERA
Hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko la matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo mamba na boko kujeruhi na wakati mwingine kusababisha vifo kwa wananchi hususan wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Bwawa la Mtera. Hali hiyo, imepelekea adha na hofu kwa wananchi wanaotegemea bwawa hilo katika shughuli za kijamii na uzalishaji mali.
Ongezeko la matukio hayo limetokana na mvua kubwa ambazo zimeendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha kuongezeka kwa mtawanyiko wa wanyamapori hususan mamba na boko kwenye maeneo ya mito na mabwawa. Ambapo katika Bwawa la Mtera mamba wamekuwa wakiletwa na maji yanayotoka mito ya Ruaha Mkuu na Kizigo.
Kufuatia hali hiyo, TAWA imekuwa ikichukua hatua za haraka kudhibiti wanyamapori hao ili kunusuru maisha ya watu na mali zao ikiwemo kuimarisha doria zinazoshirikisha Askari Wahifadhi na Askari wanyamapori wa Vijiji na kutoa elimu kwa jamii kuhusu jinsi ya kujikinga na kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao.
Kufuatia jitihada hizo, Katika kipindi cha kuanzia Januari 2024 mamba watatu (3) na boko wawili (2) waliokuwa hatarishi kwa maisha ya watu na mali zao waliuawa. Aidha, jumla ya wananchi 271 wakiwemo wavuvi 40 walipatiwa elimu katika Vijiji vilivyopo Kata ya Migoli.
Katika kuimarisha ulinzi wa maisha ya watu wanaoishi kando ya Bwawa la Mtera dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu ikiwemo mamba na boko, Mamlaka imeanzisha Kituo cha kudumu cha Askari katika Kijiji cha Migoli. Kituo hicho kina jumla ya watumishi 20 na kimepatiwa vitendea kazi muhimu kwa ajili ya udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu.
Aidha, Mamlaka inatoa rai kwa wananchi kuendelea kufanya shughuli zao kama kawaida, isipokuwa wachukue hadhari wanapokuwa kwenye mabwawa, mito na madimbwi. Vilevile, wazingatie maelekezo yanayotolewa na wataalam wa uhifadhi ikiwemo kuacha kuoga au kufua ndani ya bwawa na wavuvi kuacha kutumia mitumbwi hatarishi inayoongeza uwezekano wa kushambuliwa na mamba au boko na badala yake watumie nyenzo za kisasa katika shughuli za uvuvi. Endapo itabainika uwepo wa wanyamapori wakali na waharibifu ikiwemo mamba na boko taarifa itolewe haraka kwa wataalam wa uhifadhi au Serikali za vijiji husika ili hatua stahiki zichukuliwe kwa haraka.
Imetolewa na:
Beatus Maganja
AFISA HABARI
Kitengo cha Uhusiano kwa Umma
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA
AFISA HABARI
Kitengo cha Uhusiano kwa Umma
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA