Serikali kutoa tamko la mafuta leo
Mwandishi Wetu na Mikoani
Daily News; Monday,December 29, 2008 @07:59
Serikali imesema inalifanyia kazi tatizo la upungufu wa mafuta ya petroli uliojitokeza katika baadhi ya mikoa hapa nchini na inatarajia kutoa taarifa rasmi leo.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima aliiambia HabariLeo kuwa serikali inatambua kuwapo kwa tatizo hilo na itatoa tamko lake leo pamoja na hatua ambazo zitachukuliwa.
Petroli imeadimika katika mikoa ya Morogoro na Iringa kiasi cha kufanya bei yake kupanda na kusababisha gharama za usafiri kupanda kiasi cha magari mengine kusitisha safari zake.
Hata hivyo Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) iliuelezea uhaba huo ni wa muda na unatokana na kuchelewa kwa meli za mafuta kuingia Bandari ya Dar es Salaam kunakosababishwa na vitendo vya kiharamia pwani ya Somalia.
Ewura hata hivyo kupitia kwa Ofisa Habari Mkuu wa Ewura, Titus Kaguo imesema uhaba huo wa mafuta siyo sababu ya kupandisha bei bali ni mchezo mchafu wa wafanyabiashara hao wa mafuta.
Hali ya upatikanaji wa mafuta katika Mkoa wa Morogoro pamoja na kuimarika bei iliendelea kuwa tatizo anaripoti John Nditi kutoka Morogoro.
Utafiti uliofanywa na gazeti hili umebainisha kuwa kuna baadhi ya vituo vimeendelea kukaidi agizo la kutopandisha bei la Ewura kwa kuendelea kuuza nishati hiyo muhimu kwa bei ya Sh 1,500 hadi 1,800 kwa lita.
Uhaba wa mafuta hayo kwa Mkoa wa Morogoro ulianza kabla ya Sikukuu ya Krismasi ya mwaka huu na kusababisha watumiaji wa magari yanayotumia mafuta ya aina hiyo kupandishiwa bei kutoka Sh1,350 hadi Sh 2,000 kwa lita moja.
Hata hivyo kituo cha Simba Oil cha mjini hapa ndicho pekee kilichokuwa na mafuta ya petroli kwa juzi asubuhi na kusababisha msongamano wa watu na magari kwa ajili ya kugombea kununua mafuta hayo kwa bei ya Sh 1,800 kwa lita moja na kumalizika mchana majira ya saa 7.
Juzi hiyo saa kumi na nusu jioni kituo cha GAPCO kilichopo karibu na Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kilipata mafuta na kuanza kuuza kwa bei ya Sh 1,450 kwa lita moja.Hata hivyo uchunguzi uliofanyika jana katika vituo mbalimbali vya mafuta vilivyopo katika Manispaa ya Morogoro kuna hali ya nafuu katika upatikanaji wa mafuta hayo ya petroli.
Hata hivyo kituo cha Gapco kinachomilikiwa na mfanyabiashara ajulikanaye kwa jina maarufu 'Mzee Mella' ambapo juzi kilikuwa kikiuza mafuta hayo kwa Sh 1,450 kwa lita moja, jana kiliongeza Sh 50 na kufanya mafuta hayo kuuzwa kwa Sh 1,500 kwa lita.
Vituo vingine vilivyopata mafuta hayo kuanzia siku ya jana ni pamoja na kituo cha MT kilichopo katikati ya mji ambapo kimekuwa kikiuza mafuta hayo kwa Sh 1,600 kutoka bei yake ya kawaida ya Sh 1,350 kabla ya kuadimika kwa mafuta hayo ambapo mafuta ya dizeli ni Sh 1,250.
Katika vituo vingine vitatu vya mafuta vya Gapco vya Saddiq Service Station vimekuwa na mafuta hayo ya petroli ambavyo vinayauza kwa Sh 1,700 kwa lita moja tofauti na bei yake ya zamani ya Sh 1,350 ambapo kwa mafuta ya dizeli vituo hivyo vinauza kwa Sh 1,400 kwa lita moja.
Hata hivyo baadhi ya vituo vingine kikiwamo cha ORYX ambacho awali kilikuwa na mafuta hayo kabla ya kumalizika kilikuwa kikiyauza kwa bei ya Sh 1,436 kwa lita moja na kwa mafuta ya dizeli ni Sh 1,376 kwa lita.
Kabla ya kuadimika kwa mafuta hayo baadhi ya vituo vya mjini hapa bei yake ilikuwa kati ya Sh 1,350 hadi kufikia Sh: 1,460 kwa lita moja na kwa upande wa mafuta ya dizeli ilikuwa ni Sh: 1,250 hadi 1,280 kwa lita.
Baadhi ya watu waliohojiwa kuhusiana na sakata hilo kwa nyakati tofauti walisema kuwa hali hiyo haijawahi kutokea katika Mkoa wa Morogoro na kuitaka serikali kuangalia kiini cha tatizo hilo.
Naye mkazi wa Manispaa ya Morogoro, Abdallah Mambo, aliitaka serikali kuwa makini ambapo mamlaka inayosimamia suala la mafuta kutakiwa kuwa makini na kusimamia sheria kuanzia za uagizaji na usambazaji na kutoa taarifa kwa umma wakati kunapotokea upungufu wa mafuta nchini.
Naye Frank Leonard, akiandika kutoka Iringa anasema baada ya kuadimika kwa siku nne mfululizo, mafuta aina ya petroli yameanza kupatikana tena mjini Iringa.
Mafuta hayo yalianza kuwasili juzi usiku na kuuzwa kati ya Sh 2,200 na Sh 2,400 katika vituo mbalimbali vya mafuta mjini hapa.Hata hivyo jana Jumapili mafuta hayo yalishuka bei hadi Sh 1,500 katika vituo vya GAPCO vilivyokuwa pia na mafuta hayo.
Kupatikana kwa mafuta hayo kumerudisha upya huduma za usafiri wa baadhi ya mabasi ya kusafirisha abiria na teksi zilizosimamisha huduma hiyo kutokana na ukosefu wa mafuta hayo.
Mmoja wa wakurugenzi wa vituo hivyo vya GAPCO, Salim Asas alisema jana kwamba mafuta hayo yaliwasili kwa wingi mjini hapa jana asubuhi."Mafuta ni mengi tu, juzi Jumamosi yalipakuliwa Bandari ya Dar es Salaam na jana sisi tuliyapata na tunaendelea kuuza kwa bei ileile ya mwanzo kama kawaida," alisema.
Wakati vituo vya GAPCO vikiuza mafuta hayo kwa Sh 1,500 kwa lita, baadhi ya vituo vingine vilivyopata mafuta hayo juzi, mpaka jana vilikuwa vikiyauza kwa Sh 1,750 hadi Sh 2,400.
Madai ambayo hayakuweza kuthibitishwa na wamiliki wa vituo hivyo yanaonyesha kwamba mafuta yaliyokuwa yanauzwa kwa bei hizo baada ya kuadimika mjini hapa kwa siku nne, yalinunuliwa kutoka vituo vingine vya mikoa jirani na jijini Dar es Salaam.
"Unajua kufa kufaana, na biashara ni ujanja. Sisi tulilazimika kununua mafuta haya tunayouza kwa Sh 2,400 kutoka katika moja ya vituo vya mafuta mjini Dodoma , sijui bosi alinunua kwa kiasi gani lakini hakuna shaka hakununua kwa zaidi ya Sh 1,500," alisema mmoja wa wafanyakazi wa kituo kimoja cha mafuta ambaye hakutaka kutaja jina.
Alisema siku ya Jumamosi walileta lita 2,000 zilizowasili majira ya saa mbili usiku, hata hivyo haikuchukua zaidi ya masaa mawili yakaisha pamoja na kuyauza kwa Sh 2,400. "Jana asubuhi zikaja lita zingine 2,000 ambazo tunaendelea kuziuza kwa Sh 1,750," alisema.