Kukua kwa Pato la taifa kutatafsiri 'maisha bora'

Kukua kwa Pato la taifa kutatafsiri 'maisha bora'

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
editorial-nipashe-sept01-2013.jpg

Maoni ya Katuni



Mara nyingi mwananchi wa kawaida hawezi kuelewa dhana ya 'kukua kwa uchumi wa nchi' wakati maisha yake yanabakia kuwa magumu kutokana na gharama za bidhaa muhimu kuendelea kuwa ghali kila siku.

Wananchi wanaohamasishwa kila wakati kufanya kazi kwa bidii ili 'kukuza uchumi wa nchi', wanashindwa kuelewa tafsiri yake wanaposikia kuwa uchumi wa nchi umeongezeka kwa asilimia kadhaa... wakati hali ya nchi na maisha yao ya kawaida yanazidi kuwa magumu.

Kukua kwa Uchumi wa nchi kunatakiwa kutafsiri huduma bora kwa wengi wakiwa kama sehemu ya taifa, na ndiyo maana inaelezwa kuwa nchi maskini duniani, wananchi wake hupitia kipindi kigumu kiuchumi kwa kukosa huduma bora za kijamii kama elimu, afya, barabara, maji safi na kadhalika.

Wakati nchi hizo maskini zinapoweka jitihada za kujikwamua kiuchumi, ndipo tathmini ya kukua kwa uchumi inapotolewa ikienda sambamba na uboreshwaji wa miundombinu muhimu kwa maendeleo ya wananchi wake.

Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, Morrice Oyuke wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, mwishoni mwa wiki hii amesema pato la taifa kwa robo ya kwanza ya mwaka huu limekua kwa asilimia 7.5 ukilinganisha na mwaka jana kipindi kama hiki ambapo lilikua kwa asilimia 7.4.

Mkurugenzi Oyuke alifafanua kuwa jumla ya thamani ya pato la taifa ilikuwa milioni 4,540,456/- kwa mwaka huu ikilinganishwa na milioni 4,225,585/- kwa mwaka 2012, ambapo pia katika kipindi hicho, shughuli za uchimbaji wa madini, mawe na kokoto zilishuka kwa asilimia 4.7 ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 23.8 mwaka jana.

Aliendelea kutoa tathmini kwa maeneo mengine kama shughuli za uchumi za kilimo kuwa zilifikia kasi ya ukuaji ya asilimia 1.4 kipindi hiki, ikilinganishwa na asilimia 0.4 ya kipindi kama hiki mwaka jana, hususan na shughuli za uvuvi ikikua kwa asilimia 1.8 ikilinganishwa na asilimia 2.0 kwa mwaka jana katika kipindi hicho.

Aidha alisema uzalishaji wa bidhaa za viwandani ulifikia ukuaji wa asilimia 8.6, ikilinganishwa na kazi ya asilimia 5.7 mwaka jana kutokana na uzalishaji wa vinywaji, bidhaa za tumbaku na sukari.

Baada ya kutoa tathmini ya kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kipindi hicho, Oyuke alisema ukuaji wa shughuli za uchumi na utoaji huduma zimesababisha shughuli za biashara za jumla na rejareja, ukarabati wa magari na pikipiki na vifaa vya majumbani kupungua kwa asilimia 9.5 ikilinganishwa na mwaka jana ilipokuwa 12.1

Masuala ya uchukuzi na mawasiliano Oyule yalifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 22.2, wakati mahoteli na migahawa ilifikia ukuaji wa asilimia 3.4 wakati uendeshaji wa serikali ulifikia asilimia 3.6 na huduma za afya kukua hadi asilimia 4.3 katika kipindi hicho.

Tunaamini mwananchi wa kawaida anaweza akatafsiriwa tathmini hiyo ya 'kasi ya ukuaji wa uchumi' na kuelewa vyema maana ya kuongezeka kwa uchumi kwa maana ya faida na maslahi ya wananchi walio wengi.

Kuboreka kwa huduma za afya kwa asilimia 4.3 kuna tafsiri ya ongezeko la ubora wa huduma za afya pamoja na huduma hizo kwa wananchi wengi zaidi.

Kwa ajili ya kuboresha ukuaji wa uchumi wa taifa, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Dk. Reginald Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, mwishoni mwa wiki hii ameitaka Benki ya NBC kujikita katika ushiriki wa ukuzaji wa uchumi wa taifa ambao alisema unaonekana kukua kwa kasi.

Dk. Mengi alitoa rai hiyo wakati akifungua tawi la Benki hiyo kwenye jengo la Coco Plaza jijini Dar es Salaam akisisitiza kuwa hatua hiyo itakuza pato la benki na hatimaye kuwa na uwezo wa kuwashawishi wawekezaji wakubwa wanaokuja nchini kuwekeza, ambao pia alisema watakuwa chachu kubwa ya kuchangia uchumi kukua kwa kasi zaidi.

Tunaamini kuwa taasisi za fedha ni chanzo kikubwa cha kuinua pato la taifa, na pia zikitumia mtandao wa kibiashara na kuwahusisha wawekezaji wakubwa, uchumi wa nchi utaongezeka kwa kasi kubwa.

Kuboreka kwa huduma za kijamii ni tafsiri mojawapo ya kukua kwa uchumi wa taifa, hatua ambayo hatimaye uchumi huo utawapunguzia ugumu wa maisha wananchi unaowafanya hivi sasa waishi kwa gharama za kiwango cha juu kuliko pato lao la kila siku.

Tunaamini tathmini inayotolewa ya kukua kwa uchumi wa taifa hatimaye itawapunguzia gharama za maisha Watanzania wengi. Tunatoa wito kwa kila mwananchi kufanya kazi kwa juhudi na bidii ili kuzalisha zaidi kwa manufaa ya uchumi wa nchi yetu.




CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

 
Back
Top Bottom