Hivi karibuni, rais Xi Jinping wa China alifanya ziara ya ukaguzi katika magofu ya Yinxu mjini Anyang, katikati ya China na kusema “Maandishi ya lugha ya Kichina yameshangaza sana, na kufanya kazi kubwa katika kuunda na kuendeleza taifa la China."
Yakiwa magofu ya kwanza ya mji mkuu katika historia ya China katika kipindi cha baadaye cha enzi ya Shang miaka 3,000 iliyopita, Yinxu ilijumuishwa katika Orodha ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO mnamo Julai 2006.
Siyo tu mabaki mengi ya kitamaduni ya kupendeza yamegunduliwa hapa, bali pia muhimu zaidi ni maandishi ya mifupa ya Oracle. Maandishi ya mifupa ya Oracle ni chanzo cha maandishi ya lugha ya Kichina na yanabeba jeni za utamaduni wa Kichina. Miongoni mwa maandishi manne ya kale duniani, ni maandishi ya Kichina tu yanayowakilishwa na mifupa ya Oracle ya Yinxu ndiyo yamesalia hadi leo.
Miaka 120 iliyopita, wakati maandishi ya mifupa ya Oracle yalipogunduliwa, China ilikuwa katika jamii duni ya nusu ukabaila na nusu ukoloni, ambapo mifupa mingi ya Oracle iliibiwa na wavamizi wa Magharibi na kupelekwa uhamishoni ng'ambo.
Sasa baada ya miaka 120, China imepata mabadiliko ya kihistoria kutoka kusimama, kuwa tajiri na kuwa na nguvu. Tunaweza kusema mifupa ya Oracle imeshuhudia mabadiliko na maendeleo ya historia ya zama za karibuni ya China.
Barani Afrika, tukiuliza ni lugha gani inayoweza kubeba jukumu la kushuhudia kujipatia uhuru, na kupatikana kwa maendeleo na hadhi ya kimataifa ya nchi au hata bara zima, Kiswahili kinastahili kupongezwa. Novemba mwaka jana, Mkutano Mkuu wa 41 wa UNESCO ulitangaza tarehe 7 Julai kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, na kufanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa kwa njia hii.
Siku hii haikuchaguliwa ovyoovyo. Julai 7, 1954, Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kilichoongozwa na baba wa taifa la Tanzania, Julius Nyerere, kilitangaza Kiswahili kuwa chombo muhimu cha kutafuta uhuru wa taifa, na kilifanikiwa kuwaunganisha wananchi kupata ushindi dhidi ya ukoloni.
Baada ya uhuru, Nyerere alitangaza Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nchi na kutaka kitumike katika shughuli zote rasmi za serikali. Hatua hii pia ilivunja kabisa majaribio ya wakoloni wa Magharibi waliokuwa wakijaribu kuwagawanya na hata kurudisha ukoloni kwa lugha.
Leo, Kiswahili kimekuwa lugha kubwa zaidi barani Afrika, na kina wazungumzaji zaidi ya milioni 200 duniani kote, na kukifanya kuwa mojawapo ya lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani. Kiswahili sasa sio tu ni lugha rasmi ya nchi za Afrika Mashariki kama Tanzania, Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, bali pia kimeingia katika madarasa ya shule za Afrika Kusini na Botswana.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Ally Khalfan alisema, “Kiswahili ni mali yetu ya kiroho na utambulisho wetu tukiwa waafrika, hivyo tunapaswa kujaa hisia ya ‘umiliki’ katika kuendeleza matumizi yake."
Kuna msemo wa kale wa Kichina unaosema, "Wale wanaotaka miti ikue lazima waimarishe mizizi yake; wale wanaotaka maji yatiririke mbali, lazima wapitishe vyanzo vyake". Iwe ni China au Tanzania na nchi nyingine za Afrika, utamaduni wa kitaifa ndiyo msingi na chanzo cha maendeleo.
Leo, tuna kila sababu ya kuchukua lugha na maandishi yake kama kianzio, kukumbatia na kuchimba tamaduni bora za jadi za nchi yetu, kuongeza imani na utamaduni wetu na hisia ya utambulisho kitaifa, na kukuza utamaduni wetu kwa Dunia nzima.