Kumbukumbu: Mwana Saigon Ally Sykes (1926 - 2013)

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
KUMBUKUMBU: ALLY SYKES (1926 - 2013) MWANA SAIGON
KASOMEWA KHITMA AKIWA BAHARINI ANAELEKEA VITANI BURMA

Leo imetimu miaka saba toka mzee wetu Bwana Aly Sykes alipofariki tarehe 19 May 2013 mjini Nairobi alipokwenda kwa ajili ya matibabu.

Siku moja tumekaa ofisini kwake pale Mtaa wa Makunganya tunaandika maisha yake.

Ilinichukua muda kumshawishi kukubali kuandika historia ya maisha yake kwani kila nikimgusia alikuwa ananipuuza anasema, ‘’Ah! Bwana we, wewe ushamwandika Bwana Abdul na Julius Nyerere inatosha hao ndiyo walikuwa watu muhimu mimi nina nini bwana.’’

Siku nyingine wala sisemi kitu nakaa kimya.

Siku nyingine akinambia, ‘’Mimi nina nini?’’

Namjibu, ‘’Una fedha nyingi.’’

Hatosema kitu atanitazama usoni kanikazia macho hapepesi.

‘’Mohamed wewe ushakunywa chai leo asubuhi?’’

Nitamjibu kwa mkato kuwa sijanywa.

Basi atasema, ‘’Ndiyo maana maneno mengi sana.’’

Atafungua pochi lake atachomoa noti atanipa kisha atasema, ‘’Haya nenda kanywe chai unajua bwana mtu kama hajanywa chai inakuwa matatizo kidogo gumzo haliishi.’’

Bwana Ally alikuwa kama vile ananambia zile vurugu zangu za kumghasi kuhusu kuandika wasifu wake ni kuwa nina njaa.

Ally Sykes alikuwa mtu wa maskhara sana.

Hapo ndiyo tushaagana nami nitanyanyuka nitashika hamsini zangu.

Ikawa sasa namghasi kuhusu kuandika maisha yake hadi akakubali na si sijui kwa nini alikubali.

Hii leo nilipoangalia nyuma na kuanza kumkumbuka Bwana Ally ndipo kikanijia kisa alichonihadithia cha yeye kusomewa khitma wakati bado yu hai yuko duniani anapumua.

Iko siku Bwana Ally aliwaalika rafiki zake chakula cha mchana nyumbani kwake Mbezi Beach na mimi nilikuwako na namkumbuka mtu mweingine alikuwa Hassan Diria na mkewe Bi. Skina.

Pale nikamkuta Bi. Bahia Lumelezi wageni wengine walikuwa bado hawajafika.

Bi. Bahia akawa anamnyooshea kidole Bwana Ally ananiambia mimi, ‘’Huyu baba yenu kamtesa sana mama yake Bi. Mruguru alipotoroka kujiunga na KAR.’’

Kisa hiki nilikuwa nakijua lakini Bi. Bahia akakieleza vizuri sana kwa upande wa vipi mama yake Bwana Ally alivyoathirika kuwa na watoto wawili vitani katika Vita Vya Pili Vya Dunia (1939 – 1945).

‘’Bi. Mruguru analia anajitupa chini anaomboleza anawataja wanae kwa majina Abdul na Ally wakati mwingine hadi anazimia,’’ Bi. Bahia ananieleza.

Hapo kijitepu rekoda changu ndani ya kichwa kimefunguka namrekodi Bi. Bahia neno kwa neno sentensi kwa sentensi.

Hayo anayoeleza Bi. Bahia ni mwaka wa 1942 na yeye Bi. Bahia ni msichana mdogo na ni uzawa mmoja na Bwana Ally, yaani ni rika moja.

Nikimwangalia Bwana Ally katulia kakaa kimya anamsikiliza Bi. Bahia na Bi. Zainab mama yetu, mke wa Bwana Ally yuko hapo na yeye pia yuko kimya.

‘’Akina mama wanamwendea Bi. Mruguru wanamwambia, ‘’Mama Abdul vibaya hivyo watoto wa hai hawajafa na Allah Insha Allah atawarejesha wote salama haifai kuomboleza kama hivyo, haifai kwa maiti sembuse kwa aliye hai?’’

Bwana Ally bado yuko kimya ni wazi kuwa maneno ya Bi. Bahia yamemrudisha nyuma mwaka wa 1942 na yamekumbusha mama na baba yake na yeye kijana wa miaka 16 alipotoroka nyumbani kwenda kwenye kambi ya KAR Kilwa Road kujiunga na jeshi tayari kwenda Burma kupigana.

Mjini walikuwa wakisema anaekwenda Burma kupambana na Wajapani harudi ila jina lake.

Wazee walikuwa wanawaficha watoto wao wa kiume uani.

Ally Sykes umri haukuwa unamruhusa kujiunga na jeshi lakini Waingereza walikuwa wameelemewa na vita na wakihitaji kila askari aliyeweza kupatikana na kubeba bunduki.

Ally akapelekwa Kabete, Kenya kwa mafunzo ya jeshi na hapo ndipo alipoanza kuonyesha uhodari wake wa kulenga shabaha.

Kila akipiga anapiga ‘’bull,’’ yaani katikati ya bango la kulenga shabaha.

Waingereza wakajua wamepata askari hodari wa kupambana na Wajapani katika misitu ya Burma.

Wakati wanakwenda Burma kutokea Mombasa meli zilizobeba askari kutoka Afrika ya Mashariki zikisindikizwa na Royal Navy moja ya meli zile ilipigwa na makombora na Wajapani ikazama pamoja na askari wote wakafa ila kijana mmoja kutoka Tanga akiitwa Magembe.

Taarifa zikaletwa nyumbani kwa Mzee Kleist kuwa mwanae Ally amekufa baharini akiwa njiani kwenda Burma baada ya meli yao kupigwa mabomu.

Hapo hapo pale nyumbani kwao watu wakafunga turubai kuomboleza msiba wa mtoto wa Kleist, kijana wa mtaani Ally.

Ally Sykes akasomewa khitma watu wakashukuru na tanga likaanuliwa na maisha yakaendelea.

Nakuachia wewe ufikiri mama yake Ally Sykes, Bi. Mruguru alikuwa katika hali gani alipopewa taarifa ya kifo cha mwanae.

Lakini ukweli ni kuwa meli iliyozamishwa na Wajapani haikuwa meli aliyokuwamo Ally Sykes.

Ally Sykes alifika salama Kurnegala Colombo na ilikuwa usiku na kaka yake alikuwa kwenye kambi mbali na kambi aliyofikia mdogo wake na taarifa ikamfikia kuwa katika askari waliowasili kutoka Afrika ya Mashariki yuko ndugu yake Ally Sykes.

Amri ya kutotoka usiku ilikuwa tayari lakini Abdul hakukubali alitoka na jeep yake usiku ule ule kwenda kumlaki nduguye na kulipokucha akahakikisha kuwa taarifa zinafika Dar es Salaam kuwa Ally amewasili salama Kurunegara Camp Colombo.

Nakuachia wewe tena ufikiri mama yake Ally Sykes furaha yake ilikuwaje alipopata taarifa kuwa mwanae yu hai.

Zaidi ya miaka 30 sasa imepita lakini naona kama jana niko ofisini kwa Bwana Ally tape recorder yake inazunguka anazungumza na mimi nimeshika notebook yangu na kalamu naandika hapa na pale namtazama na kumsikiliza baba yangu.

‘’Mohamed mimi nimesomewa khitma kabla sijafa,’’ Ally Sykes ananieleza.

Naamini ni watu wachache sana duniani waliopitia hili.

Huwezi kummaliza Ally Sykes alikuwa na mengi sana katika maisha yake.

Ally Sykes alikuwa akiwa na mimi katika hizi ‘’session,’’ zetu za kuandika maisha yake anazuia simu zote na haonani na mtu hadi tumemaliza.

Leo imetimia miaka saba toka Ally Sykes atutoke.

Kwangu alikuwa baba, mwalimu na rafiki.

Bi. Bahia alimtangulia Ally Sykes mbele ya haki kwa miaka mingi na Mkewe Hassan Diria, Bi. Skina.

Allah awarehemu wazee wetu hawa wote na awatie peponi.
Amin.

Sent using Jamii Forums mobile app
 

Attachments

  • BURMA INFANTRY.jpg
    8.1 KB · Views: 3
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…