Chadema wapata msukosuko Mwanza
Monday, 13 September 2010 08:20
Boniface Meena, Ilemela
UMATI wa wafuasi wa Chadema uliokuwa ukisukuma gari la mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Dk Willibrod Slaa nusura wapigwe mabomu ya machozi, lakini katibu huyo mkuu wa chama hicho akafanikiwa kutuliza askari waliotaka kuvuruga hali ya hewa.Wafuasi hao wa Chadema walikuwa wamekaidi amri ya polisi ya kuwataka waachane na kitendo hicho cha kulisukuma gari la mgombea huyo wa uraiskutoka uwanja wa Shule ya Msingi ya Mirongo hadi katikati ya jiji la Mwanza.
Uamuzi huo wa kulisukuma gari lililombeba Dk Slaa ulisababisha barabara alizokuwa akipitia kwenda katikati ya jiji kupitika kwa shida ama kusababisha zisipitike kabisa, kiasi cha polisi kuamua kutaka kutumia nguvu za ziada kuwatawanya.
Kabla ya polisi kuchukua hatua hiyo, Dk Slaa aliibuka na kuwakemea akiowataka wasitumie nguvu kubwa kutuliza shauku ya wananchi.
Akizugumza jana kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Igombe wilayani Ilemela, Dk Slaa alilaani kitendo cha polisi kutaka kutumia mabomu ya machozi kuutawanya umati wa wananchi uliokuwa ukisukuma gari lake.
Alisema kitendo cha polisi kutaka kuwarushia wananchi mabomu ya machovu hakikubaliki na kingevuruga uchaguzi na kuonekana kuwa si huru.
"alichotakiwa kufanya (kamanda wa polisi wa wilaya) OCD ni kuwapanga askari wake ili waangalie wananchi wasipate madhara na msafara uende kwa amani... lakini alishindwa kudhibiti na ninalaani kitendo hicho cha kutaka kutumia mabomu ya machozi," alisema Slaa.
Alisema kuwa OCD wa Nyamagana hakutimiza wajibu wake na kushangaa kwamba Jeshi la Polisi liliahidi kutopendelea upande wowote wakati wa uchaguzi, lakini anaona hali tofauti na na akamtaka OCD wa Ilemela amfikishie ujumbe huo OCD mwenzake.
"Mfikishie ujumbe huo mwenzako na sisi tutaufikisha kwa wakubwa zenu," alisema Dk Slaa.
Dk Slaa, ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Karatu kwa takriban miaka 15 na sasa ameamua kugombea urais, alisema ni muhimu kwa wananchi kufanya mabadiliko kwa kuiweka Chadema madarakani.
Source: Mwananchi