Kuna demu kiboko ya mabishoo angemnyoosha mbaya Ally Kiba!

Kuna demu kiboko ya mabishoo angemnyoosha mbaya Ally Kiba!

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Joined
Apr 29, 2016
Posts
20,743
Reaction score
25,564
RAPA Hormorapa aliwahi kutoa ngoma “Kiboko ya Mabishoo”, alipigwa tafu na Mfalme wa Temeke, Sir Nature. Hivi Harmorapa ana ukiboko gani wa mabishoo?
Kuna mdada, mrembo sana, demu tu. Ukimwona ungemchukulia poa. Huyo ndiye kiboko ya mabishoo. Angekuwa ndiye aliolewa na Ali Kiba, leo hii Mfalme wa Kariakoo, aliyehamishia Ufalme wake Tabata, angekuwa analia.
Kama katika msululu wa mademu wa Diamond Platnumz, wakiwemo aliowapa mimba, wakamzalia watoto, kisha akawananga na kuwadhalilisha mitandaoni na kwenye vyombo vya habari, mmoja wao angekuwa huyo demu kiboko ya mabishoo, mbona Mfalme wa Tandale, aliyejijengea palace la kifalme Madale, angekuwa analia ukata?
Demu kiboko ya mabishoo ni Lisa Lopes, mwite Left Eye kama mwenyewe alivyopenda kuitwa. Juni 10, 1994, Lefty Eye alijisalimisha kwenye mamlaka ya Idara ya Polisi Atlanta (APD), jimbo la Georgia. Akawekwa nyuma ya nondo. Unajua alifanya nini? Alimkomesha bishoo! Alimfanyia noma ile kinoma!
Unataka kujua Lisa alimkomesha vipi bishoo? Hold on! Tuanze hivi; Lisa wa vipaji vingi, rapa halafu anaimba. Multi-talent, si ndivyo mnaita? Kundi la TLC unalinyaka? Taasisi ya mtu tatu; T-Boz, Left Eye na Chilli. Miaka ya 1990 mbona tuliwakoma? Shukurani haziwezi kutosha kwa namna TLC walivyotuhudumia kwa muziki mzuri.
TLC hawajui kula za uso, albamu ya kwanza, “Oooooohhh… On The TLC Tip” ilinyoosha mbaya ilipotoka Februari 25, 1992. Mauzo nakala zaidi milioni sita. Ngoma kama Ain’t 2 Proud 2 Beg, Baby-Baby-Baby, What About Your Friends, Hat 2 Da Back na nyingine kutoka kwenye albamu hiyo, ziliteteresha amani ya soko la wanamuziki wengine.
Novemba 15, 1994, albamu ya pili, CrazySexCool, ikachukua nafasi. Nakala zaidi ya milioni 10 ziliuzika. Watoto walikuwa na pesa ‘mingi’. Ila wao hawakuziona.
Msala ulianza kwenye albamu ya kwanza, baada ya mafanikio ya mauzo, ilitarajiwa watoto wa kike wangesukuma mikoko ya kijanja Marekani kama Mercedes, Cadillac Limo, BMW, Jaguar, Bentley, Chevrolet na mingine, heee, si wakapewa Toyota Rav4?
Wakati huo waliona magoli kuendesha Rav4, ila waljpokatiza viwanja, wana waliwatonya kuwa kwa mafanikio yao hawakupaswa kusukuma gari hizo, Toyota!
TLC walikuwa chini ya lebo ya LaFace Records. Wakati huohuo, bosi wa LaFace, Antonio Reid ‘L.A’ na meneja wa TLC, Perri Pebbles, walikuwa mtu na mkewe. Basi bwana, Reid na Pebbles wakawaita T-Boz, Left Eye na Chilli, wakawakabidhi funguo za Rav4.
Wadada wakafurahi, si walikuwa bado washamba? Walipoanza kuendesha, wakaambiwa “mnapigwa”! Wakati huo warembo hawakujali kihivyo.
Mtiti ukaja Julai 1995, TLC wakatangazwa mufilisi. Eti, walifilisika kabisa. Wakati huo “CrazySexCool” inakimbiza kwa mauzo. Watu wakanong’ona; hivi inawezekana vipi watu watoke kuuza nakala milioni 10 wafilisike? Tena mauzo yakiendelea, albamu ilikuwa na miezi nane tu sokoni.
T-Boz, Left Eye na Chilli wakawaweka kikaoni Reid na Pebbles, wakaomba hesabu, jinsi fedha zilivyotumika mpaka kufilisika. Reid na Pebbles wakaanza kabobo. “Onyesheni hesabu”, wakajibu “Ooh, mnajua.” Kwani nini? Left Eye akatoa bastola. Utani pembeni kwenye pesa. Reid na Pebbles wakaingia chini ya meza.
Wadada wakasema wanavunja mkataba, ikawa vuta nikuvute mpaka mahakamani. Ndipo LaFace wakasalimu amri. Wakarekebisha mikataba, watoto wakaanza kuwa na pesa. Albamu ya tatu ilipotoka, “FanMail” ikiwa na ngoma za matukio kama No Scrubs, Unpretty na nyingine, mauzo yalifikia nakala zaidi ya milioni 14.
T-Boz, Left Eye na Chilli, wakaanza kuishi kitajiri, ndinga za kifahari, siyo Rav4 tena, halafu sio moja. Kila mmoja na mansion yake yenye starehe zote, na kila moja ilikuwa na gereji yenye mpaka magari mtano, anabadili tu. Kama sio undava wa Left Eye kuwashikia bastola Reid na Pebbles, unadhani wangekomesha unyonyaji? Left ni kiboko ya mabishoo!
Sasa turudi kule Left Eye alipolazwa mahabusu, Fulton County, Atlanta, Georgia. Ni hivi, baada ya albamu ya kwanza ya TLC “Oooooohhh… On The TLC Tip”, Left alianza kudeti na bitozi mcheza soka la Kimarekani (American Football), Andre Rison, aliyekuwa akikipiga Klabu ya Atlanta Falcon. Andre akawa anamchukulia Left ni demu tu, kwa hiyo aliona angeweza kumfanyia chochote.
Septemba 2, 1993, Left Eye, akashitaki polisi kuwa Andre alimpiga. Andre alikanusha na polisi hawakufanya kitu. Waliona ni mizinguo ya wapenzi. Si huwa wanasema “kofi la mpenzi haliumi?” hata ngumi pia, teke kadhalika, ila ngeu huwa haijifichi! Wengine huficha ngeu kulinda wapenzi wao. Sio Left Eye!
Hilo likaisha, Juni 8, 1993, Andre alirudi nyumbani kanunua pea tano za viatu. Zake pekee. Hakumnunulia Left Eye wakati waliishi nyumba moja. Left Eye akasema “huyu ananitania”. Jioni wakaagana, kila mmoja alikwenda viwanja na marafiki zake. Saa 11 asubuhi, Left Eye alikuwa wa kwanza kurejea. Ameshalewa. Akasema halali mpaka Andre arudi!
Andre aliporejea akakutana na Left Eye aliyeboresha hasira zake kwa pombe. Akamkwida! Swali likafuata: “Kwa nini umenunua viatu vyako peke yako mimi hujaninunulia? Unaleta ubinafsi sio? Unanichukulia demu poapoa eeh?”
Kila Andre alipojitetea, Left Eye hakuelewa kitu. Andre akaona dawa yake mchakato. Kofi lililoboreshwa linaitwa kelbu na kelbu iliyoboreshwa huitwa mchakato. Andre alimchabanga mchakato. Akambeba mpaka kitandani. Akamlaza na kumkalia juu ili kumtuliza. Yupo wa kutulizwa lakini hakuwa Lisa. Left Eye kiboko ya mabishoo.
Andre alipoona Left Eye hatulii, akaona bora aondoke zake, ampe muda ili angerudi pengine angemkuta hasira zimepungua. Aah wapi! Kitendo cha Andre kuondoka Left Eye alikitafsiri kuwa dharau. Akachukua viatu ambavyo Andre alijinunulia, akavichoma moto kwenye tab ya kuogea.
Mansion waliyokuwa wanaishi ni ya Andre, akaichoma moto. Akaenda kwenye gereji ya nyumba, akaharibu magari ya Andre. Wakati nyumba inateketea, yeye akakaa kwa nje, akiitazama. Kama anayehakikisha kazi yake ilivyokwenda vizuri.
Umeona? Huyo ndiye Left Eye kiboko ya mabishoo, kosa kujinunulia viatu peke yake, ugomvi wake mpaka nyumba iliteketea, magari na viatu vyenyewe vilichomwa. Andre mchozi ulimwagikaje baada ya kurudi nyumbani?
Sasa jiulize; Ali Kiba kakosana na mke wake. Ni magomvi ya kifamilia. Hivi yule Amina wa Mombasa, Kenya angekuwa Left Eye, moto wake ungekuwaje? Si tungesikia sasa hivi mali zote za Kiba zimeteketea? Amina wa watu nasikia kakubali yaishe, kaenda zake kwao bila timbwili.
Jiulize kuhusu Diamond. Kati ya wanawake zake, mmoja angekuwa na ubongo kama wa Left Eye, si kuna siku tungesikia nyumba za Madale, Sinza au hata ofisi ya WCB na magari vimeteketea? Left Eye, Lisa, alikuwa kiboko ya mabishoo.
Bonge la mwanamuziki, lakini mtata hasa. Mtu wa noma ile kinoma. Mungu alimchukua kwa ajali ya gari Aprili 25, 2002, La Ceiba, Honduras.


Ceedit : mwanaspoti
 
Back
Top Bottom