SoC04 Kuna hadithi ya Tanzania ya kikanda kwenye nadharia ya Tanzania tuitakayo

SoC04 Kuna hadithi ya Tanzania ya kikanda kwenye nadharia ya Tanzania tuitakayo

Tanzania Tuitakayo competition threads
Joined
Sep 18, 2019
Posts
6
Reaction score
2
Na sanidi andiko hili kwa masilahi sufufu ya ardhi hii ambayo ndio chimbuko la Chifu Mkwawa, asili ya Chifu Mirambo, alipozaliwa Chifu Kimweri na Mtemi Isike na ndio taifa liongozwalo na Chifu Hangaya. Kwenye taswira za nchi nyingi zilizofanikiwa nyuma yake kuna nguzo iitwayo Nadharia ya maendeleo ya kikanda.

Nadharia ya maendeleo ya kikanda (regional development theory) ni mkusanyiko wa nadharia nyingi ndani yake, zote kwa jumla wake zinajumuisha dhana na miundo tofauti tofauti ya ukombozi wa kiuchumi inayolenga kuleta usawa wa kimaendeleo na kubainisha sababu za utofauti wa kimafanikio baina ya kanda moja na nyingine na namna bora ya kubuni sera zitakazoleta uwiano sawa wa kimaendeleo na uchumi endelevu.

Moja ya nadharia hizo ipo ile iliyoasisiwa na bwana Walter Rostow katika miaka ya 1960, ijulikanayo kama nadharia ya hatua (stage theory), kwa mujibu wa nadharia hii zipo hatua tano muhimu za kufuatwa kwa ajili ya maendeleo ya kanda yoyote ile.

Hatua ya kwanza ni kuhakikisha kuwa kuna uwepo wa usawa wa teknolojia na mifumo ya kijamii baina ya kanda moja na nyingine. Pili uwekezaji ufanyike kwenye maeneo husika kwa lengo kuu la kutumia malighafi zizalishwazo au zinazopatikana katika eneo husika, pia uwekezaji huo uambatane na miundombinu imara ya viwanda, usafirishaji na mawasiliano.

Kisha huja hatua ya tatu ambapo kanda husika inakua imeimarika kiasi cha kuwa na uwezo wa kupokea miradi mikubwa ya kimaendeleo pamoja na wawekezaji kutoka nje bila kuathiri uwekezaji wa ndani wa kanda hiyo.

Baada ya hatua hizo tatu kanda husika huingia kwenye hatua ya nne ya ukomavu, hapa kanda husika itakua na uwezo wa kuwa na mgawanyo wa vitega uchumi pamoja na muingiliano wa kibiashara na kiuwekezaji baina ya kanda na watu kutoka nje, ni katika hatua hii kanda husika huweza kuzalisha bidhaa ambazo hapo kabla zilikua zinaagizwa kutoka nje.

kisha inafuata hatua ya tano na ya mwisho, kutokana na mafanikio katika kila hatua iliyopitia kanda husika itaweza kuzalisha kwa wingi bidhaa walizokua wakiagiza kutoka nje hapo kabla. Hapa ndipo pale ambapo kanda husika inakuwa na msuli wa kutosha wa kupambana kibiashara kwenye soko la ndani na la nje kwa wakati mmoja.

Tunaweza kutabahari nadharia hii ya maendeleo ya kikanda kwa kuandaa mpango wetu wa maendeleo wa miaka 25 kwa kuzingatia vipengele na hatua rafiki katika kuziendeleza kanda zetu za kimaendeleo, tunaweza kuthubutu kuigawa nchi yetu kwenye kanda sita za kiuchumi kama tulivyoigawa katika kanda mbali mbali za kipolisi kutokana na unyeti wa sekta ya ulinzi.

Tunaweza kuigawa nchi yetu katika kanda ya mashariki, kanda ya magharibi, kaskazini, kusini, kanda ya kati pamoja na kanda ya juu kusini kisha shughuli za uzalishaji zipatikanazo katika kanda husika ziwekewe nguvu, uwe ni mpago wa kiuchumi wa kitaifa, bajeti itengwe na kugaiwa kwa kila kanda kwa usawa unaostahiki kulingana na lengo la uzalishaji la mwaka mzima kwa kanda husika.

images (25).jpeg


Kielelezo 1.1 Ramani ionyeshayo mgawanyo wa Tanzania katika kanda sita. (Picha kwa hisani ya Mapline).

Viwanda na miundombinu wezeshi katika uzalishaji ijengwe kwenye kila kanda kupitia mpango huu wa Tanzania ya kikanda, mfano kanda ya mashariki ambayo inawakilishwa na mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na pwani yaanzishwe mashamba makubwa ya miwa pamoja na viwanda vya uhakika vya uzalishaji sukari.

Pia kilimo cha mpunga kiboreshwe na kuongezewa nguvu katika kanda hii ili kuweza kuwaondoa wakulima wadogo kwenye ulimaji holela na wa kizamani na kuwafanya kuwa wakulima wa kisasa ili walime kwa ajili ya biashara na sio kwa ajili ya matumizi ya nyumbani pekee.

Taaluma mpya ya uvuvi wa kisasa ifundishwe kwa wavuvi wabobezi wa maeneo ya pwani huku viwanda vya kusindika samaki na uzalishaji bidhaa zitokanazo na samaki visimikwe kwenye maeneo husika ili kurahisisha upatikanaji wa vyakula bahari.

Jitihada kubwa iwekwe katika kuinua kilimo cha mtama, uwele pamoja na alizeti, uwepo mpango wa kuimarishwa kwa viwanda vya kuchakata mazao hayo sambamba na ujenzi wa viwanda vya kisasa vya uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na mazao hayo katika maeneo ya kanda ya kati yenye mikoa kama Dodoma,Tabora na Singida.

Huko kunako kanda ya kusini kwenye mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma serikali inaweza kuja na mpango kabambe kwenye kukiendeleza kilimo cha korosho, nazi, ufuta na mahindi, badala ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi uwekezaji ufanyike ndani ya kanda husika bidhaa kama siagi za korosho, mafuta ya korosho, mafuta ya nazi na bidhaa nyingine zitokanazo na mazao tajwa ziweze kuzalishwa ndani ya kanda hiyo chini ya viwanda vikubwa na vyenye kuhodhi teknolojia ya kisasa.

Tunaweza kuchukua mifano toka ughaibuni kwenye nchi zilizofuzu somo la maendeleo ya kiuchumi, na hapa tunaweza kuiteua China kama kiigizo chetu, mpango wa maendeleo ya kikanda nchini humo ulianzishwa mnamo mwishoni mwa miaka ya 1970 na mwanzoni mwa miaka ya 1980 chini ya uongozi wa Deng Xiaoping.

Mpango huo wa kimaendeleo ulipelekea ukuaji mkubwa wa kiuchumi kwenye miji kama Tianjin, Qingdao, Guangzhou, Shenzhen, Zhuhai, Shantou, Xiamen na mingine mingi huku ikisaidia katika kuleta usawa wa kiuchumi katika nchi na kuongeza shauku ya uwekezaji na kupunguza hali ya ukosefu wa ajira.

Kama nadharia hii ikitumika kuimarisha kila kanda husika ndani ya miaka 25 ijayo Tanzania inaweza kuongeza idadi ya mikoa zaidi ya kumi yenye hadhi ya kuitwa jiji, pia mlundikano wa watu katika mikoa kama Dar es Salaam, Arusha na Mwanza utapunguwa kwasababu ya mgawanyo wa rasilimali na uwiano wa kiuchumi unaoshabihiana kwenye kanda mbalimbali.

Nadharia hii pia itasaidia ongezeko la ajira kwasababu kila kanda italazimika kuajiri wafanyakazi waishio kwenye kanda husika kwenye ngazi ngazi za uzalishaji na uwajibikaji, mzunguko wa hela utakua juu na tija ya uwekezaji wa ndani itaongezekaa. Kupitia mpango huu matumizi ya bidhaa zizalishwazo nchini yatakuwa makubwa yatakayopunguza kiwango cha matumizi cha raia wa kawaida.

Kama tukiweza kuzalisha wenyewe sukari ya kutosha, nguo, mafuta, vyakula mbalimbali, vito vya thamani, vifaa vya ujenzi na umeme na bidhaa nyingine nyingi muhimu katika maisha yetu ya kila siku basi tutaweza kupambana na mdudu aitwae umaskini aliyedumaza akili zetu na kutufanya tubaki na njia zile zile za uzalishaji alizotuachia mkoloni miaka 63 iliyopita.

Wasalaam.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom