Hakuna mgombea binafsi
Yasema mahakama haina mamlaka kugusa Katiba
Wengi wapokea hukumu hiyo kwa mshangao
Jaji Mkuu Augustino Ramadhani, akiongoza Majaji wengine sita wa Mahakama ya Rufaa wakati akitoa hukumu kuhusu mgombea binafsi kufuatia serikali kukata rufaa katika mahakama hiyo.
Mahakama ya Rufani imesema haina mamlaka ya kuruhusu mgombea binafsi katika uchaguzi wa kisiasa, bali chombo chenye mamlaka hayo ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo ni chombo pekee cha kutunga sheria.
Uamuzi huo uliotolewa jana umetengua uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania kuruhusu mgombea binafsi. Hukumu hiyo ilitolewa kufuatia rufani ya Serikali dhidi ya Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye alikuwa mjibu rufani, aliyefungua kesi Mahakama Kuu akitaka kuruhusiwa mgombea binafsi na mahakama hiyo kumkubalia.
Uamuzi wa Mhakama ya Rufani ilisomwa jana baada ya kusikilizwa na jopo la majaji saba liloketi chini ya Jaji Mkuu Augustino Ramadhan, Jaji Eusebia Munuo, Januari Msofe, Nathania Kimaro, Dk. Stephen Bwana, Mbarouk Salim na Benard Ruanda, Februari 8, mwaka huu.
Kabla ya kusoma hukumu, Jaji Ramadhan alisema uamuzi huo unatokana na mchango uliotolewa na majaji wote saba na kwamba kwa bahati mbaya Jaji Salim hakuwepo kutokana na kuwa mkoani Tabora kikazi.
Jaji Ramadhan alisema baada ya kupitia madai ya pande zote mbili, mrufaa serikali na Mtikila, jopo hilo limeona kwamba suala hilo linatakiwa kushughulikiwa na Bunge ambalo ni chombo kinachotunga sheria na kwamba lina mamlaka ya kufanya mabadiliko.
Mbali na mahakama hiyo kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu, imeamuru pande zote mbili kujilipia gharama za kesi hiyo. Rufaa hiyo namba 45 ya mwaka jana, inaeleza kwamba serikali iliwasilisha rufaa hiyo mahakamani hapo ikipinga hukumu ya iliyotolewa na waliokuwa majaji wa Mahakama Kuu, Jaji Mstaafu Amir Manento, Salum Massati, sasa Jaji wa Mahakama ya Rufani na Thomas Mihayo (Mstaafu), ambao walikubaliana na ombi na Mtikila na kuruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi.
Awali, katika usikilizwaji wa rufaa hiyo, serikali iliendelea kungangania msimamo wa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu unaoruhusu kuwapo mgombea binafsi katika chaguzi za kisiasa, Jamhuri iliwakilishwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju.
Akitoa hoja zake wakili Masaju, alidai kuwa mahakama ilikosea kufikia uamuzi wa kuruhusu kuwapo kwa mgombea binafsi, kwa madai kwamba haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi inayohusu Katiba ya nchi na kwamba mahakama imepewa mamlaka kisheria kusikiliza tu kesi zinazohusu sheria nyingine au vitendo vyovyote vinavyokiuka Katiba na si Katiba.
Masaju aliendelea kudai kuwa mahakama haina mamlaka ya kutengua Katiba ya nchi kama ilivyofanya katika uamuzi wake na kwamba, ilikosea kuamua shauri hilo kwa kuzingatia sheria za kimataifa za haki za binadamu, wakati Katiba ya mwaka 1977 ina kifungu kinachoipa mahakama mamlaka ya kuamua.
Masaju aliliomba jopo la majaji hao kutengua uamuzi huo wa Mahakama Kuu kwa madai kwamba, haukujengwa kwa misingi inayokubalika kisheria.
Akijibu hoja hizo, wakili wa mrufaniwa, Richard Rweyongeza alidai hoja zilizotolewa na upande wa mrufani, hazina msingi, kwani malalamiko ya kutumia sheria za kimataifa za haki za binadamu, yameelekezwa kwa mahakama bila sababu yoyote.
Baadaye Mahakama ya Rufani iliwaalika marafiki wa Mahakama, ambao ni Maprofesa Kalamagamba Kabudi na Jwani Mwaikusa, ambao ni wahadhiri wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mkurugenzi wa Mashtaka wa Zanzibar, Othman Masoud na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rajab Kiravu.
Wakati wa kutoa hoja zao Aprili 8, mwaka huu walitofautiana kuhusiana na mhimili wenye mamlaka ya kubadili katiba.
Profesa Kabudi na Masoud walisema kuwa Mahakama haina uwezo huo bali Bunge wakati Profesa Mwaikusa alisema kwa mujibu wa mgawanyo wa madaraka miongoni mwa mihimili ya dola, Mahakama ina uwezo wa kuamua kuhusu katiba.
Kwa upande wake, Kiravu alilieleza kuwa uamuzi wowote utakaotolewa na Mahakama ya Rufaa kukubaliana na ule uliotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania kuruhusu mgombea binafsi, utaathiri uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Mara ya kwanza, serikali ilikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu, katika Mahakama hiyo ya Rufaa mwaka 2007, kwa madai kuwa mahakama hiyo ya chini ilikosea kisheria kutafsiri Ibara ya 21(1) (c), 39 (1) (c) (b) na 69 (1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Hata hivyo, rufaa hiyo ilitupiliwa mbali na Mahakama ya Rufaa baada ya kukubaliana na ombi la wakili wa Mtikila, Rweyongeza kwamba rufaa hiyo haina msingi na kwamba imejaa dosari za kisheria.
Awali, katika hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Mei, mwaka 2006, ililiruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi, kwa sababu Katiba ya nchi inatoa haki hiyo.
Mapema Mwaka 1993, Mtikila alishinda kesi kama hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, lakini licha ya uamuzi huo wa mahakama, Bunge lilishindwa kutunga sheria ya kuruhusu mgombea binafsi hivyo alifungua kesi hiyo ya kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambapo alishindwa tena. Akiongea na waandishi habari baada ya hukumu hiyo, Mtikila alisema hajakubaliana na hukumu iliyotolewa na jopo hilo na kwamba mahakama haijatenda haki kwa wananchi.
Waishangaa hukumu
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengondo Mvungi, alisema kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania na historia ya haki za binadamu duniani mahakama yenye mamlaka ya juu imejitia kitanzi yenyewe.
Alisema huo ndio mwisho wa uhuru wa mahakama Tanzania, lakini akasema Watanzania hawana sababu ya kukata tamaa kufuatia uamuzi huo.
Dk. Mvungi alisema mahakama kwa kusema kuwa haina uwezo wa kutafsiri Katiba na kuruhusu mgombea binafsi imejitumbukiza kaburini kwa hiyari yake yenyewe.
Katika hili hatuangalii suala la mgombea binafsi pekee tunaangalia uwezo wa mahakama wa kutafsiri Katiba ambayo inalinda haki za binadamu
Mahakama inapaswa kujua kuwa haki za binadamu zilitangulia kabla ya mahakama na dola na haki hizo za binadamu haziundwi na Katiba bali Katiba yenyewe inazitambua tu, alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema ameshtushwa na uamuzi huo na kusema kuwa inaonyesha kuwa kuna haja ya kuandika Katiba mpya itakayojali demokrasia zaidi.
Alisema ameshangazwa kusikia mahakama hiyo ikijivua wajibu wake wakati ndiyo inawajibika kutafsiri Katiba na sheria mbalimbali za nchi.
Lipumba alisema Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu kunakatisha tamaa na kunashusha hadhi ya mahakama hizo za juu.
Mkurugenzi wa Habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Erasto Tumbo, alisema hakutarajia uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Rufaa kwani kufanya hivyo ni kuinyonga demokrasia kwa makusudi. Alisema kama mahakama hiyo ya juu kuliko zote inasema kuwa haina uwezo wa kutafsiri Katiba basi kuna tatizo kubwa ambalo lazima lishughulikiwe.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema mgombea binafsi ni haki ya kila Mtanzania iliyomo ndani ya Katiba hivyo haoni sababu ya serikali kuwa na kigugumizi.
Alisema kila Mtanzania ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa hivyo suala la mgombea binafsi halihitaji mjadala mrefu kama inavyoendelea sasa.
Lazima tufikiri upya namna ya kuwatendea haki wananchi tuangalie haki zao za kushiriki chaguzi wakiwa wagombea ama wapiga kura bila kuwa katika chama chochote, alisema Dk. Bana.
CHANZO: NIPASHE