- Source #1
- View Source #1
Wakuu nahitaji kupata uhalisia wa hii taaria niliyokutana nayo huko mtandao wa X kwamba Zitto Kabwe anahusishwa na utekaji wa Nondo ni upi uhalisia wa taarifa hii?
- Tunachokijua
- Zitto Kabwe ni mwenyekiti mstaafu wa chama cha ACT- Wazalendo aliyehudumu nafasi hiyo kwa muongo mmoja. Zitto alihamia ACT- Wazalendo mwaka 2015 baada ya kuvuliwa uanachama ndani ya CHADEMA kutokana na kukiuka katiba ya chama hicho kwa kupeleka mahakamani migogoro ambayo ilitakiwa kushughulikiwa ndani ya chama kwa mujibu wa katiba. Kupitia tiketi ya CHADEMA Zitto aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini mwaka 2005 mpaka 2015. Akiwa kiongozi mstaafu ndani ya ACT- Wazalendo ameendelea kuwa mwanachama muhimu ndani ya chama hicho kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika siasa za Tanzania.
Katika kupambana dhidi ya vitendo viovu hasa utekaji na mauaji ya raia, Zitto amekuwa mstari wa mbele kukemea na kupaza sauti kwa mamlaka ili kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa huku utawala wa kisheria unaozingatia demokrasia na haki za binadamu ukitakiwa kuimarishwa.
Mnamo mwezi Disemba mosi 2024 majira ya asubuhi lilitokea tukio la utekaji ambapo mwenyekiti wa ngome ya vijana ya chama cha ACT- Wazalendo Abdul Nondo alitekwa na watu wasiojulikana na baadaye kutelekezwa katika fukwe za Coco pembezoni mwa bahari ya Hindi na baadaye kupata msaada wa wasamaria wema waliomfikisha ofisi za makao makuu ya chama hicho Magomeni akiwa amejeruhiwa katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Kumeibuka Chapisho mtandaoni lenye taarifa kuwa Zitto anahusishwa na utekaji wa Abdul Nondo.
Je, ni upi uhalisia wa taarifa hiyo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck umebaini kuwa hakuna chanzo cha kuaminika kilichotoa taarifa hiyo. Vilevile taarifa hiyo haijaweka wazi chanzo cha taarifa hivyo kushindwa kuthibitisha madai hayo na hivyo kuwa taarifa isiyo ya kweli.
Aidha taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi baada ya kupatikana kwa Nondo ilieleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kuwapata wahusika wa tukio hilo ikiwa ni sambamba na kupata ukweli wa sababu au chanzo cha tukio hilo ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Pamoja na hayo Zitto amekuwa mstari wa mbele katika kupigia kelele tukio la kutekwa kwa Nondo akitaka watekaji kumuachia salama, hata baada ya kupatikana kwake ameonekana akiendelea kushirikiana na viongozi wengine katika kuhakikisha anapatiwa matibabu dhidi ya majeraha aliyoyapata.