Kuongeza Kazi Zenye Hadhi/Staha ni Muhimu Katika Kupunguza Pengo la Usawa Duniani

Kuongeza Kazi Zenye Hadhi/Staha ni Muhimu Katika Kupunguza Pengo la Usawa Duniani

The Sheriff

JF-Expert Member
Joined
Oct 10, 2019
Posts
747
Reaction score
2,112
UPUNGUFU WA KAZI ZENYE HADHI NA STAHA DUNIANI banner.jpg


Kazi zenye hadhi/staha (decent work) ni kazi zinaofuata misingi ya haki, usawa, usalama, na fursa za maendeleo kwa wafanyakazi. Mpango wa Kazi zenye Hadhi ni wazo lililopendekezwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) na linalenga kuhakikisha kuwa kila mtu anapata kazi bora na inayostahili, ambayo inachangia katika maendeleo yao binafsi na ustawi wa jamii.

Kazi nzuri na yenye hadhi ina umuhimu mkubwa katika kufanikisha maendeleo endelevu, na hili limebainishwa vyema na Lengo la 8 la Maendeleo Endelevu ambalo linalenga "kuchochea ukuaji wa uchumi endelevu, jumuishi na thabiti, ajira kamili na yenye tija kwa wote."

ILO inasisitiza kuwa ni muhimu kuwepo kwa ajira nzuri kwa kila mtu, bila ubaguzi wowote. Hii inamaanisha kuwa watu wanapaswa kupata ajira yenye hadhi, uhakika, na kipato cha kutosha ili kukidhi mahitaji yao ya msingi. Lakini pia wafanyakazi wanapaswa kuheshimiwa na kulindwa katika mazingira ya kazi; hii ni pamoja na uhuru wa kujieleza, uhuru wa kushiriki katika vyama vya wafanyakazi, kulipwa kwa haki na stahiki zao, na kulindwa dhidi ya ubaguzi na unyanyasaji kazini.

Ili kazi iwe yenye hadhi wafanyakazi pia wanapaswa kufanya kazi katika mazingira salama na yenye afya. Hii inahusisha kuweka mikakati ya kuzuia ajali na magonjwa kazini, kutoa vifaa sahihi vya kujilinda, na kuhakikisha haki ya kupumzika na kupata likizo. ILO pia inasisitiza kuwa wafanyakazi wanapaswa kuwa na sauti katika mchakato wa maamuzi, na kushirikishwa katika majadiliano na waajiri na serikali.

Pamoja na hayo, kazi nzuri inapaswa kutoa fursa ya kujenga ustadi, kuendeleza ujuzi, na kufikia ustawi binafsi. Kazi yenye staha pia inatoa nafasi za kujifunza na kuboresha hali ya maisha, jambo ambalo linaleta furaha. Kazi nzuri inamheshimu na kumtambua yeyote kama mwanadamu anayepaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Inahakikisha kuwa wafanyakazi wanatendewa kwa haki, wanapata stahiki zao, na wanahusishwa katika mchakato wa maamuzi. Hii inakuza hisia ya thamani na kujitambua kama sehemu ya jamii.

Uhaba wa Kazi Zenye Hadhi Duniani

Hata hivyo, pamoja na mambo yote pamoja na wito wa jumuiya ya kimataifa kuhusu ubora wa kazi kwa watu wote, bado kuna safari ndefu sana mbele yetu hadi kufikia malengo. Hii ni kwasababu upungufu mkubwa wa ajira zenye hadhi unaendelea kuwepo katika maeneo mbalimbali duniani. Bado kuna mamilioni ya watu wanafanya kazi katika mazingira ya kitumwa na yasiyojali utu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kazi Duniani (ILO), takriban watu milioni 473 duniani wanakosa fursa ya kupata kipato kupitia ajira. Hii ni pamoja na watu milioni 205 wasio na ajira - wale ambao wanakidhi mahitaji ya soko la ajira na wapo tayari kupokea ajira muda wowote. Kwa hiyo, kuna watu milioni 268 ambao hawakidhi mahitaji haya lakini wanahitaji ajira.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa watu bilioni mbili kati ya wale walioajiriwa wana kazi zisizo rasmi, maana yake ni kwamba wana uwezekano mdogo sana wa kuwa na haki kazini, uhuru wa kupaza sauti au kufurahia faida za mfumo wa ulinzi wa kijamii. Ulinzi wa kijamii unajumuisha bima ya afya, bima ya ajira, na fao la uzeeni. Aidha, watu milioni 214 wako katika ajira lakini hawawezi kujinasua kutoka katika umaskini wa kupindukia – yaani wao na familia zao wanaishi chini ya dola 1.90 za Kimarekani kwa siku.

UPUNGUFU WA KAZI ZENYE HADHI NA STAHA DUNIANI.jpg

Hii inaonesha kuwa idadi kubwa ya watu duniani wanakabiliwa na ukosefu wa fursa za kazi nzuri zenye hadhi. Wanakosa uhakika wa kipato, haki kazini, na upatikanaji wa huduma za ulinzi wa kijamii. Hii inaathiri maisha yao na uwezo wao wa kujikwamua kutoka katika umaskini wa kipato. Ili kuunda jamii yenye usawa na maendeleo endelevu, juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha upatikanaji wa kazi nzuri kwa kila mtu na kuboresha hali ya wafanyakazi wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi.

Suala la upatikanaji wa msaada wa kipato kwa wale wanaopoteza ajira pia ni tofauti sana duniani kwani ni asilimia 47 tu ya idadi ya watu wanaweza kunufaika na ulinzi wa kijamii. Mwaka 2020, takriban watoto milioni 160 duniani walikuwa katika ajira za watoto, wengi wao wakifanya kazi katika kilimo. Hii, pamoja na watu takriban milioni 28 wanaofanya kazi kwa kulazimishwa, inamaanisha kuwa jumla ya watu milioni 188 wako katika aina za kazi ambazo zinapaswa kuondolewa.

Wanawake na vijana wanakabiliwa na hali mbaya sana katika soko la ajira, ambayo ni ishara ya pengo kubwa la usawa katika ulimwengu wa kazi katika nchi nyingi. Kimataifa, kiwango cha ushiriki wa nguvu kazi ya wanawake kilikuwa asilimia 47.4 mwaka 2022, ikilinganishwa na asilimia 72.3 kwa wanaume. Pengo la asilimia 24.9 linamaanisha kuwa kwa kila mwanaume asiye na shughuli za kiuchumi, kuna wanawake wawili kama hao. Vijana (wenye umri wa miaka 15-24) wanakabiliwa na changamoto kubwa katika kupata ajira nzuri na kudumisha ajira hizo. Kiwango chao cha ukosefu wa ajira ni mara tatu zaidi ya watu wazima (wenye umri wa miaka 25+).

Yapi Fafanyike?

Kuhakikisha watu wanapata ajira zenye hadhi ni changamoto kubwa ambayo inahitaji juhudi za pamoja za serikali, wafanyakazi, waajiri, na jamii nzima.

Kwa mfano, kupatia watu elimu bora na mafunzo yanayolingana na mahitaji ya soko la ajira ni muhimu kwani inaweza kuimarisha mifumo ya elimu, kutoa mafunzo ya ufundi stadi, na kuendeleza programu za mafunzo ya kuendeleza ujuzi.

Kuunda mazingira mazuri kwa ujasiriamali na kukuza sekta binafsi pia ni eneo muhimu kufanyiwa kazi. Serikali zinaweza kutoa sera na rasilimali za kuchochea ujasiriamali, kusaidia biashara ndogo na za kati, na kukuza mazingira ya biashara yenye urafiki kwa ukuaji wa ajira. Lakini ni muhimu pia kujenga mfumo thabiti wa ulinzi wa kijamii ili kuhakikisha kuwa watu wanapata msaada wanapopoteza ajira au wanapokabiliwa na hali ngumu.

Serikali pia zinapaswa kuweka sera za kazi ambazo zinalenga kukuza ajira zenye hadhi. Hii inaweza kujumuisha kuweka viwango vya chini vya mshahara, kusimamia masuala ya usalama na afya kazini, kuimarisha haki za wafanyakazi, na kuendeleza mazungumzo ya kijamii kati ya wafanyakazi, waajiri, na serikali.

Lakini pia ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kushughulikia changamoto za ajira zenye hadhi. Nchi zinaweza kufanya kazi pamoja kubadilishana uzoefu, teknolojia, n.k. Pia, ni muhimu kuimarisha ushirikiano katika masuala ya biashara, uwekezaji, na ajira ili kuhakikisha fursa sawa za ajira kwa watu duniani kote. Kwa kufanya kazi kwa pamoja na kuchukua hatua hizo, dunia inaweza kufikia lengo la kutoa ajira zenye hadhi kwa watu wote. Hii itasaidia kupunguza umaskini na kujenga jamii yenye usawa.

Kuongeza ajira na kuhakikisha kazi zina utu kwa wote ni sehemu muhimu ya maendeleo endelevu. Ajira bora na mazingira mazuri ya kazi husaidia kupunguza pengo la usawa na umaskini, na kuwawezesha watu, hasa wanawake, vijana, na wale walio katika mazingira hatarishi kama watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, tunasaidia nchi washirika katika kuunda na kukuza ajira zinazotoa kipato cha haki, kuhakikisha mazingira salama ya kufanyia kazi, kutoa ulinzi wa kijamii, na kulinda haki za wafanyakazi.
 
Back
Top Bottom