SoC02 Kupiga mswaki, sayansi na utaratibu? Au shaghalabaghala alimradi meno yawe safi?

SoC02 Kupiga mswaki, sayansi na utaratibu? Au shaghalabaghala alimradi meno yawe safi?

Stories of Change - 2022 Competition

guddi

New Member
Joined
Sep 5, 2021
Posts
3
Reaction score
2
KUPIGA MSWAKI, SAYANSI NA UTARATIBU? AU SHAGHALABAGHALA ALIMRADI MENO YAWE SAFI?

Wote tunaweza kukubaliana kuwa kupiga mswaki ni kati ya zoezi rahisi sana kufanya mithili ya kunywa maji au uji, lakini licha ya zoezi hili kuwa rahisi bado magonjwa ya kuoza kwa meno na magonjwa ya fizi yamekua yakiathiri watu wengi sana kwenye kitengo cha afya ya kinywa na meno. Kupiga mswaki kunasaidia kuondoa utando wa mabaki ya chakula ambao husababisha meno kuoza na magonjwa ya ufizi pale bacteria wanapoyameng’enya, Pamoja na kutia madini ya floridi yanayolinda meno kuoza. Hivyo basi tunaweza kukubaliana huenda sababu ni watu kupiga mswaki bila kutumia dawa ya meno yenye madini ya floridi au kutokupiga mswaki kikamilifu, hapa ina maana mtu ana dawa ya meno yenye madini ya floridi lakini kwa sababu moja au nyingine hapigi mswaki kikamilifu. Hapa wana Jamii forum tuna ndege wawili na tunawaua kwa mawe mawili na wote ni lazima wafe akifa mmoja akibaki mmoja tatizo litakua palepale.

Jiwe la kwanza ni dawa za meno na madini ya floridi. Kwa ufupi tukizungumzia dawa za meno na madini ya floridi, sio dawa zote za meno zilizopo sokoni zina kiasi cha kutosha cha madini ya floridi ambacho ni 1000 hadi 1500 ppm (parts per million). Hapa siwezi kusema moja kwa moja ni dawa gani haina madini ya floridi ya kutosha maana kusema hilo inahitaji utafiti wa kutosha hivyo kwako wewe msomaji na mwana Jamii Forum kutafiti na kupata brandi yako utakayoiamini na hii ni rahisi ukichukua dawa yako ya meno ukiangalia kwenye yaliyomo (ingredients) utaweza kuona mfano picha ifuatayo.

Chanzo Cha picha Google
Pia unaweza kumuuliza tu daktari wako au daktari yeyote wa meno. Binafsi mimi mwandishi natumia dawa ya meno aina ya colgate. Hapa ndege wa kwanza tushamuua tayari wote tunafahamu sio kila dawa ya meno ni nzuri na uzuri wa dawa tunaupima kwa kuangalia kiasi cha madini ya floridi na ushauri juu ya dawa nzuri tunaupata kwa wataalamu wa afya ya kinywa na meno, wote tunamfuata ndege wa pili kwa jiwe la pili.

Jiwe la pili ni ukamilifu wa upigaji mswaki wenyewe, je mswaki inatakiwa upigwe mara ngapi? na muda gani? na tutumie mda gani kupiga mswaki?

Nikianza na mswaki inatakiwa upigwe mara ngapi kwa kawaida inashauriwa na wataalamu wa afya ya kinywa na meno kupiga mswaki kila baada ya kula chakula, hivyo kwa wenye kula milo mitatu mara tatu, miwili mara mbili lakini wengi wetu watanzania na wanajamii forum wenzangu tutakubaliana kuwa makazini mwetu wachache sana wana sehemu za kupigia mswaki inaweza kua mabafu, vyoo au ata sink la kutemea.

Lakini wengi wetu tunatoka majumbani mwetu asubuhi kwenda kazini na tunarejea jioni kupumzika hivyo wataalamu wakazingatia mambo yote wakashauri tupige mswaki mara mbili kwa siku asubuhi baada ya kuamka na jioni kabla ya kulala. Hivyo wana jamiiforum tupige mswaki mara mbili kwa siku asubuhi na jioni.

Wataalamu wa kinywa na meno pia hawakuishia hapo waliweza kushauri njia au tekniki za kutumia wakati wa kupiga mswaki ili zoezi lifanyike kikamilifu baadhi ya hizo tekniki ni Pamoja na systematic tooth brushing, Stillmans technique, vertical, horizontal, circular Pamoja na nyingine nyingi.

Wataalamu wengi wanashauri tutumie systematic tooth brushing technique hivyo nitaielezea hio peke yake lakini kabla sijaizungumzia ningependa kuzungumzia sehemu kuu za meno kama yanavoonekana kwa nje. Meno yana sehemu kuu tatu, sehemu ya nje hii ambayo inaguswa na mashavu ndani kwa meno ya nyuma na lipsi kwa meno ya mbele, sehemu ya ndani inayoguswa na ulimi mtu akiwa kawaida amefunga mdomo na sehemu ya kutafunia ikiwa inakamilisha sehemu kuu tatu za nje za meno.

Kwa kutumia Systematic technique baada ya kutia dawa ya meno yenye madini ya floridi tunashauriwa kutia maji kidogo ili kulainisha mswaki baada ya apo tunashauriwa kuanzia upande wa nje meno ya juu nyuma kabisa halafu tunasugua kuja mbele jino moja baada ya jingine bila kuruka hata moja. Tukifika mbele tunaendelea kuelekea upande wa kushoto mpaka kufikia jino la mwisho baada ya apo tunashuka meno ya chini upande huohuo wa nje kushoto na kuanza kusugua kuja mbele vivyo hivyo pasipo kuruka jino hata moja tukisha fika mbele tunaelekea nyuma upande wa kulia.

Hapa tulipo wana jamii forum meno yetu yote yapo safi kwa upande wa nje lakini bado ndani na sehemu ya kutafunia usichoke baki na mimi kumalizia usafi wa vinywa vyetu. Upande wa ndani tunaanzia meno ya juu kulia kama ilivokua kwa upande wa nje na tunasugua kuja mbele halafu kuelekea kushoto na kushuka meno ya chini kushoto kusugua kuja mbele na kumalizia nyuma kulia.

Mpaka hapo tumesafisha nje na ndani lakini meno yetu yanatakiwa kusafishwa sehemu tatu bado sehemu ya kutafunia hii tunaanzia chini kulia na tunasugua kuja mbele halafu kushoto halafu tunapandisha juu kushoto tunasugua kuja mbele halafu tunamalizia kulia juu baada ya hapo tunashauriwa kutema mapovu na kutokusukutua na maji. Kufikia hapo wana jamii forum tumesafisha meno yetu sehemu zote tatu kwa ufanisi
Picha chini inaonyesha jinsi ya kupiga mswaki

Chanzo cha picha Google
Zoezi hili huchukua sio chini ya takribani dakika 2. Pia tunashairiwa kubadilisha miswaki yetu kila baada ya miezi mitatu. Ukiweza kuua hawa ndege wawili utajiepusha na magonjwa ya kuoza kwa meno, kinywa kutoa harufu mbaya, maumivu na gharama za matibabu.

Kwa kuongezea wataalamu wanashauri mtu aanze kufanya usafi wa kinywa na meno mara tu baada ya kuota kwa meno na Watoto watumie miswaki yao na kiasi kidogo cha dawa kiasi kama punje ya harage ili kujiepusha na madhara yatokanayo na madini ya floridi. Wataalamu wanashauri mtoto apigishwe mswaki hadi anapotimiza miaka sita, miaka 6-9 apige peke yake kwa kusimamiwa na baada ya miaka 9 anaweza kupiga mswaki peke yake.

SHUKRANI ZANGU ZA DHATI KWA UONGOZI MZIMA WA JAMII FORUM PAMOJA NA WANAJAMII FORUM KWA UJUMLA. AHSANTENI SANA.
 
Upvote 3
Back
Top Bottom