SoC04 Kupunguza ukosefu wa ajira nchini

SoC04 Kupunguza ukosefu wa ajira nchini

Tanzania Tuitakayo competition threads

Sophroniscus

New Member
Joined
May 16, 2024
Posts
2
Reaction score
1
Tanzania ni moja kati ya nchi 55 za bara la Afrika, bara linalokabiliwa na changamoto nyingi zaidi duniani. Pia ni nchi inayopatikana katika ukanda wa nchi zilizo kusini mwa jangwa la Saharra na kama ilivyo kwa nchi nyingine za ukanda huu Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika jitihada zake za kujikomboa kiuchumi na kupiga hatua kimaendeleo.

Changamoto zote ili ziweze kutatuliwa kikamilifu zinahitaji watu wenye upeo na uwezo wa hali ya juu katika kugundua uwepo na kutathmini ukubwa wa changamoto hizo ili kuandaa mpango na rasilimali zitakazowezesha kutatua changamoto hizo. Ikitokea watu hawana upeo wa kuzigundua changamoto hizo, hawana rasilimali zinazowawezesha kutatua changamoto hizo au hawana uwezo wa kuzitumia kikamilifu rasilimali zilizopo ili kutatua changamoto zilizopo ili kujipatia kipato cha kuendeleza maisha yao ya kila siku hupelekea kuongezeka kwa changamoto katika jamii na kikubwa zaidi hupelekea kuongezeka kwa idadi ya watu wasiojishughulisha kutatua changamoto hizo na kukosa kipato na ndipo kunaibuka msamiati wa “KUONGEZEKA KWA UKOSEFU WA AJIRA”.

Kila mwaka serikali inapoteza mapato mengi zaidi kwa watu wasio na ajira hata kuliko ukwepaji kodi wa baadhi ya wafanyabiashara hivyo kwa kupunguza ukosefu wa ajira ni wazi serikali itaongeza mapato yake maradufu na kuchochea maendeleo ya nchi yetu kiuchumi na kijamii.

Kwa kila mtanzania asie na ajira hutoa sababu kuu angalau moja kati ya zifuatazo; kusubiri ajira ya fani aliyosomea, kukosa wazo la nini cha kufanya, kukosa mtaji wa kuanzisha biashara, kutokuwa na uwezo wa kuendesha mradi au biashara, hofu ya kuanzisha mradi wa kilimo au biashara kwa kutokuwa na elimu husika, kukosekana masoko ya uhakika ya mazao yanayozalishwa, masharti ya uanzishwaji wa miradi na biashara.

Hatua za kuchukua ili kukabiliana na changamoto hizo ni;

Kilimo; Ni wazi katika nchi yetu hii ndio sekta yenye uwezo wa kuajiri watu wengi zaidi kuliko sekta nyingine hivyo ni lazima serikali kuweka mkazo kwa kufanya tafiti za kisasa za kilimo, kuanzisha program maalumu za muda mfupi mathalani kozi za kujifunza mazao machache anayohitaji mtu badala ya kilimo kiujumla kwa miaka 3. Kuwafundisha wanafunzi na wakulima njia bora za kilimo cha kisasa,ufugaji wa kisasa,uongezaji thamani wa mazao, ufungashaji na kilimobiashara(Agribusiness). Kufuta kodi katika zana za kilimo kama matrekta,mbolea na mbegu za mazao. Serikali kutafuta masoko ya mazao katika nchi za nje hususani zinazokabiliwa na vita,ukame na njaa na kuwatangazia wananchi mazao na kiasi cha mazao kinachohitajika zaidi duniani na bei zake ili kuwekeza zaidi kwenye mazao hayo.

Ajira za serikali; Ni vyema kufanya tathmini ya makadirio ya mahitaji ya rasilimaliwatu katika fani za ajira rasmi na kubadili mfumo wa elimu kuondoa utaratibu unaolazimisha kila mwanafunzi kusomea fani zinazotegemea kwa kiasi kikubwa ajira kutoka serikalini na taasisi binafsi kwani lengo la elimu ni kumuandaa mhitimu kutumia taaluma yake kuendesha maisha yake kwa shughuli husika.

Idadi ya wahitimu inakuwa kubwa mno kuliko fursa za ajira zilizopo hivyo kuwe na ukomo wa idadi ya wanafunzi kwa vyuo vya umma na binafsi kudahiliwa katika fani hizo ili kuepuka kuzalisha idadi kubwa zaidi kuliko mahitaji na hii itapunguza nadharia ya kusubiri ajira. Mwanafunzi anapotumia gharama kubwa na muda wa zaidi ya miaka 5 kupokea maarifa ya kumuwezesha kufanya shughuli fulani ni wazi haitakuwa rahisi kuacha uwekezaji alioufanya katika mkondo huo na kujikita kufanya shughuli tofauti na hiyo kwa ufanisi, mathalani mtu aliyehitimu Shahada ya sanaa katika Historia(Bachelor of Arts in History) si rahisi kutumia maarifa hayo katika kufanya shughuli za kilimo kwa ufanisi kwani kuna mambo mengi sana asiyoyafahamu kuhusu kilimo.

Matumizi ya taaluma; Mitaala ya elimu iweke uhusiano wa moja kwa moja wa fani inayotolewa chuoni na ni jinsi gani taaluma hiyo inaweza kutumika nje ya mfumo rasmi wa ajira mathalani Daktari, mwalimu, mwanasaikolojia, mchumi, afisa maendeleo ya jamii n.k afundishwe chuoni anaweza vipi kujiajiri kupitia kilekile alichojifunza kwa kuanzisha taasisi yake ama kutoa huduma nje ya mfumo wa ajira za serikali. Hii itachochea vijana kujiajiri kupitia fani zao. Serikali pia ipunguze masharti ya kujiajiri kupitia taaluma.

Kurasmisha shughuli zote halali katika mfumo wa elimu; Shughuli nyingi zinazofanyika katika nchi yetu katika uzalishaji mali na kuwapatia wananchi kipato ni wazi hazipo katika mfumo wa elimu na hivyo kutopewa kipaumbele na vijana waliopo masomoni kwa kuonekana ni kazi zisizo na tija na ni kwa ajili ya walioshindwa masomo na hivyo kupelekea idadi kubwa ya vijana kuhisi ajira za serikali ndio mkombozi wa maisha yao.

Mathalani taifa letu lina idadi kubwa sana ya wajasiriamali, wafanyabiashara wadogo, kati na wakubwa, wavuvi, wafugaji, wakulima, wajenzi, waendesha miradi mbalimbali midogo na mikubwa n.k lakini utagundua kuwa asilimia kubwa hufanya shughuli hizo kwa ubunifu wao binafsi na si elimu waliyoipata na hivyo kuwanyima fursa hiyo wale ambao wameshindwa kubuni shughuli hizo kwa kukosa elimu hiyo. Hii itawafanya vijana kugeukia fani zenye fursa nyingi za ajira.

Upatikanaji mitaji; Serikali itazame upya utaratibu wa upatikanaji wa fedha za mikopo yenye riba nafuu kutoka taasisi za fedha kama Benki ya maendeleo ya Afrika(ADB) na Benki ya Dunia(WB) ili kuanzisha mfuko unaojizungusha(Revolving Fund). utoaji wa fedha hizo, usimamizi na uendelezaji wa miradi itokanayo na fedha hizo, ukusanywaji thabiti wa mikopo hiyo kwa njia za kisasa kupitia usajili kwa kutumia namba ya utambulisho wa kitaifa(NIN) na anwani ya makazi(Postcode) itawezesha vijana kuanzisha miradi mbalimbali yenye tija kote nchini na kurudisha pesa hizo kwa wakati ili kuwanufaisha wengine.

Rasilimali; Ardhi yote ipimwe na kupangiwa matumizi ili kutoa fursa kufanya shughuli mbalimbali kama uchimbaji madini, kilimo, ufugaji, maeneo rasmi ya biashara, viwanda vidogo vidogo.

Sera;
Ni muhimu kuwapa kipaumbele watanzania katika sera za uwekezaji, biashara na ajira katika miradi mbalimbali kwa kuwapa nafuu katika kuanzisha biashara au miradi kwa kuwapa msamaha wa kodi kwa kipindi flani ili kuimarisha biashara hizo na hii itapelekea kuanzishwa kwa biashara na viwanda vingi. Kupandisha kodi kwa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje ya nchi ambazo pia zinazalishwa kwa wingi hapa nchini. Kuwe na kodi rafiki kulingana na biashara husika ili kuchochea kukua kwa biashara.

Miundombinu; Serikali inapaswa kujikita katika kuboresha miundombinu kama barabara,reli,vivuko na meli, masoko, minada na huduma za kijamii(simu, umeme, maji, elimu, vituo vya polisi na huduma za afya) katika maeneo ya pembezoni mwa nchi ili kuongeza upatikanaji wa malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda vidogovidogo,kuchochea maendeleo ya maeneo hayo na kuongeza soko la ndani la bidhaa mbalimbali.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom