Hivi ni kweli kuwa kula chakula kingi wakati wa usiku pamoja na kulala chali huongeza nafasi ya kukabwa na majinamizi shingoni?
- Tunachokijua
- Jinamizi la Usingizi kwa lugha ya kitaalam hufahamika kama Sleep Paralysis, ni kipindi cha mpito kinachoufanya mwili ukose udhibiti wa misuli. Hali hii inaweza kutokea muda mfupi baada ya kulala au kuamka.
Wakati wa tukio hili, mwili hutawaliwa na hisia mbaya, hofu na kupoteza uwezo wa kutumia viungo vya mwili kujinasua kwenye mtanziko wa mawazo hasi yanayokuwepo. Mathalani, mtu aliye kwenye hali hii anaweza huhisi kukabwa na kiumbe chenye nguvu kubwa kuliko yeye lakini huwa hana uwezo wowote wa kupambana au kukimbia.
Pia, unaweza kuwa macho lakini usiwe na uwezo wa kusimama, kuzungumza au kufungua macho.
Chanzo cha Jinamizi la usingizi
Sleep Paralysis ama Jinamizi la Usingizi huhusianishwa na mambo mengi ikiwemo wasiwasi, changamoto za kisaikolojia, kutokuwa na usingizi mzuri, matumizi ya pombe Pamoja na uwepo wa kumbukumbu ya matukio mabaya.
Pia, kwa mujibu wa Taasisi ya NHS, ulaji wa chakula kingi kabla ya kupumzika pamoja na kulalia mgongo (kulala chali) huongeza nafasi ya kutokea kwa jinamizi la usingizi.
Mbinu za kuepuka hali hii
Hadi sasa, hakuna tiba ya moja kwa moja inayoweza kutumika ili kuondoa changamoto hii. Hata hivyo, mbinu zifuatazo zinaweza kusaidia kuikabili;
- Kutunza ratiba ya usingizi
- Kutunza usafi wa chumba cha kulala pamoja na kutumia godoro zuri
- Lala kwenye chumba kisicho na usumbufu wa mwanga mkali na kelele
- Epuka kutazama TV ukiwa chumbani Pamoja na kusitisha matumizi ya vifaa vya kidigitali walau nusu saa kabla ya mud awa kulala.