Kutana na Matare Matiko Rais wa DARUSO enzi za mgomo UDSM 1989

Kutana na Matare Matiko Rais wa DARUSO enzi za mgomo UDSM 1989

Kashishi

JF-Expert Member
Joined
Apr 11, 2010
Posts
1,142
Reaction score
635
Kutana na Matare Matiko Rais wa DARUSO enzi za mgomo UDSM 1989

Mwandishi Wetu
Toleo la 321 16 Oct 2013

Mwaka 1989, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiliingia katika mgomo mkubwa wa kihistoria, ulioongozwa na Rais wa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO) wakiungwa mkono na wahadhiri wao, kabla ya serikali kukifunga chuo hicho na kuagiza wanafunzi wote warudi majumbani kwao na kuwa chini ya uangalizi wa wenyeviti wa vijiji vyao na serikali za mitaa yao.

Kiongozi wa DARUSO aiyeongoza mgomo huo, hadi akatekwa na Serikali kama njia ya kumnyamazisha, aliitwa Matare Joseph Matiko, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Kanda ya Kusini. Lakini pia kwa sasa Matiko ni msomi wa Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Huria cha Tanzania (OUT). Katika makala haya ya Mwandishi Wetu MAYAGE S. MAYAGE, pamoja na mambo mengine, Matiko anasimulia kisa hicho.

Raia Mwema: Kwa nini ulifukuzwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam?

Matiko: Mimi nimezaliwa na kulelewa na Wakurya ambao ni wanaharakati. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilifukuzwa kutokana na uanaharakati wangu huo wa Kikurya kwa kuwa haikuwa ni mara yangu ya kwanza kuwashawishi wanafunzi kugoma na wakagoma kweli.

Mwaka 1978, nikiwa darasa la sita katika shule ya msingi Kiagata, niliwaongoza wanafunzi kugoma, tukipinga kufanyishwa kazi za kilimo na walimu kuwatuma wanafunzi kufanya kazi za nyumbani kwao. Nilisimamishwa masomo kwa mwaka mzima, nikaruhusiwa kwenda kufanya mtihani tu wa kumaliza darasa la saba 1979. Pamoja na kuwa nje ya shule kwa mwaka mzima, nilifanya vizuri mitihani yangu, tukafaulu wanafunzi wawili tu katika kata nzima ya Kiagata.

Mwaka 1983, nikiwa katika shule ya sekondari ya Sengerema, niliwaongoza wanafunzi wenzangu kugomea mafunzo ya mgambo. Uongozi wa wilaya ya Sengerema ulitutaka tupatiwe mafunzo ya mgambo, tukakataa. Tuligombana na wanamgambo walioletwa kutoa mafunzo hayo hadi tukawashinda, lakini nikafukuzwa shule.

Nilikaa mwaka mzima nyumbani, lakini zikiwa zimebaki siku chache tu wenzangu wafanye mitihani ya kuhitimu kidato cha nne, nilifunga safari hadi Butiama kumuona Rais, Mwalimu Julius Nyerere, akanipatia barua ya kurudi shule kwa ajili ya kufanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne, hapa tena nilifaulu kwa kupata daraja la tatu, nikachaguliwa kwenda kidato cha tano, chuo cha ualimu Korogwe.

Nikiwa Korogwe, mwaka 1986 ulifanyika ufisadi, uongozi wa chuo ukawa unatupatia uji wa chumvi na chakula kibovu. Niliwahamasisha wanafunzi wenzangu tugome. Ukatokea mgomo mkubwa ulioilazimisha Serikali, kupitia wizara ya Elimu kuunda tume tano bila mafanikio. Hatima ya mgomo ule, nakumbuka Mkuu wa Chuo, akiitwa Amoni Maleo aliondolewa na mimi nikafukuzwa chuo.

Nilipofukuzwa niliamua kwenda kufunzisha shule ya sekondari ya Lake ya jijini Mwanza kati ya mwaka 1987 na 1988. Mwaka huo wa 1988 niliomba kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nikachaguliwa kujiunga na kitivo cha sheria.

Baada ya wiki moja tu kuanza masomo yangu ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ulitokea mgomo, wanafunzi tukajikusanya katika ukumbi wa Nkrumah. Kati ya wanafunzi waliozungumza sana na kushangiliwa na wanafunzi katika mkusanyiko huo wa mgomo, nami nilikuwemo na nilikuwa mwanafunzi pekee wa mwaka wa kwanza kuzungumza na jumuiya ya wanachuo.

Wanafunzi wote kwa kauli moja, wakaamua kunichagua katika mkutano huo kuwa Waziri katika Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ninayeshughulikia masuala ya Ustawi wa Wanafunzi, Afya na Malazi. Wakasema huyu ndiye rais wetu ajaye, lazima tumpatie wizara inayogusa ustawi wa wanafunzi.
Mwaka 1989, nikiwa mwaka wa pili, nikachaguliwa kuwa Rais wa DARUSO.

Ikumbukwe miaka ile, Chuo Kikuu cha Muhimbili kilikuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-Mlimani. Kwa hiyo, nilikuwa rais wa wanafunzi wote wa Mlimani na Muhimbili.

Rais wa Kampasi ya Mlimani nakumbuka alikuwa huyu Dk Cyril Chami na Makamu wake alikuwa Mosina Nyambabe, yuko NCCR-Mageuzi kwa sasa wakati rais wa Kampasi ya Muhimbili alikuwa Haruni Kimaro na makamu wake ni huyu ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Serengeti, Dk. Kebwe Stephen.

Sasa basi, wakati nikiwa Rais wa DARUSO, kilitokea kifo cha mwanafunzi wa mwaka wa kwanza aliyejulikana kwa jina la Levina Mkasa, ambaye alijiua kwa madai ya kuharasiwa na wanafunzi wa kiume wa kitivo cha Uhandisi.

Baada ya kifo cha mwanafunzi huyo hali ilikuwa mbaya sana chuoni. Kulitokea mpasoko mkubwa sana kati ya wanafunzi wa Kitivo cha Uhandisi na wale wa Vitivo vingine vyote. Nilipata shida kubwa sana kama Rais wa Daruso kusuluhisha mpasuko ule hadi hali ikawa shwari.

Wakati uhusiano wa wanafunzi wa vitivo hivyo ukiwa katika hali hiyo tete, hali na mazingira ya chuo kwa upande wake ilikuwa mbaya pia. Chuo hakikuwa na viti vya kutosha vya kukalia wanafunzi, na hata chaki za kuandikia zikawa hakuna.

Kwa mfano, kati ya wanafunzi wote 65 tuliokuwa Kitivo cha Sheria, ni wanafunzi watano tu, ndio walikuwa na viti vya kukalia, wengine wote 60 tulikuwa tunaingia madarasani na kusoma tukiwa ama tumesimama au tumekaa chini sakafuni.
Molari ya Wahadhiri kufundisha darasani ikiwa hakuna, kila Mhadhiri akawa anashughulika na mambo yake binafsi, wengine wanashinda shambani kukata nyasi za kulisha mifugo yao. Maprofesa wengi wakawa wanaondoka kwenda kufundisha nje ya nchi kutafuta maisha mazuri.

Wale waliobaki, ukiwafuata kuwauliza mbona hamuiingii darasani, wanawambia shauri yenu kama hamuungani pamoja na kuiambia Serikali irekebisha hali mabaya hiyo ya ukosefu wa vitendea kazi chuoni. Kusema ukweli, wanafunzi na chuo kwa ujumla walikuwa na imani kubwa na uongozi wangu, nami nikawa na imani na chuo.
Kama Rais wa Daruso niliitisha mkutano wa wanachuo wote katika ukumbi wa Nkrunah. Nilikusanya vitabu vya Mwalimu Nyerere, na hasa vile vinavyohusu masuala ya haki za msingi za mwanadamu na hotuba zake katika vyuo mbalimbali duniani.

Katika hotuba yangu, nikawaambia wamafunzi wenzangu kwamba sisi ni twiga tuliyoko nyikani, kuna mtu kachukua haki yetu ya kupata elimu tunayostahili kupata, vitendea kazi tunavyostahili kuwa navyo, malazi na makazi bora. Nikasema mtu huyo aliyechukua haki yetu, ni Serikali.

Nikasema sisi ni wanafunzi wa chuo kikuu tunaotegemewa na taifa hili pamoja na wananchi kwa ujumla. Sisi ambao ni tegemeo la taifa na wananchi, tunaishi maisha ya shida namna hii. Wananchi wanaishi maisha mabaya ya kimasikini zaidi. Baada ya hotuba yangu hiyo, mgomo ukaanza hatukuingia tena madarasani, na maprofesa wakatuunga mkono.

Nakumbuka; Mei 12,1989, tulifanya mkutano wa pamoja kati ya Wahadhiri na sisi wanafunzi. Tukaazimia kwamba tuufanye mgomo wetu ule uwe wa kitaifa kwa kuzungumzia mambo ya kitaifa badala ya kuzungumzia madai yetu pekee ya chuoni.
Tukaorodhesha madai yetu kwa ajili ya kuyatolea tamko la pamoja. Kulikuwa na madai ya mauaji ya wakulima na wafugaji kule Kilombero, kulikuwa na dampo la uchafu kule Tabata, kulikuwa na madai ya kivuko kibovu cha Kigamboni, kilichonunuliwa na Serikali kwa fedha nyingi lakini kikafanya kazi siku mbili kikaharibika, kuungua kwa jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani na kadhalika.
Baada ya kuorodhesha madai yetu ya chuo na yale yaliyokuwa yanaligusa taifa kwa ujumla wake, tukaamua kwamba lazima aitwe Mkuu wa Chuo, ambaye ni Rais Ali Hassan Mwinyi. Tukamwandikia barua ndefu ya kumuomba aje akuzungumze na jumuiya ya chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Katika barua yetu hiyo, tukaweka masharti mawili. Kwanza; tulimuomba Rais aje na azungumze na wanafunzi kama Mkuu wa Chuo na siyo kama Rais wa nchi ili tupate fursa ya kumuuliza maswali kwa sababu akija na kutuhutubia kama Rais wa nchi ana hiyari yeye kuomba aulizwe maswali, na lakini pia lolote analolisema akiwa na kofia ya Rais ni amri, mtu hawezi kulihoji, na sharti la pili, tulimuomba azungumze lugha ya Kiingereza.

Baada ya kupata barua yetu ile aliijibu kwamba atakuja kuzungumza na jumuiya ya chuo kikuu cha Dar es Salaam, lakini atakuja kama Rais na atazungumza Kiswahili. Sisi tukamjibu, tukamwambia hakuna kuzungumza Kiswahili kwa sababu chuo kina wanafunzi wengi tu wan je wasiojua Kiswahili, na madai yetu yanawagusa pia wanafunzi hao kwa hiyo walikuwa na haki ya kumsikiliza moja kwa moja mhusika wa majibu kuhusu matatizo yanayokikabili chuo.

Kuona hivyo, Rais Mwinyi akataka akutane kwanza Ikulu na viongozi wa wanafunzi. Tukakubali, lakini tukateua wawakilishi wetu nje kabisa ya viongozi wa Daruso kwa sababu tulijua kwamba kama tutakwenda sisi viongozi wa Daruso tukienda lolote tutakaloagizwa na Mkuu wa Chuo au Rais lazima litekelezwe, vinginevyo inaweza ikatuletea matatizo.

Tukachagua Kamati, ikaenda kukutana na Rais tukiwa katikati ya mgomo. Alikutana nao Ikulu. Rais akaiagiza Kamati ile iwaambie wanafunzi warudi darasani kwa sasa hadi atakaporejea nchini kwa sababu kesho yake alikuwa na safari ya nje katika nchi za Scandinavia.

Walipokuja kutueleza hivyo, tukarejea darasani. Lakini kumbe Rais Mwinyi hakwenda kokote. Tukawa tunamuona akisuluhisha migogoro tu ya wana ndoa na mambo mengine. Tukasema kumbe Mkuu wa Chuo, Rais, hakuwa mkweli, mgomo ukarudi, tukarudi Nkrumah.

Habari zikamfikia Rais. Akamtuma Waziri Mkuu wake ambaye pia alikuwa Makamu wa Rais, Jaji Joseph Warioba. Sisi tukakataa, tukasema tunamtaka Rais mwenyewe aje hapa. Baadaye Rais Mwinyi akamtuma Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Joseph Ngonyani ili aje kuzungumza nasi. Ngonyani alikuja ameongozana na ofisa mmoja wa Ikulu, aliyekuwa akijulikana kwa jina la Majani.

Ngonyani alipokuja Nkrumah kuzungumza nasi, akataka azungumze kwa lugha ya Kikswahili, tukasema hapana, zungumza Kiingereza. Katibu Mkuu huyo wa Elimu, akagoma kuzungumza Kiingereza, wanafunzi wakaanza kupiga kelele na kumzomea. Kuona hivyo, wakatokea mlango wa nyuma na kutoka ukumbini…hali hiyo ilitokea saa 11 jioni.
Wakati wa taarifa ya habari ya saa mbili usiku, RTD (Redio Tanzania Dar es Salaam, tukasikia kwamba Rais Mwinyi amemfuta kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu kwa sababu ya kushindwa kuisaidia Serikali kutatua mgomo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu uliokuwa unaendelea.

Siku mbili baadaye Mzee Mwinyi akaja kimya kimya chuoni akiwa ameongozana na Waziri wa Elimu, Jackson Makwetta. Walifikia Kitivo cha Uhandisi, Rais akataka kuonana tu na viongozi wa DARUSO na UDASA. Tulimpokea, tukamzungusha katika baadhi ya maeneo ya chuo yakiwemo mabweni ya wanafunzi, na yeye akakiri kuwepo kwa hali mbaya.

Baada ya kumaliza mizunguko, tukaenda kukakaa naye katika ofisi ya CCM pale Chuo Kikuu. Wakati Makamu Mkuu wa Chuo alikuwa Joffrey Mmari. Katika kuhitimisha mazungumzo yetu, Rais Mwinyi akatutaka tuwaambie wanafunzi wasitishe mugomo waingie madarasani, matatizo yetu yote yatashughulikiwa.

Lakini pia akasema hataweza kukutana na kuzungumza na wanafunzi kwa sababu wamemsikitisha kidogo. Kwamba wanafunzi wanamwita yeye Rais kwa jina la Jangara wakati Makamu Mkuu wa Chuo, Mmari yeye wanamwita Komredi, na lakini pia huyo anayeitwa Komredi ndiye kwa nafasi yake ya Makamu Mkuu wa Chuo anayemwakilisha Mkuu wa Chuo. Rais akaaga, akaondoka.

Taarifa ya RTD ya saa mbili usiku, ikatangazwa kwamba Rais Mwinyi hatakutana na jumuiya ya wanafunzi wa Chuo Kikuu kwa sababu hawana nidhamu. Kesho yake saa nne asubuhi, nikiwa kwenye mgahawa wa daruso nikiwa nakunywa soda, nikafuatwa na mtu mmoja aliyejitambulisha kwangu kuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa B.Com, alikuwa na shida na mimi, akaniambia twende kule.

Mimi kama Rais wa wanafunzi, nikasema ngoja nikamsikilize. Tukashuka bondeni kidogo kwa mbele kulikuwa na gari limesimama, tukawa tunaelekea usawa wa gari lile. Tulipolikaribia tu gari, jamaa yule akanitolea bastola, akasema uko chini ya ulinzi, nisifanye chochote niingie kwenye gari. Wakajitokeza watu wengine wawili wakanishika kwa nyuma na kuniingiza ndani ya gari lile haraka sana. Wakanifunga kitambaa usoni na kuendesha gari kwa kasi kunipeleka kusikojulikana.

Tulifika mwisho wa safari yao, wakanitoa kwenye gari na kuniigiza katika jumba moja maeneo ya kule bandarini. Huko nikayakuta majitu ya kutisha. Yamefuga ndevu hadi kifuani. Mara moja nilijiwa na wazo moja tu la kwamba huo ndio ulikuwa mwisho wa uhai wangu.

Kwa hiyo, kwa kuwa nilijua huo ndio ulikuwa mwisho wa uhai wangu, nilijisemea kwamba sihitaji kuwanyenyekea, natakiwa niwajibu hovyo tu katika kila kitu watakachoniuliza.

Wakati nikiyatafakari majitu hayo, mmoja wao akaja pale. Akamwagiza mmoja wa wale walionitaka kwa kumwambia; kama tayari kamwite aje. Nikawa nimesubiri kumuona huyo mtu. Akaingia Waziri Mkuu, Joseph Warioba.

Alipoingia tu, akaniuliza: “Unanifahamu mimi? Nikamwambia, ndiyo nakufahamu, unaitwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Jaji Joseph Warioba. Akaniuliza kwanini unataka kupindua nchi? Nasikia unajiita Rais ni kweli? Nikamwambia ndiyo, mimi ni Rais wa DARUSO. Akasema kwanini unawagomesha wanafunzi, unatoa matamko makali dhidi ya Serikali? Mwisho, akasema nataka unithibitishie yote haya.
Nikamwambia, kwanza kuanzia sasa nimefahamu jinsi Serikali inavyofanya kazi zake.

Sikutegemea kukutana na mtu kama wewe, Waziri Mkuu katika mazingira ya ovyo kama haya, na niletwe kwako kuulizwa maswali haya uliyoniuliza kwa njia hii iliyotumika kunileta hapa.

Nikamwambia Mheshimiwa Waziri Mkuu, mimi Matare Matiko, ningeweza kuja ofisini kwako hata kwa miguu, tena nikiwa nakimbia kutoka Chuo Kikuu. Lakini kwa kweli, nimesikitika sana kwa utaratibu huu wa Serikali uliotumika kunikutanisha na wewe.

Nikamwambia mimi ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Mlimani, sina kumbukumbu ya maandiko yoyote duniani, yanayoonyesha kwamba mwanafunzi wa mwaka wa pili, amewahi kupindua Serikali.

Waziri Mkuu Warioba, akaniambia wewe na baadhi ya viongozi wa DARUSO mlikuwa nje ya nchi katika ziara moja na Mwalimu Nyerere, inaelekea huko mlikuwa na agenda yenu.

Nikamwambia ni kweli tuliongozana na Mwalimu nje, lakini mavazi yangu nilishonewa na Ikulu ya Serikali hii, na hata hotuba yangu niliyoisoma katika mkutano wangu wa viongozi wa vyuo vikuu duniani, ilihaririwa Ikulu ya Serikali hii.

Warioba, akaniambia; sawa. Sasa utaijua Serikali ni nini kama ulivyosema mwenyewe. Ukitoka hapa kawaambie wanafunzi wote waingie madarasani mara moja, na usiseme chochote wala mahali popote kuhusu haya tuliyokuuliza hapa wala tukio hili la kutekwa na kuletwa hapa. Sawa? Mimi nikamwambia sawa, nimekusikia.
Warioba akawaagiza watekaji wangu wale wanirudishe chuoni. Wakaniingiza kwenye gari lao, tulipofika karibu na maeneo ya chuo, wakanisha. Mimi nikaenda moja kwa moja hadi chuoni. Nilipofika nikaitisha kikao cha USRC. Huu ni mkutano wa baraza la chuo linalowahusisha viongozi wote kuanzia wa Serikali ya Wanafunzi, viongozi wa vyama vya kitaaluma na viongozi wa mabweni.

Nikawaambia kilichonitokea, na kesho yake vyombo karibu vyote vya habari vikaandika habari juu ya kutekwa kwangu na mtu niliyekutana naye baada ya kutekwa kwa maana ya Waziri Mkuu. Wanafunzi wakaendelea na mgomo wao. Serikali ikakifunga chuo na wanafunzi wote tukaamliwa kuondoka katika eneo la chuo mara moja kurejea majumbani mwetu, na huo ndio ukawa mwisho wa masomo yangu.

Soma zaidi kuhusu:

- See more at: Raia Mwema - Kutana na Matare Matiko Rais wa DARUSO enzi za mgomo UDSM 1989

Chanzo: Gazeti la RaiaMwema
 
Naukumbuka huo mgomo, panch na hata ulikuwa ukiongelewa miaka kazaa baadae.Kamanda kweli amejitea kwenye mapambano ya kutafuta haki.
 
Du, Hata Warioba nae alifanya hivi! sikutegemea kabisa,ikiwa kama habari hii ni kweli na hayo majitu yenye ndevu mpaka kifuani ni akina nani hao? hebu wajuzi wa mambo haya tunaomba mtu saidie kutufafanulia kidogo.Labda hayo majitu ndiyo serikali yenyewe.Halafu ikiwa kama Warioba alikua muumini wa Mwalimu inamaana aliposema hao wanafunzi wanataka kupindua serikali na walienda nchi za Nnje na Mwalimu alikua anamaana Nyerere alikua anahusika? kwa hiyo alipelekewa wapelelezi na serikali? au Nyerere alikua hajui kinachoendelea? mimi kuna maswali mengi sana yanajitokeza ktk habari hii! huenda ndiyo maana Baada ya Nyerere kufariki watu wameonesha sura zao halisi.

Au warioba alikua anamtisha tu! ni habari ianayovutia kujua zaidi.
 
Nikiwa mmojawapo wa waaithrika wa mgomo huo, hii habari imenikumbusha mbali sana. Wakati ninaisoma I feel tears shade my eyes.

Ila nashukuru Mungu kusikia kwamba Matare Matiko bado yuko hai na ni mhazili OUT. Kwani viongozi wengi wa DARUSO wa wakati huo wameshafariki dunia kama Marehemu Bazigiza, Kimaro etc.

Sijui Judge Warioba atajisikiaje atakapoisoma habari hii katika gazeti hili la RAI hasa wakati huu mhimu na tete ambapo anatutengenezea katiba mpya. HIS CREDIBILITY HAS BEEN PUT IN LIMBO.

Nitalinunua hili gazeti la RAIA na kulihifadhi kama kumbukumbu kati maisha yangu yote.
 
Nikiwa mmojawapo wa waaithrika wa mgomo huo, hii habari imenikumbusha mbali sana. Wakati ninaisoma I feel tears shade my eyes.

Ila nashukuru Mungu kusikia kwamba Matare Matiko bado yuko hai na ni mhazili OUT. Kwani viongozi wengi wa DARUSO wa wakati huo wameshafariki dunia kama Marehemu Bazigiza, Kimaro etc.

Sijui Judge Warioba atajisikiaje atakapoisoma habari hii katika gazeti hili la RAI hasa wakati huu mhimu na tete ambapo anatutengenezea katiba mpya. HIS CREDIBILITY HAS BEEN PUT IN LIMBO.

Nitalinunua hili gazeti la RAIA na kulihifadhi kama kumbukumbu kati maisha yangu yote.

Ndio viongozi wetu hao. Halafu wanataka eti ICC ivunjwe!!
 
yes hii habari imenikumbusha mbali kwani maelezo ya Mpiganaji Matiko Matare ni sahihi kabisa. Mwinyi aliogopa kuja chuoni baada ya kulazimishwa kuongea kiingereza. Nakumbuka tulizuiliwa ajira ya aina yoyote wakati chuo kilipofungwa na mimi nililazimika kuuza dagaa, chumvi na mafuta ya taa kwenye magulio ili kupata pesa ya kujikimu. Kuweka kumbukumbu sahihi, Matiko Matare hakufukuzwa chuo bali aliondolewa busary ya serikali na kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kujilipia mwenyewe, aliachia ngazi yeye na wengineo.

Tumetoka mbali.

Tiba
 
Hayo majitu nadhani ndo mang'oa kucha bila ganzi ya enzi hiyo.au ndo serikali yenyewe kama mchangiaji mmoja alivyo sema.hatari sana.
 
CCM ni kaukoo ka panya, hadi warioba nae ni mtekaji kama Ighondu
 
habari ina mafunzo mengi, ninaamini sasa serikali inaweza kuamrisha watu wake wauwawe hata kwa kupigwa mabomu.
 
Aisee,kumbe ndivyo serikali inavyofanya kazi hivyo?hatari sana wandugu.
 
Nashangaa hii thread haijapigwa kufuli

Yaani unataka thread zinazoongelea udhaifu na ulegelege zifungwe??? Tena hii thread idumu hapa milele kwa aibu ya serikali na viongozi wake!! Wewe unasema hivyo kwa kuwa hujui ni jinsi gani elimu ya Tanzania hasa higher learning ilivyoathirika tangu awamu wa pili hadi leo!!! ukifika UDSM hutaamini kuwa ni chuo kwa kuwa hata shule ya private ya secondary ina maandhari nzuri kuliko, sembuse private universities!!! Hakika Matiko ni mpambanaji na bora ameweka wazi. Tunamwomba kamanda aje amalizie baada ya 1989 aliendeleaje na maisha na kwa sasa yuko out anasoma!!! Bravo Matiko!!! Tunashukuru hawakukunyoa kucha, meno na macho bila ganzi!!
 
..Raia Mwema wamegoma kumalizia habari ya Matiko Matare.

..huenda wametishwa na serikali.
 
sijaamini kuiona hii post ,manake miongoni mwa majina ambayo nimeyasikia utotoni na mpaka sasa lipo kwenye kumbukumbu zangu ni MATIKO MATARE binafsi nilikuwa najua huyu bwana walimuua.Du nimefurahi sana kusoma hii post
 
Back
Top Bottom