SoC02 Kutekeleza Uthabiti wa kifedha kwa vitendo

SoC02 Kutekeleza Uthabiti wa kifedha kwa vitendo

Stories of Change - 2022 Competition

dee100

New Member
Joined
Feb 25, 2018
Posts
1
Reaction score
1
Fikiria jinsi unavyoweza kuishi kwa furaha pasipo msongo wa mawazo unaosababishwa mara nyingi na mkwamo-kiuchumi. Fikiria unayo pesa ya kutosha kulipa bili zako zote, matumizi ya kawaida kama chakula, kodi, usafiri n.k. Mbali na hilo, fikiria kuhusu kusimamia fedha zako hatimaye uweze kumudu kuishi unavyotaka. Inawezekana iwapo utafikia uthabiti wa kifedha.


Nini maana ya uthabiti wa kifedha?

Uthabiti wa kifedha ni mbinu au mikakati madhubuti ya kujiwekea akiba na kuwekeza. Ni pamoja na bajeti, matumizi ya huduma za kibenki, bima na uwekezaji. Kutokuwa na madeni, kuwa na akiba ya kutosha kwa ajili ya malengo ya baadaye, na pia, akiba kwa ajili ya dharula.

Uthabiti wa kifedha sio kuwa tajiri, hauhusiani na mtu kuwa na mali nyingi. Uthabiti wa kifedha ni kuwa na mtazamo chanya kuhusu fedha. Ni hali ya kutokuwa na msongo wa mawazo unaotokana na matatizo ya kiuchumi kuanzia ngazi ya familia, kuwa huru kifedha, kuwa na muda wa kushiriki mambo mengine ya kijamii na kufurahia maisha.


Hatua ya kwanza: Fanya taarifa zako za fedha kuwa binafsi

Ni muhimu hatua hii ya kwanza ieleweke moja kwa moja. Taarifa/hali ya mtu kifedha ni jambo binafsi, lakini haimanishi kuwa hutozungumzia kamwe na mtu yeyote kuhusu fedha zako, la hasha!, bali ni kuzingatia hali yako ya uchumi na kutokuwa na wasiwasi kuhusu hali za watu wengine.

Hii ni hatua muhimu katika kufikia uthabiti wa kifedha. Ukweli ni kwamba-tumezoea kuishi kwa kujilinganisha na wengine, tumekua tukiaminishwa kuwa; aina fulani ya maisha ni kwa matajiri (waliofanikiwa) na aina fulani ya maisha ni kwa watu masikini (wasiofanikiwa). Hizo ni fikra potofu zinazotakiwa kukemewa., haijalishi rafiki yako ana kipato kikubwa kukuzidi; jambo la muhimu-ni kiasi gani unamiliki na jinsi gani unaweza kutumia kiasi ulichonacho kufikia malengo yako.

Kukosea au kupatia katika kufanya maamuzi ya kifedha ni moja kati ya maeneo muhimu katika hatua hii ya kwanza. Ni sahihi kusema kwamba tunatofautiana ubora kwenye kufanya maamuzi ya kifedha kwa maana ya kuwa kuna maamuzi bora na maamuzi dhaifu, lakini ikumbukwe kuwa masuala mengi katika uchumi wa mtu binafsi yanategemea uthabiti wa fikra wa mhusika mwenyewe.


Hatua ya pili: Kuwekeza katika muda ni uwekezaji mkubwa na muhimu

Kabla hujawahi kufikiri kuwekeza pesa kwenye masoko ya hisa, unatakiwa kufikiri kwanza jinsi ya kujiwekeza mwenyewe. Hii ni maana ya msingi ya ujasiriamali. Wekeza muda, nguvu na pesa kujifunza fani, ujuzi/stadi., unavyovihitaji.

Kujumuisha shahada za vyuoni na elimu nyingine tofauti tofauti kwani kujifunza maatifa mapya mengine ambayo hayahusiani moja kwa moja na kazi yako, inaweza kukusaidia kama ujuzi wa ziada unaohitajika katika utendaji. Kutokana na ukweli kwamba, waajiri wangependelea kufanya kazi na watu wenye uelewa na sifa za ziada-ambao wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika maeneo mengi kwenye taasisi zao.


Pia, wanataka watu wanaoonesha msukumo na matamanio makubwa ya kujiendeleza.

Siku zote, kujiendeleza ndiyo uwekezaji muhimu, kwani kuwekeza katika kujiendeleza ni kufungua milango ya fursa mbalimbali na kujiongezea kipato kutokana na hizo fursa (career-earning potential).


Hatua ya tatu: ingiza kipato kwa kufanya kitu unachokipenda

Kwa kawaida, kitega uchumi cha kwanza kwa watu wengi ni kazi. Unapofikiri kuhusu uthabiti wa kifedha, fikiria kufanya kazi inayokuingizia kipato cha uhakika., Muhimu zaidi ni kufanya kazi unayoipenda na kuifurahia. Inawezekana kuna mitazamo tofauti juu ya hatua hii katika kujenga uthabiti wa kifedha, kwa baadhi ya watu, hatua hii inaweza kutizamiwa kama kubalisha fani au kazi, kubadili taasisi kiutendaji au kampuni., mwingine anaweza kuamua kutafuta kazi ya muda mtandaoni, au hata kupambana kwa namna yoyote ya halali katika kujikwamua kiuchumi ila jambo muhimu linabaki kuwa furaha kwanza na utimamu.


Hatua ya nne: Tengeneza bajeti na uifuate

Si mara moja tumesikia shauri nyingi kuhusu bajeti. Bajeti sio kitu kibaya, bajeti ni nyenzo muhimu sana inayokusaidia kusimamia matumizi ya pesa zako kama unavyokusudia. Unapounda bajeti, unaweza sasa kufuatilia na kujua mwenendo wa matumizi yako ya pesa. Ni kama sheria za mwendo kisayansi zilivyohalisi-kwamba ni rahisi sana kutumia pesa hovyo ikiwa hujui kiasi cha matumizi yako ya pesa kwa kipindi cha muda fulani.

Mara unapogundua mienendo ya matumizi yako ya pesa kutokana na bajeti uliyojitengenezea, unaweza kuunda na mpango kuhusu matumizi yako ya fedha. Mfano; kwa kutambua vipaumbele vyako (mahitaji yako muhimu kama chakula, kodi, n.k.) na kuvielekezea nusu ya bajeti yako.

Zingatia: wataalamu wanashauri-kodi isizidi asilimia 30 ya matumizi yako ya mwezi. Sasa ili kuhakikisha matumizi muhimu yanapata asilimia yake (50%) ndani ya bajeti, ni muhimu sana kutambua kuwa haijalishi matumizi yako yakoje, lakini mara zote tanguliza vipaumbele vyako ambavyo umevitaja ndani ya bajeti yako., na ikiwa kuna matumizi mengine nje ya bajeti, basi yawe ni kwa malengo mazuri ya kiujasiriamali.


Hatua ya tano: Ishi maisha kulingana na uwezo wa kipato

Jambo la muhimu hapa ni kuishi chini ya kipato, yaani; kuepuka matumizi makubwa yanayozidi kipato. Lakini mara zote, kama ilivyo katika kufuata bajeti, hii nayo imekuwa ni changamoto kubwa katika kutekeleza kwa vitendo. Kulingana nyakati, tumekua tukisikia mara kwa mara ni vitu gani tununue au vitu tunavyotakiwa kumiliki. Sasa kutumia pesa hovyo nje ya malengo kwa kununua vitu visivyokua na umuhimu ni rahisi sana ingawa ili upate mafanikio ya kudumu kiuchumi ni lazima ujifunze kuishi chini ya kile unachoingiza. Ule utaratibu wa kutumia kipato chote kinachoingia, unazorotesha ustawi wa fedha. Muhimu; hatua hii inaenda sambamba na bajeti, kwa kuwa bajeti inaelekeza mtu ana pesa kiasi gani na kiasi anachotakiwa kutumia kila mwezi na ndipo mtu huweza kuifuata hiyo bajeti na kuhakikisha havuki viwango alivyojiwekea.


Hatua ya sita: Lipa madeni

Siku zote madeni hukwamisha katika kufikia uchumi imara. Pindi tu unapojua matumizi yako kwa kipindi cha muda fulani mfano; kwa mwezi (kwa kutumia bajeti), juhudi nguvu na maarifa vielekezwe kwenye kulipa madeni kama yapo; inawezekana ni mkopo wa wanafunzi, vicoba n.k.,jiongeze kimapato na ushughulikie madeni haraka iwezekanavyo. Unapolipa madeni mapema unaepuka riba kubwa na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwekeza.


Hatua ya saba: Usisahau kuishi wakati unapoendelea kupambana katika kujikwamua kiuchumi

Unapojikita katika kutafuta kipato inawezekana ukasahau kuishi na kufurahia maisha. Sio jambo baya kuweka bidii katika kutafuta kipato, lakini isipite kiasi cha kujisahau na kusahau kwamba muhimu ni kuwa na furaha inayotokana na kuishi vizuri. Hata hivyo kufurahi ni muhimu pia kiafya. Mara zote unapo-plan bajeti yako hakikisha unaingiza kiasi fulani kwa ajili ya kuenjoy na kufurahi.


Hitimisho;

Uthabiti wa fedha ni kuwa na uhuru katika kugharamia mahitaji yako kwa kuwa na uhakika wa kuzimudu gharama hizo (bills) zilizopo na zitakazokuja. Ingawa, hii ni kama ndoto kwa watu wengi lakini ni jambo ambalo limo ndani ya uwezo wetu. Fuata na zingatia hatua hizi ili ujiweke kwenye mlengo mzuri wa kuwa na uthabiti wa fedha.

images%20(1).jpg
 
Upvote 1
Back
Top Bottom