SoC04 Kutoa ufadhili wa masomo na mafunzo ya michezo na sanaa nje ya nchi kwa watoto wenye vipaji

SoC04 Kutoa ufadhili wa masomo na mafunzo ya michezo na sanaa nje ya nchi kwa watoto wenye vipaji

Tanzania Tuitakayo competition threads

Frajoo

Member
Joined
May 28, 2024
Posts
12
Reaction score
3
Salamu Mabibi na Mabwana;


Dibaji.

Sekta ya michezo ni moja ya Sekta zenye uwezo wa kujiendesha zenyewe kwa asilimia kubwa,kupitia namna ambavyo zinaingiza mapato makubwa na inazalisha fursa nyingi za biashara dunuani kote.

Tunapozungumzia michezo yenye msisimko na ushabiki mkubwa zaidi duniani,basi hatuachi kutaja mpira wa miguu.Mchezo huu umekua ni biashara kubwa sana duniani kwa sasa.Mfano miaka hii ya karibuni tumekua tukitaarifiwa jinsi Vilabu vya mpira wa miguu vikipata mapato makubwa,na zaidi Wachezaji wakivuna fedha nyingi za sajili na mishahara,makampuni mengi ya michezo ya kubahatisha yakiongezeka,ambayo yanaingizia taifa fedha kwanzia kwenye vibari hadi tozo,biashara za vifaa vya michezo na kuzalisha maudhui kwenye vyombo vya habari.

Katika nchi yetu mpira wa miguu umepiga hatua kubwa sana za ukuaji ,nadhani ndio mchezo pekee ambao unatupa matumaini ya kututangaza vyema kimataifa na kunufaisha Watanzania .Tanzania tayari inao wawakilishi kwenye nchi zilizoendelea kupitia mpira wa miguu.Sote tunajivunia akina Mbwana Samatha,Norvatus , Kelvin John na wengine ambao wanapeperusha vyema bendera ya nchi yetu.Pia kwa sasa Vilabu vya Tanzania vimepanda ngazi ya hadhi kwa mujibu wa viwango vya FIFA,hii inaleta hamasa sana kwa wenye vipaji na kushawishi wazazi kuwaruhusu vijana wao kujikita kwenye mchezo huu.

Sanaa nayo ni sekta inayoongoza kutengeneza watu maarufu wenye kuwakilisha mataifa yao huku ikizalisha ajira nyingi zaidi kwa watu wasio na ajira rasmi.Kwa nchi yetu sanaa imekua kwa kasi kubwa sana na kutengeneza ajira nyingi, hususani Sanaa ya muziki wa kizazi kipya na Sanaa ya Uigizaji.Lakini moja ya changamoto inayoweka wigo wa kufanya vizuri zaidi kimataifa ni kukosa maarifa na ujuzi zaidi wa Sanaa husika, japo wapo wasanii wanaofahamika nje ya mipaka ya nchi yetu.Elimu juu ya uzalishaji wa sanaa yenyewe,kufanya masoko ya kisasa, kujenga utambulisho ili kuwa na upekee mfano kuwa na mavazi ya taifa au utambulisho wa sanaa yenyewe pasi na kuenenda kwa kufuata wengine.Bado Wasanii wanahitaji elimu zaidi kwenye nchi zilizoendelea kwenye eneo hili la sanaa.

Utangulizi.

Kwa miaka mingi kumekuepo utaratibu wa kuwalipia vijana gharama za masomo ndani na nje ya nchi ili kuwarahisishia watu wasio na uwezo wa fedha za kulipa ada,usafiri na mahitaji ya msingi ili waweze kupata elimu yenye ubora. Ni ufadhili wa Serikali na wadau mbali mbali wa ustawi wa jamii.

Sasa ni wakati wa kuielekezea taa ya elimu kwenye sekta ya michezo na Sanaa ambazo kimsingi tunahitaji kupata ujuzi unaoenda sambamba na ushindani wa kimataifa.Tanzania kuna vijana wengi wenye vipaji na tunawashuhudia kupitia timu za taifa katika michezo tofauti tofauti na kwenye sanaa tunatazama kazi zao kupitia mitandao ya kijamii na televisheni.


Uhalisia.

Kinachonigusa zaidi ni huu mpira wa miguu ambao kimsingi ndio mchezo wenye msisimko mkubwa na maarufu zaidi ulimwenguni kote.Ni mchezo wenye thamani kwa maana ya mapato ambayo Vilabu vya mpira na wachezaji huingiza na hata umaarufu wanaoupata huwawezesha kuingiza mapato hata nje ya viwanja ,ikiwa ni pamoja na kushiriki matangazo ya biashara, kushiriki kwenye filamu,kusaidia kwenye harambee na uhamasishaji katika harakati mbalimbali zakijamii na habari zao hutengeneza maudhui ambayo yana tija kwenye vyombo vya habari vya kimataifa.

Timu zetu za Taifa za mpira wa miguu nikiwa na maana kwa miaka mingi tumekua tukiunda timu ya Taifa ili kushiriki mashindano ya kimataifa,zimekua zikifanya vibaya au kushindwa kumudu mashindano hivyo tumekua tukikosa nafasi ya kupeperusha vyema bendera ya taifa letu nje ya mipaka ya nchi yetu.

Mpira wa miguu kwa sasa unahitaji uwekezaji mkubwa ili kuweza kupata wachezaji wenye vipaji na wenye ujuzi na sifa za kuwa wachezaji wakimataifa.Moja ya uwekezaji muhimu ni mafunzo ya mchezo husika,na kwenye hili nchi zilizofanikiwa kwenye Sekta ya michezo, huanzia kwa watoto wadogo wenye umri ambao wadau wa elimu-malezi na michezo hupendekeza ili wakuzwe vyema katika mazingira hayo na hatimaye kupata kizazi cha dhahabu cha mpira wa miguu.

Sote tunafahamu wazungu wana vituo maalumu vya mafunzo ya mpira wa miguu yaani Football Academy, huko ndiko kiwanda cha wachezaji wengi hodari kwa wakati huu.Kwa mataifa masikini ni vigumu kujenga vituo hivi kwa haraka kwasababu ni ghali.

Nafahamu Serikali yetu tayari ina mipango ya kuja kuanzisha hivyo vituo vya mafunzo ya mpira wa miguu na michezo kwa ujumla,lakini kulingana na gharama zake bilashaka itachukua muda kuwa navyo hasa kwa idadi inayokidhi uhitaji uliopo.Nafahamu pia wapo ambao wameanzisha vituo vyenye huduma hio hapa nchini,lakini kiuhalisia havina ubora stahiki wa kuzalisha wachezaji watakaoleta ushindani kwenye mashindano ya kimataifa.

Zipo familia zenye uwezo wa kuwapeleka watoto wao nje ya nchi kwenye hizo Football Academy na vyuo vya Sanaa,na kwa utafiti wangu nimegundua kuna matokeo yanayoridhisha sana na kutoa mwanga kwamba tunakokwenda ni pazuri ipo siku kuna watanzania wataishangaza dunia baada ya kizazi hiki cha akina Mbwana Samatha

Tubadili vipaumbele.

Sasa Serikali iwe ya kwanza kuonesha nia ya dhati kabisa katika kutoa ufadhili wa mafunzo ya michezo na sanaa nje ya nchi ambazo zina Football Academies zenye ubora, kama ilivyoweza kutoa ufadhili kwenye masomo mengine ya kitaaluma .Lakini pia ni wito kwa Mashirika, Taasisi na watu binafsi kujitolea ili kuwafadhili watoto kwenye mafunzo hayo nje ya nchi hususani bara la Ulaya ambako wamepiga hatua kubwa za maendeleo kwenye eneo hili la michezo.


Utekelezwaji wake.

Mchakato wa kuwapata watoto wenye vipaji na uhitaji wa kupata ufadhili,lazima kuwe na sheria, taratibu na kanuni maalumu ili kusiwepo urasimu au aina yeyote ya upendeleo.Tunafahamiana vizuri sisi Watanzania tuna janjajanja nyingi kama sio udanganyifu hasa kwenye maeneo yenye fursa,asiyestahili atapitishwa na anayestahili atapita kwa tabu kama sio kukosa kabisa nafasi.

Ushirikishwaji wa wazazi au walezi na waalimu ni moja ya hatua muhimu ya awali ili kupata watoto wenye vipaji vya mchezo husika.Maandalizi ya kisaikolojia kwa watoto kabla ya kuondoka ili wafahamu dhumuni hasa la wao kupata nafasi hizo ,japo umri wao ni mdogo lakini lazima waambiwe wao ni mashujaa tegemezi wa kesho wa Tanzania kwenye kuiwakilisha nchi kimataifa kupitia mpira wa miguu .

Kadri umri unavyoongezeka ndivyo motisha,hamasa na elimu ya utambuzi vitaongezeka kwa vijana hao ili wajitunze na kuthamini urijali wao.Utamaduni wetu usipotee hata wakiwa Ulaya au Asia, na wawe mabalozi wazuri wa utalii wa nchi yetu .


Faida zake kwa nchi.

Kwanza kabisa lazima tukubaliane kwamba nchi zilizoendelea haziamini sana ujuzi tulionao pasi na wao kuuongezea maarifa,kwa tafsiri hio nadhani watoto watakaopata elimu nje ya nchi ni rahisi zaidi kupata kazi nchi hizo.Hivyo ni matarajio yangu kuona Watanzania wengi wakishiriki Ligi zenye nguvu zaidi duniani kwa kusajiliwa na Vilabu vikubwa. Na zaidi, tutaingiza fedha za kigeni kupitia wachezaji wetu ambao kimsingi itakuwa rahisi kucheza kwenye Vilabu vikubwa vya nchi zilizoendelea.Na kuwa chachu ya kupanda kiuchumi kupitia mpira wa miguu.

Pia kimkakati hao watoto ndio watakaokuwa mifano bora kwa wengine ambao watakosa nafasi ya kupata ufadhili,hii maana yake mifano kwenye kupanda mbegu za kujiamini na kuja kuwa waalimu na wakufunzi katika vilabu na Footbal Academies.

Aidha timu ya taifa itafanya makubwa zaidi kwenye fainali za kombe la dunia (World Cup)na AFCON.Kwakuwa tayari tutakuwa tuna kizazi chenye umahiri zaidi yaani kizazi cha dhahabu.Wazungu wanaita Cream players.

Na zaidi ,itapelekea kukua kwa mpira wa miguu na sekta ya michezo kwa ujumla.Pia itachochea ushiriki wa watoto wenye vipaji kwenye michezo na sanaa.

Hata kwenye Sanaa hatutakuwa nyuma kwani tutaweza kuzalisha kazi za sanaa zenye viwango vya kimatiafa ,hivyo tutaingiza kazi zetu kwenye soko la dunia na kuitangaza nchi pamoja na kuiingizia nchi fedha za kigeni,huku tasnia itatengeneza ajira nyingi kwa watu wenye vipaji.

Inawezekana kwa kupitia maamuzi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Napokumbuka mazuri ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu naona ni vyema mchakato huu uhusike mpaka Zanzibar maana watu wengi hata viongozi wetu baadhi ukiwatajia Tanzania wanafikiria Tanzania bara peke yake ,tunasahau maana halisi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni pongezi zisizo na unafiki ninapo tambua kujitoa kwa makusudi kwa Mama wa nchi kwenye maendeleo ya mpira wa miguu.Ametoa Hamasa kubwa, na bado ameonesha jitihada katika kufanikisha hatimaye imewezekana sasa Tanzania kuwa mwenyeji mwenza wa mashindano ya Afcon mwaka 2027.

Ukiacha kwamba mpira wa miguu ni sehemu ya utalii au ni chambo cha kuwafanya wageni kufika Tanzania ili washuhudie vivutio vilivyopo nchini, lakini ni mchango mkubwa sana katika kuukuza mpira wa miguu na sekta ya michezo kwa ujumla.

Baada ya hizi hamasa zake nadhani baadaye tutaketi chini kujiuliza tufanye nini zaidi ili kamera za dunia zinapoelekezwa Tanzania basi dunia ivutiwe zaidi?

Kuna Msemo napenda kuutumia unaitwa “Njooni muone iwe na mshangao” nikiwa na maana kwamba tunaweza kufanya matangazo wateja wakaja kwa wingi hadi huo wingi ukatushangaza wenyewe lakini tukapungukiwa bidhaa za kuwashangaza wateja,hivyo hupelekea siku nyingine mkiwaita hawaji hata kama mmeshaboresha.Hii ni changamoto kwenye eneo la maandalizi ya sekta ya michezo,nadhani tuanze juhudi za kuwapika watoto ili baada ya miaka 15 tupate kizazi cha dhahabu kwenye mpira wa miguu.Sambamba na urithi wa maarifa na ujuzi wa mpira wa miguu , kwanzia kuucheza,nidhamu,uongozi na biashara.

Hivyo hivyo iwe kwenye Sanaa, nimeona Rais alitangaza na kutekeleza nia yake ya kusafiri na waigizaji pamoja na waandaaji wa filamu nchini kwenye ziara zake nchini Korea. Haya ni maono mazuri sana lakini sasa tunahitaji kujenga taifa endelevu hivyo tuanze kuwaangalia watoto wetu.

Ni jambo lenye siha kwenye tasnia na taifa kwa ujumla kuwafadhili watoto waende huko Korea, America, Uturuki na nchi nyingine zilizoendelea kwenye tasnia hii wajivunze ABC za sanaa ili kuongeza maarifa na ujuzi zaidi ya waliokuwa nao wazee wetu waanzilishi wa fani hii, ili tujidhatiti kuingiza kazi zetu kwenye soko la dunia.Na hii iwe kwa aina zote za Sanaa kama Muziki ,Uchoraji lakini kwa kuanza tunaweza kuchagua vile vyenye tija zaidi kama Uigizaji, Muziki na mpira wa miguu ili kuchochea vingine baada ya kufanikiwa.


Mtazamo juu ya hoja hii.

Najua ni gharama lakini katika kila mpango-mkakati lazima kujinyima kitu ili kupata kitu.Hii inamaana yapo mambo tuliyofanya kwa miaka mingi ambayo kwa namna fulani yameigharimu serikali fedha nyingi ,lakini hayajaleta matokeo chanya kwa taifa .Nadhani wabobezi wa uchumi na mipango yakimaendeleo wanafahamu zaidi ni maeneo yapi haswa yanahitaji kupisha mchakato huu wa kimkakati.

Binafsi naona fursa iliopo kwenye magawio ya sekta na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi kwa Serikali kwa kila mwaka, mathalani Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeripotiwa hivi karibuni kwamba imetoa gawio kubwa zaidi kwa serikali kiasi cha Bilioni 153.9.Nadhani ni bora kutumia magawio kwakuwa si mavuno-tarajiwa sana ukilinganisha na vyanzo vingine vya mapato.

Kwa mfano fedha zote ambazo zinaingia Serikalini kama gawio zikielekezwa kwenye jambo hili ,hakika tutafikia lengo kwa asilimia kubwa.

Aidha, kama Serikali itatangaza dhamira yake ya kutoa ufadhili kwa watoto bilashaka taasisi mbalimbali zitaunga mkono ili kufanikisha dhamira hii ukiachilia mbali kuelekeza magawio kutoka kwenye sekta na taasisi mbalimbali.

Pia kwa zile taasisi za fedha za kimataifa kama Stanbic bank, Standard Chartered na zinginezo wataona fursa ya kuwafungulia watoto hao Accounts ili kufanya miamala kwaajili ya nauli ,ada na mahitaji kwa kutumia kadi za kibenki, pamoja na kuwatumia kwenye matangazo baada ya kuchangia kwenye mfuko wa Ufadhili huo.

Na bado yapo mashirika mengi ya ustawi wa jamii ya kimataifa ambayo kimsingi yanaweza kuomba ruzuku kwa wahisani kwaajili ya kufanikisha jambo hili ikiwa ndio uelekeo wetu kama nchi katika kukuza Soka letu na Sanaa.

Kama ilivyo kwa mikakati mingine endelevu ya kimaendeleo,jambo hili linahitaji pia muitikio wa sekta nyingine saidizi ili kufanikisha, lugha ya kigeni tunasema jambo hili linahitaji Cross Sector Response.Kwa mfano Sekta ya Madini, Serikali inaweza kutangaza kwa wawekezaji dira yake ili kuhamasisha zoezi la kulipa kodi na tozo zote stahiki kwa wakati kwakuwa kuna mkakati wa kuwasomesha watoto wetu ili baadaye tuje kujivunia.

Vile vile sekta nyingine kama ya utalii na maliasili nayo inaweza kutoa mchango mkubwa kwenye mkakati huu,kupitia tozo mbalimbali za ndani ya kiwanda cha utalii.

Baada ya hapo ndipo tutaweza kuandaa miundombinu yetu kwaajili ya Football Academies zenye hadhi ya kimataifa.

Zaidi nadhani kama ilivyo kwenye Sanaa wanahitajika wasanii pamoja na watayarishaji wa kazi za sanaa,pia kwenye mpira wa miguu wapelekwe watoto wenye vipaji lakini pia na vijana ambao watakwenda kuchukua mafunzo ya ukufunzi kwenye eneo la kukuza watoto na ualimu,uamuzi, na uongozi wa michezo, japo msisitizo mkubwa uwe watoto wenye vipaji.

Hitimisho.

Nahitimisha kwa kukumbusha kwamba Tanzania tunayohitaji kuiona ni ile itakayofuta kabisa majina ya fedheha tuliyojibatiza kwenye michezo kama “Kichwa cha mwendawazimu” na viwanja vyetu visiitwe tena “Shamba la bibi” nasi ifike pahala Vilabu vya mpira wa miguu vikubwa duniani vichague kuja Tanzania kwaajili ya maandalizi kabla ya msimu mpya wa ligi (Pre season.)na hata kutumika katika ligi mbalimbali.

Izingatiwe kuwa mchakato wa kuwekeza kwenye Football Academy ni wa lazima ili tujitosheleze zaidi.Napongeza uthubutu na juhudi za makusudi kwa vituo vyenye huduma hii kama Moro Kids pale Morogoro,Dogout Footbal Academy, Kids Sports Academy za Dar es Salaam na nyinginezo ,huu ni mwanzo mzuri.Lakini kwa sasa tuanzie hapa,kuwapeleka watoto wetu nje ya nchi wakapate ujuzi unaokidhi ushindani wa kimataifa.


Asanteni kwa muda wenu;


Nawasilisha.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom