Kutoka maktaba za kijeshi

Joined
Oct 5, 2015
Posts
90
Reaction score
482
KUTOKA MAKTABA ZA KIJESHI

Baada ya jaribio la mapinduzi kushindwa, Nyerere aliamua kuchukua hatua kadhaa zilizobadili taswira ya jeshi la Tanzania.

Muhtasari.
Ilikuwa jioni ya January 20, 1964, wakati wanajeshi wa vyeo vya chini walipoamua kuasi, kwa sababu zilizoelezwa kuwa ni maisha duni yaliyotokana na mishahara midogo, pia walitaka kuwaondoa maofisa wa ngazi za juu waliokuwa Wazungu.
Haifahamiki kama wanajeshi hao walitaka kupindua nchi au la, lakini tukio hilo lilizua kasheshe kubwa.

Wakati huo jeshi la Tanzania lilikuwa ni mabaki ya jeshi la kikoloni liloitwa King African Rifles (KAR). Maofisa wote wa ngazi za juu walikuwa wazungu au machotara isipokuwa waafrika wanne tu waliokuwa na vyeo vya Luteni.

Waafrika hao wanne wenye vyeo vya Luteni ndiwo walikuwa waafrika wenye vyeo vikubwa kabisa kuliko waafrika wote ndani ya KAR.

Alikuwepo Luteni Mrisho Haggai Sarakinkya, ambaye baada ya uasi kuzimwa alipandishwa ngazi na Waziri wa Ulinzi, Oscar Salathiel Kambona, akawa Meja Generali na kupewa ukuu wa majeshi. Wakati Sarakinkya akipewa cheo hiko, mwenyewe hakujua. Wakati huo alikuwa mkuu wa kambi ya Tabora na Kambona aliamua kumpa cheo hiko ili asifanye uasi kutokea Tabora.

Mwingine alikuwa Luteni Alexander Nyerenda, mzaliwa wa Nyasaland (Malawi ya leo) huyu ndiye alipandisha bendera ya Tanganyika na kuikita kwenye kilele cha uhuru (Uhuru peak) cha mlima Kilimanjaro usiku wa manane wa Desemba 9, 1961, siku ya uhuru wa Tanganyika.

Mwafrika mwingine aliyekuwa na cheo cha Luteni ni Luteni Ameenullah Kashimiri aliyekuwa ametoka
kwenye mafunzo ya u-ofisa kadeti huko Sandhurst, Uingereza. Kabla ya kwenda Uingereza, Luteni Kashimiri alipata mafunzo yake ya awali katika mji wa Jinja nchini Uganda chini ya Sajini Idd Amini Dada, aliyekuja kupindua nchi na kuwa mtawala wa Uganda.

Siku hiyo ya uasi, Luteni Kashimiri alikuwa mkaguzi wa zamu katika makambi ya mkoa wa Dar es Salam. Alipofika kukagua kambi la Colito, alikamatwa na kuwekwa chini ya Ulinzi na kufungiwa kwenye chumba. Luteni Kashimiri ni moja ya watu muhimu walitumika kulisuka upya jeshi la Tanzania, JWTZ.

Mwafrika mwingine aliyekuwa ndani ya jeshi la KAR, mwenye cheo cha Luteni ni Elisha Kavana.

Luteni Kavana anatajwa kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi akishirikiana na Kanali Hingi. Ingawa alikuwa na umri mdogo lakini alikuwa na heshima zaidi na upendeleo zaidi ndani ya jeshi. Luteni Kavana alifanya safari nyingi za nje ya nchi, akitembelea kambi za kijeshi huko Nairobi, Kenya na Kampala Uganda.

Baadhi ya wachambuzi wanaoamini kuwa uasi huo ulikuwa na lengo la kumpindua Mwalimu wanatumia sababu hiyo ya Kavana kukutana na wanajeshi wa nchi za Kenya na Uganda katika mipango yake. Vilevile, kulikuwa na uasi huko Kenya na Uganda muda uleule ulipotokea uasi wa Tanganyika.

Taarifa za uasi zilivuja wiki mbili kabla ya uasi lakini hazikuwa na uhakika. Mkuu wa majeshi wa Tanganyika, Muingereza Brigedia Douglas Sholto aliwatahadharisha maofisa wake wa jeshi kuwa makini na kujiandaa kwa lolote.

Siku ya Tukio.
'Afande Teremka'! 'Uko chini ya ulinzi'. Mwanzoni Luteni Kashimiri alifikiri ni utani lakini aligundua haraka kuwa kuna kitu kinaendelea. Kambi lote la Colito na maeneo ya jirani lilikuwa na giza totoro, waasi walivamia kituo cha kusambaza umeme na kuamuru umeme ukatwe.

Kulikuwa na upinzani kutoka kwa Polisi wa jiji la Dar es Salaam. Lakini Polisi hawakuwa na uwezo wa kupambana na waasi, lakini pia walikuwa wachache kwani baadhi yao walipelekwa Zanzibar kulinda amani baada ya mapinduzi, wiki moja tu iliyopita.

Wananchi nawo walianza vurugu zao. Katika maeneo ya upanga waswahili walivamia maduka ya washindi na kuanza kupora mali. Lakini Polisi baada ya kusalimu amri kwa waasi, waliendelea na jukumu lao la kutuliza ghasia.

Maofisa wa jeshi wa kizungu walikamatwa na wengine walioweza kukimbia walijificha kwenye pori la mlimani, mahali ambapo palikuja kujengwa chuo kikuu cha Dar es salaam. Wazungu hao walifanikiwa kubeba simu za upepo (radio call) na kuwasiliana na wenzao wa karibu ili wakiweza watume taarifa nchini Uingereza.

Hata hivyo, Brigedia Douglas Sholto na msaidizi wake Kanali Brian Marciandi hawakukamatwa. Brigedia Sholto alijituliza kwenye jengo la Standard Bank, mahali zilipo ofisi za British Council leo hii.

Serikali yote ya Mwalimu Nyerere ilijificha. Mwalimu alifichwa na Askofu wa jimbo Katoliki la Dar es salaam, maeneo yanayosadikiwa kuwa ya Kanisa la St. Peters - Oysrebay ambapo baadae katika maisha yake alipenda sana kufanyia ibada. Kutokea eneo hilo, alihamishiwa maeneo tofautitofauti ikiwemo Kigamboni, kwenye nyumba ya Jaji Mustapha ili isifahamike mahali rasmi alipo.

Akiwa ndani ya nyumba ya Jaji Mustapha ndipo alipoanza kutafuta msaada kutoka Uingereza.
Makamu wa Rais Mh. Rashidi Kawawa alijificha katika msikiti mmoja jijini Dar es salaam. Mawaziri wengine walijificha kusikojulikana isipokuwa Job Lusinde na Oscar Kambona.

Job Marecela Lusinde alikuwa waziri wa mambo ya ndani. Yeye hakujificha kwa makusudi, na kwa hiyo alikamatwa na kuwekwa kizuizini. Lakini kwa heshima ya nafasi yake alijitahidi kushirikiana na Kambona ili kutuliza maasi. Oscar Kambona alikuwa waziri wa Ulinzi, naye hakujificha lakini hakukamatwa bali alitumia nafasi yake kuzungumza na waasi.

Kambona alikuwa mtiifu kwa Mwalimu, mpigania uhuru na mwanaharakati wa ukombozi wa Afrika. Hadi wakati huo wa maasi, hakuwa na wazo la kumpindua Mwalimu Nyerere, lakini kama angalikuwa na haja hiyo, kwa jinsi hali ya mambo ilivyokuwa, angeweza kufanya mapinduzi kirahisi.

Lakini kitendo cha kuambatana na Luteni Kavana, aliyetajwa kuongoza maasi kunaweka fumbo kubwa ambalo Kambona mwenyewe ndiye mwenye jibu lake. Jambo ambalo ni uhakika, ni kuwa miaka miwili baadae, Kambona alijuta kutoitumia nafasi hiyo.

Wakati wa kutafuta suluhu, Kambona aliwakubalia wanajeshi ombi lao la nyongeza ya mshahara lakini si kwa kiasi walichotaka. Wanajeshi walitaka kuongezewa kutoa Shilingi 105 hadi 260 kwa mwezi. Kambona aliomba wakubali shilingi 150, wakakubali.

Kutuliza Maasi.
Siku moja wakati wa mkutano mkuu wa OAU uliofanyika mwishoni mwaka mwaka 1964, aliyekuwa Rais wa Ghana, Kwame Nkurumah alimuita Nyerere - Coward, maana yake Bwege. Nkurumah alimuita Nyerere kwa jina hilo kwa sababu Nyerere aliomba msaada kutoka Uingereza ili wamsaidie kurejesha madaraka yake.

Miaka mitatu iliyopita, Nyerere aliwafukuza watawala wa kiingereza na kuwataka warudi kutalii miaka 10 ijayo waone Tanganyika ilivyoendelea. Zaidi Nyerere hakutaka msaada wa kuongoza kutoka kwa Uingereza badala yake aliamini kuwa watu wake wako tayari kujiongoza wenyewe. Wakati huo wa uasi, Mwalimu alikula maneno yake.

Meli kubwa ya kubebea ndege za kivita aina ya HMS Canteur, iliyokuwa ikiambaa ambaa kwenye bahari ya hindi, ilifika karibu na fukwe za jiji la Dar es Salaam siku ya januari 25, kisha helkopter iliyobeba makomandoo ilipaa kuelekea kambi la Colito. Makomandoo wengine walitumia gari aina ya LandRover kufika katika kambi hilo, risasi zilirushwa kutoka kwenye helkopta na zingine kutoka kwenye LandRover.

Baada ya masaa machache, Askari watatu wa upande wa maasi walifariki na wengine wengi kujeruhiwa. Waliosalia walikimbia na kutupa silaha vichakani. Shughuli ya kuzima maasi ilihamia huko Nachingwea ambako napo maasi yalianza. Kwa mtindo uleule, maasi yalizimwa.

Hata hivyo, bado kulikuwa na mabaki ya uasi ndani ya jeshi. Jeshi la Uingereza lilipaswa kubaki kwa muda wa angalau mwezi mmoja ili kulinda serikali ya Mwalimu Nyerere wakati akijiandaa kuunda upya jeshi la Tanganyika. Lakini Uingereza hakuwa imejiandaa kwa kazi hiyo, kwa hivyo ilibidi kualika jeshi la Nigeria, kuja kusaidia kuilinda serikali ya Mwalimu.

Lawama kwa Kambona.
Nyerere na viongozi wengi walimshukuru sana Kambona. Ingawa Ombi la msaada liliandikwa na Nyerere mwenyewe, lakini aliyeweza kujitokeza hadharani na kufanya mawasiliano na Waingereza ni Oscar Kambona. Awali, Kambona na Lusinde walikataa kuwaita Waingereza na Jeshi la Kenya (Kenyan Rifles) wakiamini wangeweza kudhibiti hali ya uasi, lakini baadae walisalimu amri. Kambona ndiye aliyekubaliana na waasi kuwaondoa maofisa wa kizungu ndani ya jeshi, pia kuondoa meli ya kivita ya kiingereza aina ya HMS Rhyl, iliyokuwa katika fukwe za Oysrebay, ili kuwahakikishia usalama waasi.

Lakini Kambona hakuweza kukwepa lawama za kuchangia maasi hayo yatokee. Akiwa kama waziri wa ulinzi, aliwajibika moja kwa moja kwenye maslahi ya wanajeshi. Kosa alilofanya Kambona ni kutoa ahadi za kuwaboreshea maisha mara kwa mara bila kuzitekeleza. Lakini kosa kubwa zaidi ni vile alipowaunganisha vijana wa TANU (TANU Youth League) ndani ya vyombo vya ulinzi bila kuwa na taaluma za ulinzi za kutosha.

Vijana wengi wa TANU walioingizwa ndani ya jeshi kwa mkono wa Kambona, hawakuwa na nidhamu kwa maofisa wa jehsi wa ngazi za juu, zaidi waliwasiliana na kufanya kazi moja kwa moja na waziri Oscar Kambona. Moja kati ya vitengo yalioathiriwa na utaratibu huo ni ukusanyaji wa taarifa ndani ya jeshi, jambo lililosababisha kutokea kwa uasi bila serikali kuwa na taarifa.

Nyerere naye Apindua.
Maasi ya jeshi la Kings African Rifles yalimchefua mwalimu na kumfanya achukue hatua madhubuti. Ingawa Mwalimu alikubali kuwa madai ya wanajeshi yalikuwa ya msingi lakini uasi hauvumiliki. Madai yao ya nyongeza ya mshahara yalikuwapo tangu siku ya uhuru. Maisha yalikuwa duni tofauti na Rais Nyerere alivyowaahidi, vitanda vyao vilikuwa mbao na/au sakafu ngumu na magodoro yao yalikuwa blanketi. Kila askari alipewa mablanketi mawili, moja la kutandika na lingine la kujifunika. Madai mengine ni ya kupandishwa vyeo, kwakuwa nafasi nyeti za juu zilikuwa bado zikishikwa na wazungu na machotara wa kizungu.

Maasi yale yalizaa matunda kwa kiasi. Wanajeshi wa kizungu wote walipakiwa kwenye ndege na kurudishwa kwao. Lakini vijana wote waliohusika na uasi walifukuzwa jeshini. Kisha mwalimu alifanya mapinduzi yake ambayo baadhi yametugharimu hadi leo.

kwanza alifuta jeshi lote la KAR, na kuanzisha Jeshi la wananchi ambalo baadae liliitwa JWTZ. Akaanzisha utaratibu mpya wa kudahiri vijana wadogo wenye umri wa miaka 18, badala ya watu wazima ambao tayari walikuwa na itikadi zao.

Pili aliamua kuliunganisha jeshi na chama cha TANU. Kila aliyehitaji kwenda jeshini alipaswa kuwa mwanachama wa TANU. Utaratibu huu ulikuja kuwa na madhara makubwa baadae, hadi leo hii. Huu ni mjadala mwingine.

Tatu Mwalimu aliamua kupunguza idadi ya makabila yenye nguvu ndani ya jeshi. Kulikuwa na makabila matatu yenye nguvu ndani ya jeshi kutokana na wingi wao. Hii ilianzia tangu kipindi cha ukoloni wa kijerumani na kwa sababu jeshi la Tanganyika lilikuwa ni mabaki ya ukoloni, hali ilikuwa hivyo hivyo.

Makabila hayo ni Wahehe, Wajinga na Wanyamwezi ambao historia inawataja kuwa wapiganaji hodari katika eneo la Afrika mashariki. Mwalimu Nyerere aliamua kuanza kudahiri kabila lingine la Kikurya, ambalo nalo lina historia ya uhodari lakini hawakuwa wengi ndani ya jeshi la Tangayika. Utaratibu huo ulifanya Wakurya kuingizwa kwa wingi ndani ya jeshi la JWTZ.

Zaidi ya hilo, Mwalimu alitumia mwanya huo wa upendeleo kwa Wakurya kuwafanya watu wa kumpa taarifa kutoka jeshini. Aliwapa fursa za kusoma na vyeo vikubwa ndani ya jeshi. Baadhi wa wanufaika wa utaratibu huu ni Jaji Joseph Warioba, na wakuu wengine wa serikalini na jeshini.

Ngome ya Colito ambapo maasi yaliasisiwa, ilibadilishwa jina na kuitwa Ngome ya Lugalo, kwa heshima ya eneo ambalo Mtwa Mkwawa alifanya mapambano makubwa dhidi ya Wakoloni wa kijerumani huko Iringa. Jina Colito halikuwa na maana yoyote katika historia ya Tanganyika.

Mengne next time...
#British_National_Archives.
#Army_Affairs
#Making_Of_Tanganyika
 
Huu uzi una maana gani kuuleta wakati ni kitu kilishapitwa au una lako jambo
 
Nina mwezi mzima JF sijakutana na uzi wenye akili kama huu. Kila kona unakutana na uzi mtu anaomba ushauri wa kuongeza nguvu za kiume, mwingine anauza kuku, mwingine sijui karogwa, mwingine anaomba ushauri wa kuweka mikeka (kubeti).

Congrats mkuu kwa historia yenye tija.[emoji120]
 
Note
 
..mwandishi amefanya kitu kinaitwa PLAGIARISM.

..naweza kusema habari hii haijatoka ktk maktaba ya Jeshi.

..Jeshi haliwezi kukosea jina la mkuu wa majeshi wa kwanza mzalendo.

..Anaitwa Mirisho Sarakikya. Ni mwenyeji wa Meru, Arusha.

..Haitwi Mrisho, ambalo ni jina la wenyeji wa Pwani, na Tanga.

..Wengine walikosewa majina yao ni Job Melecela Lusinde, na Alexander Nyirenda.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…