SoC03 Kutoka ugonjwa hadi fursa

SoC03 Kutoka ugonjwa hadi fursa

Stories of Change - 2023 Competition

Marebu

New Member
Joined
May 10, 2023
Posts
2
Reaction score
2
KUTOKA UGONJWA HADI FURSA.

Mwaka 2018 nikiwa na umri wa miaka 20 niligundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa homa ya ini (Hepatitis B) baada ya kuchangia damu katika Mpango wa Taifa wa Damu Salama.

Nilijawa na hofu kwasababu sikujua lini na wapi nimepata hayo maambukizi. Mwaka huo nilikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha tano muhula wa pili wa masomo katika shule ya sekondari Rungwe.

Baada ya kugundua kuwa ninamaambukizi ya ugonjwa huo, nilienda hospitali ya wilaya ya Rungwe (Makandana) na kisha kukutana na Daktari. Daktari alipendekeza vipimo kwa ajili ya uhakiki wa maambukizi hayo. Nilienda Maabara ya hospitali hiyo kwa ajili ya uchunguzi.

Uchunguzi ulionyesha kuwa ninamaambukizi ya ugonjwa huo na daktari alieleza kuwa hakuna dawa ya kutibu ugonjwa huo na tena sitapona huo ugonjwa hadi mwisho wa maisha yangu. Daktari aliniandikia barua ya rufani Kwenda Hospitali ya Rufani Kanda ya Mbeya.

Nilitoka hapo hospitali nikiwa nimekata tamaa ya kuishi tena kwani nilijua kuwa muda mfupi tu nitafariki.

Baada ya siku chache kupita, niliomba ruhusu kutoka kwa Makamo Mkuu wa Shule ili niende Hospitali ya Rufani Kanda ya Mbeya kwa ajili ya matibabu. Nilifika hospitali na nilipokelewa vizuri katika Idara ya Magonjwa ya Dharura.

Nilisubiri kwa muda mchache kisha nikaelekezwa chumba alipodaktari. Niliingia katika chumba hicho na daktari akanikaribisha kuketi katika kiti.

Daktari aliniuliza “Nini kinakusumbua?” baada ya daktari kuuliza swali hilo nilimpatia barua ya rufani niliyopewa kutoka hospitali ya wilaya ya Rungwe (Makandana).

Daktari aliuliza “Umewahi kushiriki ngono?” Nilijibu hapana. Daktari aliuliza tena “Umewahi kuchangia vitu vyenye ncha kali na mtu mwingine?” nilijibu labda mashine za kunyolea.

Baada ya maswali hayo daktari alisema niende Maabara kwa ajili ya vipimo. Nilichukuliwa damu na kisha nikaambiwa nisubiri masaa 3. Baada ya masaa hayo nilikwenda kwa wahudumu wa Maabara na kisha walinielekeza niende katika chumba cha daktari. Daktari alieleza kuwa ni kweli ninamaambukizi hayo. Daktari aliniandikia dawa ambazo nilitakiwa kutumia kwa miezi mitatu. Daktari alisisitiza kurudi hospitalini hapo baada ya miezi sita ili kujua maendeleo yangu. Nilienda duka la Famasia nikanunua dozi ya mwezi mmoja. Nilifanya hivyo kwa miezi miwili iliyofuata na hali yangu ya afya ilikuwa nafuu lakini, nilipunguza juhudi katika masomo yangu kwa kuwa nilijuwa baada ya muda mchache tu ningeweza kufariki.

Mnamo tarehe 23/05/2019 nilihitimisha kufanya mitihani ya Taifa kidato cha sita katika mchepuo wa sayansi (PCB) na kisha nilirudi nyumbani, Tabora.

Miezi sita ya kurudi hospitali ilifika lakini, sikuweza kurudi hospitali kwasababu ya hali duni ya maisha nyumbani.

Nikiwa hapo kijijini kwetu nilianza kuazima simu janja kwaajili ya kutafuta taarifa mbalimbali kuhusiana na ugonjwa nilionao.

Taarifa ya kwanza kutafuta ilikuwa “je mtu mwenye homa ya ini huweza kuishi kwa muda gani baada ya maambukizi? Kivinjari (google) kilionyesha kuwa maambukizi hayo hukoma ndani ya miezi sita baada ya maambukizi ikiwa kinga ya mwili itakuwa mathubuti na imara. Lakini pia, kivinjari hicho kilionyesha kuwa maambukizi hayo yakiendelea kuonekana zaidi ya miezi sita, basi ugonjwa utabaki hata mwisho wa maisha.

Nilijitahidi kutafuta huo mwisho wa maisha huwa ni miaka mingapi baada ya maambukizi lakini sikufanikiwa. Kisha nilitafuta kisababishi cha ugonjwa huo na kivinjari kilionyesha kuwa kisababishi cha homa ya ini ni kirusi cha homa ya ini (Hepatitis B Virus).

Pia nilitafuta njia za kupatwa na kirusi hiki na kivinjari kilionyesha kuwa mtu anaweza kupata na kuambukizwa kirusi hicho kupitia kugusana na mwathirika au damu au majimaji mengine yaliyo na virusi hivyo, kuchangia vitu vyenye ncha kali kama vile wembe na sindano na kuchangia nguo au taulo. Lakini pia, nilitafuta dalili za ugonjwa huu na kivinjari kilionyesha kuwa mtu mwenye ugonjwa wa homa ya ini huwa ana dalili zifuatazo uchovu wa mwili, kichefuchefu, kutapika, maumivu ya kichwa, homa, maumivu ya misuli, maumivu ya tumbo, kukosa hamu ya kula, kukojoa mkojo wenye rangi ya kahawia, kutoa choo cheupe, kuwa na weupe wa macho, mwasho wa ngozi na kuharisha.

Mnamo mwezi wa 7 mwaka 2019, matokeo ya mtihani wa Taifa kidato cha sita yalitoka na nilifaulo japo si kwa ufaulu nilioupanga kipindi naingia kidato cha tano wa kupata daraja la kwanza kwasababu nilikuwa na mpango wa kusoma katika kada za afya. Nilimshukuru Mungu sana kwa kuniwezesha kupata ufaulu huo wa kunipeleka chuo kikuu, nilijua nisingefaulu kabisa.

Lakini nilihudhunika sana kukosa kile nilipanga kukipata yawezekana sikujua Mungu ana mpango gani na mimi. Sikuweza kuomba vyuo vya kati kwa ajili ya kuenda kusoma kada ya afya kwasababu ya hali duni ya maisha nyumbani. Hali hiyo ilinibidi kuomba chuo kikuu na mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

Namshukuru sana Mungu kwasababu nilichaguliwa chuo kikuu cha Dodoma katika kada ya sayansi na nilipata mkopo kwa asilimia zote na kuniwezesha kusoma hapo chuoni bila usumbufu wowote ule.

Mnamo mwezi wa 10 mwaka 2019 nilifika na kujisajiri hapo chuoni. Nilipofika chuoni nilienda kupima tena katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Uchunguzi ulionyesha kuwa bado nina maambukizi hayo. Maisha yaliendelea japo sikuwa na matumaini ya kuishi miaka mingi hapa duniani.

Maendeleo yangu kimasomo katika muhula wa kwanza wa mwaka wa kwanza yaliendelea kuwa duni. Baada ya siku chache, nilijiunga na kikundi cha Umishenari wa Kitabibu (Medical Missionary Movement).

Katika kikundi hiki nilijifunza na kufuata kanuni mbalimbali za kiafya na kuanza kutumia lishe tiba na mimea dawa huku nikimuomba Mungu aniponye huu ugonjwa.

Katika kipindi hiki nilijikuta nafuatilia lishe tiba na mimea dawa kwa undani zaidi na cha kushangaza zaidi kada niliyosoma ilikuwa na mahusiano makubwa ya lishe tiba na mimea dawa. Nikiwa katika mwaka wa mwisho wa masomo mnamo mwezi wa tatu mwaka 2022, nilienda kupima tena katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na vipimo vilionyesha kuwa sina tena hayo maambukizi.
DSC_0588~2.JPG


Namshukuru sana Mungu kwa muujiza huu mkumbwa alionifanyia.

Kiujumla, changamoto ni mwalimu mzuri kwasababu hufungua fursa ya kujifunza ili kukabiliana nayo.

Changamoto yangu ya kiafya ilifungua fursa ya kujifunza namna ya kukabiliana nayo.

Kupitia changamoto hii, Mungu alinionyesha fursa nyingine. Fursa hiyo ni tiba ya asili.
IMG_20230607_091247_166.jpg


Njozi yangu ni kuisaidia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Afrika kwa ujumla katika kuboresha na kuendeleza tiba asili kupitia utafiti na utoaji wa elimu na huduma katika tiba asili.
mayoge b.jpg


Pendekezo langu kwa msomaji ni kugundua fursa kupitia changamoto iliyopo.
 
Upvote 4
Back
Top Bottom