Bonge La Afya
Member
- Dec 19, 2016
- 35
- 83
Mifugo na mazao kulipia bima ya NHIF na mikakati ya Tanzania kufikia lengo la bima ya afya kwa wote
Imeandikwa na Bonge La Afya
UTANGULIZIImeandikwa na Bonge La Afya
Njia rahisi na nafuu za kulipia huduma za afya ni nguzo muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi. Katika nchi nyingi za kipato cha chini na kati, bima ya afya inachukuliwa kama njia kuu ya kulipia huduma za afya, ingawa bado inaonekana kuwa changamoto kubwa. Mwishoni mwa mwaka 2021, ni asilimia 15 tu ya Watanzania walikuwa na bima ya afya, ikionyesha umuhimu wa kuboresha na kuleta mikakati itakayowezesha kufikia watanzania wengi zaidi kujiunga na mifuko ya bima za afya. Makala hii inalenga kuonesha njia na mbinu za kufikia idadi kubwa ya Watanzania ili waweze kujiunga na bima za afya, na hivyo kuboresha afya na ustawi wao.
TAARIFA YA TATIZO
Zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanaishi maeneo ya vijijini. Kati ya jumla ya watanzania milioni 65.5 nchini, ni watu milioni 9.8 pekee wenye bima ya afya, sawa na asilimia 15 tu ya Watanzania wote. Asilimia 8 wanatumia NHIF (watu milioni 5.24) na asilimia 7 wanatumia mifuko mingine (watu milioni 4.6). Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 imepitishwa ili kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya. Lengo kuu la sheria hii ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya bila kujali hali zao za kifedha, lakini bado, kwa njia zilizopo, nasikitika kusema hatutafikia lengo hili.
MAPENDEKEZO
Mapendekezo haya yamezingatia uwezo wa watu kulipia na nia yao ya kulipia bima za afya, mambo ambayo yanaweza kuathiriwa na changamoto za kiuchumi na muktadha wa kijamii, pamoja na uelewa na mtazamo wa wananchi. Shida kubwa katika bima ya afya ni nia ya kulipia, maana hata wale wenye uwezo wa kulipia mara nyingi hawafanyi hivyo kutokana na kukosa motisha au sababu za kutosha. Sababu za kutopatikana kwa nia zinaweza kujumuisha uzoefu wa huduma mtu amewahi kukutana nayo au usumbufu alioupata alipotumia bima ya afya hospitalini. Mapendekezo yangu yamepangiliwa katika hatua, nikizingatia kwamba kurejesha imani na nia ya kulipa bima inaweza kuhitaji muda na jitihada endelevu.
HATUA YA KWANZA: Kuondoa Matabaka ya malipo na huduma kwenye Vifurushi vya Bima ya Afya ya NHIF
Kuondoa matabaka ya malipo na matabaka ya huduma kwenye vifurushi vya bima ya afya ya NHIF ni hatua muhimu katika kuboresha upatikanaji na usawa wa huduma za afya nchini. Kwa sasa, kuna matabaka mengi yasiyo na maana ambayo yanachangia kutofautiana kwa huduma na makato ya mwezi kati ya vifurushi mbalimbali vya bima ya afya ya NHIF. Wafanyakazi katika sekta rasmi (kama vile serikali na binafsi) wanatumia vifurushi tofauti na watu wasio na ajira rasmi au wenye ajira isiyo rasmi.
Mapendekezo yangu yanalenga kusitisha utaratibu huu na badala yake kuanzisha vifurushi viwili tu: kimoja kwa wafanyakazi walio katika sekta rasmi na kingine kwa wananchi wasio katika ajira rasmi. Kwa njia hii, kila kundi litachangia kiasi kinacholingana na uwezo wake, huku wote wakipata fursa sawa ya kupata huduma za afya bila upendeleo au tofauti zisizo za msingi kulingana na aina ya kazi au ajira wanayofanya. Hatua hii itapunguza matabaka na kusaidia kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za afya kwa Watanzania wote.
HATUA YA PILI: Kuweka urahisi wa kusajili na kulipia bima ya afya
Baada ya kushughulikia suala la upatikanaji wa huduma tunahitaji kurahisisha usajili na ulipaji wa huduma za afya. Kwa sasa, mchakato wa kusajili bima ya afya unahitaji mtu kufika ofisi za NHIF za wilaya, jambo ambalo linaweza kuwa changamoto hasa kwa wananchi wa vijijini ambao wanakabiliwa na umbali mrefu na changamoto ya usafiri.
Ninapendekeza njia mbili za kuboresha usajili wa bima ya afya: kwanza, kutumia watoa huduma za afya ngazi ya jamii (community health workers). Hawa ni wataalamu walio katika mitaa na vitongoji vyetu ambao wanafahamu vyema jamii zao. Wanaweza kutembelea nyumba kwa nyumba kusajili watu kwa kutumia namba za kitambulisho cha taifa (NIDA). Hii itarahisisha wananchi kusajiliwa na kupata elimu ya bima ya afya bila haja ya kufika ofisi za wilaya.
Pili, tunaweza kuwaruhusu mawakala wa bima ya afya ambao watapata kamisheni ndogo kusaidia katika usajili.
HATUA YA TATU: Kuungana na Wizara ya Kilimo na Mifugo, kutumia mifugo na mazao kama njia kulipia bima ya afya.
Hatua ya tatu katika kuboresha mfumo wa bima ya afya ni kuungana na Wizara ya Kilimo na Mifugo ili kutumia mifugo na mazao kama njia mbadala za kulipia bima ya afya. Tumejionea mafanikio katika kuhakikisha huduma za afya zinapatikana bila ubaguzi na tumewafikia Watanzania wengi kupitia hatua za awali. Sasa tunahitaji kuanzisha njia rahisi na inayoendana na maisha ya watanzania wengi kwa kuzingatia kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini na wanajishughulisha na kilimo na ufugaji.
Kwa kuzingatia hali halisi ya nchi yetu, napendekeza kuwa badala ya kutumia pesa taslimu, tuwe na utaratibu wa kuwa na thamani ya mifugo na mazao wanayomiliki wananchi kama mtaji wa kulipia bima ya afya. Hii inaweza kufanyika kupitia ofisi za bima katika kata na wilaya, ambapo mazao na mifugo ya mtu yanaweza kuthaminishwa na maafisa kilimo au mifugo wa wilaya. Baada ya thamani kupatikana, mtu anaweza kukatwa bima na serikali inaweza kuuza mifugo au mazao haya katika minada ili kukusanya sehemu ya malipo ya bima.
Wizara ya Afya pia inaweza kushirikiana na wakulima ambao huuza mazao yao kwa serikali, na kuweka utaratibu ambao badala ya kulipwa pesa taslimu, sehemu ya malipo yao ya mazao yanaweza kutumika moja kwa moja kulipia bima ya afya. Hii itawezesha wananchi kupata huduma bora za afya bila kuhatarisha mtaji wao wa kudumu na itachochea ukuaji wa uchumi katika sekta ya kilimo na mifugo.
HITIMISHO
Ni muhimu sana kwa Tanzania kufanya maboresho katika mfumo wa bima ya afya ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kila Mtanzania. Pia, kwa kuingiza bima ya afya kwenye Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIDA) itaepusha udanganyifu na mtu kutembea na vitambulisho vingi, mtu atakapoenda hospitali atahitaji kuwa na kitambulisho kimoja tu cha NIDA badala ya vitambulisho vingi. Tanzania inaweza kusonga mbele katika kuboresha huduma za afya na kuhakikisha kuwa kila mmoja anapata huduma bora za afya kwa wakati unaofaa na bila vikwazo.
Upvote
1