SoC02 Kuwa na taaluma usiyoitumia kutimiza malengo yako ni kuikosea heshima

SoC02 Kuwa na taaluma usiyoitumia kutimiza malengo yako ni kuikosea heshima

Stories of Change - 2022 Competition

my nation

Member
Joined
Jul 15, 2021
Posts
71
Reaction score
96
Taaluma yoyote uliyonayo ina heshima yake ndio maana imekugharimu muda na mali mpaka kuipata taaluma hiyo. Bila kujali una ngazi gani katika taaluma hiyo lakini tambua ya kwamba ina heshima yake ndio maana umeihangaikia ili kuipata taaluma hiyo.

Inawezekana kwenye taaluma yako upo ngazi ya cheti, Stashahada, Shahada, Shahada ya umahiri au ya uzamivu kivyovyote vile taaluma yako inastahili heshima yake.

Siku zote ili kuzidi kuwa na weledi na uzoefu wa taaluma uliyonayo ni lazima ujishughulishe nayo, ukijishughulisha nayo kwa kufanya kazi mbalimbali zinazoendana na taaluma yako utazidi kuwa mbobevu katika taaluma husika.

Tujiulize wote kwa nini ufanye kazi kulingana na taaluma yako? Jibu ni moja tu kwa upande wangu, naamini kabisa uliisoma kwa kuipenda ili baadaye uitumie kutatua changamoto mbalimbali ndani ya jamii na kwa taaluma hiyo uweze kuyakimu maisha yako, na kama taaluma yako mpaka sasa unaona haijakusaidia ujue umepoteza uelekeo na Taifa nalo linakosa mtu muhimu lililomuandaa kwa ajili ya kulisaidia Taifa katika taaluma husika.

Ukiuliza kwa nini vijana wengi hawazitumii taaluma zao wengi watakujibu ni ukosefu wa mtaji, na wengi wao wanategemea ajira tu kutoka Serikalini, Mashirika yasiyo ya kiserikali au Makampuni binafsi lakini ni kweli mtaji ndio changamoto?

Kabla haujajibu hilo swali tutafakari yafuatayo, kuna wimbo uliimbwa na Banza Stone "Mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe" kwenye kufanya kazi pia kulingana na taaluma yako kunahtaji kujitoa na wakati mwingine unaweza kutumia nguvu zako kwa kufanya shughuli mbalimbali ili kuweza kupata kidogo kinachoendana na taaluma yako ili uweze kuiendeleza taaluma uliyonayo.

Huwa nasikitishwa sana na vijana ambao wanataaluma mbalimbali lakini baada ya kumaliza vyuo hawajawahi kuzitumia taaluma zao kwa jambo lolote, huwa nawaona kama watu wanaofedhehesha taaluma zao lakini pia wanaofedhehesha hata vyuo vilivyowanoa na kuwatunuku taaluma hizo kwamba wamekidhi kutunukiwa, kama kweli ulistahilishwa na chuo na kukutunuku kwa heshima ni lazima na wewe uitendee haki taaluma yako.

Kwa mfano unakuta mtu kasomea masuala ya kilimo ila kijijini alipo hana hata bustani unadhani hiyo taaluma anaitendea haki?, Mtu kasomea TEHAMA lakini unamkuta hajishughulishi nayo, Mwingine kasomea Sheria hata hawezi kutoa ushauri wa kisheria ndani ya jamii na yuko busy na kilimo ambacho hajakisomea na kimegoma kumtoa, ni kwa uchache tu ila mifano ni mingi.

Ndugu zangu, naamini wengi humu tuna taaluma mbalimbali tuzitumie kufikia malengo yetu kama tulivyoamua kuzihangaikia vyuoni, kwa kufanya hivyo tutafanikiwa kufikia malengo yetu kwa sababu tutafanya shughuli mbambali kwa weledi na ufanisi mkubwa.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom