LGE2024 Kuwe na utaratibu wa kutoka kazini mapema kipindi cha kampeni za uchaguzi ili tukasikilize sera. Au kama vipi mtuletee wagombea wajinadi maofisini

LGE2024 Kuwe na utaratibu wa kutoka kazini mapema kipindi cha kampeni za uchaguzi ili tukasikilize sera. Au kama vipi mtuletee wagombea wajinadi maofisini

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024

Don Gorgon

Member
Joined
Nov 21, 2024
Posts
35
Reaction score
68
Nimekaa, nikawaza: kwa nini kusiwe na utaratibu kwamba wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu au Serikali za Mitaa, wafanyakazi wa umma na binafsi waruhusiwe kutoka kazini mapema ili wakasikilize sera za wagombea wa maeneo yao?

Wafanyabiashara walioko masokoni, madukani, na maeneo mengine yenye mikusanyiko mikubwa mara nyingi hupata fursa ya kusikiliza sera kwa sababu wanasiasa huwafuata kwenye maeneo yao ya kazi. Hii ni rahisi kwao kwa sababu biashara zao zipo mitaani, ambako wagombea hupendelea kufanya kampeni.

Lakini vipi kuhusu wafanyakazi wa maofisini (wale wa Nine-to-Five)? Wao mara nyingi hawapati nafasi ya kusikia sera za wagombea wao, na wanajikuta mwisho wa siku wakifanya maamuzi ya kupiga kura bila kuwa na taarifa za kutosha kuhusu mipango ya wagombea hao. Hili si jambo bora. Kupiga kura bila kuelewa sera na mipango ya mgombea kunamaanisha kufanya maamuzi yasiyo na msingi wa taarifa (uninformed decisions).

Ukiangalia, kampeni nyingi zinafanyika mchana au jioni, wakati ambao waajiriwa wanakuwa kazini wakikamilisha matarajio ya waajiri wao na kukanda unga wa mkate wa familia zao. Hali hii inakuwa changamoto zaidi kwa wakazi wa miji mikubwa kama Dar es Salaam, ambako changamoto ya foleni huwafanya wafike nyumbani usiku, wakikosa kabisa nafasi ya kusikia hata tu muhtasari wa kampeni za siku hiyo.

Kwa wale wenye muda na mawazo ya kuuliza, wanaweza kupata mawili au matatu kutoka kwa waliohudhuria kampeni. Lakini vipi kuhusu mfanyakazi aliye na utayari wa kupiga kura lakini hajasikia wala kuweza kuhoji sera za mgombea wa eneo lake? Je, maamuzi yake yanapaswa kuongozwa na nini — mapenzi ya chama, rangi za chama na kelele za wafuasi, au ushabiki usio na taarifa za msingi?

Ni kweli kuwa serikali na wadau wengine wamekuwa wakiwahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura. Lakini wananchi watapigaje kura zenye maana kama hawajui wanapiga kura kwa misingi gani?

Kwa hili, niombe kuwe na utaratibu maalumu wa kuhakikisha waajiriwa wa sekta ya umma na binafsi wanapata fursa ya kusikiliza sera za wagombea. Kwa mfano, wafanyakazi wa maofisini wapewe siku kadhaa za kutoka kazini mapema, angalau saa 7 au 8 mchana badala ya saa 11 jioni. Hii itawapa nafasi ya kwenda maeneo yao kusikiliza kampeni na kufanya maamuzi yenye taarifa za kutosha.

Iwapo utaratibu huu hauwezekani, basi hatua nyingine inaweza kuwa ni kuandaa mikutano ya wagombea katika maeneo ya ofisi. Kwa mfano, ikiwa ofisi ina wafanyakazi kutoka mitaa 20 tofauti, wagombea wa maeneo hayo, kutoka vyama vyote, waalikwe kufika kazini na kuwasilisha sera zao mbele ya wafanyakazi wakiwa na vipaza sauti vyao. Keyboards zikiendelea kubinywa na ripoti kucharazwa, wagombea wateme sera. Naona hiyo ni njia bora ya kuhakikisha kila mfanyakazi "ameelewa" sera za kila mgombea, au siyo? 😉

Nihitimishe bandiko langu kwa kusema tu kuwa, ni muhimu kwa wananchi kuwa na taarifa sahihi kuhusu wagombea wao ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi. Uchaguzi si tu kuhusu kupiga kura siku moja; ni kuhusu kufanya maamuzi yaliyojengwa kwenye uelewa wa changamoto na mipango ya kuyatatua.

Kwa niaba ya waajiriwa sugu, naomba hili liangaliwe kwa uzito unaostahili.

Nawasilisha.

PIA SOMA
- LGE2024 - Nimeshuhudia kampeni za vyama tofauti hapa Dar es Salaam, sioni sera za Wagombea zaidi ya kupigana vijembe
 
Back
Top Bottom