WATU wanne wanashikiliwa Polisi mkoani Singida kwa tuhuma za kuvamia kituo cha kupigia kura na kupora sanduku la kura za maoni kwa wanachama wa CCM na kuzichoma moto kabla hazijahesabiwa .
Uvamizi huo ulifanyika juzi kwenye Kijiji cha Iglansoni katika jimbo jipya la Singida Magharibi na kusababisha matokeo ya kura za maoni kutotolewa mpaka jana mchana.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Celina Kaluba uvamizi huo ulifanyika Agosti mosi mwaka huu majira ya saa 12:30 jioni.
Kaluba aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Shambuli Shija (44), Manyanda Lazima (46), Clement Richard (36) na George Petro (38) wote wakazi wa Kijiji hicho cha Iglansoni katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Alisema siku ya uvamizi, baada ya kumalizika kwa upigaji kura za maoni kwa wana-CCM, watuhumiwa hao walipora sanduku la kura kabla ya kuhesabiwa na kisha kuchoma moto.
Kaluba alisema ingawa haijafahamika rasmi sababu za kufanya hivyo, lakini inadhaniwa kuwa huenda walifikia uamuazi huo ili kuharibu matokeo baada ya kuona dalili za kushindwa kwa mgombea waliyekuwa wakimuunga mkono.
Kutokana na hali hiyo alisema wanaendelea kuwashikilia watu hao kwa ajili ya uchunguzi zaidi kabla ya kupandishwa kizimbani.