mashikolo mageni
Member
- Aug 26, 2017
- 28
- 14
KWA NINI SI VYEMA KUANZIA DUKA LA DAWA (PHARMACY) PINDI UNAPOUGUA
Neno Pharmacy linaelezwa katika kamusi ya mtandaoni ya Merriam Webster likiwa na maana mbili (tafsiri imefanywa na mimi mwenyewe): 1. Ujuzi ama fani ya kuandaa, kutunza, kuweka pamoja na kutoa madawa. 2. Mahali ambapo madawa yanawekwa pamoja ama kutolewa. Katika Makala hii nitarejea maana ya pili ambayo kwa Kiswahili nitaitaja kama Duka la Dawa.
Imekuwa ni kawaida miongoni mwetu tunapohitaji huduma ya afya kuanzia kwenye maduka ya dawa ili kupatiwa huduma tunayohitaji. Baada ya kuhisi tunaumwa ama tunataka kujikinga na kuumwa huenda kwenye maduka ya dawa na kuwaeleza wataalamu wa dawa wanaopatikana katika maduka haya na kisha wao kutupatia huduma. Wengine miongoni mwetu hujiridhisha kabisa kuwa wanaumwa ugonjwa Fulani na kwenda duka la dawa na kununua dawa wanayojua inatibu walichonacho.
Zipo sababu nyingi zinazopelekea watu kufikia maamuzi haya. Baadhi ya sababu hizi ni kama vile: kuepuka gharama; kuepuka kupoteza muda; kutokuridhika na utoaji huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za afya; kuepuka adha ya msongamano kwenye vituo vya kutolea huduma za afya; kutokuwa na uelewa wa jinsi mifumo ya kutolea huduma za afya inavyofanya kazi; na nyinginezo.
Huenda maamuzi haya yamewahi kukusaidia wewe ama mtu unayemfahamu pindi ulipougua/alipougua, lakini pia maamuzi haya yana madhara yake makubwa zaidi ya faida yalizo nazo. Kwenye maduka ya dawa hukaa watu ambao wana ujuzi hasa juu ya madawa na ni kweli kuwa wanayajua madawa kuliko wataalam wengine wa afya. Lakini katika mafunzo yao, wataalamu hawa hawakuzama sana katika kuyatambua magonjwa kwa kusikiliza dalili, kuona na kugusa mwili wa mgonjwa, kuomba vipimo vya kuthibitisha magonjwa wanayohisi yanamsumbua mteja wao, kuyatibu, kuwafatilia wagonjwa na kutoa ushauri juu ya ugonjwa husika.
Mbali na hayo, eneo ambalo mgonjwa anasikilizwa na mtaalamu wa duka la dawa huwa si lenye mazingira rafiki katika kuweza kutambua ugonjwa unaomsumbua. Ni eneo la duka ambapo mtu yeyote anaingia wakati wowote; ni eneo ambalo mtaalamu kuna vitu hawezi kufanya, kwa mfano hawezi mwambia mwanamke anayelalamika kuwa anahisi kivimbe kwenye titi kutoa titi nje aone; ni eneo ambalo huwezi kumchunguza mwanamke anayelalamika kutokwa damu ukeni hata wakati hayupo siku za hedhi; ni eneo ambalo huwezi kumchunguza mwanaume anayelalamika kuwa na shida ya kukojoa; yapo mengi sana ambayo hayawezi kufanyika kutokana na mazingira ya duka.
Ukiachilia mbali kutokuwa na mazingira rafiki ya kuweza kuutambua ugonjwa, wataalamu waliomo kwenye maduka ya dawa pia hawana ujuzi wa kuyatambua magonjwa kwa kuangalia, kugusa na kusikiliza aidha kwa kutumia milango yetu ya fahamu ama kwa kusaidiwa na vifaa vidogo vidogo kama vile stethoscope ( ile ambayo daktari hukuwekea kifuani kusikiliza mapafu na moyo), nyundo ya goti na kadhalika. Hata madaktari wanaoyafahamu haya vizuri huwachukua miaka mingi sana kusema kuwa wameyabobea kiuhakika. Pia ni eneo ambalo sio kila atakaehudhuria basi atapimwa uzito, urefu na shinikizo la damu ili kuweza kupata ushauri wa kujikinga na magonjwa nyemelezi yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo kubwa la damu na baadhi ya saratani kwani magonjwa haya huja bila dalili na yanazuilika.
Hapa najaribu kukuoneha jinsi kulivyo na uwezekano mkubwa wa ugonjwa ulionao kushindwa kugundulika mapema kama utaanzia kwenye duka la dawa kwa ajili ya kupatiwa huduma. Binafsi nimeshakutana na magonjwa ambayo yalimuanza mgonjwa taratibu ila kutokana na kutokutana na watu sahihi yakaja kugundulika baadae sana na kipindi ambacho hakuna cha kufaanya kwa kiasi kikubwa. Nimewahi kukutana na wagonjwa wenye saratani za tumbo ambao wametibiwa kama wagonjwa wa madonda ya tumbo kwa miaka mingi; nimekutana na wagonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ambao wametibiwa kama wagonjwa wenye shida ya mzunguko wa hedhi kwa miaka mpaka ugonjwa unafikia pabaya kabisa; list ni ndefu sana.
Mtu sahihi wa kuanza naye pindi unapojisikia kuumwa ni Daktari/Daktari msaidizi/Tabibu akuone kwenye kituo cha kutolea huduma ya afya kama vile zahanati(dispensary), kituo cha afya( health centre), hospitali ama kliniki ya daktari bingwa. Huyu amejikita Zaidi katika kuweza kuyatambua magonjwa kwa kumsikiliza mgonjwa, kuangalia na kuugusa mwili wa mgonjwa; huyu huagiza kipimo ambacho kitathibitisha ugonjwa husika (kama unahitaji kipimo) na baada ya kujiridhisha kuwa mteja wake anasumbuliwa na ugonjwa Fulani basi huanzisha matibabu kwa miongozo iliyowekwa na wizara ya afya ama na madaktari wengine duniani. Haishii hapo bali humfuatilia mgonjwa katika siku zinazofuata kuona anaendeleaje na kufanya maamuzi kutokana na mgonjwa alivyo, anaweza kumpa rufaa aende katika ngazi inayofuata ama kufanya kipimo cha kuona kama ugonjwa umeisha. Mbali na hayo, huyu aweza kuyatambua mambo ambayo si mazuri kwa afya ya mteja wake japo siyo yaliyompeleka kituoni hapo, kwa mfano kwa kuangalia shinikizo la damu la mteja wake anaweza kushauri njia za kubadili mtindo wa maisha zitakazoshusha shinikizo hilo na kuzuia asiingie kwenye ugonjwa wa shinikizo kubwa la damu.
Tunafahamu kuna msongamano mkubwa wa watu kwenye vituo vya serikali ambako huduma ni za bei nafuu, ni wakati sasa watu binafsi wanaomiliki vituo vya kutolea huduma za afya nao wakaweka bei ambazo watanzania wengi wataweza kumudu ili kuwahimiza kuhuzuria kwenye vituo hivi na si kwenda kuanzia kwenye maduka ya dawa. Pia uwekezaji kwenye sekta ya afya bado upo kwa kiwango cha chini hasa katika miji midogo na vijijini, ni wakati sasa watu binafsi wenye uwezo wakaangalia fursa hizi kwenye maeneo haya. Wanaouza madawa pia wanapaswa kuwa na utu na si tu kuangalia pesa wanayopata, pindi waonapo mgonjwa ana shida wasiishie tu kumuuzia dawa bali wamuelekeze akaonane na daktari kwanza. Na mwisho niwakumbushe tu watanzania wenzangu afya yako ni miongoni mwa mambo ya muhimu kabisa katika maisha yako, hata maendeleo ya sehemu hupimwa kwa kuangalia upatikanaji wa huduma za afya kama kigezo kimojawapo.
Dr. Joseph J. Masalu, M.D