Kwa Nini Tanzania tunahitaji Kuwa na Serikali Tatu

Damaso

JF-Expert Member
Joined
Jul 18, 2018
Posts
3,978
Reaction score
6,739
Tanzania ni nchi yenye historia ndefu na utajiri wa tamaduni mbalimbali, zinazochangia umoja wa taifa. Hata hivyo, kuna hoja inayozidi kujitokeza kuhusu ufanisi wa mfumo wa utawala wa sasa wa nchi, hasa kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.


Ni suala la wazi kuwa Muungano huu umeleta umoja na maendeleo makubwa, lakini umekuwa na changamoto ambazo zinahitaji kuzingatiwa kwa makini. Katika muktadha huu, wazo la kuwa na serikali tatu linaweza kuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania, kwa sababu itatoa fursa ya kuimarisha utawala wa ndani na kukuza maendeleo katika kila sehemu ya nchi.

Katika makala hii, nitajadili sababu tatu muhimu kwa nini Tanzania inahitaji kuwa na serikali tatu.

Kila sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yaani Tanganyika na Zanzibar, ina historia ya changamoto na fursa za kipekee zinazohitaji usimamizi maalum na mikakati ya maendeleo inayoendana na mazingira yake. Sidhani kama ni afya kuona Mmaasai akizungumzia maisha na historia ya Mpemba na kukosoa maisha ya Wapemba.


Tanganyika, ambayo ni eneo kubwa la kijiografia na lenye idadi kubwa sana ya watu, inahitaji utawala ambao utaweza kuzingatia masuala yake ya kiuchumi, kijamii, na kisiasa kwa ukamilifu kuendana na idadi ya watu husika.


Hali kadhalika, Zanzibar, licha ya kuwa ni kisiwa kidogo, ina historia yake ya kipekee, na changamoto maalum zinazohitaji utawala na sera zinazozingatia mahitaji yake na wakazi wake wanaopatikana ndani ya Zanzibar.


Kwa kuwa na serikali tatu, kila upande utakuwa na Waziri Mkuu wake atakayekuwa na jukumu la kusimamia maendeleo katika eneo lake husika.


Hii itasaidia kupunguza mzigo wa usimamizi wa kisiasa na kiuchumi ambao kwa sasa unashirikiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na badala yake kila sehemu itakuwa na uwezo wa kuamua na kusimamia rasilimali zake kwa ufanisi zaidi.


Hii ni muhimu kwa kukuza uchumi, kupunguza umaskini, na kuhakikisha kuwa kila sehemu inapata fursa za maendeleo zinazohitajika kwa haraka kulingana na mapato husika ya eneo hilo.


Kila nchi itakuwa na mamlaka binafsi ya kujiendeleza bila kutumia mfuko wa sehemu nyingine, kodi za Biharamulo zitaendeleza Biharamulo na sio Pemba. Vivyo hivyo Ajira ambazo zitatoka kwa ajili ya vituo vya Afya vya Mjini Magharibi zikawanufaishe Wazanzibari.


Moja ya masuala ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara katika historia ya Muungano wa Tanzania ni tofauti za kijamii, kiutamaduni, na kisiasa kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Wakati Tanganyika ina historia ya kipekee sana, na ina utamaduni na mila zake ambazo ni tofauti na za Zanzibar, hali hiyo mara nyingine imesababisha migogoro ya kisiasa na malalamiko ya kutoelewana kuhusu ushirikiano katika muungano huu. Utamaduni na desturi za Mkurya ni tofauti sana na Mshiraz, Utamaduni na mila za Msafwa ni tofauti sana na Mpemba.

Mfano mzuri kabsa ni sherehe za Siku ya Uhuru wa Tanganyika kwa sasa zinaelekea kupotea kabsa, na zimebatizwa jina jipya, SIKU YA UHURU WA TANZANIA BARA, watu wanaogopa kusema SIKU YA UHURU WA TANGANYIKA ilihali watu hao hawawezi kusema SIKU YA MAPINDUZI YA TANZANIA VISIWANI bali watasema SIKU YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR. Tunapaswa kuvifundisha historia kamilifu vizazi vyetu bila kupepesa macho wala kuficha ukweli.


Kwa kuwa na serikali tatu, kila upande utaweza kulinda na kuendeleza utamaduni na mila zake bila kuathiri utamaduni wa pande nyingine. Serikali ya Zanzibar itakuwa na uwezo wa kuhakikisha kuwa tamaduni na lugha ya Kiswahili pamoja na mila na desturi za Wazanzibari zinahifadhiwa na kuendelezwa. Hali kadhalika, serikali ya Tanganyika itakuwa na nafasi ya kutatua changamoto za kijamii na za maendeleo zinazohusiana watanganyika.

Pia, kuwa na serikali tatu kutatoa nafasi ya kutoa haki na usawa kwa wananchi wa pande zote mbili. Kwa sasa, baadhi ya wananchi wa Zanzibar wanahisi kuwa hawana uwakilishi wa kutosha katika muungano, hali inayosababisha kutokuelewana na migogoro.


Huku pia baadhi ya watanganyika kukosa haki ya umiliki wa ardhi ndani ya Zanzibar, ilihali wazanzibari wana haki zote za kupata ardhi ndani ya Tanganyika. Kwa kuwa na serikali tatu, kila upande utaweza kushiriki kikamilifu katika utawala wa nchi na hivyo kuboresha hali ya kisiasa.

Serikali tatu zitaleta ufanisi mkubwa katika usimamizi wa rasilimali na utawala bora. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa na jukumu la kusimamia masuala ya kitaifa ya Muungano, kama vile ulinzi, sera za nje, na masuala ya ushirikiano wa kimataifa.


Hali kadhalika, Waziri Mkuu wa Tanganyika atakuwa na jukumu la kusimamia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa upande wa Tanganyika, huku Waziri Mkuu wa Zanzibar akisimamia maendeleo ya kisiwa hicho kwa kutumia mapato ya Zanzibar.


Hii itasaidia kudhibiti utoaji wa huduma kwa wananchi kwa ufanisi zaidi. Serikali itakuwa na uwezo wa kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo inayohusiana na mazingira ya kila eneo, bila mzigo mkubwa wa kuhamasisha utekelezaji wa miradi katika maeneo mengine ya nchi. Hii itasaidia kupunguza urasimu na kuongeza uwazi katika utendaji wa serikali.

Aidha, kuwa na serikali tatu kutaleta ufanisi katika utawala wa ndani. Serikali ya kila eneo itakuwa na uwezo wa kuchukua hatua haraka katika kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika maeneo yake bila kutegemea maamuzi ya utawala kuu wa muungano. Hii itasaidia kuleta maendeleo haraka na kupunguza urasimu katika utendaji wa serikali.


Ni wakati muafaka kwa Tanzania kuangalia kwa makini mfumo wa utawala wa sasa na kuzingatia wazo la kuwa na serikali tatu kama njia ya kuleta maendeleo endelevu na umoja wa kweli. Ni wakati ambapo nafasi ya Saleh Juma Mussa kama Katibu Mkuu Kiongozi anaweza kuwa Waziri Mkuu wa Zanzibar na upande wa Tanganyika kukawa na Kassim Majaliwa kama Waziri Mkuu wa Tanganyika.

MUNGU IBARIKI AFRIKA! MUNGU IBARIKI TANZANIA.
 
Wewe binafsi na familia yako hio serikali tatu itakusaidia nini?
 
Kuwe na serikali mbili ,kila nchi na mambo yake sema kusiwe na visa kuingia pande mbili hizi.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…