Ni mwaka mzuri na mwema wa kihistoria kwa Tanzania kupata uongozi kwa ngazi ya madiwani, wabunge na Rais. Watanzania wote haya shime shime tuweke historia yetu kwa ulimwengu kuwa Awamu ya Tano ya uongozi inaingia madarakani kwa amani. Hilo linawezekana na ni dhahiri kwani Tanzania ni nchi yenye kufuata utawala wa sheria uliojengwa kwenye Katiba ya nchi ya 1977 na sasa Tanzania ipo kwenye mchakato wa kupata Katiba Mpya ambapo sasa Katiba Inayopendekezwa ipo kwa wananchi kwa ajli ya kusomwa ili muda muafaka wa kuipigia kura ukifika wananchi waweze kuipigia kura. Wakati ukifika wote wenye sifa tushiriki kupiga kura ili kupata Katiba yenye namna bora ya kuendelea kupata viongozi wetu kwa haki na amani nchini.