Kwa tuliowahi kupotea ama kupotezana na watu wa karibu

Socw

JF-Expert Member
Joined
Aug 27, 2016
Posts
1,329
Reaction score
2,644
Habarini wakuu….

Nasikia mkuu wa kaya ameteua baraza jipya la mawaziri. Wacha tu waendelee kuchaguana ili wakaze vyuma ila ni poa tu hakuna noma.

Niende kwenye mada yangu ya msingi…

Leo nataka tushirikishane matukio yaliyotupata pale tulipopotea ama kupotezana na ndugu zetu katika maeneo mbalimbali.

Nikianza mimi

Nakumbuka nilikuwa na miaka 11 nikisoma darasa la sita, baba yangu mzazi aliniambia kuwa siku iliyokuwa inafuata tungeenda mjini. Yeye alikuwa na mwalimu wa shule wa msingi na ilikuwa anaenda mjini kwa kuwa alikuwa ni msimamizi wa mirathi ya bibi yangu. Hivyo kwa kuwa aliona kijana wake nimekaa sana kijijini aliona sio mbaya kama tungeenda wote kusafisha macho.

Siku ikawadia tukaamsha kwenda mjini dodoma.

Tukafika pale mahakama ya mkoa na wao wakaitwa kuingia ndani ya chumba kimojaa hivi na mimi nikaachwa nje na wakaniambia kuwa niwasubiri pale nje hadi watakapotoka. Muda huo mfukoni nina pakiti mbili za karanga za kukaanga na gazeti la sani nikisoma katuni na udaku mwingine.

Kwa wakazi wa Dodoma nadhani watakuwa wanaufahamu ule mnara wa saa ulioko katika kanisa katoliki amboa ulikuwa unalia kila baada ya kutima saa kamili, kwa sasa umeshaachaga sijui nao unaringa siku hizi au nao unapitia kipindi hiki kigumu cha awamu ya tano kwamba vyuma vimekaza hadi unashindwa kutekeleza majukumu yake. Anyway, nisiusimange sana mnara wa watu. Sasa nikiwa pale nikausikia kwa mara ya kwanza, saa nane hiyo.. nikapuuza. Nikaendelea kusoma gazeti. Ukasikika kwa mara ya pili, saa tisa hiyo.. nikastuka na nikaanza kuingiwa na wasiwasi. Lakini nikajikaza. Nilisoma kila kitu kwenye lile gazeti hadi matangazo ya kuongeza nguvu za kiume na makalio sijui handsome up sijui manalisa belt na takataka zoote.. lakini wapi.. mshua na bibi hawatoki tu. Nilianza kurudia tena kusoma yale makatuni ya kipepe na lodolofa upya ili kuvuta kasi ya muda. Mara paaaaap kengele ya tatu, saa kumi hiyoo. Nikasema mmmh, hapa kuna kitu. Masaa matatu wanaongea tu? Wanaongea nini? Kijana nikaamuka na kuanza kuzunguka ile eneo la mahakama huku nikiwa nimejawa na huzuni kwa kutowaona watu wangu vipenzi.

Nilizunguka sana eneo lile lakini sikupata kuwaona popote. Niliishia kuwaona watu wengine wakiendelea kufanya yao bila kinijali kwa maana hata mwonekano wangu ulikuwa wa kishamba..shati la kitenge na suruali…na mimi nilikuwa jeuri kinyama, sikutaka kuomba msaada wala kuuliza. Nilipanga kulimaliza soo kimya kimya kama don yen. akili ikanijia kuwa huenda walimaliza maongezi yao na kuondoka kurudi kijijini na kunisahau mimi mjini. Roho ya hasira ikawaka juu ya baba yangu na kuwaza ni kwa nini aniache. Lakini nikasema siwezi kuwa mjinga, ni lazima niende ziliko stendi za magari ya kweda kijijini ketu kabla hayajaondoka ili niwawahi. Na kwa muda kwa wakati huo gari lilikuwa ni moja tu ukilikosa ndo basi tena na mimi mwenyewe siyo mtaalam wa mji maana nilikuwa sisafiri sana mjini. Gari lenyewe sasa, ni canter (sina uhakika kama ndo inaandikwa hivi), au niseme ni mtoto wa fuso. Magari haya yalikuwa yanamilikiwa na waarabu wale akina musa. Yaani mnakaa humo humo mizigo na watu. Yaani unakaa juu ya mfuko wa maembe, mguu umeweka juu ya mfuko wa dagaa na mkono unauegesha kwenye mfuko wa sementi huku ukiwa umeegama kwenye tenga la nyanya. Mvua ikinyesha unalowa saafiiii.

Nikala karanga zote kwanza, kisha nikalikunja gazeti na kulitia mfukoni na nikaanza safari ya kwenda stendi. Nashukuru neema ya mungu iliniongoza hadi nikafika mahali zilipo stand za gari la kwetu japo kwa kubahatisha sana. Nadhani nilifanikiwa kwa sababu Dodoma ni kamji kadogo sana, unaweza kukakato koote kwa mguu. Lakini kitu cha kuhuzunisha ni kuwa sikulikuta gari. Yaani lile canter la kwenda kwetu lilikuwa lishasepa yaani..daah niliumiavibaya.

Licha ya hayo sikutaka kukata tamaa. Kama komamdo vile nikasema ni lazima nifike nyumbani kwa namna yoyote ile. Na namna niliyoichagua ni kutembea kwa mguu hadi kijijini kwetu. Na ikumbukwe kuwa kutoka Dodoma mjini hadi kijijini kwetu unapita vijiji vine ambavyo ni nala, chigongwe, msembeta ibihwa then unaiacha ile babarabara ya kwenda singida na kukunja kulia na kuelekea kijijini kwetu mnkola. Na muda huo ilikuwa imeshatimu saa 11. Safari ikaanza. Nikaanza kukimbia pembeni yay a ile barabara ya Dodoma-singida.

Tatizo jipya likazuka, tumbo la kuhara. Zile karanga za kukaanga nilizokuwa nazitafuna zikaanza kuniletea shida. Tumbo la kuhara lilinibana kweli na kwa muda huo nilikuwa bado niko town. Nikakaza mwendo huku nikibinya breki zote mzigo usishuke. Nikakimbia kwa kasi kama bombadia. Daah, nimekumbuka, hivi bambasia yetu imesharudi au bado? Anyway, nilitoka nduki hadi nikaanza kuuacha mji wa Dodoma na kukikaribia kipori flani pale mitaa ta mnadani. Nikaenda nikashusha mzogo. Amani tele, safari ikaendelea na muda huo kiza kilikuwa kishaanza kutanda. Na mimi nilijiapiza kutembea hata kama ni usiku wa manane ilimradi tu nifike nyumbani. Dadeq, nilikuwa kauzu zaidi ya anodi shozniga

Nikaenda na kuenda ikafika mahali kiu ikanibana. Nikaona isiwe shida. Nikasogea kwa nyumba moja ya wanakijiji nikaomba maji, wakanipa ila sura ilikuwa inaonyesha kuwa sikuwa sawa. Wakaniuliza mtoto kwani kuna nini mbona uko hivyo. Ohooooo, ikawa kama waliniambia “lia kijana, lia kwa nguvu zako zote” maana kilio nilichokishusha pale hakikuwa na uraia wa Tanzania. U doniyeni na ushozniga wote kwishaa. Wakaanza kunibembeleza na kunisihi niseme. Nami nikawaeleza yoote huku kilio juu. Wakaendelea kunializa ‘kwenu wapi’ nani nikawajibu mnkola, ‘sasa jioni hii unaenda wapi?‘nikawaambia hukohuko. Wapigwa na butwaa kuu. Kutoka pale nala hadi mnkola kwa mguu unaweza chukua siku moja na masaa kadhaa kutembea. Nikaulizwa namba za simu za mzazi wangu au mtu yoyote ninayemfahamu…..waaaapi, sijui namba hata moja.

Basi wakashauriana nipelekwe kwa mkuu wa mtaa ili nikalale huko kwanza huku tararibu za kunifikisha nyumbani ziendelee hiyo kesho. Baiskeli ikaitishwa, nikapakiwa hadi kwa mkuu wa mtaa, nakumbuka alikuwa ni mwanamke. Nikalala nikaamka. Nikapelekwa mahali nikapata chai na maandazi yale yenye kitobo katikati, nikashiba haswa. Then, nikapelekwa kwa maaskari barabarani wa pale nala nikaombewa lifti kwa gari kubwa la mizigo. Yule dereva alikuwa na mwanamke flani hivi, sasa nilipoingia Yule dame akaanza kusema eti nimeingia na nzi. Daah, nikamcheki kwa jicho kali sana…nadhani alijiuliza “huyu dogo jasisi nini! Mbona ana macho mabaya hivi?” safari ikaisha, nikashushwa ibihwa na kisha mzee nikatembea kwa mguu kutoka ibihwa hadi mnkola.. mwendo wa masaa matatu kwa miguu. Tena nakumbuka siku hiyo ilikuwa ni siku ya mnada huko kijijini kwetu.

Nikafika zangu nyumbani, kumepoa sio kawaida. Wadogo zangu wamelia hadi wamechoka baada ya kupokea taarifa kuwa kaka yao kipenzi kapotea. Hata Yule mdogo wangu wa kike aliyekuwa ananifuata ambaye kila siki tulikuwa tunadunndana na kesi zilikuwa haziishi kati yangu na yeye naye alikuwa na huzuni. Macho yake yalikuwa mekundu kama kakamuliwa tomato sosi. Kweli nikajua damu ni nzito kuliko maji. Mama yangu naye alikuwa na huzuni kuu, pia nilimkuta na bibi yangu upande wa baba pia. Na kwa kipindi hicho mama yangu alikuwa hana simu kwa hiyo ilibidi kwenda kwa mwalimu Fulani jirani yetu kuazima simu ili ampigia baba kuwa kijana wao nimerudi. Ila kwa bahati mbaya sana mwalimu huyo hakuwapo, nadhani alikuwa mnadani..

Basi nikafika nyumbani nikawahadithia ilivyokuwa. Kumbe huko mjini hali ilikuwa si shwari. Muda wakati mimi nahangaika kuwatafuta wao walikuwa ndani tu kwenye maongezi. Kutoka mtoto haonekani…tafuta koooooote waaaap…wakatoa matangazo kituo cha polisi. Na kesho yake taarifa zikapelekwa radio mwangaza. Sasa cha kuchekesha zaidi ni kuwa, wakati radio mwangaza fm 90.8 sauti ya amani na upendo wanatoa tangazo la mimi kupotea, nilikuwa tayari nimeshafika nyumbani na nililisikia nikiwa nyumbani. Muda si mrefu baada ya tangazo kutoka, niliona marafifki zangu na ndugu na jamaa wakija nyumbani kutaka kujua ni nini kimetokea hadi nikapotea kiasi cha kutangazwa redioni. Wananikuta nimelala zangu kwenye mkeka.

Muda kidogo mida ya saa moja hivi, mara mshua huyu hapa….

Je, wewe umewahi kupotea ama kupotezana na watu wako wa kaeibu, ilikuwaje?
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…