Kwa wanamaendeleo

Kwa wanamaendeleo

Bavaria

JF-Expert Member
Joined
Jun 14, 2011
Posts
53,092
Reaction score
53,496
[h=5]Miaka 10 au zaidi nyuma, pale mtaani kwetu Fundikira, Magomeni Makuti jijini Dar es Salaam, ninapoishi alihamia jamaa mmoja akiitwa Kimaro akitokea Moshi, mkoani Kilimanjaro. Wakati anahamia mtaani, Kimaro alikuwa ndio kwanza ameingia mjini kutafuta maisha.
Nyumba aliyoishi Kimaro inatazama na nyumba yetu. Katika nyumba hiyo, Kimaro alikodi chumba kidogo ambacho ni sehemu ya genge la biashara aliloendesha mbele ya nyumba hiyo isiyokuwa na umeme wala maji.
Katika genge hilo alilokuwa akiliendesha huku usiku likigeuka kuwa makazi yake, Kimaro aliuza nyanya, vitunguu, mboga za majani. Kimaro, alitokea kuwa rafiki yangu mkubwa, kwa sababu wote tulipenda kujadili siasa wakati ule Augustine Lyatonga Mrema akiwa kinara wa upinzani nchini Tanzania.
Kwa jinsi nilivyomjua, Kimaro aliishi maisha ya kujibana sana. Baada ya muda, Kimaro, ambaye alifanya kazi siku saba zote za wiki bila mapumziko, akafungua duka dogo pale pale huku akiendelea pia na genge. Siku pekee Kimaro alipumzika ni msimu wa Krismasi.
Punde nilisafiri kwa ajili ya masomo kwa miaka kadhaa na kumuacha Kimaro akiendelea na biashara yake. Lakini niliporudi miaka miwili mbele, Kimaro alishahama Makuti.
Majirani wakaniambia Kimaro sasa ni tajiri jambo ambalo nililithibitisha siku moja nilipokutana naye akitembelea moja kati ya maduka yake mengi. Kwa sasa yeye hakai tena dukani, ameajiri watu.
Kuna simulizi nyingi kuhusu matajiri mbalimbali maarufu wa Tanzania walioanza na biashara ndogo kama Kimaro na sasa ni matajiri wakubwa.
Na hapa sizungumzii wale jamaa zangu wauza dawa za kulevya na nyara za serikali ambao utajiri wao haukufuata njia za asili. Najua wapo, lakini pia najua pia wapo waliopata utajiri wa halali kwa bidii zao za kazi.
Bilionea Mswedish Ingvar Kamprad ambaye jarida moja la biashara Veckans Affarer liliwahi kuripoti mwaka 2004 kwamba yeye ndiye tajiri namba moja duniani akimpiku Bill Gates, ni mfano hai miongoni mwa matajiri wanaotingisha ulimwengu. Yeye alianza biashara akiwa kijana mdogo kwa kuuza vibiriti rejareja.
Nisikuchoshe kwa mifano kwani nina hakika hata wewe unawajua watu wawili watatu ambao ni matajiri lakini walianza biashara katika mazingira magumu, wakajinyima, wakahifadhi pesa, wakawekeza, mtaji ukakua na wakapata mafanikio.
Pale mtaani, wakati Kimaro anahangaika kulikuwa pia na watu wenye maisha mazuri. Lakini kwa kuwa Kimaro alijua wapi anataka kuelekea hakushawishika kuiga mtindo wa maisha wa watu ambao walikwishafanikiwa. Alijua umuhimu wa kutunza fedha na kuwekeza.
Kadhalika, pale pale mtaani tulikuwapo wenye hali kama ya Kimaro lakini tulioishi maisha ya kitajiri, huku wakati fulani hadi tukikopa kwenda sambamba na maisha tunayoyatamani lakini ambayo hatujayafikia.
Sisi hali zetu bado ziko vile vile. Kimaro, yule kijana mshamba wa kichaga wa enzi zile, ametuacha na anacheza ‘ligi’ kubwa. Tofauti ni kama La Liga na hii yetu, sijui nini vile Premier league.
Mfano nilioutaja hapo juu unaweza kuutumia katika kuelezea umaskini wa mataifa yetu ya ulimwengu wa tatu, mataifa ambayo tunaishi kama matajiri wakati ni masikini, ombaomba wa kutupwa.
Kama nchi, ili maendeleo yaweze kupatikana tunahitaji kuiga mambo mawili kutoka kwa Kimaro, uchapakazi na nidhamu ya matumizi ili kingi katika kile kinachopatikana kipelekwe katika sekta za kiuchumi na kijamii ambazo zitatujengea uwezo wa kuwekeza na kukua.
Ifikie wakati Watanzania tuuinue utamaduni wa kujituma na uchapakazi kutoka kuwa sifa ya raia mmoja mmoja, (kama Kimaro) na badala yake tuufanye uwe utamaduni wa taifa.
Tukizungumzia mataifa ambayo watu wake wanasifika kwa uchapakazi, mojawapo ni China. Uhodari wa utendaji kazi wa Wachina umethibitika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali mikubwa, ndani na nje ya nchi yao, kwa kasi ya ajabu, jambo ambalo limeifanya ipate mafanikio ya kiuchumi kwa muda mrefu.
Mwaka jana, taasisi ya utafiti ya Pew ilichunguza kuhusu mtazamo wa Wamarekani kuhusu Wachina. Kwa mujibu wa utafiti huo, Wamarekani waliowaelezea Wachina kama wachapakazi ni asilimia 93 huku kwa upande mwingine ni Wamarekani asilimia 78 ambao walijielezea wao kama wachapa kazi.
Hoja yangu hapa ni kwamba hata mataifa ya magharibi wanakiri uchapakazi wa Wachina, pamoja na hoja za ukosoaji zinazotolewa sambamba na sifa hizo.
Wageni wengi wanaotembelea China wanashangazwa na uchapakazi wa Wachina viwandani, mashambani, maofisini na katika taasisi za elimu. Ni kawaida kwa wachina kufanya kaiz hata siku za sikukuu kutokana na hamu ya mafanikio.
Katika kuelezea hali hii, mwandishi mmoja, Valerie Sartor katika makala iliyochapwa katika mtandao wa Beijing Review wazazi wa China humfundisha kijana kuwa uchapakazi ni uongofu (virtue) ambapo kwa nchi za magharibi uchapakazi ni hitaji (necessity) la kimaisha.
Katika falsafa hizi mbili, kwa kadiri ya ufahamu wangu mdogo wa historia yetu, kwa Afrika, uchapakazi ulikuwa ni uongofu mpaka pale tulipopotoka na kuingia katika usasa.
Kwa mujibu wa Sartor, sababu nyingine iliyopalilia uchapakazi China ni maadili ya taifa, ambayo uchapaji ni kipengle muhimu, yaliyojengwa na Serikali ya Kikomunist inayolenga kujenga China yenye nguvu na mafanikio ulimwenguni.
Ni wiki iliyopita kulikuwa na sikukuu siku tatu mfululizo kuanzia Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi na ilinishangaza kuambiwa kuwa Jumapili itakuwa siku ya kazi ili kufidia sikukuu.
Sasa, ambapo Tanzania, tunaandika Katiba Mpya, ni wakati muafaka wa kuingiza maadili ya taifa yanayopigiwa kelele na watu wengi, ikiwemo kipengle cha uchapakazi, ingawa hatua hiyo pekee inaweza isitoshe kujenga utamaduni wa uchapakazi.
Sambamba na katiba na sheria, serikali inatakiwa ichukue hatua kadhaa za kiuchumi, kisiasa na kijamii za kujenga mazingira mazuri ya uzalishaji na pia kuwawezesha watu kujiajiri na kuajiriwa.
Nilitaja vitu viwili vya kuiga kutoka kwa Kimaro. Kingine ni matumizi mazuri ya rasilimali. Sio siri kuwa katika hali yetu ya umaskini kuna matumizi ya anasa mengi ambayo tungeweza kuyaepuka na badala yake kutenga fedha katika sekta zitakazochochea uzalishaji kama vile kuboresha miundo mbinu na kuwekeza katika rasilimali watu.
Baadhi ya matumizi ya anasa katika nchi zetu ambayo vyama vya upinzani na taasisi za kiraia zimekuwa zikikosoa ni pamoja na ununuzi wa magari ya anasa, tafrija, ujumbe wa maafisa wengi unaosindikiza misafara ya viongozi wakuu katika safari hususan za nje, ukubwa wa serikali, takrima, na baadhi ya vipengle vya maandalizi ya sherehe mbalimbali.
Kama hatutarekebisha matumizi yetu na kuhifadhi na kupeleka rasilimali katika sekta zitakazochochea uwekezaji zaidi na ujenzi wa miundo mbinu ya kiuchumi, tutasikia tu harufu ya maendeleo.
Mimi ni mmoja kati ya watu wanaoamini ili kuvunja huu mzunguko wa umaskini (cycle of poverty), lazima tuanze kufikiria nje ya boksi. Kufikiria nje ya boksi ni pamoja na kuja na bajeti tofauti sio zile za ‘ku kopi na ku-pesti’ (copy and paste) kutoka katika ile ya mwaka jana na juzi. Kufikiri nje ya boksi ni kujiuliza maswali magumu, je tunahitaji kutenga fedha kwa ajili ya jambo hili na kwa nini?
Tumeanza? Kwa tathmini yangu kidooogo, ingawa bado kwa kiasi kikubwa tunafanya kama ambavyo namna mambo yamekuwa yakifanyika, namna ya kurudia kufanya kitu kile kile tukitegemea matokeo tofauti, namna ambayo imelifikisha Bara la Afrika hapa.[/h]
 
Asante kwa kutukumbusha maana ukiangalia maisha ya watanzania hata sie wafanyakazi matumizi, akiba na kuwekeza na msamiati mgumu. Kiasi fulani uwepo wa kazi za mikataba ndo umetuamsha wengi kuwa na malengo vinginevyo ni kukopa na kujenga nyumba ya kuishi vile tu nyumba serikali haipangishi tena baada ya hapo ni kula bata. Ukijaribu kuwekeza kwa ajili ya ustaafu unaonekana kituko sana mtaani maana watu ni kukopa na kubadili magari, harusi za gharama, shopping za nje nk. Tujitahidi jamani tunakoenda ardhi ndo inauzwa yote. Yale ya wazee ya 'akastaafu akarudi kijijini kulima' hakuna tena.
 
Back
Top Bottom