Polisi yalipua mabomu kutuliza upigaji fataki
na Sitta Tumma, Mwanza
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
JESHI la Polisi mkoani Mwanza, juzi usiku lililazimika kufyatua mabomu ya machozi kwa baadhi ya maeneo jijini hapa kwa ajili ya kuwatawanya watu waliokuwa wakisherehekea mwaka mpya 2009 kwa kupiga fataki na baruti.
Sanjari na hayo, jeshi hilo kupitia askari wake lililazimika pia kuwatia mbaroni baadhi ya vijana ambao walionekana kukaidi amri ya jeshi hilo ya kutokulipua baruti wakati wakisherehekea kuuaga na kuupokea mwaka mpya.
Katika kudhibiti hali hiyo juzi usiku, hususan maeneo ya Igoma, Kirumba, Kitangiri, Kilimahewa, Mabatini, Nyakato na maeneo mengine kadhaa ya jiji la Mwanza, askari polisi waliokuwa doria walipata wakati mgumu kutokana na wananchi kuendelea kulipua baruti hewani.
Juzi, jeshi hilo kupitia Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Khamis Bhai, ilitoa onyo dhidi ya watu wanaolipua fataki na baruti nyakati za usiku, na kusema ni marufuku kufanya vitendo hivyo.
Kauli hiyo ya polisi ilionekana kutotekelezwa vema na baadhi ya wakazi wa jiji hilo, kwani watu wengi vijana na wanawake walionekana kuzagaa na kutanda barabarani hususan maeneo ya Igoma hali ambayo iliwalazimu askari polisi hao kufyatua mabomu ya kutoa machozi.
Kizaazaa hicho kilichukuwa takriban saa mbili kutoka saa 6:00 usiku hadi saa 8 usiku, ambapo polisi walifanikiwa kutuliza hali kama hiyo ya ulipuaji wa fataki kabla ya watu waliokuwa wakihusika na ulipuaji huo wa baruti kuanza kukimbia kukwepa mabomu hayo ya machozi.
Ofisa mmoja wa polisi mkoani Mwanza aliyeshiriki katika doria hiyo, aliiambia Tanzania Daima kuwa walilazimika kufyatua mabomu hayo ili kudhibiti na kuleta utulivu kwa wananchi wa maeneo husika.
Imetubidi kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kuwadhibiti watu waliokuwa wakifyatua baruti
..pia tumefanya hivyo kwa kuleta utulivu na kuondoa hofu kwa wananchi waliokuwa majumbani, alisema.
Hata hivyo, Tanzania Daima ilishuhudia baadhi ya watu katika maeneo ya Mabatini, Igoma na Nyakato wakiwa wametanda barabarani wakishangilia kuupokea mwaka mpya huku wakiwa na matawi ya miti na wengine wakipiga madebe pasipo kujali onyo la Jeshi la Polisi lililotolewa na jeshi hilo mkoani hapa.