Ilikuwa jioni moja tulivu mwalimu Nyerere alipokutana na mwalimu kashasha (mchambuzi mahiri wa mpira wa miguu). hii ni mara ya tatu wanakutana tangu kuwasili kwa mwalimu kashasha kwenye jumba la milele la watu wote. wakati wanangojea zamu yao ya kucheza drafti ifike, walianza kutaniana huku wakifundishana kwa staili tofauti iliyojaa ustadi, hekima na heshima. safari hii kashasha alikuwa anatamani kusikia zaidi kutoka kwa nguli huyu wa siasa kama awamu ya mwisho walivyozungumza. mazungumzo yao yalikuwa kama ifuatavyo:
Nyerere: Kashasha mwanangu, nimefurahi kukuona. Habari yako?
Kashasha: Asante sana baba, habari zangu ni njema sana. Haswa ukizingatia kwamba vita tumevipiga mwendo tumeumaliza.
Nyerere: Kweli kabisa. Tumevipiga haswa. Vipi una taarifa zozote za Yanga yangu?
Nyerere: Ahahhah, Kashasha acha majungu yako bwana.
Kashasha: Mwalimu, mimi nina swali nje ya mpira. Naweza nikakuuliza?
Nyerere: (akitabasamu). Uliza tu mwanangu.
Kashasha: Mwalimu, nimesikiliza hotuba zako. Natamani ungetuandikia nyaraka, kama zile za mtume Paulo.
Nyerere: Ahahahah, kama za Paulo. Nyaraka niliandika labda kama hukuwa mtafutaji na msomaji.
Kashasha: Nilikuwa mfuatiliaji na msomaji wa football sio siasa. Huko ndiko nilikotoa teminolojia nilizotumia katika kazi yangu.
Nyerere: Kama ilivyo ada, jungu kuu halikosi ukoko. Unataka nikupe wosia unaohusu nini haswa?
Kashasha: Mwalimu wangu, uonavyo wewe ni sawa.
Nyerere: (akitafakari huku akichezea fimbo yake) KATIBA. YES, KATIBA KAMA MSINGI WA TAIFA.
Kashasha: (akishangaa) Katiba? Katiba hazijengi miundombinu wala kuleta maendeleo ya kiteknolojia na kisayansi. Exactly, vitu tunavyovihitaji.
Nyerere: Mwanangu, uliyoyataja ni matunda na katiba ni mzizi. Ila naelewa kwamba kizazi hiki kinapenda mavuno kuliko kupanda. Kuna swali au niendelee?
Kashasha: (Kwa umakini) Endelea mwalimu nakusikiliza.
Nyerere: Kwanza kabisa, katiba sio siasa bali siasa ni kajisehemu ka katiba. Pale katiba ikianza kufanywa kama biashara ya siasa (uuzaji wa ahadi ili kununua kura zitakazokupa cheo kwa ajili ya maslahi binafsi) basi taifa hilo liko karibu kuangamia.
Kashasha: Biashara ya siasa? au Public vocation?
Nyerere: Siasa ni wito wa kijamii endapo itatumika kwa maslahi ya taifa. Tofauti na hapo ni biashara kama biashara nyingine.
Kashasha: Mkuu, unanifumbua macho sana leo.
Nyerere: Mkuu ni Mungu peke yake. Tuendelee tulipoishia, katiba ni msingi wa uendeshwaji wa taifa husika uliowekwa na wanachi wenyewe, unaoweka wazi kuhusu taifa, utaifa na vitambulisho vya taifa {bendera, wimbo wa taifa n.k }, mfumo wa haki za msingi za wananchi,muundo wa serikali na mfumo wa utawala, usimamizi wa rasilimali za taifa na mapato yake. Ni jambo la msingi sana katiba kukubalika kimataifa. hivyo basi, lazima ikidhi vigezo vya kidemokrasia { uwakilishi na haki za binadamu}.
Nyerere: (akimnyoshea kashasha fimbo yake) Lazima tuwe na ufahamu kuhusu kazi za katiba. kwa ujumla, kazi hizo ni kuelezea mipaka ya taifa na utaifa, kuelezea haki na wajibu wa wananchi, kutoa muongozo kuhusu nguzo za serikali na taasisi zake{ uundwaji, majukumu na mipaka}, kufafanua mgawanyo wa madaraka wa ngazi mbalimbali za serikali, kuweka bayana udini wa nchi husika na kuainisha malengo ya pamoja ya kijamii, kiuchumi na kimaendeleo kama taifa.
Kashasha: (akitabasamu huku akitikisa kichwa). Hakika mambo ni mengi na muda ni mchache.
Nyerere: Ahahahah, haswaaa. Ila natoa ya muhimu na kwa ufupi sana. Ni lazima tufahamu kwamba, katiba bila utaratibu wa kikatiba ni kazi bure. Ukiweka mikono yako kwenye ndoo ya maji kashasha na kuitoa. Hakika, yale maji yatasahau uwepo wa mikono yako pindi tu uitoapo. Vivyo hivyo, katiba bila utaratibu wa kikatiba katika nchi husika.
Kashasha: Kweli, mvi ni zaidi ya rangi ya nywele.
Nyerere: Utaratibu wa kikatiba ni mwenendo wa serikali na wananchi katika kuzishika na kuzifata taratibu na misingi ya katiba. Utaratibu huu unajidhihirisha katika utaratibu wa kisiasa pamoja na maisha ya haki, usawa na uhuru ya wananchi. Nguvu ya wanachi ndiyo inayobadili katiba sio nguvu ya serikali wala mihimili yake. Katiba sio kanzu/sare ya watu wachache kuamua wapendavyo juu yake.
Kashasha: Ahahahahah, kanzu kama kanzu.
Nyerere: Katiba lazima iheshimiwe na kufuatwa na watu wote bila kujali cheo, jinsia, elimu, dini, rangi wala umri. Nia ikiwa ni kujenga utaratibu wa kikatiba thabiti utakaostahimili mitihani ya muda na majira yake.
Kashasha: Uko sahihi sana mwalimu, ila hiko ni kipengele na kinahitaji moyo mkuu.
Nyerere: Ni kweli na inawezekana.
Kashasha: Mwalimu, tupate wakati wa wadhamini kidogo.
Nyerere: Hakuna shida ila wasiwe mabepari.
Kashasha: Ahahahaha, mabepari. Mwaka jana nilimsindikiza rafiki yangu Kimaro kumzika shangazi yake aliyemlea. Tukiwa njiani, wakaanza kugawa vinywaji { bia/soda} kwa wasafiri. Nikamnong'oneza kimaro vipi mbona kama mnafurahia kifo cha shangazi?
Kashasha: (akimuigiza Kimaro). Aisee rafiki yangu,kauli mbiu ni moja tu, wacha wafu wazike wafu wao. Mjomba wake wa mwisho akaongezea " hasara roho mwanangu, tumia pesa ikuzoee". Bila kusita nikawaambia wanipasishie chui kubwa {serengeti lager} mbili.
Nyerere: Ahahahaha, na wewe ukawa mchaga mwanangu?
Kashasha: Hapana mwalimu, niliacha wafu wazike wafu wao. Ingawa, sisi ni wafu tunaijadili katiba, naamini malaika wa zamu ataipeleka kwa wahusika.
Nyerere: Mwanangu umenena vyema sana.
Kashasha: asante mku...nope mwalimu. Haya, kazi kwako mwalimu.
Nyerere: Tuanze na umuhimu wa katiba halafu sifa za katiba nzuri. (huku akihesabu vidole vyake kwa fimbo)
- Kwanza, inahakikisha taifa halimilikiwi na serikali bali linaongozwa na kusimamiwa na serikali.
- Pili, inaweka mipaka mahali nguvu ya serikali inapoishia na mahali nguvu ya wananchi inapoanzia kwa kulinda haki za binadamu na utu wa mtu. Hizo ni baadhi lakini kubwa kuliko nyingine.
Nyerere: Ni shauku ya kila nchi kuwa na katiba nzuri. katiba hiyo lazima iwe na sifa zifuatazo;
- iwe na uwezo wa kubadilika kuendana na mabadiliko ya nyakati ikizingatia nguzo za maadili ya jamii husika,
- iweke wazi taratibu za mchakato wa kubadili katiba,
- inalinda haki za binadamu,
- iwe wazi na inayoeleweka,
- izingatie nguvu na uwezo wa mahakama kujitegemea { kesi ya kima hakimu hapaswi kuwa ngedere},
- ibainishe mgawanyo wa nguvu za serikali,
- ibainishe uwakilishi wa wananchi katika serikali,
- iwe na misingi ya kusimamia uwazi na uwajibikaji wa serikali na watumishi wake,
- isimamie haki, uhuru na usawa kwa watu wote,
- iwe kamilifu, yafaa kwa matumizi ya nchi nzima.
Kashasha: Hakika wewe ni muasisi wa taifa na gwiji wa siasa.
Nyerere: Sasa ni zamu ya wale ndugu zangu wapendao mavuno. Matunda ya katiba nzuri na utaratibu wa kikatiba thabiti ni mengi sana. Kwa ufupi wake ni haya: utulivu wa nchi, utawala bora na uwajibikaji, uendeshwaji wa taifa kwa misingi ya kidemokrasia, ukuaji wa sayansi na teknolojia, ukweli na uwazi katika shughuli za kiserikali, haki, usawa, na uhuru wa wanachi pamoja na mahusiano mazuri na jamii za kimataifa na mataifa mengine.
Nyerere: Kwa kuhitimisha,katiba lazima ikubaliwe na watu wengi kama sio wote. Katiba lazima itambue kwamba serikali ni ya muhimu ili kuwa na watu huru na wenye haki na usawa lakini haijitoshelezi. Hivyo basi, utaratibu wa kisheria unahitajika. Katiba lazima iwe na matumaini kwamba umoja kamili utajengwa baina ya serikali na wananchi wake bila shuruti.
Kashasha: Ama kweli, chuma hung'oa chuma.
Nyerere: Kwenye hilo suala la vyuma kung'oana. Rafiki yangu, kwanini tusijitahidi kuongea lugha fasaha na adhimu ya kiswahili? Pili, ni kheri upumzike na mtu anayechana bendera na kujifunika na katiba kuliko kupumzika na anayechana katiba na kujifunika na bendera.
Kashasha: Asante sana mwalimu, kwa leo inatosha. Muda umewadia wa kumtafuta malaika wa zamu atusaidie kupeleka wosia kwa wahusika.
Nyerere: Sasa ni zamu ya wale ndugu zangu wapendao mavuno. Matunda ya katiba nzuri na utaratibu wa kikatiba thabiti ni mengi sana. Kwa ufupi wake ni haya: utulivu wa nchi, utawala bora na uwajibikaji, uendeshwaji wa taifa kwa misingi ya kidemokrasia, ukuaji wa sayansi na teknolojia, ukweli na uwazi katika shughuli za kiserikali, haki, usawa, na uhuru wa wanachi pamoja na mahusiano mazuri na jamii za kimataifa na mataifa mengine.
Nyerere: Kwa kuhitimisha,katiba lazima ikubaliwe na watu wengi kama sio wote. Katiba lazima itambue kwamba serikali ni ya muhimu ili kuwa na watu huru na wenye haki na usawa lakini haijitoshelezi. Hivyo basi, utaratibu wa kisheria unahitajika. Katiba lazima iwe na matumaini kwamba umoja kamili utajengwa baina ya serikali na wananchi wake bila shuruti.
Kashasha: Ama kweli, chuma hung'oa chuma.
Nyerere: Kwenye hilo suala la vyuma kung'oana. Rafiki yangu, kwanini tusijitahidi kuongea lugha fasaha na adhimu ya kiswahili? Pili, ni kheri upumzike na mtu anayechana bendera na kujifunika na katiba kuliko kupumzika na anayechana katiba na kujifunika na bendera.
Kashasha: Asante sana mwalimu, kwa leo inatosha. Muda umewadia wa kumtafuta malaika wa zamu atusaidie kupeleka wosia kwa wahusika.
Upvote
2