Kupuuzwa kwa maoni ya wananchi kama yalivyoainishwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba. Rasimu hii ya Pili iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilizunguka nchi nzima ikakusanya maoni ya wananchi lakini maoni hayo yamepuuzwa. Jibu
Katiba Inayopendekezwa imezingatia kwa kiasi kikubwa maoni yaliyotolewa na wananchi moja kwa moja, hoja za makundi na taasisi mbalimbali pamoja na zile zilizotolewa na wabunge wa Bunge Maalum la Katiba. Ndani yake haki za makundi mengi zimetajwa na kulindwa, mifumo mbalimbali ya utawala na namna ya kuendesha nchi imeboreshwa na kero nyingi zimepewa ufumbuzi. Watanzania waliotoa maoni yao moja kwa moja kwa Tume ni 684,303 kutoka Bara na 49,671 toka Zanzibar. Hawa ni watu wachache sana ukilinganisha na Watanzania wapatao 20,000,000 wenye umri na sifa za kupiga kura. Mawazo yao pekee hayawezi kuwa ndio mawazo ya Watanzania wote. Hivyo kudai haya yawe ndiyo mawazo pekee ya kuzingatia na kuachia wengine haingekuwa haki. Rasimu ya pili ya Katiba ilipaswa kuzingatia maoni toka katika Mabaraza ya katiba ya wilaya na yote ya taasisi ambao wajumbe wake walichaguliwa na wananchi kuingia katika mabaraza haya. Maoni mengi sana toka kwenye Mabaraza haya hayakuzingatiwa na Tume kwenye Rasimu yake ya pili. Ndani ya Bunge Maalum la Katiba Watanzania waliwakilishwa na Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao waliwachagua wenyewe kuwawakilisha na ili hoja toka makundi mbalimbali kuzingatiwa walichaguliwa wajumbe 201 toka makundi mbalimbali ya kijamii kwenye hili Bunge Maalum. Hii yote ilikuwa ni kupanua na kuimarisha ushiriki wa wananchi. Hoja Muundo wa Bunge Maalum ulifanya Bunge lijae wanasiasa kwani lilikuwa na wabunge wote, wawakilishi wote hivyo kufanya idadi ya wanasiasa kuwa robotatu ya Bunge lote. Hata wajumbe 201 nao ndani yake kulikuwa na wanasiasa 40 wawakilishi wa vyama. Vilevile kulikuwa na wawakilishi wa AZAKI pia ni makada wakongwe wa vyama vya siasa. Suala hili lilipelekea majadiliano kufuata mrengo wa kisiasa. Jibu Bunge Maalum la Katiba liliundwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilisomwa, ikajadiliwa kwa kina Bungeni na kufanyiwa marekebisho kadhaa. Hakuna mtu wala kikundi au chama cha siasa kilicholeta hoja hii iangaliwe na ikibidi ijadiliwe. Kuileta hoja hii sasa ni wazo la baadae.(An afterthought) Majadiliano ya kupata katiba mpya ya nchi huhusisha mchakato wa kutengeneza muundo wa serikali, mfumo wa uongozi wa nchi, mfumo wa uchumi wa nchi na mfumo wa ulinzi na usalama wa nchi. Katika kuijadili hii miundo na mifumo haiyumkiniki mitazamo yenye mirengo tofauti ya kisiasa ikasikika katika majadiliano hayo. Wabunge, wawakilishi na wawakilishi wa AZAKI wanawakilisha wananchi moja kwa moja au makundi mbalimbali ya jamii na wao pia ni sehemu ya wananchi hivyo kushiriki kwao katika kazi hii ni sawa, haki na muafaka. Hoja Bunge Maalum la Katiba lilikosa uhakika wa kisheria na kisiasa pale lilipoendelea na majadiliano ilhali baadhi ya wajumbe walikuwa wametoka nje ya ukumbi. Ingepaswa maridhiano yafanyike ndipo Bunge hilo liendelee. Jibu Bunge Maalum la Katiba lingeweza kukosa uhalali wa kisheria kama lingefanya shunguli zake kinyume na sheria iliyoliunda mfano kutozingatia akidi, kufanya maamuzi ambayo halina mamlaka nayo, kufanya kazi nje ya siku lilizopangiwa nk. Bunge Maalum la Katiba lilifanya shunguli zake zote kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kanuni zake hivyo lilikuwa halali kisheria na lilifanya kazi zake kwa uhalali. Bunge Maalum la Katiba lingeweza kukosa uhalali wa kisiasa iwapo lingefanya mambo yake nje ya sheria au kwa ubaguzi wa namna yoyote, ubabe au kutozingatia kanuni lililojiwekea. Hili halikutokea kwani Sheria na Kanuni zilifuatwa kwa uwazi na usahihi. Maridhiano ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kutafuta Katiba mpya. Lakini ni budi pande zinazotofautiana zikubaliane kukutana, kuongea bila masharti yenye kulenga kulazimisha upande mwingine na kila upande ukubali kuwa katika maridhiano kila upande upate na baadhi ya vitu utapoteza. Kundi lisilo rasmi lililojiita UKAWA lilitoka nje ya ukumbi wa Bunge na tofauti na matukio ya nyuma hawakutaka majadiliano ya aina yoyote wala kurudi Bungeni. Mwenyekiti wa Bunge Maalum aliitisha Kamati ya Maridhiano ikutane Dar Es Salaam UKAWA wakakataa, viongozi wa madhehebu yote ya dini waliowaomba warudi Bungeni na wakae kwenye kwenye meza ya mazungumzo wakakataa, Rais wa Jamhuri ya Muungano akawanasihi kufanya kurudi Bungeni wakakataa. Mwishowe Msajili wa Vyama vya Siasa akaitisha vikao vya kutafuta kiini cha tatizo lakini napo UKAWA wakagoma suluhu. Kama kutoka kwa UKAWA kungekuwa na athari ya kisheria na kisiasa kwa mustakabali wa nchi yetu lakini kwa bahati nzuri haiupo, basi lawama ni kwao. Hoja Kuweka kwa makusudi kura za wazi na siri ili kuwabana wanachama watakaokwenda kinyume na maslahi ya vyama husika. Jibu Bunge Maalum la Katiba lilikuwa linaendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria ililoliunda na Kanuni iliyotunga na kupitishwa na wajumbe wake. Uendeshwaji wake ulikuwa hausimamiwi wala kuratibiwa na chama chochote cha siasa hivyo hapakuwa na namna ya kushawishi au kushinikiza aina ya upigaji kura. Uamuzi wa wajumbe kuamua kupiga kura ya wazi au siri ulikuwa ni Bunge lote tena kwa maridhiano na kwa mujibu wa Kanuni hivyo hapakuwa na kulazimishana. Wakati wa kupiga kura wajumbe walio wengi hata waliojiita UKAWA walipiga kwa hiari yao kura ya wazi. Hata katika kura ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa wapo wajumbe kwa hiari yao walipiga kura ya wazi kuikataa Katiba Inayopendekezwa.
Hoja Kuweka kanuni ya kuruhusu upiganaji kura kwa watu waliokuwa hospitali, hijja na kwingine ili akidi itimie. Jibu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ndiyo iliyounda Bunge Maalum la Katiba ililipa uwezo Bunge hili kutunga kanuni juu ya namna ya kuendesha mambo yake. Bunge Maalum la Katiba lilipitisha kanuni inayompa mjumbe ambae hayuko kwenye eneo la Bunge na ana ruhusa ya Mwenyekiti kupiga kura yake atakapokuwa kwa kuwekewa utaratibu kama akiomba kwa maandishi kwa Mwenyekiti. Kwa mujibu wa Kanuni iliyotajwa hapo juu wajumbe waliokuwa wamelazwa hospitalini, wako likizo ya uzazi au kwenye ibada ya hijja Saudia waliomba nafasi ya kupiga kura na utaratibu ukafuatwa na wakapiga kura. Hapakuwa na busara ya kuwanyima haki yao ya kupiga kura wakati walishiriki mchakato wote wa majadiliano hadi mwisho na walitaka kupiga kura. Kumnyima mjumbe kupiga kura kwa sababu kaenda kuhudhuria ibada ya hijja au ni mgonjwa hospitalini au kwenye uzazi ni kumnyima haki yake ya msingi. Hoja:rip::juggle:
Kutokutimia kwa akidi za kamati mbalimbali walipokuwa wanajadili ndani ya Kamati Rasimu ya Katiba. Akidi ilikuwa haitimii kwani wengi wa Zanzibar walitoka na UKAWA. Jibu Hakuna ushahidi wa kitakwimu unaothibitisha kuwa akidi zilikuwa hazitimii hasa za Wabunge toka Zanzibar. Kamati nyingi akidi ilitimia. Kanuni ziliweka wazi kuwa hata kama 2/3 ya upande wowote haitapatikana katika kupitisha vifungu hii haitazuia ripoti ya Kamati hiyo kuwasilishwa kwenye Bunge kwa majadiliano na ndipo kura ya mwisho itapigwa na kupitishwa kwa kupata 2/3 toka kila upande wa Muungano. Hoja Kulikuwa na kura za maruhani na watu wasiokuwepo Bungeni. Jibu Kura zilizopitisha Katiba Inayopendekezwa ni zile zilizopigwa kwa wazi au siri Bungeni na kuhesabiwa chini ya mawakala na matokeo kusomwa. Hapakuwa na kura ya mtu toka nje. Madai kuwa marehemu Shida Salum aliyefariki mwezi Juni 2014 alihesabiwa amepiga kura ni ya uongo na yana sababu ovu kwani yanalenga kuamsha uchungu kwa familia yake kwani hayana ukweli wowote. Madai ya Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Zanzibar kuwa alihesabiwa kupiga kura hayana ukweli kwani utaratibu wa kupiga kura na kuhesabu ulikuwa ndani ya Bunge na hakuwa mmoja wa wapiga kura. Jina lake lilionekana kwenye orodha ya majina ya wajumbe kwenye nakala maalum za Katiba zilizotolewa kwa ajili ya uzinduzi kimakosa na Naibu Katibu wa Bunge alilitolea maelezo kuwa yalikuwa ni makosa ya kiuchapaji kuingiza jina lake. Hoja Baadhi ya Wabunge wa Bara kuonekana wamepiga kura Zanzibar na kinyume chake mf Zakhia Meghji. Jibu Orodha ya Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba ilionyeshwa kwenye orodha maalum zilizotolewa na Bunge zikionyesha wabunge toka pande zote za Muungano. Mheshimiwa Zakhia Hamdani Meghji ni Mzanzibar kwa kuzaliwa, kukulia na kwa sehemu kubwa alisomea Zanzibar. Yeye ameolewa Bara na amekuwa kwenye utumishi Serikalini kwa miaka mingi. Kuolewa na kufanya kazi Bara hakuwezi kumwondolea Uzanzibar wake. Aliingia Bungeni kama Mbunge wa Bunge la Muungano kwa kuteuliwa na Rais. Wapo Wazanzibar walioolewa na kufanya kazi Bara na haki yao ya kufanya siasa Zanzibar haijawahi kuhojiwa mfano Mama Fatma Maghimbi na Anna Maulida Komu.