Kwanini nilinyanyua kalamu kuandika historia ya TANU?

Kwanini nilinyanyua kalamu kuandika historia ya TANU?

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
KWA NINI NILINYANYUA KALAMU?

Naona ukumbi kama vile umejaa na kinachosubiriwa ni kuanza mazungumzo.

Najiuliza mwenyewe kwa nini niliamua kuandika kitabu hicho hapo juu kueleza historia ya TANU ilhali tayari historia ya TANU mbayo ndiyo historia ya uhuru wa Tanganyika ilishaandikwa na Chuo Cha CCM Kivukoni?

Kitabu hiki kilichapwa mwaka wa 1977 mwaka wa kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hii si historia ya TANU pekee na historia ya uhuru wa Tanganyika bali pia ni historia ya Julius Kambarage Nyerere.

Ukweli ni kuwa kitabu hiki hakikuwa historia ya TANU wala historia ya uhuru wa Tanganyika wala historia ya Mwalimu Nyerere.

Kilichonishangaza sana ni kuwa vipi kwanza Mwalimu Nyerere mwenyewe alikubali kitabu hiki kuwa ndiyo historia ya TANU na yeye kama Mwenyekiti wa CCM aruhusu kichapwe kama ndiyo historia ya uhuru wa Tanganyika?
Huenda msomaji wangu na wewe utajiuliza mimi nimejuaje kuwa historia ya TANU imekosewa?

Mimi nimejuwa kuwa historia ya TANU iliyokuwa imeandikiwa si historia ya kweli kwa kuwa nilizaliwa katika kipindi Tanganyika inaanza harakati za kudai uhuru.

Nimezaliwa mwaka wa 1952 Mtaa wa Kipata nyumba no. 33, Dar es Salaam.

Huu ndiyo mwaka Mwalimu Nyerere amefika Dar es Salaam na kuanzi kazi ya Ualimu Pugu.

Mtaa huu wa Kipata ni sehemu ya eneo linalojulikana kama Gerezani na linaanza nyuma ya Mtaa wa Kitchwele (Mtaa wa Uhuru) na linakwenda hadi Arab Street (Mtaa wa Nkrumah).

Mitaa ya Gerezani inaanza Kipata (Kleist Sykes), Kirk (Lindi), Somali (Omari Londo), Kiungani, Mbaruku, Kisarawe (Makamba) na katika mitaa hii kuna mitaa miwili Somali na Mbaruku inayoitwa Somali Kipande na Mbaruku Kipande.

Sababu ya kuitwa ‘’kipande,’’ ni kuwa sehemu ya mitaa hii imekatika na kuingia sehemu nyingine.

Huu mtaa wa Kirk ambao ulikuja kuitwa Lindi ulikuwa unaanza Msimbazi na unaishia Nkrumah.

Baadae wakati Kitwana Kondo ni Meya wa Dar es Salaam alibadili majina ya mitaa mingi kwa kuwaenzi wapigania uhuru wa Tanganyika na Mtaa wa Lindi ukagawiwa sehemu mbili.

Kuanzia Mtaa wa Msimbazi hadi Mtaa wa Nyamwezi ukawa Bi. Tatu bint Mzee na kuanzia Nyamwezi hadi Nkrumah ukabakia na jina la Lindi.

Kitendo hiki cha kubadili majina ya mitaa hakikuwafurahisha baadhi ya watu ndani ya mamlaka za nchi.

Kitendo hiki kiliwakera kwa kuwa majina mengi ya wapigania uhuru walioadhimishwa ni Waislam ikawa kama vile historia ya TANU iliyofutwa sasa inarejeshwa kwa mlango wa uani.

Gerezani wameishi watu wengi maarufu katika historia ya Dar es Salaam kama Kleist Sykes na wanae Abdulwahid, Ally, Abbas na mama yao Bi. Mruguru bint Mussa, Aziz Ali na mkewe Mama Ali na watoto wao Dossa, Hamza na Ramadhani Aziz (kwa kuwataja wale waliokuwa maarufu), Ibrahim Hamisi na Omari Londo.

Babu yangu Salum Abdallah alikuwa na nyumba Mtaa wa Mbaruku lakini alipanga nyumba Mtaa wa Kipata, nyumba ya rafiki yake Abdallah Simba aliyekuwa Liwali wa Songea.

Sababu ya babu yangu kutaka kuishi Kipata nimeambiwa kuwa barza yake ilikuwa hapo na akikuona Mbaruku kuwa ni mbali.

Nyumba hii ya Abdallah Simba ilikuwa inatazamana na nyumba ya Kleist Sykes na wote walikuwa wakifanya kazi Tanganyika Railways.

Nyumba hii hivi sasa haipo ilipokuwa nyumba hiyo leo ni petrol station na nyumba ya Kleist ni gorofa ndefu yenye nyumba za kuishi watu na chini kuna maduka na ofisi.

Kleist Sykes alikuwa Accounts Clerk babu yangu akiwa katika karakana kama mfua chuma.

Hii ilikuwa katika miaka ya 1920.

Hii ndiyo Gerezani niliyoikuta mimi nilipozaliwa mwaka wa 1952 na kwa ajili hii nikajaaliwa kuwaona baadhi ya wazalendo waliounda African Association mwaka wa 1929 iliyokuja kuwa TANU mwaka wa 1954.

Mimi ni sehemu ya historia hii.

Nilishangaa nilipofungua kitabu cha historia ya TANU na kuwakuta wazee wangu hawa wote hawakutajwa.

Historia yao haipo.

Tatizo la kutokea baadhi ya watu ndani ya TANU kuichukia historia ya kweli ya TANU lilianza baada ya Uchaguzi wa Kura Tatu mwaka wa 1958 ilipokuwa dhahiri kuwa uhuru utapatikana karibuni.

In Shaa Allah nitaeleza hili katika makala ijayo.

1666881531842.png
 
Jazakallah Kheir ama hakika wewe ni hazina ya msingi sana kwa maisha ya watanzania juu historia ya kweli iliyopotea.

Wengi hatujui hilo kwa kuwa wengi hatujui umuhimu wa historia ya kweli na athari ya maisha ya kila siku, katika jambo lolote linalo tengeneza sehemu ya maisha au muelekeo fulani katika maisha ya kila siku.

Kuthibitisha hilo tuangalie vitabu vya dini vyoote vimeandikwa katika mtindo wa historia na ndio utaona kuwa msingi wa imani zetu umejengeka katika historia hizo na ambazo ndizo zinajenga mustakabali wa maisha yetu ya kila siku kiimani na hatimae kuathiri maadili na mtindo wa maisha yetu ya kila siku kama vile namna ya staha, amani na utulivu miongoni mwetu.

Ili kuelewa hilo ni kuwa kila jambo lina chimbuko lake na ndio huo msingi wake, kwa sababu msingi huchimbwa hivyo basi ukipotosha msingi au chimbuko lake maana yake utapoteza mustakabali wa maendeleo ya maisha ya jambo hilo kwakuishi katika dira ya uongo na hatimae kuathiri namna sahihi ya mtindo wa maisha ya jambo hilo kwa jinsi inavyopaswa kuishi kila siku.

Ahsante sana Ndg. Mohamed Said kalamu yako inatugusa wengi sana Allah akulipe wema kwa hilo.
 
Back
Top Bottom