BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,165
Pengo amtaka Mkapa kwenda kuhiji Butiama
Basil Msongo
Daily News; Saturday,February 21, 2009 @19:00
Basil Msongo
Daily News; Saturday,February 21, 2009 @19:00
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo, amemtuma Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kwenda kuhiji alipozikwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na kufikisha shukurani zake kwa kazi aliyoifanya kujenga mazingira yaliyoliwezesha Kanisa kupata mafanikio.
Kadinali Pengo pia alimshukuru Mkapa, marais waliomtangulia na mrithi wake, Rais Jakaya Kikwete, kwa kuendeleza mazingira hayo yaliyoliwezesha Kanisa kufanikiwa katika shughuli zake za kiroho na kijamii. Nenda kamwambie nakushukuru, alisema Kadinali Pengo katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph Dar es Salaam jana kwenye ibada ya kuadhimisha miaka 25 tangu alipopata daraja la uaskofu Januari 6, 1984.
Baba wa Taifa alifariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, London, Uingereza na alizikwa katika kijiji cha Butiama mkoani Mara. Kadinali Pengo (55) alianza kazi hiyo ya kichungaji katika jimbo la Nachingwea mkoani Lindi na baadaye akapanda daraja kuwa Askofu wa kwanza jimbo la Tunduru, Masasi Februari 12, 1987. Kuanzia Julai 22, 1992 amekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Kadinali Pengo pia ameshatimiza miaka 11 tangu alipopata Ukadinali, Januari 18, 1998 ambapo Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II alimpa daraja hilo na kumsimika Februari 21 mwaka huo huo, katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Rome, Italia.
Licha ya majukumu ya kuongoza waumini zaidi ya milioni moja katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kadinali Pengo pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Afrika na Madagascar na mlezi na mdhamini wa Mabaraza ya Maaskofu Mashariki ya Afrika. Kiongozi huyo alisema Kanisa limepata mafanikio kwa kuwa nchi imekuwa ikitoa mazingira ya kuweza kufikia mafanikio hayo.
Alitoa mwito kwa viongozi na wananchi wasikubali kuipoteza tunu ya amani iliyopo nchini. Amani tuliyonayo katika Taifa letu si kitu cha kuchezea, alisema katika ibada hiyo iliyohudhuriwa na Mkapa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, maaskofu wa majimbo, majimbo makuu, mapadre, watumishi wa kanisa wa kada mbalimbali, na waumini wengine.
Tusiruhusu ukabila, udini na utaifa kuharibu amani ya Taifa letu, alisema kiongozi huyo na kusisitiza kuwa hilo ni ombi la dhati kutoka kwake na ni muhimu likazingatiwa.Naye Askofu Mkuu Msaidizi wa Jimbo hilo, Methodius Kilaini, alimweleza kiongozi wake huyo kuwa anapendwa na waumini na wanathamini kazi anazozifanya katika jimbo.
Wanathamini moyo wako kwa wanyonge na kwa wenye shida, alisema Askofu Kilaini na kuongeza kuwa, zawadi kuu aliyoichagua Kadinali Pengo kwa ajili ya Jubilei yake ya Fedha (miaka 25), ni gari kwa ajili ya wananchi wa Mafia mkoani Pwani.
Wakati wa mahubiri katika ibada hiyo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Josephat Lebulu, alimtaka Kadinali Pengo aendelee kukemea maovu bila kuogopa na asiache kufanya kazi za kichungaji na akichoka, atambue kuwa bado ana kazi za kufanya na atapata mafanikio. Usichoke, kazi yetu haina kuchoka bali tunaishia kuwa mishumaa, alisema kiongozi huyo wa Kanisa na kuwataka waumini wamuombee Kadinali Pengo amudu majukumu aliyonayo kuchunga kanisa kiroho na kimwili.
Aliwataka waumini kuacha kuwashutumu viongozi wa kiroho kwa kuwa wao ni wanadamu, hivyo wana udhaifu sawa na wanadamu wengine lakini kwa kuwa wanatekeleza matakwa ya Mungu, hata kama wanadamu wakiwakataa, kazi za kichungaji zitaendelea.
Februari 17 mwaka huu, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Benedict wa XVI aliandika ujumbe wa kumpongeza Kadinali Pengo kwa kutimiza miaka 25 ya uaskofu. Alimsifu kwa unyenyekevu, ukarimu, utii na upendo alionao kwa kanisa na juhudi zake za kuhimiza umoja na amani.