Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Madini aina ya Uranium
KWA UFUPI
Maliasili nyingine za madini, gesi na mafuta iwapo hazitasaidia kutatua matatizo na kuboresha huduma za kijamii kama afya, elimu umeme na barabara ni sawa na nchi kuwa na laana, kwani rasilimali zilizopo zikisimamiwa kikamilifu zinaweza kuleta maendeleo nchini
Utafiti unaonyesha hapa nchini kuna zaidi ya aina 30 za madini. Kulingana na ramani mpya ya madini kutoka wizara ya nishati na madini, kila wilaya inakadiriwa kuwa na aina hizo 30 za madini.
Maliasili nyingine za madini, gesi na mafuta iwapo hazitasaidia kutatua matatizo na kuboresha huduma za kijamii kama afya, elimu umeme na barabara ni sawa na nchi kuwa na laana, kwani rasilimali zilizopo zikisimamiwa kikamilifu zinaweza kuleta maendeleo nchini.
Utafiti wa mwandishi wa makala haya unabainisha kuwa zipo sababu mbalimbali zinazoendelea kusababisha madini kushindwa kuwanufaisha Watanzania.
Kinachoonekana ni kwamba madini yameendelea kuwa neema kwa wawekezaji ambao wengi wao ni makampuni ya kigeni.
Mwanasheria kutoka chuo kikuu cha Havard nchini Marekani ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Lawyers Environmental Action Team (LEAT), Dk Nshala Rugemeleza anasema sekta ya madini inashindwa kuwanufaisha Watanzania.
Anataja mojawapo ya sababu kuwa ni kumilikiwa na wawekezaji kutoka nje ambao wanalindwa na sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inafanya rasilimali ya madini kuendelea kumilikiwa na wageni.
Dk Nshala anasema Sheria ya Madini ya 2010 ina vipengele vingi ambavyo vinawabeba wawekezaji, kwani sehemu kadhaa zimechukuliwa kutoka mkakati wa Benki ya Dunia uliodhamiria kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kumilikiwa na wageni.
Mkakati madhubuti wa Benki ya Dunia wa mwaka 1992 ulikuwa ni kuhakikisha nchi za Afrika zinaendelea kupoteza na kushindwa katika soko la dunia kwa madai kuwa serikali zao hazina uwezo wa kumiliki mfumo wa uchimbaji badala yake mfumo huo umilikiwe na makampuni binafsi ya nchi za magharibi.
Kulingana na Dk Nshala Benki ya Dunia imeweka msukumo wa kuhakikisha nchi za magharibi zinaendelea kunufaika na sekta ya madini ya Afrika.
Benki hiyo ilisimamia na kutoa mkopo wa Dola 50 milioni za Kimarekani kwa ajili ya kuifanyia mabadiliko ya Sheria ya Madini ya 1998 na kuanzishwa kwa sheria mpya ya madini ya mwaka 2010.
Katika sheria hiyo vifungu vingi vimenukuliwa kutoka mapendekezo ya Benki ya Dunia na kwamba mabadiliko ya sheria ya madini ya 2010 haijagusa mabadiliko katika kipengele cha kodi.
Matokeo yake ni kwamba makampuni hayo yanaendelea kukwepa kodi, mfumo wa ulipaji kodi tangu mwaka 1992 hadi sasa bado unawabeba wawekezaji kulingana na mapendekezo ya Benki ya Dunia. Kulingana na Benki ya Dunia, sekta ya madini ni ya kiulimwengu na kwamba ili iweze kuwa ya kidunia ni lazima kampuni binafsi za uchimbaji zifanye kazi hiyo kwa kuwa zina mtazamo wa kiulimwengu katika utafutaji na uchimbaji wake na kwamba kampuni hizo zinatoka katika nchi za Australia, Canada, Afrika ya Kusini, Ulaya na Marekani.
Mkakati huo wa Benki ya Dunia umeeleza wazi kuwa haupo tayari kuwekeza katika Serikali ambayo inachukua hisa nyingi zaidi ya kampuni binafsi. Watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha ndiyo wanaotakiwa kuwekeza katika sekta ya madini, gesi na mafuta na kwamba sekta ya madini inahitaji kuwa na mikataba migumu.
Mkakati mwingine wa kuhakikisha kuwa sekta ya madini inaendelea kuwanufaisha wawekezaji ni kuhakikisha utafutaji na uchimbaji wa madini unafanyika katika nchi za Afrika na kusababisha athari za kimazingira wakati uchenjuaji, usafirishaji na utengenezaji wa bidhaa unafanyika katika nchi za wawekezaji ambazo hupata faida kuwazidi wenye raslimali hizo.
Dk Nshala anabainisha zaidi kuwa sekta ya madini inaendelea kuwanufaisha wawekezaji badala ya wageni ni kutokana na mfumo wa profit transfering (PT) ambao unafanywa na makampuni ya uchimbaji. Mfumo huu unaziwezesha kampuni hizo kufanya biashara kwa faida kubwa baada ya kuhamishia faida toka nchi moja yenye kodi kubwa kwenda nchi zenye kodi ndogo.
Kwa mfano kampuni ya BAP Biliton ya Australia inafanya kazi katika nchi tisa na kusababisha kuongeza kiwango cha ukilitimba hadi katika kampuni nyingine ndogo ndogo zinazochimba madini. Mfano mwingine ni kampuni ya Anglo America mwaka 1970 ilimiliki zaidi ya kampuni 1000 nchini Afrika ya kusini.
Mkakati wa mataifa ya magharibi kuendelea kumiliki sekta ya madini katika nchi za Afrika, yalitumia mbinu mbalimbali ikiwemo mbinu ya kuwa na siri kubwa katika utoaji wa taarifa ambapo kampuni hizo hazitoi taarifa za kweli kuhusu utafutaji wa madini, uchimbaji, uchenjuaji, usafirishaji hadi uzalishaji wa bidhaa katika masoko hali ambayo inasababisha kwa mfano Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) haijui inawezeje kutoza kodi kwenye makampuni hayo.
Wawekezaji wanashiriki katika sehemu ya kuongeza thamani katika bidhaa za madini na kujipatia faida kubwa kwa kuwa wanaongeza thamani mara nne hadi 20 katika hatua madini kutengenezwa bidhaa za sokoni.
Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka 2007 barani Afrika kulikuwa na kampuni binafsi zilizowekeza katika sekta ya madini zaidi ya 4,000 ambazo zilishughulikia na utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, usafirishaji na utengenezaji wa bidhaa za madini ambazo ni zao la mwisho.
Pia katika kipindi hicho cha mwaka 2007 kulikuwa na kampuni tanzu ambazo zinaitwa junior companies zipatazo 3,067 ambazo kazi yake kubwa ilikuwa ni kugundua madini na kuyaacha makampuni makubwa kuanza uzalishaji. Mfano mzuri ni kampuni ya MANTRA ilihusika na kutafuta na kuchimba imeachia kampuni ya kutoka Urusi.
Machapisho mbalimbali yaliyotolewa kuanzia mwaka 2007,2008 na 2009 yanaonyesha namna bara la Afrika linavyoibiwa katika sekta ya madini na kubakia maskini na kwamba lengo la Benki ya Dunia sio kusaidia nchi za Afrika, bali ni kuzidisha umaskini katika nchi zenye utajiri wa madini kama ilivyo Tanzania.
Takwimu zinaonyesha kuwa nchini Ghana licha ya uzalishaji wa madini kuwa mkubwa mwaka 2001, kodi ya mapato ambayo nchi hiyo ilipata ilikuwa ni Dola 31 milioni tu ambayo ni asilimia nne ya mapato ya kodi ya nchi hiyo na hapa Tanzania kuanzia mwaka 2002 hadi 2007 nchi ilipata Dola 21.7 milioni kati ya madini yenye thamani ya Dola 2.5 bilioni. Katika kipindi hicho watu 400,000 walipoteza ajira migodini.
Utafiti unaonyesha licha ya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye utajiri wa madini ya aina mbalimbali umaskini unaendelea kuongezeka na ripoti ya serikali ya mwaka 2002 inasema umaskini katika maeneo ya vijiji uliongezeka kwa asilimia 57, hata hivyo sababu kubwa ya ongezeko hilo ni kufukuzwa kwa wachimbaji wadogo na kunyang'anywa ardhi ingawa serikali inadai sababu kubwa ni tofauti ya kipato. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani, Professa Reuven Avi katika moja ya machapisho yake kuhusu wawekezaji, anasema dhana ya kuweka vivutio kwa ajili ya wawekezaji ni potofu na haina faida yeyote kwa nchi badala yake imekuwa na malengo ya muda mfupi kujijenga kisiasa na hakuna unafuu wowote wa kodi.
Wachumi na watafiti hawajaona ushahidi wa vivutio kwa wawekezaji kuleta unafuu katika uwekezaji na ukuaji wa uchumi.
Manufaa ambayo jamii inatarajia kupata katika mikataba ya madini yanaishia katika kampuni za uwekezaji kuneemeka na wananchi kuendelea kuwa masikini kwa kuwa kampuni hailipi kodi endapo haijapata faida katika uwekezaji. chanzo.Kwanini sekta ya madini hainufaishi Watanzania? - Makala - mwananchi.co.tz