Msaada wa Dola za Marekani milioni 500 kupitia Mkataba wa Makubaliano uliosainiwa kati ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kampuni ya usafirishaji ya DP World ya Dubai, utafadhili miradi mbalimbali inayolenga kuboresha ufanisi wa bandari za Tanzania. Kampuni hiyo ina utaalam wa usafirishaji wa mizigo, shughuli za bandari, huduma za baharini na maeneo ya biashara huria. Makubaliano ya msaada huo yalitiwa saini katika maonyesho ya Dubai Expo kati ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eric Hamissi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa DP World Sultan Ahmed Bin Sulayem na kushuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Fedha za mkataba huo zitatumika katika kuendeleza bandari za Tanzania, zikilenga maeneo muhimu ya habari na mawasiliano, mifumo ya teknolojia (ICTs), mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa TPA na uboreshaji wa miundombinu ya bandari. Fedha hizo pia zinatarajiwa kuziwezesha bandari za nchi kuongeza uwezo wa kiushindani katika ngazi ya kikanda na kimataifa na kuboresha huduma.
Sent using
Jamii Forums mobile app