MAUDHUI KATIKA RIWAYA YA KUSADIKIKA
Beba April 11, 2018
I Utangulizi
Kitabu cha
Kusadikika kimetungwa na Shaaban Robert; yule mtunzi maarufu wa vitabu vya Kiswahili duniani. Kurasa za hadithi ya
Kusadikika ni hamsini na saba (57), lakini kama zitahusishwa kurasa za awali na mwisho wa kitabu,
Kusadikika ni riwaya yenye kurasa 80.
Kusadikika ni kitabu kinachojumuisha vitahu vyapata 18 vya Shaabani Robert.
Kusadikika ni kitabu kinachoisimulia nchi iliyo katikati ya mipaka sita. Ni nchi inayoelea angani.
II Muhtasari
Kusadikika ni riwaya yenye sura 9. Kila sura inajadili suala ama jambn muhimu ambalo mwandishi amedhamiria liwafikie wasomaji wake. Pengine tuziangalie sura hizo kifupi.
Sura ya kwanza inahusu mashtaka ya Waziri Mkuu wa Kusadikika yaliyoelekezwa kwa Karama. Aidha, sura hiyo inamwelezea Waziri Mkuu, bwana Majivuno kuwa ni mtu mwenye haiba kubwa na uhodari usiolinganishwa na chochote.
Katika sura hiyo, raia wa Kusadikika aitwaye Karama anadaiwa kuwa:
· Anapata haki ya kulindwa lakini hana shukrani
· Karama anadaiwa kuwa ana tamaa na si mtii. Hofu ya majivuno ni kuwa kama Karama angeachwa afanye atakavyo, angeweza kudai udiwani, uwaziri na hatimaye ufalme.
Baada ya Waziri Mkuu kutoa shtaka lake, baraza lilitakiwa kutoa hukumu kwa mshtakiwa Karama. Aidha, imeelezwa katika sura hiyo kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi ya Kusadikika mshtakiwa aliruhusiwa kujitetea; na utetezi ulichukua muda wa siku sita.
Sura ya pili inaanza na maelezo juu ya taaluma ya uanasheria. Katika maelezo yake, mstakiwa anazumgumza kwa ufasaha mkubwa. Karama anatumia wahusika mbalimbali katika kutoa utetezi wake. Aidha anaelezea kwanza maana ya uanasheria.
Sura ya tatu inaanza utetezi wa Karama. Karama anaelezea madhila yaliyomfika Mwanakusadikika aitwaye Burhani baada ya kuifanyia makubwa nchi ya Kusadikika.
Buruhani alifanya safari ya mbali ya Kaskazini kwa ajili ya kuitafutia maarifa nchi ya Kusadikika. Baada ya kurudi nchini Kusadikika na kuelezea mazuri aliyoyaona alikokwenda na ambayo yangewafaa watu wa Kusadikika, Buruhani alitumbukizwa kifungoni - kifungo cha maisha!
Sura ya nne inaelezea madhila yaliyompata mjumbe wa Mashariki aitwaye Fadhili. Inaelezwa katika sura hiyo kuwa
Fadhili alileta ujumbe kutoka Mashariki uliohusu kufutiliwa mbali chuki, watu kusikilizana na kushirikiana kwa upendo. Badala ya kufurahiwa na kukubalika, Fadhili aliitwa mwongo, mwoga na mwota ndoto zisizokubalika. Alidharauliwa, hakuthaminika hata kidogo!
Katika sura ya tano, mshtakiwa alisimulia kisa cha Kabuli, mjumbe aliyetumwa Kusini. Karama alielezea safari ya
Kabuli aliyesafiri katika nchi tatu: nchi za Juju, Hasira na Kiasi. Kabuli alipata matatizo mbalimbali. Ujumbe aliouleta haukuthaminiwa na alipewa hukumu ya kifungo cha maisha na kazi ngumu.
Sura ya sita inaelezea kuhusu mjumbe aliyetumwa Magharibi ajulikanaye kwajina la Auni. Karama alieleza kuwa
Auni alisafiri mbali, akapata matatizo mengi. Auni alielezwa kuwa alikutana na vipofu waliopata madhila kutokana na tabia mbalimbali. Baada ya kupata matatizo makubwa, Auni alirudi Kusadikika, akapata madhila, hakuthaminiwa.
Sura ya saba inahusu mjumbe aliyetumwa Mbinguni. Mjumbe huyu aliitwa Ridhaa.
Ridhaa alileta habari mbalimbali zikiwemo kuhusu haki, bidii, thamani ya muda na kadhalika. Taarifa hii ilipofika Kusadikika mjumbe Ridhaa alipatwa na adha zilezile.
Mjumbe wa Ardhi alikuwa wa mwisho, na alielezwa katika sura ya nane. Sikuhiyo Karama alieleza kisa cha mjumbe Amini.
Amini alileta habari za watu kuwa waadilifu wakubwa. Kulitolewa rai kuwa watu hawa waigwe, lakini ujumbe huu ulifanya anyang'anywe milki yake na kufungwa maisha.
Baada ya usimulizi wa wajumbe hawa sita, Mfalme aliliamini Baraza litoe hukumu. Upeo wa hadithi hii ni sura ya tisa ambapo inatolewa hukumu. Katika sura hii, inasemekana wale waliohudhuria Baraza waligawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza lilisema mshitakiwa aangamizwe. Kundi la pili lilimwonea huruma kwa sababu alikuwa akitetea haki. Hukumu ilitolewa na mshtakiwa alionekana hakuwa na hatia. Hii ni kwa sababu mshtakiwa alikuwa akitafuta jinsi ya kusaidia Sheria ya Kusadikika kwa njia mpya. Baraza liliamua kwamba Karama pamoja na wale wafungwa sita ambao visa vyao vilisimuliwa wafunguliwe, wapewe fidia na yote waliyoleta Kusadikika yafuatwe.
III Maudhui
Riwaya ya
Kusadikika ina dhamira muhimu ambazo ndizo zinaunda maudhui yake. Dhamira hizo zinaweza kuchambuliwa moja baada ya nyingine. Dhamira muhimu zinazojitokeza katika riwaya hii ni pamoja na hizo zifuatazo.
· Umuhimu wa Elimu
· Suala la Haki katika Jamii
· Lila na Fila hawatangamani (ukweli)
· Hasara za wivu na tamaa zisizo mpaka
· Nafasi ya Ushauri katika Uongozi
· Nafasi ya Ndoa na Malezi n.k.
(a) Elimu katika Jamii
Riwaya ya
Kusadikika imeleta jambo moja muhimu sana katika mfumo wa maisha ya jamii. Jambo hili linahusu elimu. Elimu inatakiwa ipewe tafsiri inayostahili na ikishatafsiriwa katika misingi na mkabala unaotakiwa, ni muhimu kuhakikisha wanaohusika wanapata elimu inayotakiwa. Katika riwaya ya
Kusadikika kuna tafsiri zaidi ya moja ya “elimu ya uanasheria”. Tafsiri ya kwanza inaonyesha chuki na imepotoshwa.
Mudir wa Sheria za Kusadikika alipotakiwa kueleza maana ya uanasheria alisema: “Uanasheria ni elimu ya kupingana na sheria” (uk.8).
Lakini Karama mwenyewe (ambaye ni mshtakiwa) alitoa tafsiri ya kuridhisha: Uanasheria ni elimu ya hukumu kwa mujibu wa Sheria zilizokubaliwa. (...) Elimu hii hasa husaidia sheria kwenda katika njia yahaki ...” (uk.9).
Katika riwaya ya
Kusadikika, tumeonyeshwa kuwa elimu iliyofika nchini Kusadikika ilikuwa ya manufaa makubwa. Manufaa haya yanatokana na matumizi bora ya elimu hiyo. Mwandishi anaeleza kuwa: “Baada ya miaka michache kupita, mafunzo yote yaliyoletwa Kusadikika na wajumbe wake yaliziamsha bidii zilizokuwa zimelala. Mavuno ya mafunzo hayo yaliifanyiza Kusadikika kuwa nchi moja katika nchi zilizostawi kabisa.” (uk.57)
Kauli hii inaonyesha jamii ya Kusadikika ilitumia elimu vyema. Ni muhimu kuelewa hapa kuwajambo hilo la mafanikio halikuja kwa mara moja.
Mifano imeonyesha kuwa wengi wa watu waliokuwa madarakani, kama vile Mudir wa Sheria za Kusadikika, ilimchukua muda mrefu kukiri elimu na uwezo aliokuwa nao Karama. Ingawa Mudir wa Sheria anaonekana alikuwa na elimu, lakmi elimu yake haikutumiwa vyema kwa muda mrefu. Ndiyo maana pale mwanzoni Kusadikika ilikwama, na elimu ya Uanasheria ilipoanza kutumiwa vyema, mafunzo ya wale wajumbe kutumiwa vyema, Kusadikika ilibadilika!
(b) Haki katika Jamii
Mara nyingi watawala mbalimbali wamekuwa wakikataa kutoa
haki kwa baadhi ya watu waliopata kuonyesha uwezo maalumu wa kiuvumbuzi. Kwa mfano, inaonyeshwa katika riwaya ya
Kusadikika kuwa lengo la Karama la kuanzisha taaluma ya Uanasheria lilikuwa ni la kutaka
haki itumike katika mambo mbalimbali. Nchi ya Kusadikika inaonyeshwa kuwa ilikosa haki kwa watu wake kwa muda mrefu. Imeonyeshwa kuwa watu waliokuwa wamepewajukumu la kulinda na kutetea haki kama vile Mudir wa Sheria hawakuwa wakijua misingi ya haki yenyewe. Katika mazingira kama haya, haki haiwezi ikatendeka.
Utoaji wa haki katika jamii huleta utulivu na maendeleo makubwa. Haki huleta demokrasia ya kweli kabisa. Aidha, imebnyeshwa katika riwaya ya
Kusadikika kuwa msimamizi wa haki anatakiwa afuate misingi ya
kweli tu, Asijali cheo, dini, kabila na kadhalika. Hali, hii imeonyeshwa na Mfalme wa Kusadikika ambaye alikubali ushauri wa
Madiwani waliomwona kwanza Karama kutokuwa na hatia.
Mfalme alikiri akisema: “Taibu, hiyo ni hukumu njema. Naafikiana nanyi kabisa. Hapana hukumu nyingine iliyowezekana juu ya ushahidi uliokuwa mbele yetu. Zaidi ya hayo, natoa amri kuwa watu sita waliotajwa katika kesi hii: Buruhani, Fadhili, Kabuli, Auni, Ridhaa na Amini, wafunguliwe mara moja”. (uk.57). Aidha, mfalme anamaliza “... Kusadikika inamshukuru sana Karama kwa kuitanabaisha wajibu wake...” (uk.57).
Hapana shaka uamuzi wa aina hii haukumfurahisha waziri Majivuno; ambaye ni mtu anayesemekana alijaa
inda na tadi. Lakini angefanyaje kupingana na ukweli? Si rahisi! Majivuno hafai kuwa kiongozi wa watu.
(c) Kweli na Uongo Haviwezi kuwa pamoja
Hii ni dhamira inayoelezea juu ya kutokuwa au kutokubalika kwa mambo mawili yanayopingana pamoja. Ubaya na uzuri haviwezi vikafikia masikilizano.
Katika riwaya ya
Kusadikika mwandishi anaelezea kuwa kuna watu walipendelea kuishi katika “miiba ya mashaka ya dunia... Lila na Fila hawatangamani. Kinywa cha Lila kikasema, sikio la Fila hujidai halisikii. Jicho la Lila likiona, lile la Fila hujifanya halioni; moyo wa Lila ukijilazimisha kwa mapenzi na huruma, ule wa Fila hujifanya mgumu kamajiwe lisilo maisha kwa chuki na uadui...”
Nchi ya Kusadikika ilikuwa na maisha ya namna hii kwa muda mrefu. Wachache (Fila) waliyashika mamlaka ya Kusadikika, lakini wengi (Lila) walikuwa chini ya mamlaka haya. Riwaya ya
Kusadikika imeonyesha kuwa “vinywa vingi vikisema kwa umoja ... ni lazima mafanikio yatatokea”. Madiwani walisema kwa umoja wakashinda. Aidha,
Kusadikika imeonyesha kuwa haki ya mtu haipotei na penye ukweli uongo hujitenga. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.
Mwandishi amesisitiza sana dhana ya ukweli katika riwaya hii ya
Kusadikika. Katika moja ya kauli zake katika riwaya hii anasema hivi kuhusu msema ukweli.
“Msema kweli hukimbiwa na marafiki zake..” Hapana shaka watu walio wengi ni waongo na wanafiki, jambo ambalo Shaaban Robert analiona kama ajali. Na kwa sababu hii, Shaaban Robert anasema: “Nikipatwa na ajali kama hiyo sitaona wivu juu ya watu wawezao kudumu na marafiki zao siku zote. Siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo, nikajinyima ushirika wa milele unaotazamiwa kutokea baada ya kushindwa kwa uongo...” Katika andiko lakejingine lihusulo ukweli, Shaaban Robert anasema:
Kweli itashinda mwisho
Namna tunavyoishi
Lauongo lina mwisho
Kweli kitu cha aushi
Kweli haihofu tisho
Wala nguvu za majeshi
Kweli itashinda kesho
Kama leo haitoshi!
Falsafa ya
kweli kuhusu maisha ndiyo inayoelekea kutawala katika riwaya hii ya
Kusadikika. Falsata hii ndiyo inayojenga migogoro mbatimbali mingine ambayo inasukwa kwenye mgogoro mkubwa wa mastaka unaokuwa kati ya Waziri Majivuno na Karama anayetaka kuanzisha taaluma ya uanasheria ili kuisaidia Kusadikika.
(d) Hasara ya Wivu na Tamaa isiyo kiasi
Riwaya ya
Kusadikika inasimulia piajuu ya tatizo la wivu na tamaa isiyo na mipaka. Katika riwaya hii mwandishi anaelekea kutokubaliana na tabia hii. Mwandishi analielezajambo hili kupitia vipofu wawili, Salihi na Sapa. Salihi alikuwa na bahati ya kuomba chochote akakipata. Sapa alipoona hiyyo naye akatamani awe na uwezo huo; ikiwa na maana kuwa aliomba naye angekuwa na uwezo wa aina hii. Huu ni
wivu!
Mwandishi anaendelea kufafanua kuwa Salihi na Sapa waliandikiana mkataba wa kugawana chochote kipatikanacho, na ndipo Salihi akaomba upofu na wote wakawa vipofu. Ni wazi kuwa Sapa hakupenda hilo, lakini hii ndiyo
thamani ya chuki na wivu.
Falsafa ya mwandishijuu yamaisha inadai amani, upendo, hurumana mengineyo yanayohusu haki, uvumilivu na ukweli kwa mtu. Wivu au chuki hatimaye huleta hasara kama ilivyotokea kwa Sapa. Mwandishi, kwa kebehi na kejeli anamtumia mjumbe Auni kumshauri Sapa: “Pole, Sapa, lakini huna budi kuvumilia mazao ya wivu wako sasa ili ujifunze kuwa bahati ya mwenzio usiilalie nje! Kila mtu ana bahati yake njema” (uk.33).
Sapa alikuwa na wivu mbaya. Wivu mzuri huambatana na juhudi ya kutaka kujua maarifa na kujitahidi kufanya vizuri zaidi, lakini bila kudhuru maisha ya mtu.
(e) Nafasi ya Ndoa na Malezi
Ingawa suala hili halijitokezi kwa wazi sana, lakini mwandishi anaelekea kuamini kuwa suala la ndoa lina msingi wake imara. Mwandishi analaani tabia ya watu wenye mali lakini huzifuja kwenye tafrija na ngoma za kufurahisha. Vibaya zaidi, wenye fedha hutumia fedha hizo kwa
kuoana na kuachana kila siku. Kwa mshangao mkubwa, mwandishi anahoji hivi. “Mume mmoja ana fedha kiasi gani ya kuwaolea na kuwakimu wanawake wote wazuri, au mke mmoja ana uzuri gani wa kuolewa na kila mwanaume?”
Mwandishi anaona tatizo kubwa la kuoa au kuolewa ili kufurahisha nafsi. Thamani ya ndoa hapa haipo na kimsingi jambo hili halikubaliki. Kuhusu malezi ya watoto, mwandishi kwa kumtumia mhusika
Auni anaelezea: “Tunazaa watoto wengi lakini hatuwalei kiungwana kwa kuwafunza kuzijua dhima zao katika dunia...” (uk.36).
Ndoa ni mahusiano kati ya mwanamke na mwanamme pamoja na uwajibikaji wa msingi kuhusu masuala yote ya msingi yanayohusu unyumba. Mambu hayo ni pamoja na malezi ya watoto, matunzo na mwenendo mwema na kadhalika.
(f) Uongozi Imara unaozingatia Ushauri mzuri
Riwaya, ya
Kusadikika inaonyesha kuwa katika nchi ya Kusadikika Mfalme alikuwa mtu mwenye busara na pia watu wema walimshauri vema Mfalme.
Uongozi wa nchi yoyote ile unatakiwa uwe na nguzo za msingi katika mambo mbalimbali. Kiongozi anatakiwaawe mtu mwenye busara na anafuata haki bila kujali dini, kabila au rangi kama ambavyo mwandishi anasema; “Watu wenyewe walihitalafiana kwa rangi, lakini kwa akili zao za namna ya ajabu walipatana sana”. Mfalme wa Kusadikika ameonyesha tabia hii pia, kinyume na Waziri Majivuno au Mudir wa Sheria wa Kusadikika. Nguzo nyingine muhimu ni kuwa na washauri wanaostahili na wanaojua nini wanakifanya. Nao, kama vile ilivyo kwa Kiongozi Mkuu, wanatakiwa kuzingatia haki na ukweli, wasiwe watu wanaopendelea upande mmoja. Madiwani watiomshauri Mfalme kuhusu kesi ya Karama wameonyesha kuwa na tabia hii.
Kinyume na nguzo hizo za uongozi, nchi itaingiwa na malalamiko, dhuluma, fujo na kadhalika. Jambo hili linaweza kuiingiza nchi katika angamizo kubwa! Mshikamano miongoni mwa watu; mshikamano kati ya viongozi na waungozwa utatetereka!
(g) Hatari ya Kuamini bila Kuhoji
Nchi ya Kusadikika, imeelezwa kuwa ilikuwa na watu waliokuwa wanaamini (wanasadiki) kilajambo bila kuhoji umaana wake; wala kuwa na wasiwasi wowote. Lakini kauli hii ni ya kushangaza, na kusema kweli imewekwa kikejeli kabisa. Kwa mfano, imeelezwa kuwa
“Wakati mataifa mengine yalipojifaharisha kwa mambo kama vile enzi, uwezo na fahari nyingine, taifa la Kusadikika litijivuna kwa sababu ya kusadiki mambo yaliyotoka vinywani mwa watu wake...” Swali ni kuwa, je, mambo yenyewe yalikuwa kama hayo yanayozungumzwa na Majivuno? Kama ndiyo, tunaonyeshwa “unyonge” wa kuamini au kusadiki kila neno lililokuwa likisemwa na wasadikika. Majivuno ni mroho wa enzi na fahari.
Suala la kuhoji jambo lolote miongoni mwa nchi yoyote ni la kuimarisha demokrasia ya kweli. Kwa kutohoji, au kwa kutopewa nafasi ya kuchangia katika sera na maisha ya nchi ya Sadiki, watu wake walihitaji ukombozi mpya ambao ulikosekana.
Waziri Majivuno anaelekea kuwa kiini cha muhtasari wa tabia za serikali mbalimbali za Kusadikika ambazo kimsingi, zilikuwa za kukera. Salama ya watu wadogo ilikuwa kidogo sana katika nchi hii. Hii ni kwa sababu sheria za wasadiki zilikuwa hazimruhusu mshtakiwa kujitetea dhidi ya ushahidi wa mashtaki. Mashtaka mengi yalikubaliwa bila swali, wala kiapo, jambo ambalo hapana shaka liliongeza kero na mzigo kwa wananchi wa Sadiki wa kawaida. Kwa wenye mamlaka, jambo hili kwao linawapendeza na huwani nguzo ya ukandamizaji.
Riwaya ya
Kusadikika kwa kupitia mhusika Karama hatimaye imeonyesha umuhimu au nafasi ya demokrasia ya kujieleza na kujitetea kila pale lizukapo shtaka dhidi ya mtu yeyote. Kujitetea kwa Karama, na kushinda kwake kumetoa mafunzo makubwa kwa wasomaji wa riwaya hii. Demokrasia ya kweli ni ile inayothamini uhuru wa kauli na inayolinda sheria.
(h) Umuhimu wa Kutunza siri
Shaaban Robert anaelekea pia kusisitiza umuhimu wa kutunza siri. Siri kama haitunzwi si rahisi kuwa na mipango ya kiutawala ambayo ni ya manufaa kwa watu. Kabla jambo halijafanyika ni lazima mipango iwe ya siri kwanza. Penye siri pana
thamani kubwa katika mazingira ya kawaida. Lakini ni kweli pia penye siri panaweza pawe na mauaji, fujo, fitina na kunyimwa haki kwa baadhi ya watu. Katika
Kusadikika, imeelezwa kuwa
Karama alikuwa na siri “kama Kaburi lifunikavyo maiti. Alijizoeza kuvitumia vipawa hivi mpaka vilikuwa tayari kutumika siku yoyote katika maisha yake”. Muda wa matumizi ya siri hiyo ulikuwa umefika!