Unaona sura ya Bunge Maalum? Hakuna sehemu kwenye Sheria Mabadiliko ya Katiba sura ya 83 (toleo la mwaka, 2014) inayoonesha vyama vya siasa. Vyama hivi ni watu tuu ndiyo wanavitanguliza badala ya utaifa. Hebu angalia sehemu ya tano ya sheria hiyo kuhusu Kuitisha Bunge Maalum, inasema Kuitisha Bunge Maalum ni halali kwa kuzingatia Sheria Na. 9 ya mwaka, 2013 na kuatangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 394 la mwaka 2011 Amri ya 2 aya (r) 22.-(1) kwamba kutakuwa na Bunge Maalum litakalokuwa na wajumbe wafuatao: (a) wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano; (b) wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Kuhusu wajumbe hawa 201 watakaoteuliwa na Rais kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar idadi hiyo inakamilika kutokana na mchanganuo huu: (i) wajumbe ishirini kutoka Taasisi zisizokuwa za Kiserikali. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba [Sura ya 83 Toleo la mwaka 2014] inasema (ii) wajumbe ishirini kutoka Taasisi za Kidini; (iii) wajumbe arobaini na mbili kutoka Vyama vyote vya Siasa vyenye usajili wa kudumu; (iv) wajumbe ishirini kutoka Taasisi za Elimu; (v) wajumbe ishirini kutoka katika makundi ya watu wenye ulemavu; (vi) wajumbe kumi na tisa kutoka Vyama vya Wafanyakazi; (vii) wajumbe kumi kutoka Vyama vinavyowakilisha Wafugaji; (viii) wajumbe kumi kutoka Vyama vinavyowakilisha Wavuvi; (ix) wajumbe ishirini kutoka Vyama vya Wakulima; (x) wajumbe ishirini kutoka makundi mengine yoyote ambayo yana malengo yanayofanana.
Ninafurahi kuwa wapo Watanzania wanaojali taifa lao na wamegundua ni vema kujenga utaifa badala ya kuendekeza malumbano na matusi yasiyo tija kwa nchi yetu. Tujenge misingi imara juu ya Katiba Inayopendekezwa ifae hata zaidi ya miaka 50 ijayo.